4x4

HOTUBA YA RAIS DK. MAGUFULI, WAKATI WA UFUNGUZI WA MKUTANO MKUU WA 33 WA JUMUIYA YA TAWALA ZA MITAA TANZANIA (ALAT), ULIOFANYIKA OKTOBA 3, 2017 KATIKA UKUMBI WA MWALIMU JULIUS NYERERE, DAR ES SALAAM

HOTUBA YA MHESHIMIWA DK. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA UFUNGUZI WA MKUTANO MKUU WA 33 WA JUMUIYA YA TAWALA ZA MITAA TANZANIA (ALAT), KATIKA UKUMBI WA MWALIMU JULIUS NYERERE, DAR ES SALAAM, TAREHE 03 OKTOBA, 2017Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu
          wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

Gulamhafeez Mukadamu, Mwenyekiti wa ALAT
na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga,

Mheshimiwa Stephen Peter Mhapa, Makamu Mwenyekiti wa ALAT
na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya  ya Iringa,

Mheshimiwa Seleman Jafo, Naibu Waziri wa Nchi
Ofisi ya Rais-TAMISEMI;

Mheshimiwa Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;
Waheshimiwa Wabunge mliopo hapa;

Wastahiki Mameya wa Majiji na Manispaa pamoja na
Waheshimiwa Wenyeviti wa Halmashauri za Miji na Wilaya;

Waheshimiwa Madiwani wa Dar es Salaam, mkiongozwa
na Mstaiki Meya Isaya Mwita;

Mstahiki Meya wa Zanzibar pamoja na Viongozi mbalimbali
kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar;
Mhandisi Mussa Iyombe, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – TAMISEMI;
Prof. Faustin Kamuzora, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais;
Bwana Abdallah Ngodu, Kaimu Katibu Mkuu wa ALAT;
Wakurugenzi wa Majiji, Manispaa, Miji na Halmashauri za Wilaya;
Wawakilishi wa Jumuiya za Serikali za Mitaa kutoka
Nchi za Afrika Mashariki mliopo;

Wawakilishi wa Wadhamini kutoka Makampuni
na Mashirika ya Serikali na Yasiyo ya Kiserikali,

Wawakilishi wa Vikundi vya Wajasiriamali;
Ndugu Waandishi wa Habari;
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana:
Napenda nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Muumba wetu, ambaye ametupa uhai na kutuwezesha kukutana hapa. Aidha, nakushukuru sana Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tawala za Serikali za Mitaa Tanzania (Association of Local Government Authorities of Tanzania – ALAT), Mheshimiwa Mukadamu, kwa kunialika kufungua Mkutano huu Mkuu wa 33 wa ALAT. Nasema Ahsante sana.

Natambua baadhi yenu hapa mmesafiri umbali mrefu kuja kuhudhuria Mkutano huu, ambao awali ulipangwa kufanyika Jijini Mbeya, lakini siku za mwishoni ukalazimika kuhamishiwa hapa Dar es Salaam. Hivyo basi, kwanza, napenda kuwapa pole kwa uchovu wa safari. Lakini pili, kama mnavyofamu, mimi pamoja na kuwa na majukumu ya Urais, nina dhamana kwenye Wizara ya TAMISEMI; hivyo basi, napenda niwakaribishe wajumbe wote hapa Dar es Salaam na katika Mkutano huu wa 33 wa ALAT. Karibuni sana ndugu wajumbe.

Napenda pia hapa mwanzoni kabisa nimshukuru Mwenyekiti wa ALAT Taifa kwa salamu za pongezi alizozitoa kwangu, hususan kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano wa nchi yetu. Namshukuru pia kwa pongezi zake kuhusu utendaji kazi wa Serikali ya Awamu ya Tano. Nasema ahsante sana. Mmezidi kutupa moyo wa kuendelea kufanya kazi kwa bidii. Lakini nami ningependa kutumia fursa hii kuwapongeza, wewe Mheshimiwa Mwenyekiti na Makamu wako, Wastahiki Mameya wa Majiji na Manispaa pamoja na Wenyeviti wa Halmashauri zote nchini kwa kuchaguliwa kwenu. Napenda niwaahidi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itashirikiana nanyi kwa karibu katika kuhakikisha tunaleta maendeleo kwa wananchi na nchi yetu kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti;
Ndugu Wajumbe, Mabibi na Mabwana;
Kwangu mimi, Mkutano huu ni muhimu sana. Ni muhimu kwa sababu, kama mnavyofahamu, ALAT ni chombo kinachounganisha pamoja mamlaka na wadau mbalimbali wanaohusika na masuala ya Serikali za Mitaa hapa nchini. Na sote hapa tunatambua kuwa Serikali za Mitaa ni mamlaka ambazo zipo karibu zaidi na wananchi. Kwa sababu hiyo, binafsi naona kuwa hii ni fursa nzuri kwangu kuzungumza kwa kina na Watanzania wenzangu; na hasa kwa kuzingatia kuwa hii ni mara yangu ya kwanza kuhudhuria Mkutano huu wa ALAT, tangu nimechaguliwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano wa nchi yetu. Hivyo basi, nina imani Mheshimiwa Mwenyekiti pamoja na ndugu wajumbe mtaniruhusu, kabla ya kuzungumzia masuala yaliyotuleta hapa, kueleza hatua mbalimbali ambazo tumechukua tangu tumeingia madarakani pamoja na mipango na mikakati tuliyonayo ya kuleta maendeleo kwa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti na Ndugu Wajumbe;
Tangu tumeingia madarakani, takriban miezi 23 iliyopita, tumefanya mambo mengi ya kuleta maendeleo kwa nchi yetu. Mtakumbuka, tulianza kwanza kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kudhibiti ubadhirifu wa mali za umma. Tulibana mianya ya ukwepaji kodi na hivyo kutuwezesha kuongeza ukusanyaji wa mapato kutoka wastani wa shilingi bilioni 850 kwa mwezi hadi kufikia shilingi trilioni 1.3. Sambamba na kuongeza ukusanyaji mapato, tuliamua kudhibiti ubadhirifu wa mali za umma. Tumezuia safari za nje, warsha na semina zisizo na tija. Hivi majuzi tu mmesikia kuwa ujumbe wetu kwenye Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ulikuwa na watu watatu tu na walituwakilisha vyema.

Kutokana na kuongeza mapato na kubana matumizi, hivi sasa tunawalipa mishahara ya watumishi wetu kwa wakati. Aidha, tumeweza kulipa madai mbalimbali ya watumishi, ikiwa ni pamoja na michango yao kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii. Zaidi ya hayo, tumeweza kuongeza bajeti yetu ya maendeleo kutoka wastani wa asilimia 26 hadi kufikia wastani wa asilimia 40 hivi sasa.

Hii ndiyo imetuwezesha kupanua wigo na kuboresha huduma mbalimbali za jamii, hususan elimu, afya na maji. Kama mnavyofahamu, kwenye elimu, baada ya kuingia madarakani, tulianza kutoa elimu bila malipo kuanzia shule ya msingi hadi sekondari, ambapo mwanzoni tulikuwa tukitenga kila mwezi shilingi bilioni 18.77. Mwezi Julai 2016, kiasi hicho kiliongezwa hadi kufikia shilingi bilioni 23.868, na hivyo kufanya hadi mwezi Agosti mwaka huu, kuwa tumetumia kiasi cha shilingi bilioni 465.6 kugharamia elimu bila malipo. Matokeo yake, bila shaka, nyote hapa mnafahamu. Idadi ya wanafunzi wanaoanza darasa la kwanza na kidato cha kwanza imeongezeka maradufu; darasa la kwanza kwa takriban asilimia 90 na kidato cha kwanza takriban asilimia 25. Tumeongeza pia idadi ya wanafunzi wa elimu ya juu wanaopata mikopo kutoka 98,300, wakati tunaingia madarakani, hadi kufikia takriban 125,000.  Hii imewezekana baada ya kuongeza bajeti ya mikopo kutoka shilingi bilioni 365 hadi kufikia shilingi bilioni 483.

