4x4

WAJUA KWA NINI HAYATI MZEE KAWAWA ALIITWA SIMBA WA VITA WAKATI WA UHAI WAKE?

Na Hamis Shimye, UPL
HAYATI Mzee Rashid Mfaume Kawawa alikuwa ni kiongozi shupavu aliyewahi kutokea, ambapo alikuwa kiongozi adhimu sana na mwenye moyo wa ajabu katika kuipigania nchi yake katika ufanyaji wa kazi mbalimbali za maendeleo.

Alikuwa ni mtu asiyeogopa kazi hadharau kazi, hana makuu, hana makundi, hana majungu. Mdogo wake akifanywa mkubwa wake atafanya kazi chini yake kwa moyo wake wote, na uwezo wake wote; bila manung’uniko, na bila kinyongo.
Katika TANU alikuwa akiitwa SMBA WA VITA. 

Haogopi maamuzi mazito. Mkishafanya maamuzi ndani ya vikao yeye basi lazima atakuwa mstari wa mbele, ambapo wengine baadaye wanaweza kusita kuyatekeleza, au wanaweza kuyatekeleza kwa shingo upande na hasa kama walikuwa hawayapendi.

Hayati Mzee Rashid Kawawa alikuwa ni mtu wa kutekeleza mambo hasa pale viongozi wakishaamua kwa pamoja, atayatekeleza kwa moyo wake wote na uwezo wake wote. Kwa ajili hiyo mara nyingi amebeba lawama peke yake kwa maamuzi ambayo yamefanywa na uongozi mzima wa Chama na serikali kwa pamoja, au ambayo nimeyafanya mimi.

Hayati Mwalimu Julius Nyerere alitoa hotuba katika mkutano maalumu wa Taifa wa CCM mwaka 1990, ambapo sehemu ya hotuba ilikuwa inamzungumzia Mzee Kawawa, ambapo Mwalimu Nyerere alisema mambo mengi ya kumsifu Kawawa.

"Nilipokwisha kutangaza kwamba baada ya kikao hiki nitang’atuka uenyekiti wa Chama chetu, Ndugu Kawawa alinijia na kusema kuwa yeye pia angependa kung’atuka. Lakini tulikubaliana kwamba si vizuri wote wawili tukang’atuka wakati ule ule. Tutakuwa kama tunamtelekeza mwenzetu. Ni bora yeye abaki ili aendelee kumsaidia mwenyekiti mpya wa Chama chetu.

Ndugu Kawawa ni Askari. Hajitafutii madaraka; lakini hasiti kupokea madaraka yoyote anayopewa na chama chake.

Ndugu Kawawa, sijui jinsi ya kukushukuru kwa niaba yangu mwenyewe na niaba ya nchi yetu na Chama. Kwangu mimi imekuwa ni bahati na faraja ya pekee kwamba kwa muda wote wa uongozi wangu umekuwa makamu na msaidizi wangu. Unastahili kupumuzika, kama mwenyewe ulivyoomba. 

Badala yake tunakuomba uendelee kumsaidia mwenyekiti na Rais wetu; na hivyo uendelee kukisaidia Chama chetu na Nchi yetu. Umekubali Ahsante sana".

*Hotuba aliitoa Mwalimu Nyerere katika mkutano Mkuu Maalum wa Taifa, Agosti, 1990.

MAKALA: CHAMA CHA DEMOKRASIA NA UBAKWAJI WA DEMOKRASIA HALISIA

Mathias Canal (Picha na David Mtengile
CHAMA CHA DEMOKRASIA NA UBAKWAJI NA DEMOKRASIA HALISIA

Na Mathias Canal
Katika sehemu ya maelezo yake Raisi wa 16 wa Marekani Bw Abraham Lincoln namnukuu aliwahi kusema kuwa Demokrasia ni mfumo wa serikali ambapo wananchi wote ni sawa mbele ya sheria na wanashiriki katika kufanya maamuzi ya kitaifa juu ya masuala ya umma. Wakati mwingine wananchi hushiriki moja kwa moja - hii ina maana kwamba wao hupiga kura moja kwa moja kwenye masuala kama vile katika chaguzi. 

Kabla sijaanza kuzungumzia uchaguzi wa CHADEMA Kanda ya Nyasa Tutazame Mwongozo wa kumteua muaniaji Urais nchini Marekani Kabla ya Wamarekani kuamua nani wanayemtaka awe rais ajaye, wao kwanza huteua nani atakayewania kiti hicho.


Mchakato huo hungo'oa nanga kwa mchujo wa kamati za wajumbe ambapo wananchi hupata fursa ya kumchagua muaniaji kiti cha urais kwa tiketi ya chama cha Democratic au kile cha Republican.Mshindi wa mchujo huo huwakusanya wajumbe - hawa ni wanachama wenye nguvu ya kupiga kura kumchagua mgombea katika mikutano ya chama.

