4x4

SALAMU ZA MWAKA MPYA ZA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MHESHIMIWA DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE KWA WATANZANIA, TAREHE 31 DESEMBA, 2013

Utangulizi
Ndugu zangu;
Watanzania Wenzangu;
RAIS KIKWETE
Niruhusuni nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kutujalia uzima mpaka kufika  na kuiona siku hii ya leo ya kuuaga mwaka 2013 na kuukaribisha mwaka 2014.  Wapo ndugu, jamaa na marafiki zetu wengi ambao hawakupata bahati tuliyoipata sisi kwa vile wametangulia mbele ya haki.  Tuendelee kumwomba Mola wetu awape mapumziko mema na azilaze roho zao mahali pema peponi. Ameen.

Hali ya Usalama
Ndugu Wananchi;
Tunaumaliza mwaka 2013 nchi yetu ikiwa salama na tulivu. Mipaka iko salama na ile hali ya wasiwasi tuliyokuwa nayo kwa nyakati fulani mwaka huu sasa haipo tena. Uhusiano wetu na majirani ni mzuri na tutaendelea kufanya kila tuwezalo kuhakikisha kuwa hali inaendelea kuwa hivyo au hata kuwa bora zaidi mwaka 2014 na daima dumu.
Hali ya usalama wa ndani ya nchi nayo ni nzuri.  Hali ya wasiwasi tuliyokuwa nayo mwaka wa jana na mwanzoni mwa mwaka huu kuhusu uhusiano baina ya Wakristo na Waislamu haipo.  Ni matumaini yangu kuwa haitajirudia tena. Pepo mbaya amepita tuombe atokomee kabisa.

Ndugu zangu;
Watanzania wenzangu;
Napenda kurudia kuwasihi kuwa tuchague kuendelea kuishi pamoja kwa upendo, umoja, kuvumiliana na kushirikiana. Tuepuke kugeuza tofauti zetu za kisiasa, kidini, rangi, kabila au maeneo tutokayo kuwa chanzo cha uadui na mifarakano.  Kwa sasa tuna mwelekeo mzuri nawaomba tuudumishe. “Mjenga nchi ni mwananchi na mbomoa nchi ni mwananchi”. Tuchague kuijenga nchi yetu badala ya kuibomoa.  Tusiwasikilize watu hasidi wanaochochea uadui na mifarakano miongoni mwetu. Watatuvurugia nchi yetu nzuri.

Uhalifu
Ndugu Wananchi;
Katika mwaka 2013 vyombo vya dola vikishirikiana na wananchi viliendelea kupambana na vitendo vya uhalifu.  Mafanikio ya kutia moyo yameendelea kupatikana ingawaje bado kuna kazi kubwa ya kuendelea kufanya mwaka 2014 na miaka ijayo.

Dawa za Kulevya
Ndugu Wananchi;
Kati ya Januari na Desemba 2013, kilo 1,261 za heroin, kilo 3 za cocaine na kilo 89,293 za bangi zimekamatwa na watuhumiwa 1,631 wametiwa mbaroni.  Tatizo la biashara na matumizi ya dawa za kulevya ni kubwa na mapambano yanazidi kuwa makali. Mafanikio yanaendelea kupatikana ingawaje bado tuna kazi kubwa na ngumu ya kufanya mbele yetu. Ni makusudio yetu kuongeza maradufu nguvu ya kupambana dhidi ya uhalifu huu.
 Tupo hatua nzuri katika matayarisho ya kuanzisha Kikosi Maalum cha Kupambana na Dawa za Kulevya katika mwaka wa fedha 2014/15.  Pia tutaitazama upya sheria ya adhabu kwa makosa ya kufanya biashara ya dawa za kulevya ili kuifanya iwe na meno makali zaidi.  Vilevile, tutaongeza uwekezaji katika vituo vya tiba na kuwarekebisha watu wanaotumia dawa za kulevya. Mafanikio yanayopatikana Muhimbili na Mwananyamala yanatupa moyo wa kufanya zaidi.

Ujambazi
Ndugu wananchi;
Jeshi la Polisi limeendelea kupambana na ujambazi wa kutumia silaha na mafanikio yameendelea kupatikana. Matukio ya ujambazi yemepungua mwaka 2013 ukilinganisha na mwaka 2012.  Takwimu zifuatazo zinathibitisha ukweli huo.  Mwaka 2012 matukio ya ujambazi yaliyoripotiwa yalikuwa 6,872 na kwa mwaka 2013 yameripotiwa matukio 6,409.  Mwezi Julai mwaka huu, niliamua kulihusisha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania katika kupambana na ujambazi wa kutumia silaha na utekaji wa magari katika Mikoa ya Geita, Kagera na Kigoma. Katika Mikoa hiyo tatizo la ujambazi lilikuwa limefikia kiasi cha kulazimisha watu kusindikizwa na Polisi kutoka Ngara kwenda Karagwe, Biharamulo kwenda Muleba na kutoka Nyakanazi hadi Kakonko.  Hali hii haikubaliki na hatuwezi kuiacha iendelee.

Ndugu Wananchi;
Uamuzi wangu huo ndiyo ulioanzisha Operesheni Kimbunga ambayo imekuwa na mafanikio ya kutia moyo. Hali ya usalama katika Mikoa hiyo inaelekea kuimarika ingawaje ni mapema mno kusema tatizo limedhibitiwa.  Silaha nyepesi na nzito zipatazo 650 zikiwemo za kijeshi na za kiraia pamoja na mabomu ya kutupwa kwa mkono 11 zilikamatwa kwenye operesheni hiyo. Aidha, watu 31,203 waliokuwa wanaishi nchini kinyume cha sheria walirudi makwao.  Kati yao, watu 21,758 walirudi kwa hiari na 9,445 walirudishwa wakati wa Operesheni.

Ndugu Wananchi;
Nimepata minong’ono kuwa baadhi ya watu walioondoka wanarudi kinyemela. Napenda kuwatahadharisha kuwa wasifanye hivyo.  Wanajisumbua bure. Hawatadumu.  Ushauri wangu kwao ni kuwa kama wanapenda kuishi Tanzania wafuate njia halali za kufanya hivyo.

Ujangili wa Wanyamapori
Ndugu Wananchi;
Mwaka huu tuliongeza nguvu katika kupambana na ujangili wa wanyamapori na uvunaji haramu wa rasilimali za misitu. Hili ni tatizo la siku nyingi lakini katika miaka ya hivi karibuni limekuwa kubwa mno na kuwazidi nguvu Askari wa Wanyamapori na Maafisa Misitu.
Kwa nia ya kuwaongezea nguvu, mwaka 2010 niliagiza Jeshi la Polisi lisaidie Idara ya Wanyamapori  na Idara ya Misitu katika kupambana na uhalifu huo.  Operesheni kadhaa ziliendeshwa maeneo mbalimbali nchini na mafanikio ya kutia moyo yalipatikana.  Lakini, kwa kutambua ukubwa wa tatizo na hasa kwa upande wa aina ya silaha na mbinu zinazotumiwa na majangili niliamua kuhusisha vyombo vingine vya usalama likiwemo Jeshi la Ulinzi.  Nia ni kuongeza nguvu ya mapambano. Ndipo ilipoanzishwa “OPERESHENI TOKOMEZA”.

Ndugu Wananchi;
Kazi nzuri imefanyika chini ya Operesheni hiyo.  Mafanikio ya kuleta matumaini yameweza kupatikana.  Mitandao ya ujangili imeweza kutambulika na wahusika wake kadhaa wametiwa nguvuni.  Mitandao hiyo inahusisha watu wa aina mbalimbali.  Wamo raia wa kawaida, wapo watu maarufu, wapo watumishi wa idara mbalimbali za Serikali wakiwamo wa Idara za Wanyamapori na Misitu. Watu 1,030 walikamatwa pamoja na silaha za kijeshi 18,  za kiraia 1,579 na shehena kubwa za meno ya ndovu na nyara nyingine navyo vilikamatwa.Watu kadhaa tayari wameshafikishwa mahakamani.

Ndugu Wananchi;
Wahenga wamesema “kwenye wengi pana mengi”. Katika utekelezaji wa Operesheni hii kumekuwepo na taarifa za kufanyika makosa kinyume na malengo na madhumuni ya Operesheni.  Niliagiza baada ya kumalizika kwa awamu ya kwanza, zoezi lisitishwe kwa muda ili uchunguzi ufanyike, kasoro zitambuliwe na waliofanya makosa wachukuliwe hatua zipasazo. Wakati kazi hiyo inafanyika suala hilo lilijadiliwa Bungeni na Kamati Teule kuundwa.  Matokeo yake sote tunayajua.  Mawaziri wanne wamewajibika kisiasa.
   
Ndugu Wananchi;
Napenda kutumia nafasi hii kuwapa pole Mawaziri wetu hao kwa matatizo yaliyowakuta. Nawapongeza kwa uamuzi wa kukubali kuwajibika kwa makosa yaliyofanywa na maofisa wa chini yao. Wameonesha  ukomavu wa kisiasa na kiuongozi wa  hali ya juu na moyo wa uzalendo.
Kama mlivyosikia nitaunda Kamisheni ya Uchunguzi itakayoongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu. Uchunguzi wa kina utafanywa kuhusu kadhia yote hiyo.  Makosa yaliyofanyika yataainishwa na waliofanya kutambuliwa ili wachukuliwe hatua zipasazo kwa mujibu wa sheria na kwa mujibu wa kanuni za utumishi wa umma.

Ndugu Wananchi;
Ni muhimu kufanya hivi ili haki itendeke ipasavyo.  Mtindo wa mzigo wa makosa ya watumishi wa umma kubebwa na viongozi wa kisiasa pekee, tena wasiokuwa na hatia ya moja kwa moja, siyo sahihi.  Lazima kila mtu abebe mzigo wake inavyostahili.  Ni matumaini yangu pia kwamba katika siku za usoni kunapotokea matatizo ya namna hii uchunguzi uwe wa kina ili wale hasa waliohusika na kutenda makosa wawajibishwe.  Uwajibikaji wa wana-siasa peke yao hautoshi, kwani huwaacha waharibifu waendelee na kazi isivyostahili.  Mtindo huu utawafanya watumishi wasione umuhimu wa kutokurudia makosa.  Hata hivyo, pale kwenye ushahidi wa wazi kwamba kiongozi wa kisiasa angeweza kuchukua hatua za kuzuia madhara lakini hakufanya hivyo lazima kiongozi huyo awajibike.

Ndugu Wananchi;

Tunakamilisha matayarisho ya kuanza awamu ya pili ya Operesheni Tokomeza.  Ni muhimu kuendelea nayo kwani tusipofanya hivyo majangili wataendelea na vitendo vyao viovu.  Hali ni mbaya sana kwa upande wa uwindaji wa ndovu. Nilipolihutubia Bunge tarehe 7 Novemba, 2013, nilieleza kuwa tutafanya sensa ya ndovu katika Pori la Hifadhi la Selous.  Sensa hiyo imekamilika lakini taarifa yake inatisha.  Kuna ndovu 13,084 tu wakati mwaka 1976 walikuwa 109,419.  Tusipoendelea na Operesheni hii baada ya miaka michache ijayo hakutakuwa na ndovu hata mmoja.  Halikadhalika, zoezi la kuondoa mifugo katika mapori ya hifadhi ya taifa litaendelea.  Katika awamu ya pili ya Operesheni hii, washiriki watasisitizwa kutokutenda maovu yaliyofanyika katika awamu ya kwanza.

Mchakato wa Kuunda Katiba
Ndugu wananchi;
Tumefika mahala pazuri katika mchakato wetu wa kutayarisha Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  Jana Mwenyekiti wa Tume, Mheshimiwa Jaji Joseph Warioba, alitukabidhi Rasimu ya Pili ya Katiba, mimi na Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein.  Kama nilivyosema jana kinachofuata sasa ni kuitangaza Rasimu hiyo katika Gazeti la Serikali kwa kila mtu na hasa Wajumbe wa Bunge la Katiba, kuiona na kuisoma.  Baada ya hapo kitafuata kitendo cha kuifikisha Rasimu kwenye Bunge Maalum la Katiba kwa ajili ya kujadiliwa na hatimaye kupatikana Rasimu ya Mwisho itakayofikishwa kwa wananchi kupigiwa kura.

Ndugu Wananchi;
Mchakato wa kupata Wajumbe 201 watakaoungana na Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuunda Bunge Maalum la Katiba umeanza.  Ni matarajio yetu kuwa katika wiki ya tatu ya Januari, 2014, uteuzi utakamilika.  Siku 21 baada ya hapo Bunge la Katiba litaanza.  Hii ni kwa nia ya kuwapa nafasi Wajumbe hao kusoma Rasimu ya Katiba.  Baada ya Bunge la Katiba kumaliza kazi yake, utaanza mchakato wa Kura ya Maoni itakayopigwa na wananchi ndani ya siku 74 baada ya Rasimu ya Katiba kupitishwa na Bunge Maalum na kukabidhiwa kwa Rais.
 Iwapo Rasimu itakubaliwa na wananchi hapo tutakuwa tumepata Katiba Mpya. Lakini, iwapo Rasimu itakataliwa ina maana kuwa Katiba ya sasa itaendelea kutumika mpaka hapo mchakato mwingine utakapoanzishwa na Katiba mpya kupatikana.  Ni matumaini yangu na, ni maombi yangu na rai yangu kuwa Rasimu hiyo itakubalika ili nchi yetu isonge mbele.

Pongezi
Ndugu Wananchi;
Niruhusuni nitoe pongezi zangu za dhati kwa Mwenyekiti na Wajumbe wote wa Tume kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya.  Najua haikuwa kazi rahisi hata kidogo lakini wameweza.  Kwa namna ya pekee nawashukuru wananchi kwa ushiriki wao mzuri uliowezesha zoezi la mabadiliko ya Katiba kufikia hatua tuliyofikia sasa.

Ndugu Wananchi;
Ni matumaini yangu na ndiyo matumaini ya Watanzania wote kuwa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wataijadili Rasimu ya Katiba kwa makini na kufanya kila wawezalo kuiwezesha nchi yetu kupata Katiba nzuri itakayoimarisha na kudumisha Muungano wetu.  Katiba itakayoendeleza umoja, upendo, udugu, mshikamano na ushirikiano miongoni mwa wananchi wa Tanzania. Katiba itakayoihakikishia nchi yetu amani, utulivu na ustawi wa kiuchumi na kijamii.
 Ni imani yangu na ya Watanzania wote kuwa Wajumbe wa Bunge la Katiba wataweka mbele maslahi mapana ya taifa na watu wake. Wasiweke mbele maslahi yao binafsi au ya vikundi vyao vya kisiasa au kijamii. Wakifanya vinginevyo kuna hatari ya kupata Katiba isiyokidhi haja na itakuwa hasara kubwa kwa taifa letu na kwao pia.  