Kwenye afya, nako tumeimarisha na kuboresha upatikanaji wa huduma hiyo. Tumeongeza bajeti ya kununua madawa kutoka shilingi bilioni 31 wakati tunaingia madarakani hadi kufikia shilingi bilioni 269, mwaka huu wa fedha. Hii imeongeza sana upatikanaji wa madawa kwenye hospitali zetu, na hasa baada ya Serikali kuanza utaratibu wa kununua dawa moja kwa moja kutoka kwenye viwanda zinakozalishwa. Aidha, Serikali imegawa katika kila halmashauri vifaa tiba, ikiwemo vitanda ya kawaida, vitanda vya kujifungulia, magodoro na mashuka, ambavyo thamani yake kwa ujumla ni shilingi bilioni 3.58. Halikadhalika, katika kuboresha Huduma za Afya ya Mama na Mtoto, Serikali ilipata fedha jumla ya shilinigi bilioni 161.9 kutoka Benki ya Dunia pamoja na wadau wengine wanaosaidia sekta ya afya kwenye Mfuko wa Pamoja (Busket Fund). Fedha hizo zimepangwa kutumika kuboresha vituo vya afya 170 ili kuviwezesha kutoa huduma za uzazi za dharura kwa lengo la kuokoa maisha ya mama na mtoto; na zinatumwa moja kwa moja katika vituo vya afya husika katika mwaka huu wa fedha.
Kuhusu sekta ya maji, miradi mingi ya maji hivi sasa inatekelezwa sehemu mbalimbali nchini. Karibu kwenye mikoa yote kuna miradi mikubwa ya maji inatekelezwa. Mathalan, mwezi Machi 2017, nilikuwa Mkoa wa Lindi ambapo nilitoa maelekezo ya kukamilishwa kwa haraka mradi wa maji wa Ng’apa wenye thamani ya shilingi bilioni 32, ambao nimeambiwa unaendelea kukamilika. Mwezi Juni mwaka huu, nilizindua Mradi wa Maji wa Ruvu Juu pale Mlandizi kwa ajili ya kuhudumia Jiji hili la Dar es Salaam na sehemu za Mkoa wa Pwani. Aidha, mwezi Julai, nilizindua mradi mkubwa wa maji pale Sengerema wenye thamani ya shilingi bilioni 22.4. Mwezi Julai pia niliweka Mawe ya Msingi kwenye mradi wa maji wa Kigoma wenye thamani ya shilingi bilioni 42 na Mradi Mkubwa wa Maji kutoka Ziwa Victoria kwenda miji ya Nzega, Tabora na Igunga wenye thamani ya shilingi ya shilingi bilioni 550. Juzi mmeshuhudia Mheshimiwa Waziri Mkuu akizindua mradi wa maji kule Longido wenye thamani ya shilingi bilioni 16; lakini nafahamu pia mradi wa maji wa Musoma umekamilika na unasubiri kuzinduliwa. Halikadhalika, nafahamu kuwa kuna mradi mkubwa wa maji unatekelezwa katika jiji la Arusha wenye thamani ya shilingi bilioni 476, na wakati wowote tutaanza utekelezaji wa mradi mwingine mkubwa wenye thamani ya shilingi bilioni 250 kwa ajili ya miji ya Bariadi, Legangabilili, Maswa, Meatu na Busega. Kama hiyo haitoshi, mwezi Julai mwaka huu, Serikali ya India ilitupatia mkopo wa masharti nafuu wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 500, sawa na takriban shilingi trilioni 1.2, kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji kwenye miji 17, ikiwemo Zanzibar. Kwa ujumla, miradi mingi inatekelezwa sehemu mbalimbali nchini. Hivyo basi, nina imani kuwa baada ya muda mfupi, tutakuwa tumepunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la maji nchini. Nitoe wito kwenu viongozi wa Serikali za Mitaa kuendelea kuwahamasisha wananchi kutunza mazingira pamoja na vyanzo vya maji. Bila kufanya hivyo, itafika wakati tutakuwa na miundombinu mizuri isiyotoa maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti na Ndugu Wajumbe;
Mbali na kuboresha huduma za jamii, tumeweza kuimarisha miundombinu ya kiuchumi, hususan usafiri na nishati. Tumeanza ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza na Kigoma na kisha nchi za Burundi na Rwanda, kwa fedha zetu wenyewe. Ujenzi wa kipande cha kilometa 300 kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro tayari umeanza, ambapo kiasi cha shilingi trilioni 2.74 kitatumika.  Na hivi majuzi (ijumaa), tumesaini mkataba wa kuanza ujenzi wa kipande cha kilometa 412 kutoka Morogoro hadi Dodoma (Makutopora) kwa thamani ya shilingi trilioni 4.328; na hivyo gharama za ujenzi kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma kufikia shilingi trilioni 7.062.
Tunafanya upanuzi wa Bandari zetu za Mtwara na Dar es Salaam. Mwezi Machi mwaka huu, niliweka Jiwe la Msingi la Upanuzi wa Bandari ya Mtwara kwa thamani ya shilingi bilioni 130. Aidha, mwezi Julai mwaka huu, niliweka Jiwe la Msingi la Upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam, ambao thamani yake ni shilingi bilioni 926.2.  Kama hiyo haitoshi, wakati nikiwa Tanga katika sherehe za kuweka Jiwe la Msingi la Mradi wa Bomba la Mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga, nilimwagiza Waziri wa Ujenzi kuanza taratibu za kutafuta mkandarasi wa kupanua Bandari ya Tanga kwa thamani ya shilingi bilioni 16. Vilevile, tumetengeneza meli mbili za Mv. Iringa na Mv. Ruvuma, ambazo zinatoa huduma katika Ziwa Nyasa. Aidha, tupo katika hatua za mwisho za kupata wakandarasi kwa ajili ya ukarabati wa meli mbili za Mv. Victoria na Butiama pamoja na ununuzi wa meli mpya kwa ajili ya Ziwa Victoria.
Sambamba na hayo, tunakamilisha upanuzi wa Viwanja Vikubwa vya Ndege vya Mwalimu Julius Nyerere kwa gharama ya shilingi bilioni 560 na Kilimajaro kwa thamani ya shilingi bilioni 91. Aidha, tunaendelea na ukarabati wa viwanja takriban 11 vya ndege sehemu mbalimbali nchini, ikiwemo Mwanza (shilingi bilioni 90); Mtwara (shilingi bilioni 46); Shinyanga (shilingi bilioni 49.2); Sumbawanga (shilingi bilioni 55.9); Musoma (shilingi bilioni 21), Songea (shilingi bilioni 21) na Iringa (shilingi bilioni 39). Tumenunua ndege mpya sita, mbili tayari zimewasili na kuanza kazi, kwa ajili ya kutoa huduma ya usafiri na kukuza sekta ya utalii. Kama mnavyofahamu, ukuaji na ustawi wa sekta ya utalii kwa kiasi kikubwa unategemea uwepo na ubora wa usafiri wa anga katika nchi. Vilevile, ujenzi wa barabara unaendelea vizuri. Tangu tumeingia madarakani tumeshajenga takriban kilometa 1,500 za lami kwa thamani ya shilingi trilioni 1.8. Na nyingi bado tunaendelea kuzijenga. Nikianza kuzitaja tunaweza kumaliza kesho. Lakini kwa kuwa leo tupo hapa Dar es Salaam, niseme tu kuwa, moja ya barabara tunayotarajia kuanza kujenga hivi karibuni ni barabara ya njia sita kutoka Dar es Salaam hadi Chalinze. Aidha, tunaendelea na ujenzi wa barabara za juu pale TAZARA (shilingi bilioni 94.031) na Ubungo (shilingi bilioni 177.424); na muda si mrefu tutaanza ujenzi wa Awamu ya II, III na III za miundombinu ya magari ya mwendokasi kwa thamani ya shilingi bilioni 891. Tunajenga miundombinu hii ili kupunguza tatizo la msongamano wa magari katika Jiji hili.
Kuhusu umeme, nako tunaendelea vizuri. Lakini tunafahamu kuwa mahitaji ya umeme nchini bado ni makubwa. Hivyo, tunaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kuzalisha umeme, ikiwemo Kinyerezi I na II, ambayo kwa pamoja inatarajiwa kuzalisha Megawati 565, kwa kutumia gesi yetu asilia. Miradi hii kwa ujumla ina thamani ya shilingi trilioni 1.2. Aidha, maandalizi kwa ajili ya miradi ya Kinyerezi III na IV, ambayo itazalisha takriban Megawati 600, inaendelea vizuri. Tumeanza pia maandalizi ya ujenzi wa mradi mkubwa wa kuzalisha umeme wa maji pale Stiglier’s Gorge, ambao utazalisha Megawati 2,100. Tunataka, hadi kufikia mwaka 2020, nchi yetu iwe na angalau Megawati 5,000 kutoka Megawati 1,460 za sasa. Sambamba na hilo, tunaendelea na jitihada za kupeleleka umeme vijijini. Mpaka sasa, tumeshapeleka umeme kwenye vijiji zaidi ya 4,000. Aidha, mwaka huu tumeanza Awamu ya Tatu ya Mpango wa Umeme vijijini. Lengo letu ni kufikisha miundombinu ya umeme kwenye vijiji vipatavyo 7,873 ifikapo mwaka 2020/21.  Katika bajeti ya mwaka huu, tumetenga shilingi bilioni 469.09 kuanza kutekeleza mradi huo. Tunataka dhana ya viwanda inasambae hadi vijijini.
 Mheshimiwa Mwenyekiti na Ndugu Wajumbe;
Mbali na kuongeza ukusanyaji mapato na kudhibiti matumizi, tumeimarisha nidhamu na kurejesha heshima kwenye utumishi wa umma. Tumewachukulia hatua za kinidhamu baadhi ya watumishi wazembe na wala rushwa. Zaidi ya hapo, tumewaondoa takriban watumishi hewa wapatao 20,000, ambao walikuwa wakiigharimu Serikali takriban shilingi bilioni 19.848 kwa mwezi; na kwa mwaka shilingi bilioni 238.176. Vilevile, tumewaondoa watumishi wenye vyeti feki wapatao 12,000, ambao kwa mwaka waligharimu Serikali shilingi bilioni 142.9. Tumefanya hivyo ili kurudisha nidhamu na kuenzi elimu na ueledi katika utumishi wa umma. Mtakubaliana nami kuwa, uwepo wa watumishi hewa na wenye vyeti feki ulikuwa ukizorotesha na kupunguza ufanisi katika utoaji huduma kwenye taasisi za umma. Aidha, uwepo wa watumishi wenye vyeti feki ulikuwa unapunguza heshima na hadhi ya elimu na ujuzi, na hivyo, kushusha ari na morali miongoni mwa watumishi wenye sifa.
Sambamba na hilo, tumejitahidi kuondoa kero mbalimbali, ambazo zilikuwa zikiwasumbua wananachi. Mathalan, tumeondoa kero za utitiri wa kodi kwa wakulima, wafugaji na wavuvi. Tumefuta tozo 80 kwa wakulima, tozo 7 kwa wafugaji na tozo 5 kwa wavuvi. Tumepiga marufuku kutoza kodi mazao yanayosafirishwa kutoka Halmashauri moja kwenda nyingine, ambayo uzito wake hauzidi tani moja. Na kwa kuwa tozo hizi nyingi tulizozifuta zilikuwa zikisimamiwa na ninyi watu wa Serikali za Mitaa, niwaombe kupitia vikao vyenu, mkafanye taratibu za kuzifuta kama bado hamfanya hivyo. Lakini, kama hiyo haitoshi, kwa wakulima pia, kufuatia uamuzi wa Serikali wa kuanzisha utaratibu wa kununua mbolea kwa pamoja (Bulk Procurement System – BPS), tumeweza kupunguza bei ya mbolea ya kupandia na kukuzia kuanzia mwezi uliopita (Septemba). Mathalan, Mkoani Lindi, bei ya mfuko mmoja wa mbolea ya kupandia imeshuka kutoka shilingi 100,000 hadi kufikia shilingi 51,000. Mikoa mingine bei zimepungua kutegemeana na gharama za usafirishaji. Na huu ni mwanzo tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti na Ndugu Wajumbe;
Baada ya kuchukua hatua za kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kudhibiti matumizi; kuboresha huduma za jamii; kuimarisha miundombinu ya uchumi; kurejesha heshima ya utumishi wa umma na kushughulikia baadhi ya kero zinazowakabili wananchi wetu; ambazo kimsingi, bado tunaendelea nazo, sasa tumeanzisha vita ya uchumi. Kama mnavyofahamu, nchi yetu ni tajiri. Tuna rasilimali za kila aina. Tunayo madini misitu, rasilimali za misitu na majini, n.k. Aidha, nchi yetu inashika nafasi ya pili kwa vivutio vya utalii duniani baada ya Brazil. Lakini pamoja na kuwa na rasilimali nyingi kiasi hicho, bado hazijatunufaisha. Wanaonufaika ni watu wengine.