Nchini Marekani inakumbukwa kuwa kulikuwa na upinzania mkali katika uchaguzi wa nafasi ya Rais kati ya vyama viwili ambapo ni Republican na Demokratic, Kwa upande wa Democrats upinzani mkali ulikuwa kati ya Hillary Clinton na Seneta Bernie Sanders ambaye alionekana nae kupata uungwaji mkono zaidi dhidi ya Clinton. Kwa upande wa Republican kulikuwa na wagombea kama Marco Rubio na Ted Cruz sambamba na Donard Trump aliyeibuka kuwa mshindi wa chama hicho na mshindi wa nafasi ya Urais wa Marekani.

Tutakubaliana wote kwa pamoja kwamba Vyama vyote nchini Marekani vilisimamisha wagombea katika kura za awali kabisa ambao wote kwa pamoja walipigiwa kura na wajumbe wao hapakuwa na kura za Ndio na Hapana kwa maana ya Kivuli/Jiwe na Mtu sasa tutazame mchakato ulivyo kuwa kwenye vyama vinavyounda umoja wa katiba ya Wananchi UKAWA vikiongozwa na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA jinsi vilivyompata mgombea wake wa Urais.

Julai 30, 2015 nikiwa natazama Luninga majira ya saa tatu na dakika moja usiku niliona katika kipindi cha Dira ya Dunia kinachorushwa na chombo cha habari cha BBC kupitia Televisheni ya Star Tv kikiarifu kuwa WANACHAMA wapya wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa pamoja na na Juma Duni Haji wamepitishwa katika Mkutano Mkuu wa chama hicho kugombea ngazi ya urais na umakamu wa rais kwa asilimia 99.3 ambapo jumla ya wajumbe 2021 kati ya 2035 waliotakiwa kuhudhuria kwenye mkutano huo, walipiga kura za NDIO kwa kuwa hapakuwa na wagombea wemngine na kuibua kishindo katika mkutano huo uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam.

Awali kabla ya kufanyika uchaguzi huu Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa Mhe Freeman Alikael Mbowe Akizungumzia utaratibu wa kuteua mgombea huyo alisema kuwa, kwa mujibu wa katiba hiyo kifungu namba 7.16, mgombea urais pamoja na makamu wake wanateuliwa na sio kupigiwa kura.

Yaani kama kuna mtu hakuelewa vyema hapo katika maelezo hayo naomba nimsaidie kwa hili naamini ataelewa vyema zaidi Mbowe alisema kuwa kwa mujibu wa katika huku akitaja kifungu Mgombea Urais hapigiwi kura na wajumbe bali anateuliwa. Hii ni kauli ya kishujaa nay a ubakaji wa Demokrasia kwa uwazi kabisa.

Tujikumbushe Demokrasia ni nini kabla ya kuendelea na mjadala ili tuende sawa: Utawala wowote wa Demokrasia ni ule unaotokana na ridhaa ya wananchi, ambao kutokana na utaratibu waliojiwekea hufanya maamuzi ya kuwapata viongozi wao. Wananchi hushiriki moja kwa moja - hii ina maana kwamba wao hupiga kura moja kwa moja kwenye chaguzi. Tukubaliane sasa ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA hakuna Demokrasi kama ambavyo inahubiriwa katika vijiwe na majukwaa ya kisiasa. Na kama demokrasia ni pamoja na kushirikisha wananchi kufanya maamuzi kwa nini Mbowe aliamua yeye kwamba Lowassa na Duni wateuliwe sio kupigiwa kura na wajumbe zaidi ya 2000, kwa akili ya kawaida tu na karne hii unaweza kuwaambia watu fanyeni maamuzi kati ya Jiwe/kivuli na mtu...? Lakini katika hili sikuwaona vijana wa CHADEMA wakihoji wala wale wa Umoja wa Kizazi cha Kuhoji (UTG) wakihoji. Huenda walipitiwa hawakuliona hili sasa tuendelee.

UCHAGUZI KANDA YA NYASA 

Kwa kunukuu gazeti la Rai linalochapishwa na KAMPUNI ya New Habari (2006) Ltd ambayo pia inachapisha magazeti ya Mtanzania, Bingwa, Dimba na The African, la Disemba 8, 2016 liliandika habari ilikuwa na kichwa cha habari kilichosema UCHAGUZI CHADEMA NI ‘VITA’ KALI 

‘NI vita’, hivyo ndivyo tafsiri inapatikana kufuatia mvutano mkali ulioibuka ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kati ya Mchungaji Peter Msigwa na Patrick Ole Sosopi ambao walikuwa wanapambana kuwania nafasi ya uenyekiti kanda ya Nyasa.

Msigwa ambaye ni Mbunge wa Iringa Mjini alipamba na kijana Machachari katika Siasa za Tanzania Patrick Ole Sosopi ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), kuwania Kanda hiyo ya Nyanda za Juu Kusini (Nyasa) inayojumuisha mikoa ya Iringa, Mbeya, Rukwa, Njombe na Songwe.