Uchumi
Ndugu wananchi;
Katika mwaka tunaoumaliza leo, Tanzania iliendelea kupata mafanikio katika nyanja mbalimbali za maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Jambo la kufurahisha ni kuwa mafanikio hayo yamepatikana licha ya kuwepo changamoto kadhaa hapa nchini na hali ya uchumi wa dunia kuwa bado haijatengemaa vya kutosha.
Pato la taifa limekua kwa asilimia 7.1 ukilinganisha na asilimia 6.9 mwaka jana.   Tunategemea kuwa mwaka 2014 pato la taifa litakua kwa asilimia 7.3.  Mfumuko wa bei umeshuka kutoka asilimia 12.1, Desemba, 2012 hadi asilimia 6.2, Novemba 2013. Lengo letu ni kufikia asilimia 5 mwezi Juni, 2014.

Ndugu Wananchi;
Hadi Novemba, 2013, Tanzania ilikuwa imeuza nje bidhaa na huduma zenye thamani ya dola za Marekani milioni 7,720.8 ukilinganisha na dola milioni 7,916.6 za mwaka ulioishia Novemba 30, 2012.  Kushuka kwa bei za kahawa, pamba, katani, chai, karafuu na dhahabu ndiko kulisababisha kupungua kwa mapato yetu ya fedha za kigeni.  Hali hii inatukumbusha umuhimu na uharaka wa kuendeleza viwanda vya kuongeza thamani mazao na bidhaa zetu tunazouza nje.  Jambo hili tutalipa msukumo maalum mwaka 2014 na kuendelea.
Pamoja na kushuka kidogo kwa mapato ya mauzo yetu ya nje akiba yetu ya fedha za kigeni iliendelea kuwa nzuri.  Hadi Novemba 30, 2013 akiba yetu ilikuwa dola za Marekani 4,538 milioni.  Hata hivyo, akiba hiyo inatuwezesha kuagiza bidhaa toka nje wa miezi 4.4 ni chini ya lengo letu la miezi 4.5.  Sina wasiwasi kuwa mwaka 2014 tutaliziba pengo hilo.

Ndugu Wananachi;
Sekta zilizochangia sana katika kasi ya ukuaji wa uchumi mwaka 2013 ni pamoja na mawasiliano asilimia 20.6, huduma ya fedha asilimia 13.2, uzalishaji viwandani asilimia 8.2, madini asilimia 7.8, ujenzi asilimia 7.8, biashara asilimia 7.7 na uchukuzi asilimia 7.1.  Bado kasi ya ukuaji wa sekta ya kilimo ilikuwa ndogo kwani ilikuwa asilimia 4.3.
Pamoja na hayo, kilimo kinaendelea kutoa mchango mkubwa kwa ustawi wa uchumi wa Tanzania na watu wake.  Kilimo kinachangia asilimia 24.7 ya pato la taifa na asilimia 10.7 ya mapato ya fedha za kigeni. Kilimo kimeiwezesha nchi yetu kujitosheleza kwa chakula na kuvipatia viwanda malighafi.    Kwa upande wa mazao ya chakula, kwa mfano, mwaka huu uzalishaji ulikuwa tani 14,383,845.  Ukilinganisha na mahitaji yetu ya chakula ya tani 12,149,120 hivyo tunajitosheleza na kuwa na ziada kidogo. Ziada hii ni kidogo mno hivyo inatulazimu mwaka ujao tuongeze maradufu juhudi na uwekezaji katika kutekeleza shabaha na malengo ya kilimo.

Ndugu Wananchi;
Kwa ajili ya uzalishaji wa chakula kuwa mzuri, mwaka huu Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula wameweza kununua tani 233,689.8 za nafaka hadi kufikia Desemba 27, 2013 kiasi ambacho hakijawahi kufikiwa miaka ya nyuma.  Mwaka 2012 wakati kama huu Wakala ilikuwa na kiasi cha tani 93,047.8 tu  na kutulazimisha kutafuta chakula nje ya nchi. Kwa ajili hiyo tulilazimika kuruhusu wafanyabiashara kuagiza mahindi, mchele na sukari kutoka nje kwa nafuu ya kodi.  Uamuzi huo umesaidia nchi kuwa na chakula cha kutosha na kuuzwa kwa bei nafuu kwa walaji.  

Ndugu Wananchi;
Ni matarajio yangu, na ndiyo hasa dhamira yetu, kwamba mwaka 2014 tutapata mafanikio makubwa zaidi kwa upande wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Naamini tutaweza kwa vile tumejipanga vizuri.  Tunayo miradi ya kimkakati iliyoainishwa vizuri katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano na chini ya Utaratibu wa Matokeo Makubwa Sasa.  Miradi hiyo kama itatekelezwa kama ilivyopangwa uchumi utakua kwa kasi kubwa zaidi, ajira nyingi zitapatikana na huduma za kiuchumi na kijamii zitaboreka sana.
Bahati nzuri tumeweka utaratibu mpya na mzuri wa kufuatilia utekelezaji wa mipango, miradi na shughuli za Serikali.  Katika Ofisi ya Rais kumeanzishwa Ofisi maalum ya ufuatiliaji ijulikanayo kama Presidential Delivery Bureau.  Na, kila Wizara ina kitengo cha namna hiyo kijulikanacho kama Ministerial Delivery Unit. Kwa ajili hiyo utekelezaji wa miradi ya kimkakati na shughuli za Serikali utakuwa mzuri zaidi.

Mazingira ya Uwekezaji
Ndugu Wananchi;
Ni makusudio yetu kuwa kuanzia sasa tutaihusisha sekta binafsi kwa nguvu zaidi katika utekelezaji wa miradi na shughuli za maendeleo. Nimeagiza Presidential Delivery Bureau ishughulikie suala la uboreshaji wa mazingira ya uwekezaji nchini.  Sifa ya nchi yetu kuhusu mazingira ya uwekezaji siyo nzuri.  Kwa mujibu wa tathmini inayofanywa kila mwaka na Benki ya Dunia, mwaka 2007 nchi yetu ilikuwa kati ya nchi 10 bora duniani kwa kufanya mageuzi makubwa ya kupunguza gharama za kufanya biashara. Mwaka huo tulikuwa nchi ya 142 kati ya nchi 175.  Mwaka 2008 tukapanda na kuwa wa 130 kati ya nchi 176, mwaka 2012 tulikuwa wa 134 kati ya nchi 185 na sasa ni wa 145 kati ya nchi 185.  Hali hii si nzuri hata kidogo kwa uchumi unaokusudiwa kujengwa kwa kutegemea uwekezaji wa sekta binafsi.  Tunategemea PDB itatupa ushauri mzuri wa nini kifanyike kurekebisha mambo.

Ndugu Wananchi;
Utekelezaji wa miradi ya Big Result Now (BRN) katika kilimo, umeme, reli, barabara, bandari, maji, elimu na kuongeza mapato ya Serikali umeanza kwa kasi inayoleta matumaini. Kama upande wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali utakwenda inavyotarajiwa tutegemee mambo mengi mazuri kufanyika kuanzia mwaka 2014 mpaka 2016.
Mpaka sasa hali ya ukusanyaji wa mapato ya Serikali si mbaya.  Wastani kwa mwezi unakaribia shilingi bilioni 700 kuelekea shilingi bilioni 800.  Makusanyo ya mapato ya Serikali kwa miezi ya Julai hadi Novemba yaliongezeka kutoka shilingi bilioni 3,008.1 kipindi kama hicho mwaka 2012 hadi shilingi bilioni 3,555.5 mwaka 2013.  Hata hivyo makusanyo ya Julai hadi Novemba, 2013 ni asilimia 88.1 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 4,036.8. Lengo halijafikiwa kwa sababu ya kuchelewa kutekelezwa kwa baadhi ya marekebisho ya mfumo wa kodi, hususan tozo ya simcard, kodi za mishahara kutokana na kutokupandishwa kwa kima cha chini katika sekta binafsi na ya uhawilisho wa fedha (money transfer). Pia kuendelea kwa mvutano baina ya TRA na wafanyabiashara kuhusu bei za mashine za kodi.  Ni matumaini yangu matatizo hayo yatashughulikiwa na kumalizwa mapema iwezekanavyo ili tuweze kupata mafanikio makubwa zaidi katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali mwaka 2014.

Elimu
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa elimu tumeendelea kupata mafanikio katika kupunguza tatizo la upungufu wa walimu wa shule za msingi na sekondari. Mwaka huu tuliajiri walimu 28,666. Kwa ajili hiyo upungufu wa walimu ni 57,755 kati yao  20,625 wa shule za msingi na 37,130 wa shule za Sekondari.  Mapema mwaka ujao tutaajiri walimu wapya 36,100 kati yao 18,100 wa shule za msingi na 18,000 wa sekondari. Kufanya hivyo kutafanya pengo lililopo liwe dogo zaidi.
Kwa upande wa shule za sekondari, tatizo la walimu wa masomo ya sanaa tunakaribia kulimaliza. Changamoto yetu kubwa itakuwa kwa walimu wa masomo ya sayansi.  Upungufu ni walimu 26,998 na uwezo wa vyuo vyetu ni kutoa walimu wa sayansi 2,300 kwa mwaka.  Mapema mwaka 2014 tutakutana na wadau wa elimu nchini kujadiliana juu ya mkakati wa haraka wa kulikabili tatizo hili. Nilipanga tufanye hivyo mwaka huu lakini mambo yaliingiliana sana hatukuweza.

Ndugu Wananchi,
Tumeendelea kupunguza tatizo la uhaba wa vitabu na vifaa vya kujifunzia na kufundishia.  Tuliongeza fedha katika bajeti ya elimu kwa ajili ya vitabu.  Hivi sasa usambazaji wa vitabu vyenye thamani ya shilingi bilioni 76 za bajeti ya mwaka 2012/13 unaendelea.  Kwa sababu hiyo hivi sasa upungufu wa vitabu umeshuka na kufikia kitabu kimoja kwa wanafunzi 3. Naamini shilingi bilioni 49 zilizotengwa katika bajeti ya mwaka huu wa fedha kwa ajili ya vitabu itafanya mambo kuwa nafuu zaidi. Tukiendelea kuwekeza kama tufanyavyo sasa shabaha yetu ya kila mwanafunzi wa msingi na sekondari kuwa na kitabu chake kwa masomo yote ifikapo 2016 itatimia.

Ndugu Wananchi;
Mwaka huu tumeanza utekelezaji wa mpango mkubwa wa kujenga nyumba za walimu.  Kwa kuanzia tumetenga shilingi milioni 500 kwa kila Halmashauri. Tumeanza na Halmashauri 40, mwaka ujao na miaka inayofuata tutaongeza fedha zinazotengwa na kuzifikia Halmashauri zote.  Kwa upande wa ujenzi wa maabara katika sekondari za kata napenda kuwakumbusha Wakuu wa Mikoa na Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya na Miji, kuwa kila mmoja ahakikishe kuwa ifikapo Novemba, 2014 malengo yanatimia.  Wasisubiri kuulizwa.

Maji
Ndugu Wananchi;
  Kwa kutambua umuhimu wa maji kwa maisha ya wanadamu na uchumi katika bajeti ya mwaka huu wa fedha sekta ya maji imepewa upendeleo katika mgao wa fedha. Tutaendelea kuongeza fedha katika bajeti mbili zinazofuata ili watu wengi zaidi mijini na vijijini wapate maji safi na salama. Kama fedha zitapatikana kama ilivyopangwa na utekelezaji ukasimamiwa vizuri tunatarajia kuwa katika mwaka 2013/14 watu milioni 7.1 watapata maji.  Katika mwaka ujao wa fedha 2014/15 tumepanga kuwapatia maji watu wengine milioni 7 na mwaka utaofuata (2015/16) tutaongeza tena huduma hiyo kwa watu milioni 1.3 na kufanya tufikie asilimia 74 ya Watanzania wanaopata maji safi na salama ifikapo 2015/2016.
  
Afya
Ndugu wananchi;
Tumeendelea kupata mafanikio katika kuendeleza upatikanaji wa huduma ya afya kwa wananchi wa Tanzania.  Zahanati, vituo vya afya na hospitali zimeendelea kujengwa kote nchini. Aidha, hospitali za wilaya, mikoa, kanda na Hospitali ya Taifa Muhimbili zimeendelea kuboreshwa.  Kwa ajili hiyo idadi ya Watanzania wanaoweza kupata huduma ya afya iliyo bora inazidi kuongezeka.  Hali kadhalika, wataalamu wa afya wa fani mbalimbali wameongezeka na hali ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba imezidi kuboreshwa.  Pamoja na yote hayo bado kuna kazi kubwa ya kufanya mbele yetu.  Kufanya hayo ndiyo dhamira yetu kuu kwa mwaka 2014.

Ndugu wananchi;
Tumeendelea kupata ushindi katika mapambano dhidi ya magonjwa yanayoua watu wengi nchini.  Kwa upande wa malaria, kwa mfano, maambukizi ya ugonjwa huo kwa watoto na mama wajawazito yamepungua kutoka asilimia 18 hadi 9.5. Tutaendelea kugawa vyandarua kwa wajawazito na watoto kwa kutumia hati punguzo pamoja  na kusisitiza matumizi ya dawa mseto na kupulizia dawa ya kuua mbu majumbani.   Aidha, tunatarajia kupata mafanikio zaidi miaka ijayo kiwanda cha kuzalisha viuadudu vya kuua viluilui vya mbu wanaoeneza malaria kitapoanza kazi.

Ndugu Wananchi;
Mambukizi ya UKIMWI yameshuka hadi asilimia 5.1. Inaleta faraja kuona watu wengi wamejitokeza kupima afya zao kwa hiari.  Mpaka sasa watu milioni 18 wamepima. Tunao watu 1,298,402 walioorodheshwa kwa ajili ya kupata huduma ya tiba na kati yao 485,715 wanapata dawa.  Waliosalia watapata wakati wao ukifika.    
  Mpaka sasa vituo 4,603 vinavyotoa huduma ya kuzuia maambukizi ya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto vimeanzishwa nchini kote tangu mpango huo uzinduliwe tarehe 1 Desemba, 2012.  Idadi yake inaendelea kuongezeka. Ni dhamira yetu kuendeleza jitihada za kupunguza maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwa Watanzania.  Mafanikio ya kampeni hii pamoja na ile dhidi ya malaria ndiyo chachu ya mafanikio tuliyopata katika kupunguza vifo vya watoto nchini na kufikia lengo la Milenia mwaka huu.