Kutokana na hali hiyo, tumeamua kuchukua hatua za makusudi kulinda rasimali zetu. Mlisikia kuwa tuliunda Tume za kuchunguza biashara ya madini na vito vya thamani. Matokea yake, kila mmoja wetu hapa amesikia.  Lakini kwa kifupi, tulikuwa tunaibiwa sana. Kwa sababu hiyo, mwezi Julai 2017 tulipitisha Sheria za kulinda rasilimali zetu, hususan madini. Aidha, kwa lengo hilo hilo la kulinda rasilimali zetu, hivi majuzi nikiwa Mererani niliagiza kuanza mara moja kwa ujenzi wa uzio kuzunguka eneo lenye rasilimali nyingi ya madini ya Tanzanite, ili kudhibiti vitendo vya wizi. Nafurahi ujenzi huo tayari umeanza. Lakini niseme tu kuwa huu ni mwanzo tu. Hatutaishia kwenye madini pekee. Tutaenda pia kwenye rasilimali zetu nyingine, ikiwemo za utalii, misitu na za majini. Tunataka kuona, rasilimali za nchi yetu, zinatunufaisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti na Ndugu Wajumbe;
Katika kuchukua hatua hizi, ni dhahiri kuwa wapo watu walioathirika na kuumia. Na natambua kuwa wapo watu wanalalamika. Lakini kwangu mimi, hili ni jambo la kawaida, kama kweli tunahitaji maendeleo. Maendeleo hayaji kirahisi. Maendeleo sio lelemama. Maendeleo ni mapambano. Hivyo basi, niwaombe Watanzania wenzangu tujidhatiti katika harakati za kuleta maendeleo kwa nchi yetu. Waingereza wana usemi wao usemao “No Pain, No Gain” au “No sweet without sweat”.  Lakini ningependa kusema tu kuwa watu wengi wanaolalamika hivi sasa ni wale waliokuwa wakinufaika na mfumo ulikuwepo zamani.  Huwezi kutegemea mmiliki wa benki iliyokuwa ikinufaika kwa kufanya biashara na Serikali afurahie hatua tunazozichukua; Haiwezekani mtu aliyekuwa akilipwa mishahara na posho za watumishi hewa afurahie hatua tunazochukua; Huwezi kutegemea mtu aliyekuwa akikwepa kodi afurahie hatua tunazozichukua; Huwezi kutegemea mtu aliyezoea kusafiri nje kila wiki afurahie hatua tunazozichukua; huwezi kutegemea mtu aliyepata ajira kwa kutumia cheti feki alichokinunua Kariakoo afurahie hatua tunazozichukua. Lakini pia huwezi kutegemea mtu aliyekuwa akinufaika na fedha za pembejeo hewa (ambapo katika Halmashauri 140 zilizofanyiwa uchunguzi, imebainika kuwa zilitolewa pembejeo hewa zenye thamani ya shilingi bilioni 57.963) na kaya masikini hewa (56,000) kupitia TASAF, afurahie hatua tunazozichukua.  Ni dhahiri kuwa watu waliokuwa wakinufaika, watalalamika.

Hivyo basi, binafsi sishitushwi sana na malalamiko yanayotolewa na baadhi ya watu. Natambua, ukitumbua mtu jipu ni lazima atalalamika. Sana sana tu, kelele zinazopigwa hivi sasa zinatuongezea nguvu zaidi ya kuendelea na jitihada tulizozianza, ambazo kwa hakika kabisa, naweza kusema sio tu zinaungwa mkono na wananchi walio wengi bali pia zimeanza kuleta matokeo chanya ya kiuchumi kwa nchi yetu.   Kama mnavyofahamu, nchi yetu ni miongoni mwa nchi zinaongoza kwa ukuaji uchumi Barani Afrika hivi sasa, ambapo mwaka huu uchumi wetu unatarajiwa kukua kwa asilimia 7.1. Hii inafanya nchi yetu kushika nafasi ya tatu. Sambamba na hilo, tumeweza kudhibiti mfumko wa bei.  Mathalan, mwezi Julai, mfumko wa bei ulikuwa asilimia 5.2, lakini mwezi Agosti ulishuka hadi kufikia asilimia 5.0. Hii ni dalili njema. Lakini zaidi ya hapo, kinyume na baadhi ya watu wanavyosema, nchi yetu imeendelea kung’ara katika kuwavutia wawekezaji wengi. Hivi majuzi mmemsikia Mkurugenzi Mkuu wa Kituo Cha Uwekezaji (Tanzania Investment Centre – TIC) akieleza kuwa mwaka uliopita nchi yetu iliongoza kwa kuvutia wawekezaji wengi kwenye Ukanda wetu wa Afrika Mashariki. Tathmini hii inaenda sambamba na Ripoti ya African Economic Outlook Toleo la 16 iliyotolewa kwa pamoja na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), ambayo inataja nchi yetu kuwa miongoni mwa nchi kumi bora Barani Afrika kwa kuvutia wawekezaji mwaka 2016. Na hiki ni kielezo kuwa hatua tunazochukua ni nzuri na mwelekeo wetu ni mzuri. Na huenda hii ndio sababu viongozi wengi wa nje wanatembelea nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti;
Ndugu Wajumbe, Mabibi na Mabwana;
Niliona nianze na hayo ili kuwapa taswira halisi ya hali ilivyo hapa nchini. Na kwa kuwa ninyi mko karibu zaidi na wananchi na mnashirikiana nao kwenye mambo mengi, nina uhakika kuwa mtaenda kuwafafanuliwa kuhusu hatua hizi tunazozichukua. Baada ya kusema hayo, sasa naomba nizungumzie masuala yanayohusu Mkutano huu wa leo.

Kwanza kabisa, napenda kuipongeza ALAT pamoja na mamlaka za Serikali za Mitaa kote nchini kwa kazi kubwa mnazofanya katika kuleta maendeleo kwa nchi yetu. Mafanikio mengi ya Serikali niliyoyataja hapo awali, yamepatikana kutokana na jitihada mnazozifanya ninyi lakini pia ushirikiano mnaotupa sisi wa Serikali Kuu. Kwa kutumia vyanzo vyenu vya mapato, mmeweza kutekeleza miradi mingi ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa shule, hospitali, vituo vya afya, zahanati, miradi ya maji pamoja na barabara. Aidha, mara nyingi, ninyi ndio mmekuwa wasimamizi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali Kuu kwenye maeneo yenu.  Kwa sababu hiyo, sina budi, kuwapongeza.

Lakini pamoja na pongezi hizo, hampaswi kuridhika na mafanikio yaliyopatikana. Kama mnavyofahamu, nchi yetu bado ina safari ndefu ya kufikia kule tunakotamani. Mathalan, nimeeleza hapo awali kuwa Serikali hivi sasa inatekeleza elimu bila malipo, lakini ukiachilia mbali tatizo la uhaba wa madawati ambalo tumelipunguza kwa kiwango kikubwa, bado tuna upungufu wa madarasa, maabara, vyoo, nyumba za walimu, n.k.  Hivyo basi, Mamlaka za Serikali za Mitaa, hazina budi, kubuni mikakati ya kushughulikia matatizo hayo. Aidha, kwa kuwa mko karibu na wananchi, mnao wajibu wa kuwahimiza wananchi kupeleke watoto wao mashuleni ili wanufaike na fursa iliyotolewa na Serikali ya kutoa elimu bila malipo.

Kwenye afya pia, bado kuna upungufu mkubwa ya miundombinu, ikiwemo hospitali, vituo vya afya, zahanati, nyumba za watumishi, n.k. Huko nako hamna budi kubuni mikakati ya kushughulikia matatizo hayo. Aidha, kwa kuwa hivi sasa Serikali imeongeza upatikanaji wa madawa kwenye hospitali zetu, niwaombe waheshimiwa Madiwani na Wakurugenzi mwendelee kuhamasisha wananchi kujiunga na mifuko ya bima za afya ili kupata matibabu bila vikwazo. Vilevile, hakikisheni mnasimamia vyema fedha na matumizi ya dawa, ikiwemo kuanzisha mifuko ya dawa (Drug Revolving Fund) kwa kila Halmashari, ili kuhakikisha upatikanaji endelevu wa fedha za dawa.

Sambamba na hayo, ili kuhakikisha mnakuwa na uwezo wa kutosha wa kuboresha huduma za jamii nilizozitaja na kutekeleza miradi ya maendeleo, hamna budi kuimarisha ukusanyaji wa mapato. Nafahamu hii ni changamoto kubwa inayozikabili mamlaka za Serikali za Mitaa. Na kimsingi, nionavyo mimi, tatizo sio kwamba hakuna vyanzo vya mapato. Hapana. Hali hii inatokana na sababu kubwa mbili. Kwanza, fedha nyingi zinazokusanywa hupotelea kwenye mifuko ya “wajanja” wachache. Pili, watendaji wengi wanakosa ubunifu katika kubuni vyanzo endelevu vya mapato. Ndio maana kila siku utaona wanaongeza tozo kwenye mazao ya wakulima, wavuvi au wafugaji. Hivyo basi, nitoe wito kwenu kuhakikisha mnatengeneza mifumo madhubuti ya ukusanyaji mapato, hususan ukusanyaji mapato kwa njia ya kielektroniki. Na katika hili,  ningependa kuwasisitiza kutumia Wakala wa Serikali Mtandao katika kutengeneza mifumo yenu ya ukusanyaji kodi. Aidha, nawahimizeni kubuni vyanzo endelevu vya mapato.

