4x4

REA YAWEZESHA WANANCHI KUANZISHA MIRADI YA KIUCHUMI VIJIJINI

Na Jovina Bujulu-MAELEZO
USAMBAZAJI wa nishati ya umeme unaofanywa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umewezesha Wananchi wengi walioko vijijini kuanzisha miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa REA nchini Dkt. Lutengano Mwakahesya, nishati bora inachangia ukuaji wa uchumi wa Taifa jambo ambalo linasaidia kuboresha hali ya maisha ya Wananchi wengi walio vijijini. Kwa kutambua umuhimu huo REA kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali imeweza kuibua miradi mbalimbali ya nishati vijijini ili Wananchi waweze kufaidika nayo.

Wadau hao ni pamoja na Shirika la Umeme Nchini (TANESCO), Mamlaka ya Udhibiti wa Bei za Bidhaa (EWURA), Wizara ya Nishati na Madini, Asasi zisizo za Kiserikali (AZISE), Asasi za Kijamii (AZAKI) na Sekta binafsi. Dkt. Mwakahesya ameainisha miradi ya nishati za umeme kuwa ni pamoja na zile zinazotumia nguvu ya upepo, jua, maji na bayogasi.

Dkt. Lutengano ameeleza kwamba, lengo kubwa la ushirikiano baina ya REA na Wadau hao ni kuibua miradi mbalimbali ya nishati,  kutoa ruzuku na kuwezesha upatikanaji wa ushauri wa kitaaluma kwa waendelezaji wenye sifa katika masuala ya kiufundi, usimamiaji, uchanganuzi wa kifedha,  ugharamiaji wa miradi na mienendo mizuri ya miradi hiyo.  

Amesema, REA inahakikisha kwamba uendelezaji wa miradi ya nishati vijijini unazingatia utumiaji wa mazingira ili kutunza vyanzo vingine vya nishati. Ameongeza kusema kuwa REA inaongozwa na Bodi ya Nishati vijijini ambayo husimamia uendeshaji wa Mfuko wa Nishati vijijini (REF). Mfuko huu unasaidia kuongeza kasi ya upatikanaji wa miradi ya Nishati.

Serikali kupitia mfuko wa Nishati vijijini ilifadhili miradi kabambe ya usambazaji wa umeme vijijini awamu ya kwanza na ya pili ambayo inatekelezwa na Wakandarasi binafsi katika mikoa yote ya Tanzania Bara.

Utekelezaji wa mradi huu umekamilika kwa asilimia 90 na ambapo kilometa 1600 za msongo wa kati na kilometa 97 za msongo mdogo zimejengwa na vipoza umeme vilifungwa na wateja wa awali 18,253 wameunganishiwa umeme.

Katika awamu ya pili mradi ulilenga kujenga vituo 6 vya kuongeza msongo wa (umeme 11/33 KV) katika miji ya Kigoma, Kasulu, Kibondo, Ngara, Mbinga na Tunduru, ujenzi wa njia za umeme msongo mdogo na wa kati na kufunga mashine umba (transfomer) 3100. Mradi ulilenga kuunganisha wateja 225,000 na vijiji 2,500 pindi ukikamlika na kupeleka  umeme makao makuu ya Wilaya 13.

Mradi huu uliweza kujenga vituo 6 vya kuongeza nguvu Kigoma Vijijini, Kasulu, Kibondo, Ngara, Mbinga na Tunduru.Aidha mradi ulikamilisha ujenzi wa njia za msongo mdogo na wa kati,na wateja 61,023 walipatiwa umeme. Jumla ya vijiji 1,162 viliunganishwa kwenye gridi. 

Akielezea juu ya shughuli za kiuchumi na kijamii zilizoanzishwa vijijini Dkt. Lutengano amesema, kutokana na upatikanaji  wa nishati ya umeme vijijini maisha ya Wananchi yamekuwa mazuri kutokana na kuwepo kwa shughuli za kibiashara kama vile, mashine za kusaga na kukoboa nafaka, viwanda vya uselemala, utengenezaji wa milango na madirisha ya chuma, uuzaji wa vinywaji baridi n.k.