Magonjwa ya Moyo
Ndugu Wananchi;
Katika mwaka 2013 tunaoumaliza leo, tumeshuhudia mambo kadhaa mazuri yakifanyika yanayoelezea mafanikio tunayoendelea kuyapata katika jitihada zetu za kujenga uwezo wa tiba kwa maradhi tunayopeleka wagonjwa nje ya nchi.  Niruhusuni niyataje baadhi yake.  La kwanza, ni kuanza kazi kwa Kituo cha Tiba na Mafunzo ya Magonjwa ya Moyo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Hiki ni kituo kikubwa na cha aina yake cha matibabu ya maradhi ya moyo hapa nchini.  Huduma za kisasa za uchunguzi na matibabu ya maradhi ya moyo ambazo zamani zilikuwa zinapatikana nje ya nchi sasa zinaweza kupatikana hapa hapa nchini.  Kwa kuwa na vitanda 100 vya kulaza wagonjwa, Watanzania wengi wataweza kuhudumiwa na maisha yao kuokolewa.
  
Ndugu Wananchi;
Katika kituo hiki watu wanaweza kufanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo (open heart surgery), uwekaji wa mashine ya kuongezea nguvu  kwenye moyo (pacemaker), uwekaji wa vyuma vidogo katika mishipa ya damu ya moyo ambayo imebanana (stent).   Tangu kituo kianze kazi rasmi tarehe 30 Aprili, 2013 mpaka sasa watu 347 wamefanyiwa upasuaji wa moyo na watu watatu wamewekewa pacemaker tangu huduma hiyo ianze Novemba, 2013.  Mapema mwakani kituo kinatarajiwa kuanza huduma ya kuweka stent.
Kituo hiki ni kipya hivyo katika mwaka 2014 tutaendelea kukijengea uwezo wa vifaa tiba, wataalamu na mahitaji mengine muhimu ili kulipunguzia taifa mzigo wa kupeleka wagonjwa nchi za nje. Serikali, pia itaendeleza ushirikiano wake na uongozi wa Hospitali ya Kanda ya Bugando kuboresha huduma ya upasuaji mkubwa wa moyo katika hospitali hiyo.  Huduma hiyo ilizinduliwa tarehe 26 Oktoba, 2013 na Makamu wa Rais Mheshimiwa Daktari Mohamed Ghalib Bilal.

Saratani
Ndugu Wananchi;
  Kwa upande wa maradhi ya saratani, Februari, 2013 jengo jipya la kulaza wagonjwa 170 lilifunguliwa katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road. Kufunguliwa kwa jengo hilo kumeongeza uwezo wa taasisi yetu hiyo kulaza wagonjwa 290 badala ya 120 tu kabla ya hapo. Ujenzi wa jengo hili jipya umesaidia sana watu wengi zaidi kuhudumiwa na kupunguza msongamano mkubwa wa wagonjwa uliokuwepo.

Figo
Ndugu Wananchi;
Kuhusu maradhi ya figo mwaka huu pia tumeshuhudia huduma ya usafishaji wa figo zenye matatizo ikipanuliwa.  Huduma hiyo imeanzishwa tena katika Hospitali ya Kanda ya Mbeya na imeanzishwa kwa mara ya kwanza katika Chuo cha Tiba katika Chuo Kikuu cha Dodoma.  Pale Mbeya tayari wagonjwa 93 wamehudumiwa mwaka huu na kuwapa matumaini mapya ya maisha yao.  Kwa pale Chuo Kikuu cha Dodoma, ujenzi wa kituo kikubwa kitakachobobea kwa magonjwa ya figo unaendelea na unategemewa kukamilika mapema mwaka 2014.

Mafunzo
Ndugu Wananchi;
Katika mwaka 2013 tumefungua ukurasa mpya katika jitihada zetu za kuongeza wataalamu wa afya nchini.  Chuo cha Sayansi ya Tiba katika Chuo Kikuu cha Dodoma kimefanya mahafali yake ya kwanza ambapo wanafunzi 50 wa Shahada ya Uuguzi walihitimu.  Tunatarajia kuanza kupata madaktari kuanzia mwaka 2014.
Kwa upande wa mchakato wa kujenga makazi mapya ya Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili kule Mloganzila mchakato umeanza. Ujenzi wa miundombinu ya barabara, maji na umeme unaendelea hivi sasa.  Mwaka 2014 ujenzi wa Hospitali ya kisasa ya kufundishia yenye vitanda 650 utaanza. Ujenzi wa Mlonganzila ukikamilika Chuo Kikuu cha Muhimbili kitaweza kuchukua wanafunzi 15,000 wa fani zote  ukilinganisha na 3,060 wa sasa.  Hatua hiyo itaongeza sana uwezo na kasi yetu ya kupunguza uhaba wa Madaktari, Wauguzi na wataalam wengine wa afya.

Nyumba
Ndugu Wananchi;
Katika mwaka 2013 ujenzi wa nyumba 35 za kuishi watumishi wa afya katika mikoa ya Mtwara (5), Rukwa (20) na Singida (10) umekamilika.  Ujenzi wa nyumba 100 unaendelea.  Nyumba hizo ni sehemu ya mpango wa ujenzi wa nyumba 580 zinazojengwa kwa ushirikiano kati ya Serikali na Global Fund kwa awamu mbili.  Awamu ya kwanza zinajengwa nyumba 310 ambapo taasisi ya Benjamin William Mkapa Foundation ndiyo mtekelezaji wa ujenzi huo.  Napenda kutumia nafasi hii kutoa shukrani za dhati kwa Rais Mstaafu Mheshimiwa Benjamin Mkapa kwa mchango wake mkubwa alioutoa na anaoendelea kutoa kwa maendeleo ya nchi yetu na watu wake.

Ujenzi wa Miundombinu
Ndugu wananchi;
Katika mwaka 2013, tumeendelea kupata mafanikio makubwa katika kuboresha miundombinu ya usafiri wa ardhini, majini na angani. Kasi ya ujenzi wa barabara imeendelea kufanyika kote nchini. Kazi ya ujenzi ingekuwa nzuri zaidi kama mtiririko wa malipo kwa Wakandarasi ungekuwa mzuri.  Tatizo hili tutalitafutia ufumbuzi mwaka 2014 ili kasi ya ujenzi wa barabara za lami nchini iwe nzuri zaidi.
Pamoja na hayo mwaka huu kilomita 877 za barabara zimekamilika. Ujenzi wa daraja la Malagarasi nao umekamilika kinachosubiriwa ni sherehe za uzinduzi. Ujenzi wa daraja la Kilombero umeanza na ule wa daraja la Kigamboni unaendelea vizuri. Tunatarajia kuwa mwakani tutaongeza zaidi kasi ya ujenzi wa barabara zilizosalia ikiwa ni pamoja na kujenga baadhi ya barabara kwa ubia na sekta binafsi.  Kwa kasi na mwenendo tunaoendelea nao sasa naamini ifikapo mwaka 2015 tutakuwa tumefikia hatua ya juu sana katika shabaha yetu ya kuunganisha mikoa yote nchini kwa barabara za lami.
  
Ndugu Wananchi;
Jitihada za kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam zimeendelea kutekelezwa.  Barabara kadhaa zilipanuliwa na kazi inaendelea.  Ujenzi wa njia ya kupita mabasi yaendayo haraka umeendelea kwa kasi ya kuridhisha.  Mchakato wa ujenzi wa barabara za juu ya nyingine katika njia panda za TAZARA na Ubungo umeshaanza.  Mwaka ujao huduma ya usafiri wa treni kusafirisha abiria Dar es Salaam itaongezwa ili watu wengi zaidi wanufaike.

Ndugu wananchi;
Mwaka huu, kwa upande wa reli ya kati, kazi ya kuboresha njia ya reli imeendelea kufanyika na itaendelea mwaka 2014.  Mwakani (2014) Shirika la Reli litapokea injini mpya 13, mabehewa ya mizigo 274 na breki 34 hivyo kuboresha sana huduma katika reli ya kati.  Kuhusu ujenzi wa reli mpya ya upana wa kimataifa ni matarajio yetu kuwa kama kila kitu kitaenda sawa mchakato wa ujenzi utaanza katika nusu ya pili ya mwaka 2014.

Ndugu Wananchi;
Tumetoa kipaumbele cha juu katika kuboresha huduma ya usafiri wa anga nchini.  Mwaka huu, tumeendelea na ukarabati, upanuzi na ujenzi wa viwanja vya ndege vya Mikoa ya Kilimanjaro, Kigoma, Tabora, Mwanza, Arusha, Mtwara na Kagera.  Ni jambo la kufurahisha kuona Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe ukianza kutumika. Hatimaye ndoto imetimia.  Mwaka wa 2014 ujenzi wa majengo mengine ya kuhudumia abiria, mizigo na ndege utaendelea katika uwanja huo.
Pia ni furaha iliyoje kwamba upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Mafia na ujenzi wa gati la Kilindoni vimekamilika.  Kero ya miaka mingi imepatiwa ufumbuzi.  Kazi ya ujenzi wa jengo jipya la abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere itaanza rasmi mwaka 2014.

Nishati
Ndugu wananchi;
Dhamira yetu ya kutaka Tanzania iwe na umeme wa uhakika na unaonufaisha watu wengi imepata sura na mwelekeo mzuri mwaka huu 2013.  Ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara na Songosongo kuja Dar es Salaam umeanza na utekelezaji unakwenda vizuri.  Kama ujenzi wa bomba utakamilika kama inavyotarajiwa na ujenzi wa mitambo ya kuzalisha umeme Kinyerezi utaenda kama ilivyopangwa, ifikapo mwaka 2015 Tanzania itafikia lengo la kuzalisha megawati 3,000 za umeme.

Ndugu Wananchi;
Bahati nzuri mwaka huu, kufuatia kuongezewa fedha za bajeti, kasi ya usambazaji umeme imekuwa nzuri.  Tunaumaliza mwaka huku idadi ya Watanzania waliounganishiwa umeme ikiwa imefikia asilimia 24 ukilinganisha na asilimia 21 mwaka 2012 na asilimia 10 mwaka 2005. Haya si mafanikio madogo. Kwa mwelekeo huu, kufikia lengo la asilimia 30 ya Watanzania kupata umeme mwaka 2015 ni jambo la uhakika kabisa sasa. Tena kuna uwezekano mkubwa wa kulivuka lengo hilo.

Ushirikiano wa Kanda
Watanzania Wenzangu;
Katika mwaka 2013, nchi yetu imeendelea kushiriki vizuri katika shughuli za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambazo sisi ni wanachama.   Mwezi wa Agosti, 2013 tulikabidhi Uenyekiti wa chombo cha SADC kinachoshughulikia Siasa, Ulinzi na Usalama kwa Namibia. Tulikuwa tumemaliza kipindi chetu cha mwaka mmoja.
Katika kipindi chetu cha uongozi tulishiriki kwa ukamilifu kutafuta suluhu kwa mizozo na migogoro ya kisiasa na kiusalama nchini Zimbabwe, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Madagascar.  Tunafurahi kuona kwamba mambo katika nchi zote hizo sasa yanakwenda vizuri. Nchini Zimbabwe utulivu umerejea baada ya kufanyika kwa uchaguzi mwezi Julai, 2013. Nchi ya Madagascar nayo imemaliza duru ya pili ya uchaguzi wa Rais kwa usalama. Matokeo yanatarajiwa kutangazwa tarehe 7 Januari, 2014.  Ni matumaini yetu kuwa watu wa nchi hiyo watayapokea matokeo hayo na wataelekeza nguvu zao katika kujenga umoja na maridhiano ili wajenge upya uchumi wa nchi yao.
Kwa upande wa Mashariki ya Kongo, tishio kubwa la  usalama kutokana na vitendo vya kundi la waasi la M23 limezimwa na Jeshi la Kongo kwa kushirikiana na Jeshi la Umoja wa Mataifa.  Kama mjuavyo Tanzania ni moja ya nchi zinazochangia maafisa na askari wa Jeshi hilo.

Ndugu Wananchi;
Napenda kutumia nafasi hii, kwa mara nyingine tena kutoa pongezi zangu za dhati kwa wanajeshi wetu kwa kazi yao nzuri na iliyotukuka waliyoifanya huko Mashariki ya Kongo. Pia nawapongeza wanajeshi wetu walioko Darfur na Lebanon kwa kazi yao njema waifanyayo. Wote nawaomba waendelee kudumisha nidhamu na weledi, mambo yaliyowafanya wapewe sifa nyingi na kuheshimiwa. Wameiletea nchi yetu heshima kubwa.
Bahati mbaya, katika kutimiza wajibu wao huo wa kimataifa tumepoteza vijana wetu 10, saba Darfur na watatu Kongo.    Narudia kutoa pole kwa Jeshi letu na familia za marehemu kwa msiba mkubwa uliowakuta.  Napenda kuwahakikishia kuwa daima tutauthamini na kuuenzi mchango wao.  Wanajeshi wote tunawatakia heri na fanaka tele katika mwaka 2014.

Jumuiya ya Afrika Mashariki
Ndugu Wananchi;
Mwaka huu, ushiriki wetu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki umepita katika mtihani kidogo kufuatia ndugu zetu wa Uganda, Rwanda na Kenya kufanya mambo ambayo yalijenga hisia ya kuwepo mifarakano.  Pia yalileta hofu kuwa hata uhai wa Jumuiya yenyewe ulikuwa mashakani.  Katika mkutano uliopita wa Wakuu wa Nchi wanachama wa Jumuiya uliofanyika tarehe 30 Novemba, 2013 mambo hayo tuliyazungumza kwa uwazi na kidugu.  Tumeelewana kuwa yaliyopita si ndwele tugange yajayo.

Ndugu Wananchi;
Katika mkutano wa Kampala tuliamua mambo matatu makubwa na muhimu katika kuendeleza agenda ya utangamano wa Afrika Mashariki. La kwanza,  tulikubaliana kuhusu Itifaki ya kuanzisha Umoja wa Fedha wa Afrika Mashariki na kutia saini.  Hii ndiyo hatua ya juu ya utangamano wa kiuchumi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.  Tumekuwa tunashirikiana katika kuwianisha sera za uchumi, fedha na bajeti, kwa uamuzi huu sasa tunaelekea kwenye kuwa na sera moja ya fedha na bajeti kwa mambo hayo na hatimaye sarafu moja.  Baada ya hatua hii, inayofuata ni ile ya utangamano wa kisiasa, yaani Shirikisho la Kisiasa.  Katika mkutano wetu wa Kampala tulikubaliana kuwa nchi wanachama ambazo hazijakamilisha kutoa maoni yao, zifanye hivyo kisha baada ya hapo tuzungumzie jambo hilo na kulipa mwelekeo.