Halikadhalika, kuhakikisheni mnasimamia vizuri fedha mnazokusanya na zile zinazotolewa na Serikali Kuu kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo. Natambua hivi sasa suala la hati chafu limepungua kwenye halmashauri nyingi. Lakini hii haimanishi kuwa ubadhirifu na wizi umekwisha kwenye Halmashauri zetu.  Ubadhirifu bado upo. Imethibitika kuwa mara nyingi taarifa za vitabuni hazifanani na hali halisi ya utekelezaji wa miradi na kazi (value for money). Kwa maneno mengine, kazi inayofanyika hailingani na thamani halisi ya fedha inayotumika. Hivyo basi, nawaomba ndugu wajumbe mlipe suala hili la usimamizi wa fedha za Serikali kipaumbele kinachostahili. Miradi inayotekelezwa ni lazima iendane na thamani ya fedha zinazotolewa. Na katika hili, msisite kuwachukuliwa hatua za kinidhamu au kuwatumbua wale wote wakatakaojihusisha na ubadhirifu wa fedha zinazotolewa kwa ajili ya maendeleo ya wananchi. Lakini niwaombe na ninyi kuacha mtindo wa kutoa zabuni kwenye makampuni yenu au ya washirika wenu, ambayo hayana uwezo wa kutekeleza miradi husika.
Masuala mengine ambayo ningetamani sana kuona mnayapa kipaumbele kwenye maeneo yenu ni kudhibiti migogoro na makundi kwenye halmashauri zetu. Haipendezi kuona, kwenye Halmashauri, kuna kundi la Meya na Naibu Meya; ama kundi la Mwenyekiti na Mkurugenzi. Hali hii inazorotesha utendaji na kupunguza kasi ya kuwapelekea maendeleo wananchi. Nawasihi pia muendelee kushughulikia kero mbalimbali zinazowakabili wananchi, hasa wananchi wa kipato cha chini, ikiwemo, kama nilivyosema awali, utitiri wa kodi kwa wakulima, wafugaji na wavuvi; na halikadhalika ukosefu wa maeneo ya biashara kwa wafanyabiashara wadogo. Vilevile, nawasihi muendelee kuwahimiza wananchi kuhusu umuhimu wa kudumisha amani na umoja wetu, kulipa kodi na kuchapa kazi kwa bidii. Nina imani, sote tukifanya haya, nchi yetu itapata maendeleo, tena kwa haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Katika risala yako umeeleza kuhusu mipango yenu mbalimbali na kuwasilisha baadhi ya maombi. Kwa ujumla, niseme tu kuwa nimeyapokea maombi yenu yote. Lakini nakiri kuwa nimefarijika sana kusikia azma yenu ya kuhamishia Makao Makuu yenu kutoka hapa Dar es Salaam kwenda Dodoma, Makao Makuu ya nchi yetu. Nawapongezi sana kwa kuunga mkono dhamira ya Serikali ya kuhamia Dodoma. Na napenda kutumia fursa hii kuwahakikishia kuwa, kama nilivyoahidi kwenye hotuba yangu ya kupokea wadhifa wa kuwa Mwenyekiti wa CCM mwezi Julai mwaka jana, hadi kufikia mwaka 2020, Serikali yote itakuwa imehamia Dodoma. Kama mnavyofahamu, tayari Waziri Mkuu, Mawaziri, Makatibu Wakuu na baadhi ya watendaji wa Wizara wameshahamia Dodoma. Makamu wa Rais anatarajia kuhamia mwaka huu. Na mimi natarajia kuhamia mwakani. Hivyo basi, narudia tena, kuwashukuru kwa uamuzi wenu wa busara wa kuhamia Dodoma. Na kuhusu jengo mnalotaka kujenga Dodoma kwa ajili ya ofisi na kitega uchumi, wakati ukifika, Serikali kulingana na uwezo wake wa kifedha, itaangalia uwezekano wa kuwaunga mkono.
Kwenye Risala yako pia umeeleza suala la ucheleweshaji wa fedha za maendeleo kutoka Serikali Kuu, suala la uhaba wa watumishi wa Serikali za Mitaa na pia posho za Waheshimiwa Madiwani. Serikali inatambua masuala hayo yote. Tutaendelea kuhimiza HAZINA kutoa fedha za maendeleo kwa haraka. Kama mnavyofahamu, tangu tumeingia madarakani, tumejitahidi sana kuhakikisha fedha zinatolewa kwa wakati. Mathalan, katika Bajeti ya mwaka 2014/2015 fedha za maendeleo zilizotengwa kwenda kwenye halmashauri (Serikali za Mitaa) ni shilingi bilioni 339.8 lakini zilizotoka zilikuwa shilingi bilioni 250.2 sawa na asilimia 62; mwaka 2015/16 zilitengwa shilingi bilioni 296.3, zikatolewa shilingi bilioni 168.8 sawa na asilimia 57; mwaka 2016/17 zilitengwa shilingi bilioni 256.7, zilizotolewa ni shilingi 251.5 sawa na asilimia 98.  Na katika mwaka huu wa fedha, tumetenga shilingi bilioni 308.6, na napenda niwahakikishie fedha zote zitatolewa. Sambamba na hilo, mwaka huu, tumeanzisha Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA), ambayo imetengewa shilingi bilioni 246, ukiachilia mbali fedha zilizoahidiwa na wafadhili mbalimbali, ikiwemo Benki ya Dunia. Hivyo basi, sina shaka, tatizo la fedha za maendeleo litazidi kupungua.
Kuhusu tatizo la uhaba wa watumishi baada ya kuwaondoa watumishi wenye vyeti feki, Serikali mwaka huu imepanga kuajiri watumishi wapya wapatao 52,000, wakiwemo watumishi wa afya, walimu na watumishi wa kada nyingine. Hivyo basi, nina imani kuwa hii itapunguza uhaba wa watumishi kwenye Serikali za Mitaa. Ombi langu tu msiajiri watumishi wasio na sifa. Lakini niwe mkweli ombi lenu la kuongeza posho kwa madiwani, kidogo litaiwia Serikali vigumu kulitekeleza kwa wakati huu. Kama nilivyosema hapo awali, kwa sasa, Serikali imeelekeza nguvu zake katika kuboresha huduma za jamii na kujenga miundombinu ya kiuchumi. Hivyo basi, niwaombe Waheshimiwa Madiwani mtuelewe katika hili. Aidha, nawaombeni mzidi kuwahamisha Watanzania kuchapa kazi kwa bidii na kulipa kodi ili kuongeza uwezo wetu wa kifedha. Uwezo wetu ukiimarika, Serikali kamwe haitasita kuboresha maslahi sio tu yenu ninyi Waheshimiwa Madiwani bali pia watumishi wote wa umma.
Umeeleza pia kuhusu ombi la kutaka kuridhiwa kwa Mkataba wa Umoja wa Afrika kuhusu Ugatuaji Madaraka (The African Union Charter on Principles and Values on Decentralization, Local Governance and Local Development) pamoja na ombi la kutaka nchi yetu kuwa Makao Makuu ya Jumuiya ya Tawala za Serikali ya Mitaa kwa Kanda ya Afrika. Maombi haya nayo tumeyapokea. Nitaziagiza taasisi husika kupitia Mkataba huo na endapo haukinzani na Katiba na Sheria zetu, uweze kuridhiwa na Bunge letu. Na kuhusu ombi la nchi yetu kuwa Makao Makuu, natambua faida za kuwa mwenyeji wa Taasisi hiyo. Hata hivyo, kabla ya kukubali kuipokea taasisi hiyo, ni vyema tathmini ikafanyika kuhusu mahitaji ya fedha yanayotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti;
Siwezi kuhitimisha hotuba yangu bila kugusia kaulimbiu ya Mkutano huu, ambayo inasema “Ardhi kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa ni chachu ya Maendeleo, Halmashauri zitenge ardhi kwa ajili ya Uwekezaji wa Viwanda Vidogo na Vikubwa”. Kama mnavyofahamu, kipaumbele kikubwa cha Serikali ya Awamu ya Tano ni ujenzi wa Viwanda. Na ili kujenga viwanda, unahitaji ardhi. Hivyo, kaulimbiu hii ni nzuri na imekuja kwa wakati muafaka. Kwenye ziara zangu maeneo mengi nchini, nimekuwa nikihimiza wakurugenzi, Wakuu wa Wilaya na Mikoa kutenga maeneo na kuweka miundombinu rafiki ili kuwavutia wawekezaji kujenga viwanda. Hivyo basi, kwa mara nyingine napenda kurudia tena wito huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Mheshimiwa Naibu Waziri wa TAMISEMI;
Ndugu Wajumbe, Mabibi na Mabwana;
 Nimezungumza mengi. Napenda kuhitimisha hotuba yangu kwa kukushukuru tena Mwenyekiti wa ALAT kwa kunialika kufungua Mkutano huu. Napenda kuwahakikishia tena kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ipo pamoja nanyi. Nitafuatilia Mkutano huu, na yote mtakayokubaliana, nawaahidi kuwa Serikali itayazingatia na kuyatekeleza. Wito wangu kwenu, mjadiliane kwa amani na uwazi.
Baada ya kusema hayo, sasa natamka kuwa Mkutano wa 33 wa Jumuiya ya Tawala za Serikali za Mitaa (ALAT) umefunguliwa rasmi.
Mungu Ibariki ALAT!
Mungu Zibariki Mamlaka zote za Serikali za Mitaa Nchini!
Mungu Ibariki Tanzania!


“Ahsanteni sana kwa kunisikiliza”
Bashir Nkoromo

Posted in

Spread the love

SABODO: UKARIBU WANGU NA MWALIMU NYERERE ULIOKOA TAIFA

Sabodo
Hayati Mwalimu Nyerere
 Mwandishi Maalum
Jina la mfanyabiashara maafuru hapa Tanzania, Mustafa Jaffer Sabodo, likitajwa siyo geni masikioni mwa wengi.

Hii ni kutokana na mchango wake kwa jamii katika kuliondoa taifa kutoka sehemu moja ya chini kwenda juu, yaani maendeleo.