Tangu maandalizi ya uchaguzi kanda nane za Chadema yalipoanza mwezi uliopita kulikuwapo na majibizano kati ya wafuasi wa wagombea hao wawili ambao kwa namna moja au nyingine wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii kuanika madhaifu ya kila mgombea.

Hata hivyo, Msigwa alionekana kushambuliwa zaidi na wafuasi wa Chadema Kanda ya Nyasa kutokana na madai mbalimbali ikiwamo tabia ya kutoshirikiana na wabunge wenzake katika kukijenga chama, pia kujiweka mbali na wabunge wa chama hicho kipindi walipokuwa wakipambana kutetea madai yao kwa Naibu Spika wa Bunge Dk. Tulia Ackson.

Kwa mujibu wa taarifa zilizolifikia gazeti la RAI zinaeleza kuwa baadhi ya wabunge na viongozi wa chama hicho walionekana kusita kumuunga mkono Mbunge huyo kutokana na madai ya ubinafsi aliouonyesha katika kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu 2015 kwa kushindwa kushirikiana na makada wa chama hicho kuzunguka sehemu mbalimbali.

Hata hivyo baadhi ya wafuasi wa Ole Sosopi walionekana kulalamika kutukanwa kwenye mitandao ya kijamii ambapo mmoja wao alisema: “Nimeshangaa sana watu kunifuata inbox na kunitukana hata wengine kutumia lugha ambayo si njema. Kumuunga mkono Sosopi ‘it’s just my perception.’ Kwa kuwa nina akili timamu siwezi kujibu matusi kama mlivyofanya “Imeniuma sana, nimeumia sana. Naomba niliweke wazi hili, Peter Msigwa ni Mbunge wangu, ni mlezi wangu na sina ugomvi naye. Sosopi na Msigwa wote ni Chadema na wote ni familia moja ndani ya chama chetu Chadema,” 

SIKU YA UCHAGUZI WA KANDA YA NYASA

Tarehe Disemba 22, 2016 ndio siku ambayo Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA kilifanya uchaguzi huo lakini mapema asubuhi kabla ya kuanza kwa uchaguzi jina la Patrick Ole Sosopi liliondolewa katika kinyang’anyiro cha kugombeanafasi ya uenyekiti Kanda ya Nyasa na Uongozi wa Kamati kuu ya Chama hicho iliyokuwa inaongozwa na Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa Freeman Alkael Mbowe.

Sosopi alipewa taarifa kwa njia yam domo kwamba jina lake limetolewa pasina kupewa hata maelezo kwa njia ya maandishi lakini pia taarifa hiyo alipewa asubuhi siku ya uchaguzi sio siku moja ama mbili kabla ya uchaguzi
Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Ubungo ambaye kwa sasa ni katibu wa Nec, Itikadi na Uenezi wa  CCM Taifa Hamphrey Polepole aliwahi kusema kuwa Huu si wakati wa siasa za kutafuta uongozi; Ni wakati wa siasa za maendeleo na kujenga nchi hapo alikubaliana na dhana ya mfumo wa kupunguza madaraka kwa viongozi inayohubiriwa naserikali ya wamu ya tano chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli ya kuwataka viongozi kuwa na cheo kimoja serikalini ikibidi kuwa na cheo kimoja pia kwenye chama cha siasa isiwe zaidi ya hapo.

Kabla ya kuendelea naomba nikurejeshe katika kauli ya Mchungaji Peter Msigwa ya Mwaka 2015 aliyoisema kwamba “Raisi apunguziwe madaraka, na wakuu wa mikoa pia wana vyeo vingi sana wapunguziwe" by peter msigwa 2015.

Lakini tutazame sasa vyeo alivyonavyo mchungaji Msigwa kwenye chama na seriakli kabla ya kutazama uchaguzi wa Mwenyekiti Kanda ya Nyasa ulivyoendeshwa

Mchungaji Msigwa ni Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini

Mchungaji Msigwa ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu Chadema
Mchungaji Msigwa ni Mjumbe wa Baraza kuu Chadema 
Mchungaji Msigwa ni Mjumbe wa Kamati Kuu Chadema
Mchungaji Msigwa ni Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Iringa
Mchungaji Msigwa ni Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa

Mchungaji Peter  Simion Msigwa amekipata cheo cha sita ndani ya Chadema na kuwa Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa baada ya wagombea wengine kuenguliwa, hivyo kuwa mgombea Pekee ambaye ni yeye Msigwa na Mgombea mwingine ambaye ni Jiwe/kivuli. Binafsi najiuliza sana lakini najiuliza kimya kimya hivi vikao vya vyeo hivyo vyote vya watu sita anahudhuriaje!