Ndugu Wananchi;
Vilevile katika kikao chetu cha Kampala, tuliridhia mpango wa utekelezaji wa uamuzi wetu wa awali wa kuanzisha Himaya Moja ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.  Lengo la mfumo au utaratibu huu ni kufanikisha utekelezaji wa malengo na madhumuni ya Umoja wa Forodha wa Afrika Mashariki.  Utaratibu huu utarahisisha na kuharakisha uingizaji na utoaji wa bidhaa katika bandari na mipaka ya nchi za Afrika Mashariki. Pia, utaondoa vikwazo visivyokuwa vya kodi katika uingizaji na usafirishaji wa bidhaa kutoka nchi wanachama kwenda nchi nyingine. Kwa jumla, Himaya Moja ya Forodha itasaidia biashara kukua na hivyo uchumi wa nchi wanachama kukua na kuboresha ustawi wa wananchi wa Afrika Mashariki.
 Narudia kuwakumbusha wenzetu wa Wizara ya Afrika Mashariki na Wizara ya Fedha kutengeneza utaratibu mzuri wa kuelimisha jamii kuhusu Umoja wa Fedha na Himaya Moja ya Forodha.  Nawataka Wizara ya Fedha, Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Afrika Mashariki, Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Uchukuzi, Mamlaka ya Bandari, Mamlaka ya Mapato na Jeshi la Polisi, kuhakikisha kuwa taratibu zote husika kuhusu Himaya Moja ya Forodha zinakamilishwa mapema.  Nia yangu na yetu sote ni kuona utekelezaji unaanza mara moja.  Hili ni jambo lenye maslahi makubwa kwa nchi yetu.

Medani za Kimataifa
Ndugu Wananchi;
Katika medani za kimataifa, mwaka 2013 ulikuwa mzuri kwa Tanzania. Nyota ya nchi yetu iliendelea kuangaza vizuri. Tumeendelea kuwa na uhusiano mwema na mataifa yote duniani  na hakuna nchi ambayo tuna uadui nayo. Pia tuna uhusiano mzuri na mashirika  ya kimataifa na kikanda yanayoshughulikia masula ya siasa, fedha na maendeleo.  Vile vile, tuna uhusiano mzuri na watu mashuhuri na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yanayoshughulikia masuala ya maendeleo na ya kibinadamu.
Kwa sababu hiyo tumepata misaada mingi ya maendeleo na ya kibinadamu iliyochangia katika mafanikio tuliyoyapata katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii mwaka 2013.  Napenda kwa niaba yenu nitumie nafasi hii kutoa shukrani zangu za dhati kwa nchi, mashirika na watu waliochangia katika maendeleo ya nchi yetu mwaka huu. Wakati tukiwashukuru, napenda kuwakumbusha kuwa misaada yao bado tunaihitaji mwaka ujao (2014) na miaka inayofuatia.

Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa wageni, mwaka huu ulikuwa wa baraka sana kwa Tanzania.  Tumepata heshima ya aina yake ya kutembelewa na Rais wa China, Mheshimiwa Xi Jiping tarehe 24 – 25 Machi, 2013 na Rais wa Marekani Mheshimiwa Barack Obama tarehe 01 - 02 Julai, 2013.  Pia tulitembelewa na Rais wa Sri Lanka Mheshimiwa Mahinda Rajapaksa tarehe 26 – 27 Juni, 2013.  Waziri Mkuu wa Thailand, Mheshimiwa Yingluck Shinawatra tarehe 30 Julai mpaka Agosti 1, 2013 Pamoja na hao, tulipokea Wakuu wa Nchi na Serikali 19 waliokuja kushiriki mkutano wa Smart Partnership Dialogue uliofanyika Dar es Salaam tarehe 28 Juni, 2013.

Ndugu Wananchi;
Vilevile, tulitembelewa na Marais Wastaafu wa Marekani, Mheshimiwa Bill Clinton na Mheshimiwa George W. Bush.  Nchi yetu inanufaika na misaada inayotolewa na mashirika yao katika nyanja za afya na kilimo.  Napenda kutumia nafasi hii kuwashukuru wageni wetu wote hao kwa uamuzi wao wa kuja kututembelea.  Wameipa nchi yetu heshima kubwa.  Ni matumaini yetu kuwa mwaka 2014 utaendelea kuwa wa baraka kama huu tunaoumaliza leo. Pia nawashukuru sana Watanzania wenzangu kwa kuwapokea vizuri wageni wetu.  Wameondoka nchini wakiwa na furaha kubwa na kumbukumbu nzuri kuhusu nchi yetu.
Licha ya kutembelewa, mimi na viongozi wenzangu Wakuu wa Nchi yetu tulialikwa na kufanya ziara katika nchi mbalimbali duniani.  Pia tumeshirikishwa katika mikutano mbalimbali ya kimataifa.   Ziara hizo zimekuwa na manufaa makubwa kwa nchi yetu.

Ndugu Wananchi;
Katika kikao cha Wakuu wa Nchi wa Umoja wa Afrika kilichofanyia mwezi Januari, 2013 nilichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Wakuu wa Nchi za Afrika ya kushughulikia masuala ya mabadiliko ya tabia nchi.  Mwenyekiti wa Kamati hiyo ndiye huwa mwakilishi na msemaji wa Bara la Afrika katika majukwaa ya kimataifa ambapo masuala hayo yanazungumzwa au kushughulikiwa.
Kwa ajili hiyo nilikwenda Warsaw, Poland kuhudhuria Mkutano Mkuu wa 19 wa Mabadiliko ya Tabia Nchi uliofanyika tarehe 11 – 22 Novemba, 2013.  Katika mkutano huo hatukufanikiwa vya kutosha. Hivi sasa matumaini yetu yapo katika mkutano wa mwakani (2014) nchini Peru.  Iwapo tutafanikiwa tutakuwa tumejenga msingi mzuri utakaowezesha Mkutano wa Paris mwaka 2015 kufanikiwa kupatikana Mkataba wa Kimataifa unaozifanya nchi ziwajibike kisheria kwa masuala yahusuyo kupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi.  Ikishindikana Peru na kama mataifa yataendelea kukaidi katika mkutano wa Paris, hatma ya dunia yetu itakuwa mashakani kwani hali si nzuri hata kidogo.

Ndugu Wananchi;
Mwaka huu tunaoumaliza nchi za SADC tumepoteza mmoja wa viongozi wetu mashuhuri, shujaa Nelson Mandela.  Nilipata nafasi ya kuwawakilisha katika sala ya kitaifa, kutoa heshima za mwisho na mazishi yake. Kule Qunu, nilipewa nafasi ya kuzungumza ambayo niliitumia kuelezea uhusiano wetu na shujaa Mandela, ANC na mchango wa Tanzania kwa ukombozi wa kusini mwa Afrika.  Hotuba yetu ilipokelewa vizuri sana na wenyeji kwani niliwaelezea baadhi ya mambo ambayo walikuwa hawayajui.  Watu wengi wa Afrika Kusini na duniani kwa jumla sasa wanaufahamu vizuri mchango mkubwa wa nchi yetu kwa ukombozi wa Afrika Kusini.  Tuendelee kumuomba Mwenyezi Mungu ailaze mahala pema, peponi roho ya shujaa Nelson Mandela.

Miaka 50 ya Mapinduzi na Muungano
Ndugu Wananchi;
Mwaka ujao (2014) ni wa aina yake katika historia ya nchi yetu.  Ni mwaka ambao tunatimiza miaka 50 tangu Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Januari 12,1964 na miaka 50  ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika ziungane na kuzaliwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Aprili 26, 1964. Ni mwaka wa kutambua na kusheherekea mafanikio tuliyoyapata.  Lakini, ni mwaka wa kuweka nadhiri ya kupata mafanikio makubwa zaidi miaka 50 ijayo na kuendelea. Tutakiane heri katika kusheherekea siku hizo adhimu.

Shukurani
Ndugu Wananchi;
Napenda kuchukua nafasi hii adhimu kuwashukuru kwa dhati Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Pinda, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Balozi Seif Ali Idd.  Viongozi Wakuu wenzangu hao nawashukuru kwa msaada mkubwa walionipa na wanaoendelea kunipa katika kuiongoza nchi yetu mwaka 2013. Naomba tuendelee hivyo mwaka 2014 kwa maslahi ya nchi yetu na watu wake.
Nawashukuru pia Mawaziri na viongozi wengine wa Serikali zetu mbili kwa kazi nzuri waliyofanya ya kuongoza na kusimamia utekelezaji wa miradi na shughuli mbalimbali za Serikali.  Kazi yao nzuri ndiyo iliyotupatia mafanikio tunaojivunia leo. Naomba sote tutambue kuwa bado zipo mbele yetu kazi nyingi na changamoto kubwa na nzito za kushughulikia katika jitihada zetu za kuwaletea wananchi na nchi yetu maendeleo.  Tunao wajibu wa kudumisha umoja, mshikamano, amani na utulivu wa nchi yetu.  Hatuna budi kuendelea kushirikiana na kusaidiana pamoja na kufanya kazi kwa bidii zaidi mwaka ujao 2014 kwa niaba na kwa maslahi ya watu waliotuchagua.

Ndugu Wananchi;
Kwa namna ya pekee nawashukuru sana Watanzania wote po pote pale walipo kwa kuunga mkono juhudi za Serikali na kufanya kazi kwa bidii na maarifa kujiletea maendeleo.  Hali kadhalika nawapongeza kwa uelewa wenu ulioiwezesha nchi yetu kuendelea kuwa kisiwa cha amani. Nawaomba tuendelee na moyo huo wa kuipenda nchi yetu na kujitolea kwa ajili ya utulivu wake na maendeleo yake na yetu sote.
Naomba pia nimalize kwa kuwashukuru viongozi wetu wa dini wa madhehebu mbalimbali pamoja na waumini wao kwa sala na maombi katika kipindi chote cha mwaka unaoisha leo. Sala zao na maombi yao yametupa nguvu na faraja katika vipindi vigumu ambavyo tumevipitia. Naomba muendelee kuliombea taifa letu ili lipate baraka na neema ya Mwenyezi Mungu.

Mwisho
 Ndugu Wananchi;
Naomba tuzidi kuombeana heri ili mwaka ujao uwe wa baraka na  mafanikio makubwa zaidi. Twendeni tukasherehekee mwaka mpya kwa amani na utulivu. Nawatakia heri na fanaka tele katika  mwaka mpya wa 2014.
Mungu Ibariki Tanzania,
Mungu Ibariki Afrika.
Asanteni sana kwa kunisikiliza.

HOTUBA YA MHESHIMIWA MIZENGO P. PINDA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA KUHITIMISHA SHUGHULI ZA MKUTANO WA 14 WA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA TAREHE 21 DESEMBA, 2013

I:    UTANGULIZI 
    Masuala ya Jumla

Mheshimiwa Spika,
Ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu mwenye wingi wa Rehema kwa kutufikisha salama siku ya leo. Tumekuwepo hapa Dodoma kwa takriban siku 15 za kazi ambapo tumeweza kutekeleza majukumu na kazi za Mkutano wa 14 wa Bunge lako Tukufu ambapo tunahitimisha shughuli zilizopangwa hivi leo.

Mheshimiwa Spika,
Nitumie nafasi hii ya mwanzo kabisa kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa Dkt. Asha Rose Migiro, (Mb.) kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais kuwa Mbunge katika Bunge lako Tukufu.  Wengi wetu tunafahamu uwezo mkubwa wa Dkt. Asha Rose Migiro na bila shaka ndiyo sababu Mheshimiwa Rais alifanya uamuzi wa kumteua kuwa Mbunge kwa kuzingatia sifa nzuri alizonazo. Pamoja na kumpongeza napenda kumtakia kazi njema ndani na nje ya Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Spika,
Tangu Mkutano wa 13 wa Bunge baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wamepotelewa na Ndugu, Jamaa na Marafiki.  Napenda kutumia fursa hii kuwapa pole wote waliofikwa na misiba hiyo. Lakini katika Mkutano huu, Waheshimiwa Wabunge walipata fursa ya kujadili Azimio la Bunge kuhusu kuungana na Nchi ya Afrika Kusini, katika kuombeleza kifo cha Muasisi, Mpinga ubaguzi wa rangi, Rais wa Kwanza Mweusi wa Afrika Kusini, Hayati Nelson Madiba Mandela kilichotokea tarehe 5 Desemba 2013.  Wote tunakubaliana kwamba huu ni msiba Mkubwa kwa Dunia nzima na hasa kwa wale wanaomfahamu Mzee Mandela na historia yake. 

Aidha, nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutuwakilisha vyema Watanzania wote katika msiba huu mkubwa wa Afrika na Dunia nzima.  Hotuba ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa wakati wa mazishi ya Hayati Nelson Mandela tarehe 15 Desemba, 2013 pale Qunu ilitosha kabisa kuitangaza Tanzania Dunia nzima katika ushiriki wake kwenye harakati za ukombozi Barani Afrika katika Karne ya 20.  Ninaamini kwamba hiyo ni Historia ambayo haitafutika vizazi vingi vijavyo. Tutaendelea kumuenzi Mzee Mandela kwa kuiga na kufuata nyayo zake.

Maswali
Mheshimiwa Spika,
Katika Mkutano huu, Waheshimiwa Wabunge waliweza kuuliza maswali ya msingi 170 na ya nyongeza 458 ambayo yote yalijibiwa na Serikali.  Aidha, maswali 17 ya msingi na 15 ya nyongeza yalijibiwa kwa utaratibu wa Maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu. Niwapongeze Waheshimiwa Wabunge wote kwa kuuliza maswali mazuri na Waheshimiwa Mawaziri kutoa majibu ya maswali hayo kwa umahiri mkubwa.


Mheshimiwa Spika,
 Pamoja na shughuli hizo za kawaida, Bunge lako lilikamilisha kazi kubwa zifuatazo:

Kwanza: Bunge lilijadili na kukamilisha Muswada wa Sheria ya Kura ya Maoni wa mwaka 2013. [The Referendum Bill, 2013];

Pili:     Kujadili Taarifa Mbili (2) za Kamati za Kudumu za Bunge za Sekta Mtambuka.