Kwa upaande wa shuhguli za kijamii, upatikanaji wa nishati wa umeme umeboresha huduma za hospitali, vituo vya afya na kumeongezeka kwa ari ya wanafunzi kujisomea wakati wote na pia matumizi ya kompyuta mashuleni, Kwa sasa wanawake wajawazito wanakwenda hoapitalini kujifungua bila kulazimika kuchukua  koroboi. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Nishati na Madini, hadi mwaka 2014 kiwango cha uunganishaji umeme katika Makao Makuu ya Wilaya na vijijini ulifikia asilimia 24 na kufanya Wananchi wanaopata huduma za umeme kufikia asilimia 36 ya Watanzania  waishio  bara ukilinganisha na mwaka 2005 ambapo kiwango cha uunganishaji umeme kilikuwa chini ya asilimia 10.

Raarifa hiyo inaonesha kwamba ongezeko hilo linatokana na juhudi mbalimbali za Serikali ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa Wakala wa Nishati vijijini (REA) na kupunguza gharama za kuunganisha umeme wa njia moja na kuhamasisha Wananchi kutumia umeme. 

Jumla ya shule za sekondari 1845, zahanati na vituo vya afya 898  na hospitali 96 zimepatiwa huduma ya umeme katika maeneo mbalimbali nchini. Aidha, Wakala kwa kushirikiana na TAZAMA pipeline na Mfuko wa Maendeleo wa Mafia umewezesha utekelezaji wa miradi miwili ya kupeleka umeme katika pampu za kusukuma maji na mafuta za TAZAMA zilizoko Kisanga (Morogoro).

Akizungumzia mafunzo yanayofadhiliwa na Wakala kwa wananchi, Meneja wa Tathmini na Ufuatiliaji wa REA , ndugu Vestina Rwelengera alisema kwamba ni pamoja na kuwapatia mafunzo yote ya nishati, mfano utunzaji wa vyakula  kwa kutumia nishati ya jua, miradi ya umwagiliaji, kukausha samaki na mboga mboga.

Alitaja maeneo yaliyonufaika na  na mafunzo hayo kuwa ni Bagamoyo, Mafia na Somanga Fungu ambapo wananchi walipata mafunzo ya kutengeneza mkaa kwa kutumia majani makavu. Pia  Wakala kupitia mfuko wa Nishati Vijijini, ulitoa ruzuku kwa vikundi vinavyotayarisha maandiko ya miradi ili kuwawezesha wanavijiji kupata mikopo kutoka kwenye benki zilizokubaliana na Mfuko huo. 

Akizungumzia miradi mingine iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa ya usambazaji wa umeme vijijini ndugu Vestina aliema kwamba ni pamoja na mradi wa SAGCOT Cluster ambao utasambaza umeme kilometa 100 , kujenga kituo cha  kupozea umeme katika mji wa Ifakara na mradi huu utaunganisha wateja 3,000.

Miradi mingine ni ya Andoya ( Mbinga), Tulila (Songea), Yovi (Kilosa), ambayo imeanza uzalishaji. Miradi ya Maguta ( Kilolo), Lupali (Njombe), na Isigula (Ludewa) ambayo imeanza kazi ya ujenzi na miradi ya Mwenga (Mufindi) ambapo jumla ya wateja zaidi ya 4,600 wameunganishwa.

Hadi kufikia Desemba 2015  vijiji 5,009 ambavyo ni sawa na asilimia 33 vilikuwa vimeunganishwa na huduma za umeme  na miradi inayoendelea itaunganisha vijiji vingine vipya 1,340 na kufanya jumla  ya vijiji 6,349 kupata huduma ya umeme miradi ikikamilika.

Akizungumzia changamoto zinazoikabili Wakala, ndugu Vestina alisema kuwa ni pamoja na Wananchi wa vijijini kushindwa kumudu gharama za kuunganishiwa umeme, upatikanaji wa rasilimali fedha za kutosha na usalama wa miundombinu kutokana na uharibifu na vitendo vya uharibifu vinavyofanywa na wananchi.