Maana ya upatikanaji wa Mchungaji Msigwa kama Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa ni kwa njia ya kuteuliwa na sio kuchaguliwa lakini Demokrasia ambayo CHADEMA huihubiri ni wazi wamekuwa wakiivunja wao maana wanawanyima nafasi wagombea pendwa na kukata majina yao na hatimaye wanakubali mgombea mmoja ashindane na kivuli pamoja na kwamba hakubaliki.

UCHAGUZI WA CHADEMA KANDA YA NYASA ULIKUWAJE BAADA YA MSIGWA KUBAKI MGOMBEA PEKEE AKISHINDANA NA KIVULI CHAKE MWENYEWE

Kwa mujibu wa andiko la lililosomeka kama “NIMEAMINI MAISHA BILA UNAFIKI HAYAENDI”
lililoandikwa na Mwalimu Pasaka Rucho mara baada ya mchakato mzima wa kumalizika na mshindi kutangazwa. Umeeleza tangu mchakato kuanza wajumbe walitaharuki sana kusikia taarifa ya kutolewa kwa jina la sosopi, tazama mchakato ulivyokuwa:

Wajumbe halali ni 98

Waliosusia 28
Waliopiga kura ni 106
Kura za ndio kwa msigwa 62
Kura za hapana ambazo zilipigia kivuli cha mgombea ni 44


Hii ikiwa na maana Ukichukua Kura 44 za Hapana dhidi ya Msigwa + na kura 28 za wajumbe waliosusia uchaguzi jumla yake ni =72 hivyo Sosospi tayari kama alikuwa mshindani alikuwa amejihakikishia ushindi kwa kura 78.

Kura zilizoongezeka kwa zile zilizopigwa ni 8 maana wapiga kura waliongezeka kutoka wapiga kura halali 98 na kuwa na wapiga kura wasio halali 8 waliofanya idadi kuongezeka na kuwa na wapiga kura 106.

Wajumbe waliopaswa kubaki ndani ukiondo waliokuwa wamekataa kuingia ndani ni 70

98-28=70.


Kwa maana halisi ni kwamba kulikuwa na wapiga kura 36 walioletwa na kuwa wajumbe wasio halali maana baada ya kura 44 za Hapana na wajumbe 28 kutoka ukumbini hivyo kulipaswa kupatikana kura za halali 28 ambazo ndizo kura za Ndio kwa Msigwa. 

Hii inamaanisha kwamba katika hali ya kawaida hata kama wajumbe wale 28 wasingeingia kama walivyofanya Msigwa angeshinda kwa kura 26 tu kwa maana ya wajumbe waliopaswa kubaki ndani 70- wajumbe 44 waliomkutaa=26 ambayo ndio idadi ya kura za Msigwa katika uchaguzi huo.


kwa ufupi kwa kutumia wajumbe halali katika uchaguzi kama Sosospi asingetolewa uchaguzi ungemalizika hivi:

Sosopi 72 (73.5%)
Msigwa 26 (26.5%)


HITIMISHO

Nianze kwa kumnukuu Dkt  Benson Bana wa Chuo Kikuu cha Dare s salaam ambaye amebobea katika masuala ya siasa alipokuwa akizungumza katika mkutano wa wadau wa siasa wa uimarishaji demokrasia ya vyama vingi. Alisema pamoja na mafanikio hayo bado kuna mapungufu mengi hasa ya kutokuwa na utamaduni wa vyama vingi, utamaduni unaoambatana na vyama kuwa na  aidolojia (itikadi), kukosekana kwa lugha za kistaarabu katika majukwaa ya siasa na hata mitafaruku ya ndani ya kivyama.

Mfumo wa vyama vingi ni hali ya kuwa na chama zaidi ya kimoja,katika nchi moja.Madhumuni ya kuwa na vyama vingi vya siasa ni kuleta ushindani wa kisiasa,ili kuleta maendeleo ya nchi,upinzani wa kisiasa sio uadui kama watu wengi kwenye nchi zinazoendelea wanavyodhani,kuwa na vyama vingi ni kuongeza wigo wa demokrasia katika jamii huska. Hata hivyo mara kadha amesema kuwa ili nchi yetu iweze kupiga hatua ni dhahiri lazima kuwe na Upinzani imara unaochukia Rushwa, na Uminyaji wa Demokrasia.

Binafsi sasa nakitoa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA katika Ukuzaji wa Demokrasi kwa kauli ya Mbowe kwa kusema kuwa Mgombea Urais hachaguliwi bali anateuliwa jambo ambalo ameliongoza pia kwa kumteua Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa Mchungaji Msigwa badala ya kuruhusu wajumbe kugombea na kuchagua kiongozi wanaomtaka.

TANZANIA ina vyama vya siasa 21 vyenye usajili wa kudumu huku kikiwepo kimoja ambacho kina usajili wa muda. Vyama hivi vimepatikana baada ya mabadiliko madogo ya Katiba yaliyotoa fursa ya kurejesha mfumo wa vyama vingi katika nchi yetu mwaka 1992.