Tatu:    Kujadili Taarifa Mbili (2) za Kamati za Kudumu za Bunge zinazosimamia Fedha za Umma; na

Nne:    Kujadili Taarifa Tisa (9) za Kamati za Bunge za Kisekta.

Aidha, Bunge lako Tukufu lilijadili kwa utaratibu wa Hati ya Dharura Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Ushuru wa Bidhaa wa Mwaka 2013 [The Excise (Management and Tariff) (Amendment) Bill, 2013]. Mwisho Muswada wa Sheria ya Baraza la Vijana la Taifa wa mwaka 2013 ulisomwa kwa mara ya kwanza.

Nitumie nafasi hii kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa kujadili Taarifa hizo na kutoa maoni na ushauri kwa uwazi mkubwa na kwa kina. Mapendekezo na ushauri uliotolewa na Waheshimiwa Wabunge umepokelewa na Serikali na utazingatiwa kwa uzito unaostahili.

II:    KILIMO
Hali ya chakula Nchini
Mheshimiwa Spika,
Kama nilivyoeleza katika Mkutano wa Bunge wa 13, hali ya upatikanaji wa Chakula Nchini kwa ujumla imeendelea kuwa ya kuridhisha katika maeneo mengi kufuatia mavuno mazuri ya msimu wa Kilimo wa 2012/2013 katika maeneo mbalimbali hapa Nchini. Tathmini ya chakula na lishe iliyofanyika mwezi Oktoba na Novemba, 2013 katika maeneo yenye matatizo ya usalama wa chakula na lishe inaonesha kuwa jumla ya Watu 828,063 wanakabiliwa na upungufu wa chakula na watahitaji msaada wa chakula wa Tani 23,312 hadi ifikapo mwezi Februari 2014. Aidha, kati ya mwezi Julai na Novemba 2013, Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ulitenga jumla ya Tani 16,119 za chakula cha mgao kwa Halmashauri zenye mahitaji ya chakula cha msaada. Hadi kufikia tarehe 16 Disemba 2013, jumla ya Tani 13,716 zilikwishachukuliwa na Halmashauri husika. Tani 2,402 zilikuwa hazijachukuliwa na Halmashauri za Mwanga, Babati, Igunga, Mpwapwa na Manyoni.

Ninawaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya ambazo hazijachukua chakula hicho kufanya hivyo kabla ya tarehe 15 Januari 2014. Ambao hawatatekeleza maagizo haya watachukuliwa hatua za kisheria. Nitumie nafasi hii kuwahakikishia Wananchi kuwa Serikali itaendelea kusimamia upatikanaji wa chakula katika Halmashauri zenye hali tete ya chakula kwa lengo la kubainisha idadi ya watu wenye uhaba wa chakula.

Mwenendo wa Bei za Vyakula Nchini
Mheshimiwa Spika,
Kutokana na miezi hii kuwa katika kipindi cha mwisho wa msimu wa ununuzi wa mazao, kiasi cha mazao yanayoingia sokoni kimeanza kupungua. Hali hii imesababisha bei za wastani za vyakula hasa mahindi na mchele katika soko hapa Nchini kuanza kupanda ingawaje si kwa kiasi kikubwa. Kwa mfano, bei ya mahindi Kitaifa imepanda kutoka Shilingi 536.86 kwa kilo mwezi Oktoba, 2013 hadi kufikia Shilingi 538.26 kwa kilo mwezi Novemba, 2013. Kwa upande wa Mchele, bei ya wastani wa Kitaifa imepanda kutoka Shilingi 1,188.60 kwa kilo mwezi Oktoba, 2013 hadi Shilingi 1,191.10 kwa kilo mwezi Novemba, 2013.

 Pamoja na kuwepo kwa hali ya kupanda kwa bei, bado bei za sasa kwa baadhi ya mazao mfano mahindi, mchele, maharage na viazi ziko chini ikilinganishwa na zile za kipindi kama hiki mwaka jana. Natoa wito kwa Wakuu wa Mikoa yenye mavuno mazuri kuendelea kuwahamasisha wakulima kuhifadhi chakula cha kutosha kwa mahitaji ya Kaya zao na kuuza ziada katika Soko ili kusaidia kupunguza bei ya vyakula katika miji yetu. Halmashauri zihakikishe kuwa zinathibiti ununuzi holela wa chakula kutoka mashambani na majumbani mwa Wakulima kwa lengo la kujihakikishia upatikanaji wa chakula cha kutosha.

Hali ya Ununuzi na Akiba ya Chakula ya Taifa

Mheshimiwa Spika,
Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula ilipanga kununua Tani 250,000 za nafaka. Wakala umeendelea na kazi hiyo na hadi kufikia tarehe 11 Desemba, 2013, Wakala ulikuwa umekwishanunua kiasi cha Tani 218,499 za nafaka sawa na Asilimia 87.4 ya kiasi kilichopangwa kununuliwa. Aidha, hadi kufikia tarehe 16 Desemba, 2013, Maghala ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula yalikuwa na akiba ya jumla ya Tani 233,808 za nafaka.  Kati ya hizo, Tani 233,315 ni za Mahindi na Tani 493 ni za Mtama.

Wakati huo huo, Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula unaendelea kuhamisha chakula kutoka katika maghala yake yaliyoko katika Mikoa iliyozalisha ziada kwenda kwenye maghala yaliyoko kwenye Mikoa yenye upungufu wa chakula ili kukabiliana na mahitaji ya chakula cha msaada kitakachohitajika kusambazwa kwa walengwa. Hadi kufikia tarehe 9 Desemba, 2013, jumla ya Tani 44,129 za Mahindi zimekwishahamishwa. Serikali inaendelea kuhamasisha wafanyabiashara kununua chakula katika Mikoa yenye ziada ya chakula na kukipeleka katika Mikoa yenye upungufu wa chakula.

Hali Halisi ya Usambazaji wa Pembejeo
Mheshimiwa Spika,
Kama nilivyoeleza katika Mkutano wa 13 wa Bunge, Serikali ilichapisha jumla ya vocha 2,796,300, kwa ajili ya pembejeo za Kilimo kwa msimu wa Kilimo wa 2013/2014. Hadi kufikia tarehe 12 Desemba, 2013, Tani 74,925 sawa na Asilimia 96 za mbolea ya kupandia na Tani 42,295 sawa na Asilimia 91 ya mbolea ya kukuzia zilikuwa zimekwishafikishwa katika Mikoa husika kulingana  na  aina  ya  mazao  yanayohitaji  mbolea  hizo. Aidha, Maghala ya Wakala wa Mbolea Jijini Dar es Salaam yana akiba ya kutosha ya mbolea hiyo. Nirejee kutoa wito kwa Wakuu wote wa Mikoa kuhakikisha kuwa vocha zote zinatolewa kwa walengwa kwa wakati sambamba na aina ya pembejeo inayomlenga Mkulima husika kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa.Malipo ya Madeni ya Wakulima ya Mahindi.

Mheshimiwa Spika,
Katika mwaka wa 2013/2014, Serikali ilitenga jumla ya Shilingi Bilioni 109.6 kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kwa ajili ya kununua Tani 250,000 za nafaka. Hadi  kufikia  tarehe  19  Desemba, 2013 NFRA ilikuwa imenunua  jumla  ya Tani 218,499  zenye  thamani  ya Shilingi Bilioni 109.25 na  kwa ajili hiyo. Kutokana na Serikali kutoa bei nzuri ya wastani wa Shilingi 500/= kwa kilo ya mahindi, zoezi hilo lilikuwa na matokeo mazuri katika msimu huu kulinganisha na miaka iliyopita na liliwavuta Wananchi wengi kupeleka nafaka katika Vituo vya kununulia nafaka. Hadi sasa Serikali imeshatoa Shilingi Bilioni 100.6 kwa ajili ya zoezi hilo na imehakikisha kuwa wananchi wote waliouza nafaka zao kwa NFRA wamelipwa fedha zao. Aidha, natambua kuwa NFRA ilitumia baadhi ya Wakala kukusanya nafaka hiyo kutoka kwa Wakulima na kama nilivyosema katika Mkutano wa 13 wa Bunge, Serikali inatambua kuwa Wakala hao kutoka Mikoa ya Arusha, Dodoma, Njombe, Shinyanga, Ruvuma, Rukwa na Tanga wanaidai Serikali jumla ya Shilingi Bilioni 8.65 Niwaombe Wakala wote wanaoidai Serikali kuendelea kuwa na subira wakati Serikali inaendelea na utaratibu wa kulipa deni hilo kwa vile kiasi cha deni lao lipo ndani ya bajeti iliyotengwa kwa ajili ununuzi wa nafaka katika mwaka wa fedha wa 2013/2014.

III:    MPANGO WA HUDUMA JUMUISHI ZA KIFEDHA

Mheshimiwa Spika,
Tarehe 12 Desemba, 2013 Serikali ilizindua Mpango wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Kifedha (yaani National Financial Inclusion Framework). Uzinduzi wa Mpango huu ulifanywa na Malkia wa Uholanzi Mheshimiwa Máxima Zorreguieta Cerruti ambaye pia ni Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Mpango wa Huduma Jumuishi za Kifedha na kushuhudiwa na Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal na Wawakilishi wa Taasisi za Umoja wa Mataifa.
Mheshimiwa Spika,
Lengo la Mpango huo ni kusimamia ukuzaji wa huduma za kifedha kwa jamii Nchini na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazoikabili Sekta ya Fedha. Vilevile, Mpango unalenga kusogeza huduma karibu kwa jamii pana zaidi ya Watanzania kwa kutumia mifumo ya Teknolojia mbalimbali katika kufikisha huduma  za  kifedha  kwa Wananchi na hasa Wakulima, Wafugaji na Wavuvi waliopo Vijijini ambao wengi wao wako nje ya mfumo rasmi wa kifedha.  Teknolojia hizo ni pamoja na:
Huduma za Kibenki za moja kwa moja na kupitia Wakala (Agent Banking);
Huduma za kifedha kupitia Mitandao mbalimbali kama vile M-PESA, TIGO PESA, AIRTEL MONEY na Easy PESA.
Vituo vya malipo kwa kutumia Wakala (Point of Sales – POS).
Aidha, Mpango huu utaweka mazingira linganifu na yaliyo bora kwa kutumia Sayansi na Teknolojia kutekeleza Sera ya Fedha kwa ufanisi, kuimarisha Sekta ya Fedha katika Pato la Taifa na Kukuza Uchumi kwa ujumla. Mpango huu pia utawezesha kuongeza kasi ya upatikanaji wa Chakula, masuala ya Lishe na Maendeleo Vijijini kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika,
Utafiti uliofanywa na Benki ya Dunia katika Nchi mbalimbali Barani Afrika unaonesha kuwa Watu wanaonufaika na Mfumo rasmi wa Taasisi za Kifedha ni Asilimia 24 tu. Kwa upande wa Tanzania, Wananchi waliopo kwenye Mfumo rasmi wa Asasi za Kifedha ikijumuisha wale waliojiunga na Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo (SACCOs) ni Asilimia 22.  Asilimia 78 ya Watanzania wapo nje ya Mfumo wa Kifedha na wengi wao ni kutoka Vijijini hasa Wakulima wadogo. Mpango huu wa Huduma Jumuishi za Kifedha unalenga kufikia Asilimia 50 ya Watu wazima wanaotumia huduma rasmi za kifedha ifikapo mwaka 2016.
Mheshimiwa Spika,
Kiwango hiki kidogo cha Wananchi walio katika Mfumo rasmi wa huduma za kifedha unatokana na changamoto zifuatazo:
Moja:    Miundombinu ya kuanzisha huduma za Kifedha Vijijini ni hafifu hususan barabara, mawasiliano, makazi na huduma za kiusalama;
Mbili:    Wananchi wengi wa Vijijini bado hawajahamasishwa kutambua umuhimu na faida ya huduma za kifedha.  Aidha, utamaduni wa kujiwekea akiba na kukopa ni mdogo; na.
Tatu:    Taasisi nyingi za kifedha zinaogopa kwamba Wananchi wengi wa Vijijini ambao ni Wakulima hawana fedha za kutosha kuweza kuweka akiba katika Taasisi hizo na uwezo wao wa kukopa mikopo ni mdogo, hivyo wakipeleka huduma zao huko hawatapata faida.
Mheshimiwa Spika,
Zipo faida nyingi za kueneza Huduma Jumuishi za Kifedha kwa Wananchi wengi wa Vijijini hasa Wakulima.  Miongoni mwa faida hizo ni pamoja na:
Moja:    Kuwezesha Wananchi kujiwekea Akiba na pia kupata mikopo ya kuwawezesha kuanzisha miradi ya maendeleo na shughuli nyingine za kijamii hivyo kujiongezea kipato na kuondoa umaskini;

Mbili:    Huduma za Kifedha Vijijini zinawawezesha Wananchi wengi hasa Wakulima kupata mikopo ya pembejeo na mikopo ya ununuzi wa mazao;

Tatu:    Huduma za Kifedha Vijijini ni Mkombozi wa Makundi maalum kama vile Vijana, Wanawake, Wazee, na Walemavu. Aidha, zinasaidia Wananchi kujiongezea kipato, kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao ya Kilimo na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na ufugaji nyuki; na

Nne:    Kuwepo kwa Huduma za Kifedha Vijijini kunaongeza Usalama wa Chakula, kulinda mazingira na kufanya Vijiji kuwa ni sehemu nzuri ya kuishi.

Mheshimiwa Spika,
Serikali imeonesha juhudi kubwa katika kuanzisha Huduma Jumuishi za Kifedha Nchini kwa mfano tumeweza kuanzisha Benki nyingi Nchini.  Tayari tunazo Benki takriban 52 zenye matawi zaidi ya 609 kote Nchini.  Lakini pia tunazo huduma za Bima kwa Makampuni Binafsi zaidi ya 27 na Mawakala wa Bima takriban 600.  Ipo Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya Umma 5, Masoko ya Mitaji na Vikundi na Taasisi ndogondogo za Fedha (SACCOS) takriban 5,600.

Aidha tunazo huduma za Kifedha kwa kutumia Huduma za Kifedha kupitia mtandao (PESA – MTANDAO) na Vituo vya malipo kwa kutumia Wakala (POINTS OF SALES – POS). Inakadiriwa kuna Mawakala na Vituo zaidi ya 55,000 ambapo Waajiriwa wa moja kwa Moja (Direct Employment) wanakadiriwa kufika takriban 100,000.