HOTUBA YA RAIS DK. JOHN MAGUFULI, KWENYE KILELE CHA SIKUKUU YA WAFANYAKAZI DUNIANI (MEI MOSI) 2016 ILIYOFANYIKA MJINI DODOMA

HOTUBA YA MHESHIMIWA DK. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWENYE KILELE CHA SIKUKUU YA WAFANYAKAZI DUNIANI MEI MOSI 2016 ILIYOFANYIKA MJINI DODOMA

      Mhe. Samia Hassan, Makamu wa Rais;
      Mhe. Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu;
Ndugu Gratian Mukoba, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA);
Mama Nortubunga Maskini, Makamu wa Rais wa TUCTA;
Mheshimiwa Jenista Mhagama, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu;
Mhe. Tulia Ackson, Naibu Spika;
Balozi Injinia John Kijazi, Katibu Mkuu Kiongozi;

Mheshimiwa Jordan Rugimbana, Mkuu wa Mkoa wa   Dodoma;
Waheshimiwa Mawaziri wote, na Waheshimiwa Wabunge mliopo;
Bi. Mary Kawar, Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO), Ofisi ya Nchi za Afrika Mashariki;
Waheshimiwa Mabalozi mliopo;
Waheshimiwa Majaji,
Mheshimiwa Almas Maige, Mwenyekiti wa Chama cha Waajiri Tanzania;
Dr. Aggrey Mlimuka, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE);
Ndugu Nicholaus Mgaya, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA);
Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi;
Viongozi na Maafisa wa Serikali mliopo;
Wawakilishi wa Vyama vya Siasa mliopo; Mzee Mangula, Makamu Mwenyekiti wa CCM
Bwana Kimbisa (Mb), Mwenyekiti wa CCM Mkoa;
Wanahabari;
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Dodoma;
Ndugu Wananchi;
Ndugu Wafanyakazi;
Mabibi na Mabwana.
Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uhai na afya njema na kuweza kukutana hapa. Leo ni siku muhimu sana. Tupo hapa kwa ajili ya kuenzi na kuthamini mchango wa wafanyakazi wa Tanzania, wake kwa waume, walioko sekta binafsi na ya umma, na  ambao kila siku tangu asubuhi hadi jioni wamekuwa wakivuja jasho kwa ajili ya maendeleo ya taifa letu.
Hii si mara yangu ya kwanza nashiriki Sherehe ya Siku ya Wafanyakazi, maarufu kama Mei Mosi. Nimeshiriki kwenye sherehe hizi mara kadhaa. Lakini leo nashiriki kipekee kabisa. Nashiriki kwa mara ya kwanza tangu nichaguliwe kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwezi Oktoba 2015. Hivyo, napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru Viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) na Vyama vyote vya Wafanyakazi nchini kwa kunialika ili nijumuike nanyi kwenye Sherehe hizi za Siku ya Wafanyakazi Duniani mwaka huu. Aidha, napenda kuwashukuru wafanyakazi wote wa Tanzania kwa kunipa kura nyingi zilizoniwezesha  kuchaguliwa kuwa Rais wa nchi hii. Naahidi kwenu kuwa sitawaangusha.
Nitumie fursa hii pia kuwapongeza sana wananchi wa  Mkoa Dodoma chini ya Uongozi wa Mkuu wa Mkoa, Mheshimiwa Jordan Rugimbana kwa kukubali kuwa wenyeji  wa Sherehe hizi pamoja na maandalizi mazuri mliyofanya kufanikisha sherehe hizi. Sherehe zimefana, hongereni sana! Nawashukuru pia wananchi wa Dodoma kwa kunipa kura nyingi wakati wa uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.
Aidha, ninawashukuru sana Wafanyakazi na Wananchi wote mliojitokeza hapa leo kwa wingi ili kujiunga na wenzetu duniani kote kusherehekea siku hii muhimu ya Wafanyakazi Duniani.
Ndugu Wafanyakazi na Wananchi kwa ujumla;
Duniani kote wafanyakazi ni nguzo muhimu ya maendeleo. Hakuna taifa lolote duniani ambalo limeweza kuendelea bila kutegemea wafanyakazi wake. Hapa nchini, wafanyakazi wametoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya taifa letu tangu kipindi cha ukoloni hadi sasa. Bila shaka wengi wetu hapa tunafahamu namna wafanyakazi na vyama vya wafanyakazi vilivyoshiriki kikamilifu katika harakati za ukombozi wa nchi yetu. Baada ya nchi yetu kupata uhuru, wafanyakazi wameendelea kutoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya nchi yetu.
Nitumie fursa hii kuwapongeza wafanyakazi kote nchini kwa kazi kubwa na nzuri mnayoifanya kwa maendeleo ya taifa letu. Ninyi ndio mmejenga miundombinu mbalimbali tunayoitumia hivi sasa, ninyi ndio mnahakakikisha Watanzania wanapata huduma bora za elimu na afya lakini hata ulinzi na usalama wa taifa letu kwa kiwango kikubwa unategemea ninyi wafanyakazi. Hongereni sana wafanyakazi!