Sabodo mfanyabiashara maarufu ambaye ni Mtanzania mwenye asili ya Asia amekuwa akitoa mchango kwa maendeleo ya Taifa katika nyanja mbalimbali kuanzia za uchumi, siasa, elimu, afya na maji.

Mfanyabiashara huyo ambaye ni mzaliwa wa mkoani Lindi takriban miaka 73 iliyopita amejitolea kujenga shule mbalimbali nchini, hospitali, visima vya maji hata kufadhili shughuli za kisiasa na kiuchumi.

Michango yake hiyo kwa jamii ya Watanzania, imefanya jina lake kuandikwa katika mioyo ya wananchi wengi kwani alidhirisha tabia yake isiyojificha ya uzalendo kwa Taifa lake Tanzania.

Sabodo anatajwa kuwahi kuvifadhili vyama vya siasa vya CCM na Chadema kwa nyakati tofauti.

Pia anatajwa kwamba alikuwa rafiki wa karibu wa Mwalimu Julius Nyerere na wanasiasa mbalimbali nchini hata kuwahi kutumwa kwenda nchini Iran kukutana na kuomba mafuta kwa aliyekuwa kiongozi wa taifa hilo la Kiislamu, Ayatolah Khomein katika miaka ya 1970 baada ya taifa kukumbwa na uhaba wa mafuta uliochagizwa na sababu mbalimbali ikiwamo ukosefu wa fedha za kigeni.

Hali hiyo ilitokea kipindi hicho wakati dunia ilikuwa bado ikishuhudia mgawanyiko kwa baadhi ya nchi kuegemea Marekani kisiasa na kimfumo, nyingine zikifuata mfumo wa iliyokuwa Muungano wa nchi za Kisovieti za Urusi (USSR).

Si hivyo tu kwa kusoma alama za nyakati, baadhi ya nchi zilikaa kando na utengano huo na kuanzisha Jumuia ya Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote.

Miungoni mwa mataifa yaliyofuata siasa za kutofungamana na upande wowote, Tanzania wakati huo chini ya uongozi wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere ilikuwa mojawapo.

Tofauti hizo za kisiasa hata kidini kati ya mataifa zilisababisha athari zilizozaa tofauti ya hali hasa kiuchumi na kisiasa hata baadhi ya nchi kuingia kwenye mahangaiko ikiwamo Tanzania iliyokumbwa na uhaba wa mafuta ya Petroli na fedha za kigeni.

Sabodo anasimulia kwamba kufuatia hali hiyo iliyoilazimu Serikali kuzuia magari yake kutembea Jumapili huku Jumamosi yakitembea hadi saa nane mchana, alipata nafasi ya kukutana na Rais Nyerere.

Anasimulia kwamba katika mazungumzo hayo alimwabia Rais Nyerere haja yake ya kutaka kwenda Iran kuomba mafuta.

“Nikamwambia wacha niende Iran. Nilifanya hivyo nikiamini Khomein atanisikiliza. Nakumbuka nilikwenda na Chifu Adam Sapi Mkwawa,” anasema.

Anasimulia: “Mimi ni Khoja, Mwislamu wa dhehebu la Shia na Khomein pia, nilipokutana naye, nikamwambia wanaoteseka Tanzania kwa shida ya mafuta wamo piaWaislamu wa Shia wengi tu.”

“Nilimwambia Tanzania ni nchi nzuri haina ubaguzi na Rais Nyerere ni mtu mwema, hata Waziri Mkuu wake ni Rashid Kawawa na Waziri wa Madini na Mafuta ni Anoor Kassam, nikamwangukia miguuni nikiliaa kuomba aipe nchi yetu mafuta, akakubali” anakumbuka Sabodo.

Hata hivyo, anasema licha ya kukubali, Khomein  akasema hawezi kumpa mafuta yeye Sabodo hadi watu wa Serikali ya Tanzania watakapofika Iran kuthibitisha ombi hilo.

“Nikarudi Tanzania na kumpa taarifa baba wa Taifa naye alimwambia Kawawa na John Malicela ikakubalika tukaenda tena Iran safari hii nikiwa na mawaziri wa Fedha, Cleopa Msuya, Anoor Kassam wa Mafuta na Usafirishaji pia alikuwepo Peter Noni kwa niaba ya Benki Kuu na Adam Sapi Mkwawa,” anasema.

Sabodo anakumbuka kuwa safari hiyo ilizaa matunda kwani Khomein aliipa Tanzania mafuta yenye thamani ya Dola za Kimarekani 80,000.

“Nakumbuka hapo urafiki wangu na Nyerere uliniwezesha kuliokoa Taifa kwa kupata mafuta baada ya kunituma kwenda Iran nilipomshauri,” anasema Sabodo ambaye wazazi wake alizaliwa Lindi.

Anakumbuka kuwa pia katika safari hiyo alimshauri Khomein kufungua ofisi ya Ubalozi wa Iran nchini naye alikubali na alifanya hiyo pia kwa Zambia, Tanzania nayo ikafungua ubalozi Iran.
Aliyekuwa Kiongozi wa Taifa la Iran, Ayatolah Khomein 

Bashir Nkoromo

Posted in

Spread the love

HOTUBA YA MWISHO YA UZALENDO YA HAYATI MZEE KAWAWA AKISHEREHEKEA MIAKA 78

NA HAMISI SHIMYE-UPL
“Historia ya Maisha yangu ni ndefu kama ilivyokwisha elezwa. Nilizaliwa Kijijini, nikasoma Kijijini na mjini na nikafanya kazi vijijini na mjini. Katika Maisha yangu yote nimetekeleza kwa nadharia na vitendo falsafa ya UMOJA Ni NGUVU. Vitendo vimejidhihirisha zaidi katika vyama vya wafanyakazi, vyama vya ushirika na katika vyama vya siasa, hususan Tanganyika African National Union (TANU) na Baadaye Chama cha Mapinduzi (CCM). Katika Utendaji kazi, nilizingatia falsafa hii ya UMOJA NI NGUVU”.

Nikiwa na umri wa mika 23 na mtumishi Serikalini, nilijiunga na Chama cha Watumishi Waafrika Serikalini (Tanganyika African Government Servats’ Association-TAGSA). Nilijiunga na chama hicho cha wafanyakazi kwa imani kwamba UMOJA NI NGUVU. Sikuona njia nyingine ya kupambana na dhuluma za Mkoloni kwa wafanayakazi Waafrika ila kuungana na kuanzisha vyama vya wafanyakazi.

Niliamini kwamba wafanyakazi Waafrika kwa kujiunga pamoja chini ya vyama vya wafanyakazi wangeweza kupigania maslahi na haki zao kwa nguvu kubwazaidi.

Kwa kuzingatia falsafa ya UMOJA NI NGUVU, vyama vya wafanyakazi viliunda Shirikisho la vyama vya Wafanyakazi (Tanganyika Federation of Labour- TFL), tarehe 10 Oktoba,1955. 

Mimi nilichaguliwa na wenzangu kuwa katibu Mkuu wa TFL wakati huo nikitokea Chama cha Watumishi Waafrika serikalini (TAGSA).
Nilichaguliwa kwa sababu ya ujasiri na ushupavu wangu katika kupigania haki na maslahi ya Wafanyakazi kupitia Chama cha Watumishi Waafrika Serikalini (TAGSA).

Kazi ya kwanza ya TFL ilikuwa ni kuviunganisha vyama vidogo vya wafanyakazi na kuviimarisha kwa madhumini ya kuwa na nguvu na sauti kubwa zaidi. TFL haikuwa Muuongano wa Vyma vya Wafanyakazi bali Shirikisho. Vyama hivyo chini ya shirikisho viliendelea kuendesha shughuli zake vyenyewe kama vyama vilivyokuwa na madaraka kamili juu ya wanachama wake.

Kazi ya kuviunganisha na kuvisimamia vyama vya wafanyakazi chini ya TFL haikuwa ndogo hata kidogo. Nililazimika kuacha kazi Serikalini tarehe 6 Machi, 1956 ili kutumia uwezo na muda wangu wote katika kutekeleza hiyo.

Katika Kupigania Maslahi ya wanachama wake, TFL ilitumia migomo kama silaha kubwa. Migomo mingi lifanyika lakini napenda kuzungumzia kidogo mgomo wa Wafanyakazi wa Kiwanda cha Bia Dar es Salaam wa Mwaka 1958, April hadi Juni. Mgomo huu uliwashirikisha wafanyakazi wapatao 300, madai yao yalikuwa ni nyongeza ya mshahara. Wafanyakazi wote waliogoma walifukuzwa kazi.

Kutokana na Mgomo huu, nilishitakiwa Mahgakamani tarehe 25 April, 1958 kwa madai kwamba niliwalazimisha Makarani wawili Waafrika Kugoma. Nilitozwa faini ya Shs, 101/= ambazo Mwalimu Nyerere alilipa. Mwalimu alifanya hivyo ikiwa ni mchango wake binafsi wa kuunga Mkono Mgomo, kuimarisha uhusiano kati ya TANU na TFL, na kuwatia moyo wafanyakazi.

Ukweli ni kwamba nilikuwa mstari wa mbele katika kuongoza Migomo. Utekelezaji kwa vitendo wa falsafa ya UMOJA NI NGUVU haikuishia kwenye vyama vya wafanyakazi peke yake. Falsafa hii niliitekeleza pia katika ushirika. Baadhi yenu hamfahamu kwamba nikiwa karani wa Uhasibu, mimi pamoja na wafanyakazi wenzangu tuliokuwa tunaishi Ilala Quarters tulianzisha Chama cha Ushirika cha Walaji wa Ilala (Ilala Consumers’ Cooperative Union).

Wakati nikiwa kiongozi Serikalini na kwenye Chama nimeshiriki kwa ukamilifu katika kuhimiza na kutekeleza kwa vitendo sera ya ushirika. Chini ya TANU, ushirika uliwekewa mkazo kwa misingi kwamba ni chombo cha kuleta maendeleo. 

Ni kwa msingi huo, ndio sababu wananchi walihimizwa kuanzisha ushirika katika maeneo ambayo hayakuwa na vyama vya ushirika. Aidha, katika maeneo yaliyokuwa na vyama vya ushirika, wnanchi walihimizwa na TANU kuimarisha vyama hivyo.