Mheshimiwa Spika,
Maisha bora kwa kila Mtanzania ni pamoja na kutumia Teknolojia na kurahisisha maisha.  Kwa mfano, huduma za M-PESA peke yake zinawezesha malipo kwenye biashara mbalimbali zaidi ya aina 300 ikiwemo manunuzi kwenye Supermarket na maduka ya kawaida. Huduma hizo ambazo zinatolewa pia kwa njia ya TIGOPESA, AIRTEL MONEY, EASY PESA zinaweza kulipia Luku, Ada za shule na Vyuo, Tiketi za ndege, kufanya marejesho Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, n.k. Aidha, baadhi ya Makampuni haya yameunganisha huduma zao na Benki zaidi ya 20 ikiwemo CRDB, NMB, Benki ya Posta, Standard Chartered, Amana Bank na Diamond Trust Bank (DTB). Vilevile, kwa kutumia huduma za jumuishi za kifedha mteja anaweza kuhamisha fedha kutoka Akaunti ya Benki kwenda M- PESA, TIGO PESA n.k. halafu akazitoa kupitia Wakala.  Kwa sasa Watumishi walio Vijijini hawana tena sababu ya kufunga Ofisi kufuata mishahara Benki bali kupitia huduma hizi za Kifedha na wanaweza kutoa pesa kupitia Wakala, na kwa kufanya hivyo ufanisi na tija kwa Watumishi unaongezaka.

Mheshimiwa Spika,
Ni kweli kwamba tunayo kazi kubwa ya kutekeleza Dhana ya Huduma Jumuishi za Kifedha Nchini.  Lakini ni ukweli kuwa Uzinduzi wa Mpango wa Kitaifa wa Huduma Jumuishi za Kifedha una  manufaa makubwa na mengi ikiwemo kuongeza kasi ya Kukuza Uchumi na Kuondoa Umaskini  kwa kupeleka maendeleo Vijijini, kuongeza Akiba ya Chakula na pia kufikia malengo ya Milenia.  Ni matumaini yangu kwamba uzinduzi wa Mpango huu utatuwezesha kusonga mbele kwa kasi kubwa zaidi.  Natoa wito kwa Mabenki, Taasisi za Kifedha na Vituo vya Kifedha kupitia mitandao (PESA MTANDAO) na Vituo vya malipo kwa kutumia Wakala kuongeza jitihada katika kusambaza huduma za Kifedha Vijijini ambako ndiko kwenye kundi kubwa la Wananchi wanaohitaji huduma hiyo. 

IV:    NISHATI NA MADINI

Mradi wa Gesi
Mheshimiwa Spika,
Kama ambavyo Wananchi wengi wanafahamu, Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) inaendelea kutekeleza mradi wa ujenzi wa mitambo ya kusafishia Gesi  Asilia  katika  maeneo  ya  Madimba, Mtwara Vijijini na Songo  Songo  Wilayani  Kilwa. Pia ujenzi wa Bomba la kusafirishia Gesi hiyo kutoka Mtwara na Songo Songo hadi Dar es Salaam unaendelea vizuri. Mradi huu utakapokamilika utaunganisha maeneo yanayozalisha Gesi Asilia hususan Mnazi Bay-Mtwara, Songo Songo, Kisiwani, Mkuranga, Ntorya na maeneo yaliyogunduliwa Gesi katika eneo la bahari ya kina kirefu. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa Gesi Asilia mbali na matumizi mengine, inatumika katika kuzalisha umeme ambao kwa sasa Asilimia kubwa unazalishwa kwa kutumia nishati ya mafuta yanayoingizwa kutoka Nchi za nje na hivyo kuligharimu Taifa kiasi kikubwa cha fedha za kigeni.Mheshimiwa Spika,
Katika utekelezaji wa mradi huu, Kazi zifuatazo zimekamilika hadi kufikia tarehe 30 Novemba, 2013:

Moja:    Kukamilika kwa upakuaji wa Shehena ya Sita (6) ya Mabomba ya Mradi yapatayo 4,444 ya umbali wa Kilomita 51.169 katika Bandari ya Mtwara. Jumla ya mabomba yaliyowasili Nchini hadi Novemba, 2013 ni 24,935 ya umbali wa kilomita 295.5;

Pili:    Kusafisha Mkuza wa Mabomba, tayari Kilomita 498.5 zimekamilika;

Tatu:    Usafirishaji wa mabomba kutoka kwenye yadi za kuhifadhia na kuyasambaza kwenye Mkuza tayari kwa kuyaunganisha kwa kuchomelea. Hadi sasa mabomba ya Kilomita 186.9 yamekwishasafirishwa;

Nne:    Uchimbaji wa njia ya kuweka bomba, yenye umbali wa Kilomita 27.0 umekamilika;

Tano:    Uwekaji wa mabomba kwenye njia yake sambamba na kuweka Mkongo wa Mawasiliano (Fiber Optic Cable) umekamilika Kilomita 21.1;
Sita:    Kufukia bomba pamoja na Mkongo wa Mawasiliano. Tayari   Kilomita 7.30 za Bomba pamoja na Mkongo wa Mawasiliano zimefukiwa; na

Saba:    Utafiti wa njia ya Bomba la Baharini nao umekamilika.
Hayo ni maeneo machache ambayo nimeona niyataje.

Mheshimiwa Spika,
Ni kweli kwamba kazi za mradi huu ni kubwa lakini kwa ujumla zinaendelea vizuri na kwa kasi. Moja ya faida za mwanzo za mradi huu ambazo tumeziona ni pamoja na upatikanaji wa ajira kwa Wafanyakazi wa Mradi ambao sehemu kubwa ya ajira ni ushirikishwaji wa wazawa katika Mradi wa Gesi na Mafuta.  Kwa kuwa kazi za ujenzi wa mitambo na Bomba la Gesi ni za kitaalamu sana, malengo ya Shirika la Petroli Nchini (TPDC) ni kuajiri wafanyakazi Wakiwemo Wazawa mapema ili waweze kushiriki na kujifunza kwa vitendo shughuli zote  zinazohusiana na ujenzi wa  mitambo na Bomba la Gesi hatua kwa hatua, tangu mwanzo hadi mwisho wa ujenzi. Utaratibu huu utasaidia kupata wataalamu wazuri na wazoefu wa Kitanzania watakaoendesha (operations) na kufanya matengenezo (Maintenance) ya mitambo na Bomba la Gesi kwa kipindi chote cha matumizi.

Mheshimiwa Spika,
Vilevile moja ya makubaliano katika Mkataba wa utekelezaji wa Mradi huu, Mkandarasi anawajibika kuwapeleka Wafanyakazi kwenye mitambo na mabomba yanayofanya kazi  kwa sasa kwa kipindi kisichopungua mwezi mmoja  ili wajifunze pia kwa vitendo na kwa nadharia shughuli zote za kuendesha mitambo ya kusafisha Gesi Asilia na Bomba la Gesi. Malengo ya TPDC ni kuwapeleka wafanyakazi husika kwa awamu tofauti tofauti wakati wa kipindi cha ujenzi ili ikifika kipindi cha kukabidhi mradi Wafanyakazi wote wawe wamekwishapata uzoefu wa kutosha.

Mheshimiwa Spika, 
Kampuni nyingi zilizopo Mtwara zinazojishughulisha na mambo ya utafiti na uzalishaji wa Gesi na Viwanda vinavyohusiana na matumizi ya Gesi, zimekuwa zikisomesha na pia kuajiri wazawa. Kwa mfano, Mpango wa kujenga mitambo ya kutengeneza  Gesi kuwa kimiminika (LNG) wa Kampuni ya British  Gas  Tanzania  utakuwa  na  utengenezaji  wa ajira nyingi za kiwango kuanzia Kada ya Chini na Kada ya Kati ambayo  itasomesha Watanzania kupitia VETA katika fani mbalimbali. Wako watakaosomeshwa katika fani ya Vyuma, wengine ujenzi, uhandisi wa miundombinu na ufundi wa vyuma na umeme.

Katika Kada ya Kati, Kampuni ya Gesi Tanzania wanatarajiwa kusomesha wataalamu 16,756 waliofaulu vizuri masomo ya Kidato cha Nne. Takwimu zinaonesha kuwa kwa Mtwara tu, kumekuwapo ajira mpya 400, na Watanzania wanaotoa huduma mbalimbali kwenye Kampuni za Gesi na Mafuta ni sawa na Asilimia 70 ya watoa huduma hiyo Nchini.  Asilimia 30 iliyobaki ya watoa huduma inatolewa na Wageni.

Katika Kada za Juu, Kampuni itasomesha na kuajiri Wataalamu wa Jiolojia, Uhandisi, Kemia na Sayansi husika kwenye Gesi na Mafuta. Matokeo yameanza kuonekana ambapo jumla ya Wanafunzi wa VETA 370 wamesomeshwa kuhusu Gesi na Mafuta kwa kiwango cha cheti cha Kimataifa na Wanafunzi 12 wa Kada za Juu wamepata ufadhili na wanasomea fani za Gesi na Mafuta ndani na nje ya Nchi.

Mheshimiwa Spika,
Napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba Kampuni ya British Gas Tanzania wamegundua gesi kiasi cha Futi za Ujazo Trilioni 13. Katika kuandaa na kuendesha mradi wa uzalishaji Gesi nyingi kiasi hicho ni dhahiri kwamba ajira zitapatikana kwa maelfu ya Watanzania. Katika hatua ya ujenzi, mradi utatoa ajira kwa maelfu; na katika uzalishaji (operations) ajira nyingine zaidi kwa maelfu zitapatikana hapa Nchini, na katika mnyororo wa usambazaji ajira nyingi pia zitajitokeza. Nitumie fursa hii kuwapa Watanzania matumaini, kwamba Mradi wa Gesi Nchini una manufaa mengi sana, kuanzia upatikanaji wa Gesi na Ajira kwa Wazawa. Nawaomba Waheshimiwa Wabunge tuendelee kuwaelimisha Wananchi wetu kuhusu manufaa ya mradi huu katika Nchi yetu.  Ni fursa ya kipekee ambayo Wananchi wetu wanatakiwa wafaidike nayo katika kuwaletea maisha bora.

V:    MATUMIZI YA MASHINE ZA KIELEKTRONIKI (EFDs)

Mheshimiwa Spika,
Katika mwaka wa fedha wa 2013/2014, Serikali ililiarifu Bunge lako Tukufu kuhusu mikakati mbalimbali itakayotekelezwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa lengo la kuimarisha ukusanyaji wa Mapato ya Ndani. Moja ya hatua hizo muhimu ni kuendelea kuimarisha matumizi ya Mashine za Kielektroniki za kutoa Risiti (Electronic Fiscal Devices- EFDs). Mashine hizi zimeunganishwa kwa Mtandao wa Kompyuta moja kwa moja na Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa lengo la kuwezesha Serikali kupata mapato stahiki bila udanganyifu. Aidha, Mashine hizi zinasimamiwa kupitia Mtandao wa Kielektroniki ambapo hupeleka taarifa moja kwa moja kwenye Hifadhi Kuu ya Kumbukumbu za Mamlaka ya Mapato Tanzania kila siku.

Mheshimiwa Spika,
Katika utekelezaji wa zoezi hili kwa mwaka huu, Serikali imelenga kuingiza Walipa Kodi 200,000 kati ya 1,500,000 ili waweze kutumia Mashine za Kielektroniki. Walengwa wa utaratibu huu ni Wafanyabiashara wenye biashara kubwa zenye Mtaji wa kati ya Shilingi Milioni 14 na Shilingi Milioni 40. Katika zoezi hili, Wafanyabiashara Wadogo wanaoendesha biashara zisizo rasmi kama vile Wamachinga na wale wanaotembeza bidhaa barabarani na Mama Lishe hawahusiki na utaratibu huu hata kidogo.
Mheshimiwa Spika,
Katika utekelezaji wa zoezi hili kumejitokeza malalamiko kutoka kwa baadhi ya Wafanyabiashara Nchini hususan wa Mikoa ya Mbeya, Morogoro, Lindi na Dar es Salaam (Kariakoo) kuhusiana na bei na matumizi ya Mashine hizi. Malalamiko makubwa ya Wafanyabiashara hao ni kuhusu: Bei kubwa ya ununuzi wa Mashine za Kielektroniki; Bei kubwa ya Karatasi za kutolea Risiti; Mchakato uliotumika kununua Mashine za Kielektroniki; Walengwa wa kutumia Mashine hizo; na Gharama za matengenezo.

Mheshimiwa Spika,
Kwa kuzingatia maendeleo ya Sayansi na Teknolojia ya Mawasiliano ya Kisasa (ICT); Wataalam wanathibitisha kwamba, Mashine za Kielektroniki zinafanya kazi zifuatazo:
Moja:    Zinatoa Risiti na Ankara za Kodi kwa urahisi na Mfanyabiashara huondokana na adha ya kuchapisha au kununua vitabu vingi vya kuandikia risiti ambavyo utunzaji wa nakala zake unaleta usumbufu;

Pili:    Zina uwezo mkubwa wa kutunza kumbukumbu za mauzo, manunuzi na mali ya biashara (stock) bila kufutika kwa muda usiopungua miaka mitano;

Tatu:    Mtumiaji anaweza kutoa kwa urahisi taarifa za mauzo yake kwa siku, kwa wiki, kwa mwezi, kwa mwaka na kwa wakati wowote kwa kipindi kisichopungua miaka mitano;

Nne:    Humwezesha Mfanyabiashara kutuma taarifa zake za mauzo moja kwa moja kwenda Ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka nyingine zenye mahitaji ya taarifa hizo, kama vile Taasisi ya Taifa ya Takwimu, Benki Kuu, EWURA, na SUMATRA;

Tano:    Mashine zinaweza kupokea maelekezo moja kwa moja kutoka kwenye Mfumo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, na kumtaarifu Mfanyabiashara taarifa yoyote ya Kodi inayomhusu;

Sita:    Kutuma na kupokea fedha kwa njia ya “Mobile Money”. Utaratibu huu unamwezesha Mtumiaji kutumia Mashine hizi kulipia kodi na huduma nyingine moja kwa moja kama vile, Ankara za Umeme, Maji, Simu, n.k;

Nane:    Mashine za Kielektroniki zinatumia lugha ya Kiswahili na Kiingereza inayoeleweka kwa Wananchi wengi;

Tisa:    Mashine za Kielektroniki zinaiwezesha Mamlaka ya Mapato Tanzania kutambua mauzo sahihi ya Mfanyabishara na hivyo kuweza kutoza Kodi halali.