Kufuatia mabadiliko haya, Chama cha Mapinduzi (CCM) ndicho kilichokuwa cha kwanza kupata usajili wa kudumu mwaka 1992, huku kikifuatiwa na vyama vipya vya CUF, CHADEMA,UMD, NCCR, NLD, UPDP, NRA, TADEA NA TLP vilivyopata usajili wa kudumu mwaka 1993.

Vyama vingine na usajili wao kwenye mabano ni:  UDP (1994), Demokrasia Makini (2001), CHAUSTA (2001), DP (2002), APPT(2003), Jahazi Asilia (2004), SAU (2005), AFP (2009), CCK (2012), ADC (2012), CHAUMMA (2013) na ACT (2014). RNP ni chama pekee kilichopo katika orodha ya vyama visivyo na usajili wa kudumu.

Katika vyama vyote hivi 21 mpaka sasa ni CHADEMA pekee ndicho kisichokuwa na Demokrasi kama ambavyo nimebainisha katika maeneo kadha wa kadha katika andiko langu.

Mwandishi Henry Mwangonde Aprili 23, 2014 katika gazeti la The Citizen, alimnukuu Dk. Benson Banna Katika makala yake ya “Vyama vingi vimeisaidia Tanzania” na kuandika; “vyama vya siasa nchini Tanzania havina nguvu katika kutanua mianya ya demokrasia kutokana na kukosa sera nzuri, mikakati pamoja na tabia ya viongozi wa vyama hivi kutokutumia mtaji wa wanachama wao kuviendeleza badala yake kuwatumia kwa masilahi binafsi.” Kwa mujibu wa Dkt Bana katika makala hiyo; vyama hivi vimeshindwa kutanua miaya ya demokrasia kwa kuwa havina demokrasia ndani yake.

Ni aibu kubwa sana kwa CHADEMA chama kinachojificha katika Mwamvuli wa Demokrasia katika Karne hii ya 21 kusimamisha mgombea Kivuli/Jiwe na Mtu…! Na bado kivuli kinapata kura 44? Watu 28 wanaishia mitini? Mtu anapata kura 66 naye anarudi kumsimulia Mkewe na Watoto kwamba ameshinda uchaguzi. 

Sasa hapa wachambuzi na wajuzi wa Siasa watahoji Tofauti ya CHADEMA na Yule mtu waliompa umaarufu kwa kumuita Bwana Yule upo wapi…? Lakini nimkumbushe Msigwa na CHADEMA kuwa raha na uzuri wa kura za Ndio na Hapana ni pale amabapo mshindi anaibuka kidedea kwa kura nyingi sio unapata kura 62 wakati zinakukataa ni kura 44 huku kura zingine 28 zikisusia namna ya Demokrasia ndani ya Chama.

Wakati vyama Vingine nchini vikiwa vinasonga mbele katika kuimarisha chaguzi zao za ndani ya Chama lakini CHADEMA wao wanarudi nyuma na kutoa mwanya kwa vyama vyenzake kusonga mbele.Naitazama CHADEMA kuanguka Kama umaarufu wa NCCR Mageuzi mwaka 1995.
Nitafurahi sana kuona na kusikia kauli za vijana mbalimbali wa CHADEMA wakiwemo UTG wakihoji kuhusiana na Uminyaji wa Demokrasia ndani ya chao chao CHADEMA ili tuzijue rangi zao katika kuhoji na kujenga hoja.

Mwandishi wa Makala haya ni Mathias Canal, Mchambuzi wa maswala ya jamii na siasa nchini Tanzania, Anapatikana kwa Barua Pepe ya canalmathias@gmail.com na kwa simu namba 0756413465

TAARIFA RASMI YA CCM KUHUSU YALIYOJIRI KIKAO CHA NEC LEO 12/12/2016 JIJINI DAR ES SALAAM







MUHTASARI WA HOTUBA YA RAIS DK MAGUFULI KWENYE MAADHIMISHO YA MIAKA 55 YA UHURU, DESEMBA 9, 2016

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
Description: Description: Description: Description: Description: Coat of ArmsKURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU
Simu: 255-22-2114512, 2116898
E-mail: press@ikulu.go.tz
Tovuti : www.ikulu.go.tz              

Faksi: 255-22-2113425


OFISI YA RAIS,
      IKULU,
 1 BARABARA YA BARACK OBAMA,  
11400 DAR ES SALAAM.
Tanzania.
 
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi mkuu Dkt. John Pombe Magufuli leo Ijumaa ya tarehe 09 Desemba, 2016 amewaongoza viongozi mbalimbali na wananchi kwa ujumla katika maadhimisho ya miaka 55 ya Uhuru wa Tanzania Bara .