Baada ya kutangazwa kwa Azimio la Arusha, ushirika umeendelea kuwa chombo cha ujenzi wa Ujamaa. Chini ya TANU na baadaye CCM, Kwakushirikiana na viongozi wenzangu nimeheimiza kwa nguvu zote uanzishaji na uimarishaji wa vyama vya ushirika, hususan vyama vya ushirika wa walaji, kuweka na kukopa, usafirishaji, maduka na ushirika wa uzalishaji mali vijijini…..,

Njia muafaka ya kuwawezesha wananchi kiuchumi ni kujiunga katika ushirika. Wananchi wasipuuze hata kidogo suala la kutekeleza sera ya Ushirika.

Usahii wa falsafa hii ya UMOJA NI NGUVU ulijidhihirisha hata wakati wa kudai uhuru wa nchi yetu. Wananchi waliungana katika mapambano dhidi ya Ukoloni wa Kiingereza. Vyama vya wafanyakazi na vyama vya Ushirika viliunga Mkono madai ya TANU ya kudai uhuru, aidha, wanachama wa vyama hivyo walihimizwa na viongozi wao kuwa wanachama wa TANU hata kwa siri kwa wale waliokuwa wanakatazwa kisheria. Kwa kutambua umuhimu wa umoja, salaam za TANU mara tu baada ya uhuru zilikuwa UHURU NA UMOJA…..

Baada ya kutangazwa kwa Azimio la Arusha, TANU ilitambua kwamba ilikuleta maendeleo ya kweli vijijini ni lazima kutumia silaha ya UMOJA NI NGUVU. Wananchi vijijini waliweza na wanaendelea kuinua hali yao ya Maisha kwa kukusanya nguvu zao.

Nilifikiri katika umri huu wa mika 78 ni vema nikawaasa viongozi wenzangu na wananchi kwa ujumla kutekeleza kwa vitendo falsafa hii ya UMOJA NI NGUVU. Binafsi naamini kwamba falsafa hii ikitekelezwa kwa ukamilifu, Taifa letu litapiga hatua kubwa zaidi kimaendeleo.

Falsafa hii, kama zilizvyo falsafa nyingine, utekelezaji wake utategemea sana uongozi. Viongozi ni lazima wawe mfano mzuri kwa wnanchi kwa maisha yao na vitendo vyao. Chama chetu cha Mapinduzi, kinatamka bayana kwamba kila kiongozi mahali alipo aoneshe nadharia ya maendeleo na vitendo kwa kuongoza kwa kutenda…

Waheshimiwa Mabibi na Mabwana ….., na fahamu kwamba mmeacha kazi zenu muhimu, hasa viongozi wa kitaifa, ilikuja kujumuika na familia ya Mzee Kawawa. Kwetu sisi huu ni upendo wa hali ya juu na niutekelezaji wa falsafa ya UMOJA NI NGUVU. Bila umoja wenu shuguli ya leo isingefanyika na kufanikiwa.

Mimi Mzee wenu nimefarijika sana kwa moyo wenu wa upendo. Sina cha kuwalipa ila kumwomba Mwenyezi Mungu awazidishie upendo.

Baada ya Kusema haya Machache, nasema tena asanteni sana kwa kushiriki pamoja nami katika sherehe ya kutimiza miaka 78 ya kuzaliwa kwangu”. Mwisho wa hotuba aliyoitoa Februari 27, 2004.
Bashir Nkoromo

Posted in

Spread the love

RAIS DK. MAGUFULI AMTUMBUA MKURUGENZI MTENDAJI TANESCO LEO

Na Bashur Nkoromo, Dar
Rais Dk. John Magufuli, leo amemtumbua Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mhandisi Felchesmi Mramba, katika hali inayoonesha kuwa Rais amekerwa na jaribio la Tanesco kupandisha bei ya umeme kuanzia leo, Januari Mosi, 2017.

Taarifa iliyotolewa leo na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu jijini Dar es Salaam, imesema, kufuatia kutenguliwa kwa uteuzi huo, Rais Magufuli amefanya 'bandika pandua' kwa kumteua Dk. Tito Esau Mwinuka kuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO.

"Kabla ya uteuzi huo Dk. Tito Esau Mwinuka alikuwa Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM)
Uteuzi wa Dkt. Tito Essau Mwinuka unaanza mara moja", imesema taarifa hiyo ya Ikulu iliyosainiwa ana Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa.

Hatua ya Rais Magufuli, imekuja ikiwa ni siku mbili baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kuiidhinisha ongezeko la asilimia 8.5 ya ya bei ya huduma za umeme kwa kilichoelezwa kuwa lengo ni kukidhi gharama za uzalishaji wa umeme.

Ongezeko hilo lilitangazwa juzi jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Felix Ngamlagosi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maombi ya kurekebisha bei za umeme ambayo yalitarajiwa kuanza kutekelezwa leo, Januari Mosi, 2017.

Ngamlagosi alisema, kuwa TANESCO iliomba kuidhinishiwa ongezeko la bei ya huduma hizo ili kuliwezesha shirika hilo kupata fedha za kulipia gharama za uendeshaji, kupata fedha za uwekezaji katika miundombinu pamoja na kuhakikisha huduma ya umeme inawafikia asilimia 75 ya wananchi wote ifikapo mwaka 2025.

”Baada ya TANESCO kuwasilisha taarifa zinazohitajika kwa ajili ya kukamilisha maombi yao, EWURA ilifanya mikutano ya taftishi, matangazo kwa umma pamoja na kushirikisha wadau mbalimbali kutoa maoni juu ya ongezeko hilo ambapo baada ya uchambuzi wa maoni hayo tulilidhia kuongeza asilimia 8.5 tu ya ongezeko la bei hizo ,” alisema Ngamlagosi.

Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) ambalo linanunua umeme wa jumla kupeleka Zanzibar limeongezewa asilimia 5.7 ya bei ya umeme badala ya asilimia 19.1 iliyoombwa na TANESCO.

Alisema kulingana na marekebisho yaliyofanyika, jumla ya mapato yanayohitajika kwa mwaka 2017 ni sh. bilioni 1,608.47 ambayo yamesababisha ongezeko la bei la wastani wa asilimia 8.5 hivyo gharama za umeme zimeongezeka kutoka sh. 242.34 kwa uniti moja hadi sh.  263.02 kwa uniti moja.

Mkurugenzi huyo alitoa maagizo kwa TANESCO yakiwemo ya kuanzisha tozo ya mwezi ya sh. 5,520 kwa wateja wa kundi linalohusisha viwanda vidogo, mabango na minara ya mawasiliano, kuboresha huduma kwa wateja pamoja na kuacha kuwaunganisha wateja wadogo kwenye kundi la wateja wakubwa na badala yake kuwaunganisha moja kwa moja katika kundi la wateja wadogo.

Aliwataka wananchi kuelewa kuwa kundi linalojumuisha wateja wa majumbani ambao matumizi yao ya umeme hayazidi uniti 75 kwa mwezi hawataathirika na ongezeko hilo la bei.

Uchunguzi uliofanywa na Mtadao huu, umebaini kuwa zipo familia nyingi zenye uwezo mdogo ambazo kwa mwezi matumizi yake ya umeme hufikia hadi uniti 150 kwa mwezi, na pia tofauti na inavyoeleza kuwa wananchi wa kawaida wasigeathirika na kupanda kwa bei hiyo ya umeme, maoni ya wadau yameonyesha kuwa watu hao wangeathirika kutokana na bei za bidhaa ambazo zingepanda bei kufidia gharama ya umeme. 
Bashir Nkoromo

Posted in

Spread the love

WAJUA KWA NINI HAYATI MZEE KAWAWA ALIITWA SIMBA WA VITA WAKATI WA UHAI WAKE?

Na Hamis Shimye, UPL
HAYATI Mzee Rashid Mfaume Kawawa alikuwa ni kiongozi shupavu aliyewahi kutokea, ambapo alikuwa kiongozi adhimu sana na mwenye moyo wa ajabu katika kuipigania nchi yake katika ufanyaji wa kazi mbalimbali za maendeleo.

Alikuwa ni mtu asiyeogopa kazi hadharau kazi, hana makuu, hana makundi, hana majungu. Mdogo wake akifanywa mkubwa wake atafanya kazi chini yake kwa moyo wake wote, na uwezo wake wote; bila manung’uniko, na bila kinyongo.
Katika TANU alikuwa akiitwa SMBA WA VITA. 

Haogopi maamuzi mazito. Mkishafanya maamuzi ndani ya vikao yeye basi lazima atakuwa mstari wa mbele, ambapo wengine baadaye wanaweza kusita kuyatekeleza, au wanaweza kuyatekeleza kwa shingo upande na hasa kama walikuwa hawayapendi.

Hayati Mzee Rashid Kawawa alikuwa ni mtu wa kutekeleza mambo hasa pale viongozi wakishaamua kwa pamoja, atayatekeleza kwa moyo wake wote na uwezo wake wote. Kwa ajili hiyo mara nyingi amebeba lawama peke yake kwa maamuzi ambayo yamefanywa na uongozi mzima wa Chama na serikali kwa pamoja, au ambayo nimeyafanya mimi.

Hayati Mwalimu Julius Nyerere alitoa hotuba katika mkutano maalumu wa Taifa wa CCM mwaka 1990, ambapo sehemu ya hotuba ilikuwa inamzungumzia Mzee Kawawa, ambapo Mwalimu Nyerere alisema mambo mengi ya kumsifu Kawawa.

"Nilipokwisha kutangaza kwamba baada ya kikao hiki nitang’atuka uenyekiti wa Chama chetu, Ndugu Kawawa alinijia na kusema kuwa yeye pia angependa kung’atuka. Lakini tulikubaliana kwamba si vizuri wote wawili tukang’atuka wakati ule ule. Tutakuwa kama tunamtelekeza mwenzetu. Ni bora yeye abaki ili aendelee kumsaidia mwenyekiti mpya wa Chama chetu.

Ndugu Kawawa ni Askari. Hajitafutii madaraka; lakini hasiti kupokea madaraka yoyote anayopewa na chama chake.