Mheshimiwa Spika,
Msingi wa bei ya kununulia Mashine hizi za Kielektroniki umezingatia pamoja na mambo mengine, manufaa na faida nyingi nilizozitaja kwa mtumiaji na ubora wa mashine zenyewe. Aidha, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania katika Nchi mbalimbali Duniani unaonesha kuwa mashine zenye ubora unaokidhi mahitaji niliyoyataja hapo juu zinauzwa na wasambazaji kwa kati ya Shilingi 600,000/= (Dola 375) hadi Shilingi 778,377/= (Dola 486) ikilinganishwa na bei za Mashine za Kielektroniki za Nchi nyingine zinazotumia mfumo unaofanana na wa Tanzania ambazo zinauzwa bei kubwa za kati ya Dola za Kimarekani 360 hadi 870. Pamoja na bei hizo, Mamlaka ya Mapato Tanzania inaendelea kujadiliana na Wasambazaji wa Mashine hizo ili kuona uwezekano wa kushusha bei hizo.

Mheshimiwa Spika,
Kuhusu bei za karatasi za kutolea Risiti uchunguzi unaonesha kuwa karatasi hizo zinauzwa kati ya Shilingi 2,200/= hadi Shilingi 4,500/= kuzingatia ubora na ukubwa mbalimbali wa Risiti hizo. Karatasi hizo zina uwezo wa kutoa wastani wa risiti kati ya Risiti 200 hadi 1,000 kulingana na urefu wa “Paper Roll”! au Bunda. Bei ya Karatasi hizi zinazojulikana kama “Thermal Paper” umezingatia kwamba ni za kisasa na hazifutiki kwa urahisi na zina Alama za Siri ndani yake kwa ajili ya kuongeza usalama.

Mheshimiwa Spika,
Kuhusu utaratibu uliotumika kuwapata Watengenezaji na Wasambazaji wa Mashine hizi za Kielektoniki na Wasambazaji wa karatasi, napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kuwa ulikuwa wa wazi na wa ushindani wa Kimataifa na haukuwa na dosari yoyote.

Mheshimiwa Spika,
Katika kutafuta Watengenezaji na Wasambazaji, kwenye Awamu ya Kwanza Watengenezaji Wanne (4) na Wasambazaji Sita (6) walipatikana kwa kutumia Zabuni ya wazi ya Kimataifa (International Competitive Tendering) kama ilivyoainishwa kwenye Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2004 na Kanuni zake za mwaka 2005. Kuanzia Mwezi Desemba Mwaka 2009 mpaka Mei 2010 makubaliano yaliingiwa kati ya kila Mtengenezaji na Msambazaji aliyechaguliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) chini ya “Memorandum of Understanding (MOU).

Kwenye Awamu ya Pili ya utekelezaji wa utaratibu huohuo wa Zabuni  ya Watengenezaji ilitangazwa kwenye gazeti la Daily News, The African, Tovuti ya TRA na Tovuti ya PPRA.  Jumla ya Wazabuni Kumi na Nne (14) walituma maombi ambayo yalifunguliwa mara moja baada ya saa Nne asubuhi tarehe 27 Septemba 2012. Watengenezaji wa Mashine Wanne (4) walichaguliwa kati ya Kumi na Nne (14) waliokuwa wameomba na Wasambazaji Watano (5) walipatikana kati ya Tisa waliotuma maombi yao ndani ya muda. Kwa kifupi, huo ndio utaratibu uliotumika ambao ulikuwa wa wazi na ushindani. 

Mheshimiwa Spika,
Ili kuhakikisha ubora wa Mashine hizi za Kielektroniki, Watengenezaji wametoa “Guarantee” ya muda wa miaka mitatu kwamba Mashine inayoharibika bila kukusudia na watawajibika kutoa mashine nyingine na pia kutoa elimu ya matumizi ya mashine hizo. Vilevile, kwa mujibu wa Mkataba ulioingiwa kati ya Wasambazaji na TRA, Wasambazaji wanawajibika kuzifanyia matengenezo mashine hizo kila zinapoharibika ili kuondoa usumbufu kwa watumiaji kutafuta watengenezaji wao wenyewe. Napenda kuwahakikishia Wafanyabiashara na Wananchi wote kwamba, utaratibu wa kutumia Mashine za Kielektroniki haukuwekwa kwa nia mbaya, bali unalenga kumrahisishia Mfanyabiashara kutunza kumbukumbu za kila siku za biashara na kuwawezesha kulipa kodi stahiki Serikalini.

Mheshimiwa Spika,
Kwa kutambua umuhimu wa mashine hizi katika kuongeza Mapato ya Ndani; na ili kuyashughulikia malalamiko ya baadhi ya Wafanyabiashara yaliyojitokeza, Serikali imesogeza mbele muda wa mwisho wa kununua Mashine za Kielektroniki hadi tarehe 31 Desemba, 2013.  Lengo ni kuwawezesha Walengwa kupata nafasi zaidi ya kujiandaa kununua mashine hizi na kujifunza namna ya kuzitumia. Aidha, Serikali kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali wa Sekta Binafsi inaendelea kutoa elimu kuhusu matumizi endelevu na faida za Mashine za Kielektroniki kwa Wafanyabiashara na wanunuzi wa bidhaa na huduma. Natoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge na Viongozi wa ngazi zote kushirikiana na Serikali kuwaelimisha Wananchi na Wafanyabiashara kuhusu manufaa ya Mfumo huu wa Mashine za Kielektroniki ili kwa pamoja tushirikiane kujenga Nchi yetu na kuleta maendeleo endelevu kwa kulipa Kodi stahiki.

VI:    USHIRIKIANO WA KIMATAIFA

Mheshimiwa Spika,
Tarehe 16 - 25 Oktoba 2013 nilifanya ziara ya kikazi Nchini China kufuatia mwaliko wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Watu wa China Mheshimiwa Li Keqiang. Katika ziara hiyo, nilifuatana na Viongozi wa Serikali wakiwemo baadhi ya Waheshimiwa Mawaziri, Wakuu wa Mikoa, Wabunge, Viongozi wa Asasi za Sekta Binafsi Tanzania  na Watendaji Wakuu wa Serikali na Mashirika ya Umma ambao walishiriki kwenye mazungumzo na Wabia wetu kwa upande wa Jamhuri ya Watu wa China.

Mheshimiwa Spika,
Dhamira kubwa ya ziara hiyo kimsingi ilihusu; kukuza mashirikiano ya kibiashara na utalii Nchini, kufanya mazungumzo na vyombo vya fedha ili kupata mikopo, kuendeleza uhusiano wa Nchi hizi mbili marafiki, kuona Sekta Binafsi ya Tanzania inavyoweza kushirikiana na wenzetu wa China na mwisho kutoa shukrani kwa misaada na mikopo ambayo Nchi yetu imepokea kutoka Jamhuri ya Watu wa China.

Mheshimiwa Spika,
Kama mnavyojua Taifa la Jamhuri ya Watu wa China ni miongoni mwa Nchi zenye uchumi unaokua kwa kasi kubwa sana na limepiga hatua kubwa sana katika maendeleo yake. Kutokana na maendeleo makubwa yanayotokea katika Taifa la China, nilitoa mwaliko wa kuwakaribisha ili kushirikiana na Tanzania na Bara la Afrika kwa ujumla wake katika Nyanja za kiuchumi, utamaduni na kisiasa. Yapo maeneo mengi ya ushirikiano ikiwa ni pamoja na soko kubwa la bidhaa za China na uwekezaji.
Mheshimiwa Spika,
Katika ziara hiyo nilipata fursa ya kutembelea Miji ya Beijing, Shenzhen, Chengdu na Guangzhou ambapo nilipata nafasi ya kukutana na Viongozi wa Makampuni mbalimbali ya China. Kutokana na Mikutano hiyo, baadhi ya Makampuni na Taasisi za Umma wameanza kuja Nchini kwa ajili ya kuendeleza mazungumzo na Serikali pamoja na Sekta Binafsi ili kuanzisha ushirikiano wa kiuchumi.  

Mheshimiwa Spika,
Kwa ujumla ziara hii ilikuwa na mafanikio makubwa. Kwa mfano, pamoja na kuendeleza na kudumisha ushirikiano ambao umeanzishwa na Viongozi waasisi wa Nchi hizi mbili yaani Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Mwenyekiti Mao Zedong wa Jamhuri ya Watu wa China, kwenye ziara hiyo, niliweza kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa China Bwana Li Keqiang, pamoja na Viongozi wa Makampuni yapatayo 30 ya China. Ninaamini tukijipanga vizuri tutaweza kufanya mengi kati ya Tanzania na China.Mheshimiwa Spika,
Ziara yangu pia ilifanikisha kutiwa saini kwa Mikataba ya ushirikiano wa Tanzania na China katika eneo la Sayansi na Teknolojia na katika Utalii.  Mikataba mingine iliyotiwa saini ni kuhusu uuzaji wa bidhaa za baharini za Tanzania Nchini China na kuanzisha Ukanda wa Kisasa wa Viwanda vya Nguo pamoja na kukuza zao la Pamba Nchini. Aidha, Mikataba ya Maelewano inayohusu Sekta za Nishati, Nyumba na Makazi baina ya Makampuni ya China na ya Mashirika yetu ya Umma yakiwepo Kampuni ya Umeme - TANESCO, Shirika la Taifa la Maendeleo - NDC na Shirika la Taifa la Nyumba - NHC ilisainiwa.

Mheshimiwa Spika,
Mafanikio mengine ya ziara hiyo ni pamoja na kuyashawishi Makampuni makubwa ya usafiri wa anga na Mawakala wa safari za kitalii kuwekeza Tanzania. Katika jitihada hizo nilikutana na Makampuni ya China Hainan, China Southern Air Line Holding Company na China Travel Service (Holdings) Hong Kong Limited.
Napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa kwa kiasi kikubwa Makampuni haya ya Usafiri wa Anga ya Nchini China yameonesha utayari wao wa kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kati ya Tanzania na China.  Aidha, Kampuni ya China Travel Service (Holdings) Hong Kong Limited ambayo inafanya biashara ya kusafirisha Watalii katika Nchi mbalimbali duniani wameonesha nia ya kuja kuwekeza hapa Nchini katika Sekta ya Hoteli kubwa za Kitalii. Kampuni ya China Merchants Holdings International Limited ambayo imehusika katika ujenzi wa Bandari kubwa na Mji wa Shenzhen katika Jimbo la Guangdong, kwa upande wake imekubali kuingia ubia na Serikali yetu katika ujenzi na kuendeleza Bandari mpya ya Bagamoyo na Mji wa Bagamoyo unaotarajiwa kuwa “Trade Hub” ya Afrika.

Mheshimiwa Spika,
Tanzania imedhamiria kuendeleza uchumi wake kwa lengo la kufikisha Tanzania kuwa Nchi ya Uchumi wa Kati kabla au ifikapo mwaka 2025.  Viashiria vyote vinaonesha hivyo, na ndio sababu Makampuni yote niliyozungumza nayo wakati wa ziara hiyo yameonesha shauku kubwa ya kuja kuwekeza Tanzania katika Sekta mbalimbali na mengine tayari yapo Nchini kutekeleza miradi mbalimbali. Napenda kuliahidi Bunge lako Tukufu kuwa Serikali kwa upande wake tutajitahidi kupokea Uwekezaji huo na hivyo kunufaika na matokeo tunayotarajia. Aidha, tutaendelea kuondoa vikwazo vya kufanya biashara na uwekezaji ili kuweza kuvutia Mitaji na Wawekezaji wengi zaidi pamoja na Watalii kutoka China na maeneo mengine duniani.

VII:    JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI

Mheshimiwa Spika,
Mtakumbuka tarehe 7 Novemba, 2013 Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alihutubia Bunge ambapo pamoja na mambo mengine alizungumzia suala la Jumuiya ya Afrika Mashariki na mustakabali wa Tanzania katika Jumuiya hiyo. Napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba katika Mkutano Mkuu wa 15 wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika tarehe 30 Novemba, 2013 Kampala Nchini Uganda, Wakuu wa Nchi hizo akiwemo Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete walikutana na waliidhinisha na kuweka Saini Itifaki ya Umoja wa Fedha wa Afrika Mashariki. Aidha, Viongozi hao walizitaka Nchi Wanachama kukamilisha taratibu za kuridhia Itifaki hiyo ifikapo mwezi Julai, 2014.Mheshimiwa Spika,
Manufaa ya Umoja wa Fedha ni pamoja na: kupunguza gharama ya kufanya biashara katika Nchi Wanachama; kuwezesha Nchi Wanachama kuwa na kiwango kidogo na tulivu cha Mfumuko wa Bei; kuwa na viwango vidogo vya riba ya kukopa; na kuepusha athari za ubadilishaji wa fedha ndani ya Jumuiya kwa kuwa na Sarafu Moja. Matarajio ni kujenga ukanda tulivu wa kifedha (Monetary and Financial Stability Zone) utakaorahisisha na kusaidia ukuaji wa biashara na shughuli za kiuchumi ndani ya Jumuiya.

Mheshimiwa Spika,
Katika Mkutano huo wa Kampala Wakuu wa Nchi pia waliridhia Mfumo wa kuanzisha Himaya Moja ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuagiza kuwa ifikapo mwezi Januari 2014, Nchi Wanachama ziwe zimeanza utekelezaji wake na kuukamilisha ifikapo au kabla ya mwezi Juni 2014. Aidha, Wakuu wa Nchi walipokea Taarifa kuhusu maendeleo ya Mpango Kazi wa kuelekea kuanzisha Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki. Walitumia muda wa Mkutano huo kujadili hali ya usalama iliyopo katika Nchi hizi na waliona kuna umuhimu wa kuongeza juhudi katika kukabiliana na Ugaidi.

Mheshimiwa Spika,
Kwa ujumla Mkutano huo ulikuwa na mafanikio sana hasa katika kuimarisha Umoja wa Jumuiya. Aidha Wakuu wa Nchi wote kwa pamoja walitumia muda huo kubadilishana mawazo kuhusu kuhakikisha kwamba mahusiano yetu kati ya Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki yanadumu na tunaendelea kuijenga Jumuiya na kuiimarisha kwa nguvu zetu zote.