Maadhimisho hayo ya miaka 55 ya Uhuru wa Tanzania Bara yamefanyika katika uwanja wa Uhuru Jijini Dar es salaam na kupambwa na gwaride maalum lililoandaliwa kwa pamoja na Majeshi ya Ulinzi na Usalama ikiwa ni pamoja na Jeshi la wananchi wa Tanzania JWTZ,Jeshi la Polisi,Jeshi la Magereza na Jeshi la Kujenga Taifa.

Akizungumza na halaiki ya watanzania waliohudhuria sherehe hizo Rais Dkt Magufuli amesema mwaka jana alilazimika kuzuia kufanyika kwa shamrashamra ya maadhimisho ya Uhuru wa Tanzania Bara kutimiza miaka 54 kwa kuwa alikuwa na mwezi mmoja tu tangu aingie madarakani na kuitaja sababu ya pili kuwa ni  bajeti kubwa ya shilingi bilioni nne iliyokuwa imetengwa kwa ajili ya maadhimiso hayo na kuona ni vyema ikaelekezwa katika upanuzi wa barabara ya Alli Hassani Mwinyi yenye urefu wa kilomita 4 ambayo inatumiwa na Watanzania wote badala ya fedha zile kutumiwa na wachache.

"Sherehe za miaka 55 nimeamua zifanyike kwasababu gharama zake ni ndogo sana,kwanza hakuna hata chakula baada ya sherehe hii,hakuna dhifa ya Taifa ,tukimaliza hapa tumemalizana ,lakini pili niliamua sherehe hii niifanye hapa Dar es Salaam kwa kuwa yatakuwa ni maadhimisho ya mwisho kufanyika jijini Dar es salaam na kwamba ni matumaini yake kuwa sherehe za mwaka kesho zitafanyika makao makuu ya nchia mbayo ni Dodoma"

Ameongeza kuwa sherehe za Uhuru ni tukio kubwa sana katika Taifa na hivyo serikali itaendelea kuipa umuhimu siku hiyo na kuiadhimisha.

Rais Dkt Magufuli pia amezitaja changamoto ambazo serikali ya awamu ya tano inazokumbana nazo kuwa ni pamoja na ufisadi na rushwa ndani ya baadhi ya watendaji na kuongeza kuwa mpaka sasa hivi wafanyakazi hewa wamefikia elfu kumi na tisa huku kaya masikini hewa zinazonufaika na mfuko wa TASAF zikiwa ni elfu 55 na wanafunzi hewa  mpaka sasa hivi wamefikia elfu sitini na tano

"Serikali ya awamu ya Tano itaendelea kuchukua hatua kali ikiwa ni pamoja na kuwatumbua hadharani wale waliozoea kutumbua hadharani mali za watanzania na tuataendelea kuchukua hatua kali katika masuala ya rushwa na ufisadi,kwasababu rushwa ni saratani"

Rais Dkt Magufuli amepongeza pia jitihada zilizofanywa na watangulizi wake katika maendeleo ya Tanzania na kuwashukuru kwa niaba ya watanzania huku akiwataka watanzania wote bila ya kujali dini,itikadi za kisiasa  na makabila yao kuendelea kudumisha amani na mshikamano ili Tanzania iweze kupiga hatua za kimaendeleo kwa haraka.

"Hivyo basi tuendelee kuilinda amani yetu na kuwafichua watu wenye nia ovu ya kuhatarisha amani yetu na sambamba na kulinda amani yetu hatuna budi kudumisha umoja na mshikamano wetu ambao ni nguvu na silaha yetu kubwa kama Taifa,lakini pia tuendelee kuulinda muungano wetu ambao ni silaha kubwa ya umoja wetu ili Tanzania tuendelee kwenda mbele"

Hii ni mara ya kwanza kwa Rais Dkt John Pombe Magufuli kuhudhuria na kuhutubia katika sherehe za Uhuru wa Tanzania Bara tangu aingie madarakani.


Emmanuel Buhohela
Kaimu Mwandishi wa habari Msaidizi wa Rais.
Dar es Salaam
09 Desemba, 2016





HOTUBA YA MGENI RASMI KATIBU TAWALA WA WILAYA YA ILALA, EDWARD MPOGOLO KATIKA UZINDUZI WA KAMPENI YA KIWILAYA YA SIKU 16 ZA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA, VIWANJA VYA SHULE YA MSINGI VINGUNGUTI, TAREHE 5 DESEMBA 2015

HOTUBA YA MGENI RASMI KATIBU TAWALA WA WILAYA YA ILALA, EDWARD MPOGOLO KATIKA UZINDUZI WA KAMPENI YA KIWILAYA YA SIKU 16 ZA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA, VIWANJA VYA SHULE YA MSINGI VINGUNGUTI, TAREHE 5 DESEMBA 2016

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala,
ACP. Salum Hamdani
Mbunge wa Jimbo la Segerea,
        Mhe. Bonnah Kalua
Naibu Meya wa Manispaa ya Ilala/Diwani wa Kata ya Vingunguti
        Mhe. Omar Kumbilamoto
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala,
        Ndugu Msongela Palela
Mkurugenzi wa WILDAF
        Mwakilishi wa Plan International
        Makamanda wa Polisi Mliopo hapa
Waheshimiwa Viongozi wote na mliopo hapa
Ndugu waandishi wa Habari, wageni waalikwa, mabibi na mabwana.    Itifaki imezingatiwa

Asalaam Alykuum! Bwana Yesu Asifiwe!