Ndugu Kawawa, sijui jinsi ya kukushukuru kwa niaba yangu mwenyewe na niaba ya nchi yetu na Chama. Kwangu mimi imekuwa ni bahati na faraja ya pekee kwamba kwa muda wote wa uongozi wangu umekuwa makamu na msaidizi wangu. Unastahili kupumuzika, kama mwenyewe ulivyoomba. 

Badala yake tunakuomba uendelee kumsaidia mwenyekiti na Rais wetu; na hivyo uendelee kukisaidia Chama chetu na Nchi yetu. Umekubali Ahsante sana".

*Hotuba aliitoa Mwalimu Nyerere katika mkutano Mkuu Maalum wa Taifa, Agosti, 1990.
Bashir Nkoromo

Posted in

Spread the love

MAKALA: CHAMA CHA DEMOKRASIA NA UBAKWAJI WA DEMOKRASIA HALISIA

Mathias Canal (Picha na David Mtengile
CHAMA CHA DEMOKRASIA NA UBAKWAJI NA DEMOKRASIA HALISIA

Na Mathias Canal
Katika sehemu ya maelezo yake Raisi wa 16 wa Marekani Bw Abraham Lincoln namnukuu aliwahi kusema kuwa Demokrasia ni mfumo wa serikali ambapo wananchi wote ni sawa mbele ya sheria na wanashiriki katika kufanya maamuzi ya kitaifa juu ya masuala ya umma. Wakati mwingine wananchi hushiriki moja kwa moja - hii ina maana kwamba wao hupiga kura moja kwa moja kwenye masuala kama vile katika chaguzi. 

Kabla sijaanza kuzungumzia uchaguzi wa CHADEMA Kanda ya Nyasa Tutazame Mwongozo wa kumteua muaniaji Urais nchini Marekani Kabla ya Wamarekani kuamua nani wanayemtaka awe rais ajaye, wao kwanza huteua nani atakayewania kiti hicho.


Mchakato huo hungo'oa nanga kwa mchujo wa kamati za wajumbe ambapo wananchi hupata fursa ya kumchagua muaniaji kiti cha urais kwa tiketi ya chama cha Democratic au kile cha Republican.Mshindi wa mchujo huo huwakusanya wajumbe - hawa ni wanachama wenye nguvu ya kupiga kura kumchagua mgombea katika mikutano ya chama.

Nchini Marekani inakumbukwa kuwa kulikuwa na upinzania mkali katika uchaguzi wa nafasi ya Rais kati ya vyama viwili ambapo ni Republican na Demokratic, Kwa upande wa Democrats upinzani mkali ulikuwa kati ya Hillary Clinton na Seneta Bernie Sanders ambaye alionekana nae kupata uungwaji mkono zaidi dhidi ya Clinton. Kwa upande wa Republican kulikuwa na wagombea kama Marco Rubio na Ted Cruz sambamba na Donard Trump aliyeibuka kuwa mshindi wa chama hicho na mshindi wa nafasi ya Urais wa Marekani.

Tutakubaliana wote kwa pamoja kwamba Vyama vyote nchini Marekani vilisimamisha wagombea katika kura za awali kabisa ambao wote kwa pamoja walipigiwa kura na wajumbe wao hapakuwa na kura za Ndio na Hapana kwa maana ya Kivuli/Jiwe na Mtu sasa tutazame mchakato ulivyo kuwa kwenye vyama vinavyounda umoja wa katiba ya Wananchi UKAWA vikiongozwa na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA jinsi vilivyompata mgombea wake wa Urais.

Julai 30, 2015 nikiwa natazama Luninga majira ya saa tatu na dakika moja usiku niliona katika kipindi cha Dira ya Dunia kinachorushwa na chombo cha habari cha BBC kupitia Televisheni ya Star Tv kikiarifu kuwa WANACHAMA wapya wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa pamoja na na Juma Duni Haji wamepitishwa katika Mkutano Mkuu wa chama hicho kugombea ngazi ya urais na umakamu wa rais kwa asilimia 99.3 ambapo jumla ya wajumbe 2021 kati ya 2035 waliotakiwa kuhudhuria kwenye mkutano huo, walipiga kura za NDIO kwa kuwa hapakuwa na wagombea wemngine na kuibua kishindo katika mkutano huo uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam.

Awali kabla ya kufanyika uchaguzi huu Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa Mhe Freeman Alikael Mbowe Akizungumzia utaratibu wa kuteua mgombea huyo alisema kuwa, kwa mujibu wa katiba hiyo kifungu namba 7.16, mgombea urais pamoja na makamu wake wanateuliwa na sio kupigiwa kura.

Yaani kama kuna mtu hakuelewa vyema hapo katika maelezo hayo naomba nimsaidie kwa hili naamini ataelewa vyema zaidi Mbowe alisema kuwa kwa mujibu wa katika huku akitaja kifungu Mgombea Urais hapigiwi kura na wajumbe bali anateuliwa. Hii ni kauli ya kishujaa nay a ubakaji wa Demokrasia kwa uwazi kabisa.

Tujikumbushe Demokrasia ni nini kabla ya kuendelea na mjadala ili tuende sawa: Utawala wowote wa Demokrasia ni ule unaotokana na ridhaa ya wananchi, ambao kutokana na utaratibu waliojiwekea hufanya maamuzi ya kuwapata viongozi wao. Wananchi hushiriki moja kwa moja - hii ina maana kwamba wao hupiga kura moja kwa moja kwenye chaguzi. Tukubaliane sasa ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA hakuna Demokrasi kama ambavyo inahubiriwa katika vijiwe na majukwaa ya kisiasa. Na kama demokrasia ni pamoja na kushirikisha wananchi kufanya maamuzi kwa nini Mbowe aliamua yeye kwamba Lowassa na Duni wateuliwe sio kupigiwa kura na wajumbe zaidi ya 2000, kwa akili ya kawaida tu na karne hii unaweza kuwaambia watu fanyeni maamuzi kati ya Jiwe/kivuli na mtu...? Lakini katika hili sikuwaona vijana wa CHADEMA wakihoji wala wale wa Umoja wa Kizazi cha Kuhoji (UTG) wakihoji. Huenda walipitiwa hawakuliona hili sasa tuendelee.

UCHAGUZI KANDA YA NYASA 

Kwa kunukuu gazeti la Rai linalochapishwa na KAMPUNI ya New Habari (2006) Ltd ambayo pia inachapisha magazeti ya Mtanzania, Bingwa, Dimba na The African, la Disemba 8, 2016 liliandika habari ilikuwa na kichwa cha habari kilichosema UCHAGUZI CHADEMA NI ‘VITA’ KALI 

‘NI vita’, hivyo ndivyo tafsiri inapatikana kufuatia mvutano mkali ulioibuka ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kati ya Mchungaji Peter Msigwa na Patrick Ole Sosopi ambao walikuwa wanapambana kuwania nafasi ya uenyekiti kanda ya Nyasa.

Msigwa ambaye ni Mbunge wa Iringa Mjini alipamba na kijana Machachari katika Siasa za Tanzania Patrick Ole Sosopi ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), kuwania Kanda hiyo ya Nyanda za Juu Kusini (Nyasa) inayojumuisha mikoa ya Iringa, Mbeya, Rukwa, Njombe na Songwe.

Tangu maandalizi ya uchaguzi kanda nane za Chadema yalipoanza mwezi uliopita kulikuwapo na majibizano kati ya wafuasi wa wagombea hao wawili ambao kwa namna moja au nyingine wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii kuanika madhaifu ya kila mgombea.

Hata hivyo, Msigwa alionekana kushambuliwa zaidi na wafuasi wa Chadema Kanda ya Nyasa kutokana na madai mbalimbali ikiwamo tabia ya kutoshirikiana na wabunge wenzake katika kukijenga chama, pia kujiweka mbali na wabunge wa chama hicho kipindi walipokuwa wakipambana kutetea madai yao kwa Naibu Spika wa Bunge Dk. Tulia Ackson.

Kwa mujibu wa taarifa zilizolifikia gazeti la RAI zinaeleza kuwa baadhi ya wabunge na viongozi wa chama hicho walionekana kusita kumuunga mkono Mbunge huyo kutokana na madai ya ubinafsi aliouonyesha katika kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu 2015 kwa kushindwa kushirikiana na makada wa chama hicho kuzunguka sehemu mbalimbali.

Hata hivyo baadhi ya wafuasi wa Ole Sosopi walionekana kulalamika kutukanwa kwenye mitandao ya kijamii ambapo mmoja wao alisema: “Nimeshangaa sana watu kunifuata inbox na kunitukana hata wengine kutumia lugha ambayo si njema. Kumuunga mkono Sosopi ‘it’s just my perception.’ Kwa kuwa nina akili timamu siwezi kujibu matusi kama mlivyofanya “Imeniuma sana, nimeumia sana. Naomba niliweke wazi hili, Peter Msigwa ni Mbunge wangu, ni mlezi wangu na sina ugomvi naye. Sosopi na Msigwa wote ni Chadema na wote ni familia moja ndani ya chama chetu Chadema,” 

SIKU YA UCHAGUZI WA KANDA YA NYASA

Tarehe Disemba 22, 2016 ndio siku ambayo Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA kilifanya uchaguzi huo lakini mapema asubuhi kabla ya kuanza kwa uchaguzi jina la Patrick Ole Sosopi liliondolewa katika kinyang’anyiro cha kugombeanafasi ya uenyekiti Kanda ya Nyasa na Uongozi wa Kamati kuu ya Chama hicho iliyokuwa inaongozwa na Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa Freeman Alkael Mbowe.

Sosopi alipewa taarifa kwa njia yam domo kwamba jina lake limetolewa pasina kupewa hata maelezo kwa njia ya maandishi lakini pia taarifa hiyo alipewa asubuhi siku ya uchaguzi sio siku moja ama mbili kabla ya uchaguzi
Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Ubungo ambaye kwa sasa ni katibu wa Nec, Itikadi na Uenezi wa  CCM Taifa Hamphrey Polepole aliwahi kusema kuwa Huu si wakati wa siasa za kutafuta uongozi; Ni wakati wa siasa za maendeleo na kujenga nchi hapo alikubaliana na dhana ya mfumo wa kupunguza madaraka kwa viongozi inayohubiriwa naserikali ya wamu ya tano chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli ya kuwataka viongozi kuwa na cheo kimoja serikalini ikibidi kuwa na cheo kimoja pia kwenye chama cha siasa isiwe zaidi ya hapo.