X:    PROGRAMU YA KUBORESHA MIJI NCHINI (URBAN LOCAL GOVERNMENT STRENGTHENING PROGRAMME-ULGSP)

Mheshimiwa Spika,
Wakati wa kuhitimisha Mkutano wa 12 wa Bunge, nilieleza kuhusu Programu ya Kuboresha Miji Nchini (Urban Local Government Strengthening Programme-ULGSP) ya miaka mitano (5) kuanzia  mwaka  2013 hadi 2018. Huu ni mwendelezo wa Programu ya Uendelezaji na Uboreshaji Miji Nchini (Tanzania Strategic Cities Programme-TSCP); ambao kwa sasa unakaribia kumalizika utekelezaji wake. Programu hii ya ULGSP  kwa  sasa  inahusisha  Manispaa 11 na Miji 7. Manispaa hizo ni Tabora, Morogoro, Shinyanga, Lindi, Sumbawanga, Musoma, Songea, Singida, Iringa, Bukoba na Moshi. Miji mingine inayohusika ni Kibaha, Geita, Babati, Korogwe, Mpanda, Njombe na Bariadi. Halmashauri hizi zinazojumuisha Manispaa na Miji 18 ziko tayari baada ya kukidhi vigezo vilivyowekwa, ambavyo ni pamoja na:

Kuongeza Bajeti ya mapato kila mwaka;
Kutokuwa na Hati Chafu za Hesabu za Halmashauri,
Kuunda Kamati za kushughulikia matatizo yanayotokana na Programu kwenye ngazi ya Halmashauri, ngazi ya Kata na Mitaa;
Kuhakikisha Programu hiyo imetangazwa na kueleweka na wakazi wa Halmashauri za Manispaa na Miji;
Kuhakikisha kuna Wakuu wa Idara wa kutosha;
Kuhakikisha Sheria za Manunuzi zinafuatwa;
Kuhakikisha Watu watakaohamishwa na Programu na kulipwa fidia hawazidi nyumba 20;
Kuhakikisha miradi iliyotekelezwa inalingana na thamani ya fedha iliyotumika;
Kutekeleza miradi ya miundombinu iliyoko kwenye menu;
Kupeleka taarifa za kila robo mwaka za miradi kwa muda unaotakiwa;
Kuhakikisha kuna Master Plan ya Mji;
Kuhakikisha ukusanyaji wa kodi ya majengo unaongezeka kati ya Asilimia 5 hadi 30; na
Kuhakikisha taarifa za Mkaguzi wa Ndani zinaenda kwenye vikao vya Halmashauri kila robo mwaka.
Ukikosa hapa fedha hizo hazipatikani.
Mheshimiwa Spika,
Nimetaja baadhi ya Vigezo kwani viko zaidi ya 200 na vinagusa kila Sekta ya Halmashauri. Upimaji wa vigezo vyote vitafanyika mara 2 kwa mwaka; na Halmashauri zitakazoshindwa kufikia Alama (Marks) 60 na kuendelea, watapunguziwa fedha za miradi yao. Hivyo, Mikoa na Mabaraza ya Madiwani lazima yahakikishe kuwa vigezo vyote vinasimamiwa na kutekelezwa kikamilifu. Aidha, TAMISEMI wawachukulie hatua za kisheria wale wote watakaozembea katika kutimiza vigezo hivi na kuathiri maendeleo ya Wananchi.

Mheshimiwa Spika,
Programu hii ambayo ni ya kwanza Afrika itatumia Dola za Kimarekani 255, fedha ambazo zilikuwa zitolewe mwezi Julai mwaka huu, lakini kutokana na matatizo ya ubadhirifu yaliyojitokeza kwa Wasimamiaji wa fedha zilichelewa kutolewa. Hata hivyo, baada ya kuwapeleka wahusika wa ubadhirifu kwenye Vyombo vya Sheria, Wafadhili waliridhika na hatua zilizochukuliwa, hivyo tarehe 27 Novemba, 2013 Wafadhili walitoa fedha za Awamu ya Kwanza, ambazo zilitumwa kwenye Halmashauri hizo 18. Miradi iliyopo kwenye Programu ni pamoja na ujenzi na ukarabati wa barabara na mifereji ya mvua, uwekaji taa barabarani, ujenzi wa Stendi za Mabasi, upimaji viwanja, utengenezaji wa madampo, kuweka miundombinu ya majitaka na uboreshaji wa makazi. Hii ni baadhi ya Miradi ya Miji iliyoibuliwa na Halmashauri zenyewe kufuatana na matatizo ya Miji hiyo. Hivyo, ninawaomba TAMISEMI - wasimamie Programu hii vizuri ili Miradi husika iweze kutatua matatizo ya Wananchi katika maeneo yao na kuhakikisha Mapato ya Halmashauri yanaongezeka. Lengo ni kuwezesha Halmashauri hizo kujitegemea baada ya Miradi hiyo kukamilika.

XI: USIMAMIZI NA UDHIBITI WA FEDHA KATIKA MAMLAKA ZA SERIKALI ZA MITAA

Mheshimiwa Spika,
Kama ambavyo itakumbukwa, wakati wa majadiliano ya Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu zilizokaguliwa za Serikali za Mitaa, kwa mwaka 2011/2012, Waheshimiwa Wabunge walionesha masikitiko yao  kwa vitendo vya ubadhirifu na ufisadi unaofanywa na baadhi ya Halmashauri Nchini. Aidha, Waheshimiwa Wabunge wengi waliochangia mjadala huo walidai kuwa Serikali imekuwa haichukui hatua dhidi ya Watumishi wanaofanya makosa katika Halmashauri. Napenda kuwafahamisha Waheshimiwa Wabunge kwamba pamoja na matatizo na changamoto mbalimbali zilizopo kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhusu usimamizi na udhibiti wa fedha za Umma, Serikali imejitahidi kuimarisha usimamizi na utendaji katika eneo hili. Jitihada hizi zimedhihirishwa na Matokeo ya Taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ambayo yanaonesha kuongezeka kwa ubora wa Hati za Ukaguzi zinazotolewa kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa hususan kuanzia mwaka 2000 hadi sasa. Kwa mfano, mwaka 2000/2001 Ukaguzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa ulifanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali unaonesha kuwa Halmashauri zilizopata Hati safi zilikuwa 16 sawa na Asilimia 14 ya Halmashauri zote. Aidha, Idadi ya Halmashauri zilizopata Hati zenye Shaka zilikuwa 23, sawa na Asilimia 20 na Halmashauri zilizopata Hati Chafu zilikuwa 75 sawa na Asilimia 65 ya Halmashauri zote.

Mwaka 2005/2006 Idadi ya Halmashauri zilizopata Hati Safi iliongezeka hadi kufikia 53, sawa na Asilimia 43 na Halmashauri zilizopata Hati zenye Shaka zilikuwa 67, sawa na Asilimia 54 na Halmashauri zenye Hati Chafu zilikuwa Nne (4), sawa na Asilimia Tatu (3).

Mwaka 2011/2012 taarifa za Ukaguzi ziliimarika zaidi ambapo Halmashauri zilizopata Hati Safi ziliongezeka maradufu hadi kufikia 104, sawa na Asilimia 78 na zilizopata Hati zenye Shaka zilikuwa 29, sawa na Asilimia 21 na hakukuwa na Halmashauri iliyopata Hati Chafu.

Mheshimiwa Spika,
Jitihada hizi ni kubwa. Hivyo, Serikali itaendelea kuimarisha Usimamizi na Udhibiti na Mapato na Matumizi ya Serikali katika Sekta zote na Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuongeza ufanisi na tija katika utendaji na kudhibiti ubadhirifu wa fedha na mali za Umma. Lengo ni kuongeza kasi ya kuwaletea Watanzania maendeleo endelevu na Kukuza Uchumi kwa haraka.

Mheshimiwa Spika,
Pamoja  na  jitihada  hizo za Serikali zinazoonekana, napenda kuwahakikishia kwamba Watumishi waliohusika na ubadhirifu wa mali na fedha za Umma wamechukuliwa hatua mbalimbali zikiwemo kusimamishwa kazi, kushushwa vyeo, na kufikishwa  mahakamani.  Aidha, kesi za Watumishi hao ziko katika Mahakamani na katika Vyombo vya nidhamu vya Halmashauri na Tume ya Utumishi wa Umma kulingana na makosa yao kuhakikisha kwamba tunajenga nidhamu. Kutokana na hatua hizo kati ya mwaka 2011/2012  hadi  Septemba,  2013  jumla  ya  Wakurugenzi 52, Wakuu wa Idara 65 na Watumishi wengine 749 wamechukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria kwa ubadhirifu wa fedha katika Halmashauri mbalimbali Nchini. Hatua hizo za kinidhamu ni kama ifuatavyo:
Waliofukuzwa kazi ni 232,
Waliosimamishwa kazi ni 186,
Waliovuliwa Madaraka ni 33,
Waliopunguziwa Mshahara ni 1,
Walioshushwa Cheo ni 32,
Walipewa ONYO ni 113,
Waliofikishwa Mahakamani ni 233,
Waliofikishwa Polisi na TAKUKURU ni 36.
Serikali itaendelea kusimamie eneo hili kuhakikisha fedha za Umma zinatumika vizuri.

Mheshimiwa Spika,
Pamoja na hatua za kisheria zinazochukuliwa kwa Watumishi hao mmoja mmoja, Serikali imeendelea kuchukua hatua  nyingine mbalimbali kukabiliana na tatizo la ubadhirifu wa mali za Umma katika Halmashauri.   Juhudi hizo ni pamoja na kuongeza uwezo kwa kuajiri Wahasibu wa kutosha katika Halmashauri zetu; kuanzisha Kamati za Mapato na Matumizi katika ngazi zote za Halmashauri na kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa Kamati za Mapato na Matumizi za Halmashauri zote.  Mbinu nyingine zinazotumika ni kufanya Ukaguzi Maalum kubaini ufisadi na ubadhirifu wowote uliojitokeza. Kwa mfano, Katika mwaka wa fedha 2011/12 kumefanyika Kaguzi maalumu kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kumi na nne (14), ambazo ni Kilindi, Kiteto, Muheza, Ruangwa, Musoma, Kilwa, Temeke, Singida, Arusha, Mvomero, Morogoro, Dodoma, Mbarali na Bunda. Kaguzi hizo zimesaidia sana katika kujenga nidhamu ya Watumishi katika Halmashauri hizo.

Mheshimiwa Spika,
Serikali pia imeweza kubadili na kuweka Mfumo wa ‘Lawson’ katika kila Halmashauri ili kumaliza tatizo la Mishahara kwa Watumishi waliofariki, walioacha kazi, wastaafu, n.k. Vilevile kuna Mfumo wa Epicor 9.05 ambao zinasaidia kudhibiti Bajeti za Mapato na Matumizi katika Halmashauri Nchini. Mafunzo kuhusu matumizi ya Mifumo hii mipya yanaendelea kutolewa ili kuweza kutumia mifumo hii kwa ufanisi. Vilevile, Wakuu wa Mikoa walikwishaagizwa kuhudhuria Vikao vya Baraza za Halmashauri; katika kujadili Hoja za Ukaguzi ili Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali aweze kufuta zile zilizojibiwa kikamilifu. Hoja ambazo hazikupata majibu kikamilifu, Sheria zifuatwe na wenye kuhusika na ubadhirifu wowote wachukuliwe hatua zinazostahili. Aidha, Maafisa Masuuli (Wakurugenzi) wanaohusika na Hoja mbalimbali za Ukaguzi wanapaswa kuitwa kwenye Halmashauri walizotoka ili kujibu hoja zinazowahusu bila kujali wamehamishiwa wapi.

XI:    HITIMISHO
Mheshimiwa Spika,
Tumekuwa na muda mzuri wa kujadili masuala muhimu yanayohusu maendeleo ya Nchi yetu hapa Bungeni kwa kipindi chetu tulichokuwa katika Mkutano huu. Napenda niwashukuru wote waliosaidia kufanikisha Mkutano huu. Kipekee nikushukuru wewe Mheshimiwa Spika, pamoja na Naibu Spika kwa kutuongoza vizuri.  Niwashukuru Wenyeviti wa Bunge kwa kazi nzuri ya kuongoza Vikao vya Bunge lako Tukufu.  Aidha, niwashukuru tena Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao wakati wa Mkutano huu. Namshukuru Katibu wa Bunge na Wasaidizi wake wote pamoja na Wataalam wote wa Serikali na Taasisi zake ikijumuisha Taasisi za Sekta Binafsi, kwa misaada ya Kitaalam na huduma mbalimbali za kufanikisha Mkutano huu. Niwashukuru pia Waandishi wa Habari kwa kazi nzuri walizofanya kuhakikisha kuwa taarifa za majadiliano na maamuzi mbalimbali ya hapa Bungeni zinawafikia Wananchi. Niwashukuru Madereva kwa kazi nzuri waliofanya ya kuwasafirisha kwa usalama Waheshimiwa Wabunge, Viongozi mbalimbali, Wataalam na Wasaidizi wote walioshiriki katika Mkutano huu.

Niwashukuru Wabunge wote kwa kujadili vizuri hoja za zilizojitokeza hapa Bungeni. Lakini kipekee niwashukuru Waheshimiwa Mawaziri Wanne waliokubali kubeba jukumu ka kuwajibika kwa yote yaliyotokea. Tunawashukuru kwa uzalendo wao kwa Nchi yetu na tunawatakia kila la kheri katika maisha yao.

Mheshimiwa Spika,
Tunahitimisha shughuli za Bunge hili tukiwa tumebakiza siku chache kabla ya kufika Mwisho wa Mwaka huu 2013. Tunamuomba Mwenyezi Mungu mwenye wingi wa Rehema atujalie katika siku hizi chache tuweze kusherehekea Sikukuu njema ya Krismas na tuvuke salama mwisho wa mwaka na kuingia Mwaka Mpya 2014 kwa Amani na Furaha!.

Mheshimiwa Spika,
Kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wote tunavyofahamu, tutakuwa na Bunge la Katiba litakalofanyika mapema mwakani na kwa tarehe itakavyopangwa.  Kutokana na utaratibu huo ni dhahiri kwamba wengi wetu tutakutana wakati wa Bunge la Katiba.  Nitumie fursa hii kuwatakia safari njema mnaporejea kwenye maeneo yenu na wengi wenu niwatakie mapumziko mema ya Sikukuu ya Krismas na Mwaka Mpya hadi tutakapokutana wakati wa Bunge la Katiba.

Mheshimiwa Spika,
Baada ya kusema hayo, naomba sasa Bunge lako Tukufu liahirishwe hadi litakapokutana kwa Mkutano maalum wa Kumi na Tano wa Bunge la Bajeti tarehe 06 Mei, 2014 saa 3:00 Asubuhi katika Ukumbi huu hapa Dodoma.

Mheshimiwa Spika,
Naomba kutoa hoja.