Utangulizi
Ndugu Wananchi. Awali ya yote, napenda kuchukua nafasi hii kutoa shukrani zangu za dhati kwa heshima kubwa ambayo mmempatia Mkuu wa
Wilaya ya Ilala kuwa mgeni rasmi kwenye Uzinduzi wa Kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia wenye kauli mbiu “Funguka, Pinga
Ukatili wa Kijinsia Elimu Salaama kwa Wote”.

Aidha, naomba kutumia fursa hii kuwakaribisha washiriki wote ambao mmejumuika nasi katika kufanikisha shughuli hii muhimu kwa ustawi wa
nchi yetu. Nimefahamishwa kuwa watu hawa, viongozi na makamanda wametoka maeneo mbalimbali katika Mkoa wa Dar es salaam, ambapo
wameacha shughuli zao za kila siku na kuja kujumuika nasi hapa Vingunguti. Asanteni kwa Kuja. Binafsi ninayo furaha kujumuika nanyi
kwenye uzinduzi huu kwani pamoja na mambo mengine imenipa nafasi ya kujifunza kutoka kwenye maelezo ya Kamanda wetu wa Mkoa wa Kipolisi
Kaka yangu Hamdun, maneno ya Kiongozi wa WiLDAF, maelezo ya Plan International na Ujumbe kutoka kwa wasanii wetu wa ngoma.

Ndugu Wananchi,
Naomba nitumie hadhara hii kulipongeza Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika (WiLDAF) Tawi la Tanzania kwa kudhamini na
kuratibu shughuli hii. Nafahamu kwamba maandalizi haya yalipewa msukumo na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala chini ya dawati la Jinsia,
sambamba na watu wa Plan International. Nawapongezeni nyote kwa kubeba dhamana kubwa ya kufanikisha maandalizi haya, kazi ambayo siyo tu ni
nzito bali umuhimu wake katika mchakato mzima wa kulinda na kutetea haki za binadamu hususan Wanawake (Mama Zetu) ni mkubwa.

Maadhimisho ya Siku 16 za Mapambano ya UWAKI
Ndugu Wananchi, Kama wengi wetu tunavyofahamu, chanzo cha maadhimisho haya ni mauaji ya kikatili ya wasichana wa Mirabelle huko nchini
Dominika mwaka 1960. Kutokana na hali hiyo, mwaka 1991,  Umoja wa Mataifa (UN) ulitenga Siku 16 kila mwaka kama siku ya kimataifa ya
kupinga unyanyasaji dhidi ya wanawake. Hivyo siku ya kuhitimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia ambayo ni tarehe 10 Desemba huwa ni
siku maalumu pia ya kuadhimisha Tamko la Haki za Binadamu.

Kuwepo kwetu hapa leo hii kunatokana na azma yetu sote kama taifa kuungana na Mataifa mengine duniani katika kuadhimisha siku hizi 16
kama sehemu ya majukumu yetu ya kimataifa na kwa sababu  taifa letu linaheshimu Haki na Utu wa mwanamke ambao ni nguzo yetu.

Juhudi za Serikali,
Ndugu Wananchi,
Masuala ya ukatili wa kijinsia yana wigo mpana na sura nyingi. Hivyo, yanataka jitihada za kila mwanajamii katika kuyashughulikia. Kwa
upande wa Serikali, tumejitahidi kuheshimu haki za binadamu na juhudi mbalimbali zimefanyika kwa uchache naomba nizitaje;-

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, Sura ya Kwanza, Sehemu ya Tatu inaelezea Haki ya Usawa. Kila mtu anastahili
heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa Utu wake; Sheria ya Makosa ya Kujamiina ya mwaka 1998 sheria hii inashughulikia vitendo vya
udhalilishaji;

Serikali inaendelea kufanyia mabadiliko makubwa katika sheria kandamizi kwa wanawake, mfano Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 na Sheria
ya Urithi na kutunga sheria za kuleta usawa wa kijinsia. Kuridhia kwa Mkataba wa Umoja wa Mataifa mwaka 1981 ambao unapinga aina zote za
ubaguzi dhidi ya wanawake (Convection on the Elimination of All Forms of Discrimination Against Women - CEDAW).