Ndugu Wafanyakazi na Wananchi kwa ujumla;
Kama nilivyotangulia kusema, hii ni sherehe yangu ya kwanza ya Mei Mosi tangu nimechaguliwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano wa nchi yetu. Hivyo, napenda kutumia fursa hii adimu kuzungumza na wafanyakazi pamoja na wananchi kwa ujumla kuhusu masuala na mipango mbalimbali ambayo Serikali ya Awamu ya Tano ninayoingoza imepanga kutekeleza katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kuona nchi yetu inapata maendeleo kwa manufaa ya Watanzania wote. Tumejipanga kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025 pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala. Sote tunafahamu kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo inalenga kuiwezesha nchi yetu kuwa ya uchumi wa kati unaongozwa na viwanda. Ili kutekeleza Dira ya Maendeleo na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala, tayari tumekamilisha Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano utakaotekelezwa katika kipindi cha mwaka 2016/17 hadi mwaka 2020/21.
Mpango huu unadhima ya kujenga uchumi wa viwanda ili kuchochea mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya watu. Lengo kuu la Mpango huu ni kuhakikisha rasilimali na fursa za nchi zinatumika vizuri ili kujenga uchumi wa viwanda na kupunguza umasikini. Baadhi ya malengo mahsusi ni kuimarisha kasi ya ukuaji mpana wa uchumi kwa manufaa walio wengi, kuongeza kasi ya kupunguza umaskini, kuongeza fursa ya ajira kwa wote, kuongeza upatikanaji na ubora wa huduma za jamii na kuongeza mauzo nje kwa bidhaa za viwandani.