Kabla ya kuendelea naomba nikurejeshe katika kauli ya Mchungaji Peter Msigwa ya Mwaka 2015 aliyoisema kwamba “Raisi apunguziwe madaraka, na wakuu wa mikoa pia wana vyeo vingi sana wapunguziwe" by peter msigwa 2015.

Lakini tutazame sasa vyeo alivyonavyo mchungaji Msigwa kwenye chama na seriakli kabla ya kutazama uchaguzi wa Mwenyekiti Kanda ya Nyasa ulivyoendeshwa

Mchungaji Msigwa ni Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini

Mchungaji Msigwa ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu Chadema
Mchungaji Msigwa ni Mjumbe wa Baraza kuu Chadema 
Mchungaji Msigwa ni Mjumbe wa Kamati Kuu Chadema
Mchungaji Msigwa ni Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Iringa
Mchungaji Msigwa ni Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa

Mchungaji Peter  Simion Msigwa amekipata cheo cha sita ndani ya Chadema na kuwa Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa baada ya wagombea wengine kuenguliwa, hivyo kuwa mgombea Pekee ambaye ni yeye Msigwa na Mgombea mwingine ambaye ni Jiwe/kivuli. Binafsi najiuliza sana lakini najiuliza kimya kimya hivi vikao vya vyeo hivyo vyote vya watu sita anahudhuriaje!


Maana ya upatikanaji wa Mchungaji Msigwa kama Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa ni kwa njia ya kuteuliwa na sio kuchaguliwa lakini Demokrasia ambayo CHADEMA huihubiri ni wazi wamekuwa wakiivunja wao maana wanawanyima nafasi wagombea pendwa na kukata majina yao na hatimaye wanakubali mgombea mmoja ashindane na kivuli pamoja na kwamba hakubaliki.

UCHAGUZI WA CHADEMA KANDA YA NYASA ULIKUWAJE BAADA YA MSIGWA KUBAKI MGOMBEA PEKEE AKISHINDANA NA KIVULI CHAKE MWENYEWE

Kwa mujibu wa andiko la lililosomeka kama “NIMEAMINI MAISHA BILA UNAFIKI HAYAENDI”
lililoandikwa na Mwalimu Pasaka Rucho mara baada ya mchakato mzima wa kumalizika na mshindi kutangazwa. Umeeleza tangu mchakato kuanza wajumbe walitaharuki sana kusikia taarifa ya kutolewa kwa jina la sosopi, tazama mchakato ulivyokuwa:

Wajumbe halali ni 98

Waliosusia 28
Waliopiga kura ni 106
Kura za ndio kwa msigwa 62
Kura za hapana ambazo zilipigia kivuli cha mgombea ni 44


Hii ikiwa na maana Ukichukua Kura 44 za Hapana dhidi ya Msigwa + na kura 28 za wajumbe waliosusia uchaguzi jumla yake ni =72 hivyo Sosospi tayari kama alikuwa mshindani alikuwa amejihakikishia ushindi kwa kura 78.

Kura zilizoongezeka kwa zile zilizopigwa ni 8 maana wapiga kura waliongezeka kutoka wapiga kura halali 98 na kuwa na wapiga kura wasio halali 8 waliofanya idadi kuongezeka na kuwa na wapiga kura 106.

Wajumbe waliopaswa kubaki ndani ukiondo waliokuwa wamekataa kuingia ndani ni 70

98-28=70.


Kwa maana halisi ni kwamba kulikuwa na wapiga kura 36 walioletwa na kuwa wajumbe wasio halali maana baada ya kura 44 za Hapana na wajumbe 28 kutoka ukumbini hivyo kulipaswa kupatikana kura za halali 28 ambazo ndizo kura za Ndio kwa Msigwa. 

Hii inamaanisha kwamba katika hali ya kawaida hata kama wajumbe wale 28 wasingeingia kama walivyofanya Msigwa angeshinda kwa kura 26 tu kwa maana ya wajumbe waliopaswa kubaki ndani 70- wajumbe 44 waliomkutaa=26 ambayo ndio idadi ya kura za Msigwa katika uchaguzi huo.


kwa ufupi kwa kutumia wajumbe halali katika uchaguzi kama Sosospi asingetolewa uchaguzi ungemalizika hivi:

Sosopi 72 (73.5%)
Msigwa 26 (26.5%)


HITIMISHO

Nianze kwa kumnukuu Dkt  Benson Bana wa Chuo Kikuu cha Dare s salaam ambaye amebobea katika masuala ya siasa alipokuwa akizungumza katika mkutano wa wadau wa siasa wa uimarishaji demokrasia ya vyama vingi. Alisema pamoja na mafanikio hayo bado kuna mapungufu mengi hasa ya kutokuwa na utamaduni wa vyama vingi, utamaduni unaoambatana na vyama kuwa na  aidolojia (itikadi), kukosekana kwa lugha za kistaarabu katika majukwaa ya siasa na hata mitafaruku ya ndani ya kivyama.

Mfumo wa vyama vingi ni hali ya kuwa na chama zaidi ya kimoja,katika nchi moja.Madhumuni ya kuwa na vyama vingi vya siasa ni kuleta ushindani wa kisiasa,ili kuleta maendeleo ya nchi,upinzani wa kisiasa sio uadui kama watu wengi kwenye nchi zinazoendelea wanavyodhani,kuwa na vyama vingi ni kuongeza wigo wa demokrasia katika jamii huska. Hata hivyo mara kadha amesema kuwa ili nchi yetu iweze kupiga hatua ni dhahiri lazima kuwe na Upinzani imara unaochukia Rushwa, na Uminyaji wa Demokrasia.

Binafsi sasa nakitoa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA katika Ukuzaji wa Demokrasi kwa kauli ya Mbowe kwa kusema kuwa Mgombea Urais hachaguliwi bali anateuliwa jambo ambalo ameliongoza pia kwa kumteua Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa Mchungaji Msigwa badala ya kuruhusu wajumbe kugombea na kuchagua kiongozi wanaomtaka.

TANZANIA ina vyama vya siasa 21 vyenye usajili wa kudumu huku kikiwepo kimoja ambacho kina usajili wa muda. Vyama hivi vimepatikana baada ya mabadiliko madogo ya Katiba yaliyotoa fursa ya kurejesha mfumo wa vyama vingi katika nchi yetu mwaka 1992.

Kufuatia mabadiliko haya, Chama cha Mapinduzi (CCM) ndicho kilichokuwa cha kwanza kupata usajili wa kudumu mwaka 1992, huku kikifuatiwa na vyama vipya vya CUF, CHADEMA,UMD, NCCR, NLD, UPDP, NRA, TADEA NA TLP vilivyopata usajili wa kudumu mwaka 1993.

Vyama vingine na usajili wao kwenye mabano ni:  UDP (1994), Demokrasia Makini (2001), CHAUSTA (2001), DP (2002), APPT(2003), Jahazi Asilia (2004), SAU (2005), AFP (2009), CCK (2012), ADC (2012), CHAUMMA (2013) na ACT (2014). RNP ni chama pekee kilichopo katika orodha ya vyama visivyo na usajili wa kudumu.

Katika vyama vyote hivi 21 mpaka sasa ni CHADEMA pekee ndicho kisichokuwa na Demokrasi kama ambavyo nimebainisha katika maeneo kadha wa kadha katika andiko langu.

Mwandishi Henry Mwangonde Aprili 23, 2014 katika gazeti la The Citizen, alimnukuu Dk. Benson Banna Katika makala yake ya “Vyama vingi vimeisaidia Tanzania” na kuandika; “vyama vya siasa nchini Tanzania havina nguvu katika kutanua mianya ya demokrasia kutokana na kukosa sera nzuri, mikakati pamoja na tabia ya viongozi wa vyama hivi kutokutumia mtaji wa wanachama wao kuviendeleza badala yake kuwatumia kwa masilahi binafsi.” Kwa mujibu wa Dkt Bana katika makala hiyo; vyama hivi vimeshindwa kutanua miaya ya demokrasia kwa kuwa havina demokrasia ndani yake.

Ni aibu kubwa sana kwa CHADEMA chama kinachojificha katika Mwamvuli wa Demokrasia katika Karne hii ya 21 kusimamisha mgombea Kivuli/Jiwe na Mtu…! Na bado kivuli kinapata kura 44? Watu 28 wanaishia mitini? Mtu anapata kura 66 naye anarudi kumsimulia Mkewe na Watoto kwamba ameshinda uchaguzi. 

Sasa hapa wachambuzi na wajuzi wa Siasa watahoji Tofauti ya CHADEMA na Yule mtu waliompa umaarufu kwa kumuita Bwana Yule upo wapi…? Lakini nimkumbushe Msigwa na CHADEMA kuwa raha na uzuri wa kura za Ndio na Hapana ni pale amabapo mshindi anaibuka kidedea kwa kura nyingi sio unapata kura 62 wakati zinakukataa ni kura 44 huku kura zingine 28 zikisusia namna ya Demokrasia ndani ya Chama.

Wakati vyama Vingine nchini vikiwa vinasonga mbele katika kuimarisha chaguzi zao za ndani ya Chama lakini CHADEMA wao wanarudi nyuma na kutoa mwanya kwa vyama vyenzake kusonga mbele.Naitazama CHADEMA kuanguka Kama umaarufu wa NCCR Mageuzi mwaka 1995.
Nitafurahi sana kuona na kusikia kauli za vijana mbalimbali wa CHADEMA wakiwemo UTG wakihoji kuhusiana na Uminyaji wa Demokrasia ndani ya chao chao CHADEMA ili tuzijue rangi zao katika kuhoji na kujenga hoja.

Mwandishi wa Makala haya ni Mathias Canal, Mchambuzi wa maswala ya jamii na siasa nchini Tanzania, Anapatikana kwa Barua Pepe ya canalmathias@gmail.com na kwa simu namba 0756413465
Bashir Nkoromo

Posted in

Spread the love