Aidha, Jitihada nyingine ni pamoja na kufanyiwa marekebisho ya sheria ya ardhi mwaka 2004 iliyokuwa sheria ya Ardhi ya mwaka 1999 ambayo
kwasasa inawapa haki wanawake kupata, kushiriki, kutumia na kumiliki ardhi. Serikali pia imetoa muongozo wa kisera wa sekta ya afya wa
kuzuia na kupambana na ukatili wa kijinsia wa mwaka 2013 ili kukabili tatizo la Ukatili wa Kijinsia (UWAKI).

Mwisho lakini siyo kwa umuhimu, ningependa kumshukuru na kumpongeza Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa jitihada zake za
kuwainua wanawake, ameendelea kuwapa wanawake nafasi za maamuzi na uongozi katika nyanja mbalimbali za uongozi wa kisiasa na utendaji wa
Umma hapa nchini. Jitihada zote hizi za serikali ni katika utekelezaji
wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG) ifikapo 2030.

Ukubwa wa tatizo la UWAKI
Ndugu Wananchi,
Utafiti uliofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO) 2000 kuhusu afya ya wanawake na ukatili majumbani kwenye nchi 10 umebaisha kuwa,
ukatili dhidi ya wanawake upo sehemu nyingi ikiwamo Tanzania. Katika Mkoa wa Dar es salaam utafiti ulihusisha wanawake 1820 kati ya hao
asilimia 41 ya waliohojiwa  waliathirika na aina mbalimbali za UWAKI. Aidha, taarifa inaonyesha kati yao asilimia 15 hadi 71 waliathirika na
ukatili wa kimwili au wa kingono ulifanywa na wanaume au wenzi wao. Utafiti ulibaini pia zaidi ya asilimia 90 ya waathirika wa ubakaji
wanawafahamu wahalifu wao.

Katika Wilaya ya Ilala mwaka 2015 kesi zilizoripotiwa zilikuwa 633 na Wilaya ya Kipolisi iliyoongoza ni Wilaya ya Ukonga. Mwaka huu hadi
kufikia Septemba 2016  jumla ya kesi 1094 ziliripotiwa na Wilaya ya kipolisi inayoongoza hadi sasa ni Wilaya ya Buguruni. Taarifa
inaonyesha kesi zinazoongoza kati ya hizo ni ndoa za utotoni na ulawiti. Ongezeko hilo kubwa la kesi zinazoripotiwa linatokana na
elimu inayotolewa na uwepo wa Kituo cha pamoja (One Stop Center) kilichopo Amana kinachohusisha Jeshi la Polisi, Madaktari, Ustawi wa
Jamii na Wanasheria.

Changamoto za UWAKI
Ndugu Wananchi, licha ya jitihada zinazochukuliwa na serikali kwa kushirikiana na makundi mbalimbali ya kijamii, takwimu bado
zinaonyesha ongezeko la Ukatili Wa Kijinsia (UWAKI). Ongezeko hili linachangiwa na changamoto zifuatazo;-
(a)     Imani za Kishirikina,
(b)     Mila na desturi – Utamaduni wa kunyamaza/ Mamlaka juu ya mke na watoto
(c)     Umaskini
(d)     Ukosefu wa Nyumba salama (Safe House)
(e)     Elimu

Nini kifanyike
Ndugu Wananchi, baada ya kuona changamoto na kwa kuzingatia kaulimbiu ya mwaka huu ya “Funguka, Pinga Ukatili wa Kijinsia Elimu Salaama kwa
Wote” kila mmoja wetu ana wajibu wa kufanya yafuatayo;-
•       Kuendelea kutoa Elimu ya kuzuia ukatili wa kijinsia katika sekta mbalimbali kama vile mashuleni na kwenye maeneo yote ya huduma za
kijamii sambamba na kupambana na ukatili huo.
•       Kuhakikisha kuwa na Sheria moja  inayohusiana na Ukatili Wa Kijinsia (UWAKI)
•       Kuendelea kuwashirikisha wanaume kwenye vita hii ya UWAKI kwani tafiti zinaonyesha wanaume ndiyo watuhumiwa wa kwanza.
•       Kujenga hadhi ya familia. (Haki, Wajibu na Maadili katika familia)
•       Ushirikishwaji wa Makundi yote ya Jamii kupambana na UWAKI

Hitimisho
Mwisho, ningependa kurudia kuwashukuru Jeshi la Polisi kwa kupitia kwako Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala, WiLDAF tawi la
Tanzania, Plan International  na Mashirika na Taasisi zilizofanikisha maandalizi ya kampeni hii ya siku 16 ya kupinga ukatili wa kijinsia.
Napenda kuwashukuru wananchi, wanahabari na wote  mliojumuika nasi na kunisikiliza. Nitoe wito wa Kufunguka, Pinga Ukatili wa Kijinsia Elimu
Salaama kwa Wote.

Baada ya kusema hayo napenda kutamka kwamba Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia katika Mkoa wa Kipolisi wa Ilala zimezinduliwa Rasmi.

Asanteni kwa kunisikiliza.