Ndugu Wafanyakazi na Wananchi;
Baadhi ya masuala muhimu yaliyomo kwenye Mpango wa Maendeleo ambayo tutayatekeleza katika kipindi cha miaka mitano ijayo ni pamoja na kufufua viwanda na kujenga vipya, hususan vinavyotumia malighafi zinazopatikana kwa wingi hapa nchini, teknolojia ya kati, nguvu kazi na ambavyo bidhaa zake zitatumika zaidi hapa nchini, ikiwemo viwanda vya nguo na bidhaa za ngozi. Aidha, tunakusudia mazingira ya uzalishaji na uendeshaji biashara kwa kuhakikisha tunajenga miundombinu ya nishati ya umeme, reli, barabara, maji, madaraja, vivuko, bandari, viwanja vya ndege na TEHAMA. Tunalenga pia kuhakikisha kuwa panakuwepo ardhi kwa ajili ya uwekezaji na upatikanaji wa rasilimali-watu yenye ujuzi. Halikadhalika, tutaboresha sera, sheria, taratibu, uratibu na ushirikiano wa kitaasisi.  
Maendeleo ya uchumi ni lazima yaende sambamba na maendeleo ya watu. Ili kuhakikisha hilo, vipaumbele vitakuwa ni kuhakikisha watu wanaondokana na umaskini, njaa na ukosefu wa ajira. Aidha, tutaboresha huduma za jamii, hususan afya na elimu, kwa kuhakikisha zinapatikana kwa uhakika na ubora unaostahili. Tutahakikisha watu wengi wanajiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii na pia panakuwepo na usawa wa jinsia na watu wenye ulemavu, utawala bora, mipango miji na kuogeza juhudi za kukabiliana na athari za tabianchi.
Matumaini yetu ni kwamba utekelezaji wa Mpango huu utaleta matokeo chanya kwa nchi yetu kwa kukuza uchumi kutoka asilimia 7 mwaka 2015 hadi asilimia 10 mwaka 2020; kuongeza mapato ya yatokanayo na kodi kutoka asilimia 12.1 ya pato la taifa mwaka 2014/15 hadi asilimia 17.1 mwaka 2020; kuongezeka kwa kasi ya kupunguza umaskini ambapo pato la wastani kwa kila mwananchi litaongezeka kutoka wastani wa dola za Marekani 1,006 mwaka 2015 hadi 1,500 mwaka 2020; umaskini wa mahitaji ya msingi kupungua kutoka asilimia 28.2 mwaka 2011/12 hadi asilimia 16.7 mwaka 2020/21; huduma za msingi za afya na elimu zitaimarika; kuongezeka kwa mauzo nje ya nchi ya bidhaa za viwandani; kuongeza idadi ya watalii na kuongeza uwekezaji wa moja kwa moja kutoka dola la kimarekani bilioni 2.14 mwaka 2014/15 hadi bilioni 5 mwaka 2021. Hayo ndiyo malengo yetu.
Ndugu Wafanyakazi na Ndugu Wananchi
Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Taifa utagharimu takriban shilingi trilioni 107, zikiwemo trilioni 59 kutoka Serikalini.Kwa kuanza, kwenye bajeti ijayo,  Serikali imetenga kiasi cha jumla ya shilingi trilioni 11.82 kwa ajili ya bajeti ya maendeleo sawa na asilimia 40 ya bajeti yote kutoka asilimia 26 mwaka uliopita.  Kati ya fedha za bajeti ya maendeleo, shilingi 8.702 trilioni sawa na asilimia 74 ya bajeti ni fedha za ndani na fedha za nje ni shilingi 3.117 trilioni sawa na asilimia 26.
Kama mnavyoona, sehemu kubwa ya ugharamiaji wa mpango huu itafanyika kwa kutumia fedha za ndani. Hii ishara tosha kuwa tumedhamiria kufanikisha azma yetu ya kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025 ili kuleta maendeleo nchini mwetu na kuwaondolea wananchi kero mbalimbali.
Ndugu Wafanyakazi na Ndugu Wananchi;
Bila shaka baadhi yenu mtashangaa kwa nini nimetumia Sherehe hii ya Wafanyakazi kuongelea malengo ya Serikali ya Awamu ya Tano katika kipindi cha miaka mitano ijayo. Jibu ni moja tu. Imenilazimu kueleza hayo yote ili sisi wafanyakazi wote hapa nchini tufahamu kazi kubwa iliyopo mbele yetu. Sisi ndio tunategemewa kuwaongoza Watanzania katika kutekeleza na kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025. Hivyo, tunaposherehekea sikukuu hii ya wafanyakazi duniani hatuna budi kila mmoja wetu kujiuliza ni kwa namna gani tutachangia katika kufanikisha utekelezaji wa Mpango huu wa Maendeleo kwa nchi yetu. Kwa kifupi, naweza kusema kuwa mipango yote mizuri niliyoieleza hapo juu haiwezi kufanikiwa kama wafanyakazi hawatashiriki kikamilifu.
Hivyo basi, nitoe wito kwa wafanyakazi kote nchi kila mmoja kwa nafasi yake kujipanga vizuri katika kutekeleza Mpango huu. Ni lazima tufanye kazi kwa bidii na kujituma, ueledi mkubwa na uadilifu. Nchi yetu haitaweza kufikia uchumi wa kati unaoendeshwa kwa viwanda kama tutaendelea kulea uvivu, uzembe, ubadhirifu, rushwa, ukwepaji kodi,  kutotimiza wajibu wetu na wafanyakazi hewa.  Kwa kutambua hilo, Serikali yenu imeanza kuchukua hatua za kuimarisha nidhamu na uwajibikaji kwa watumishi Serikalini. Tayari tumeanza kuwashughulikia watumishi wachache ambao ni wazembe, wavivu, wala rushwa, wabadhirifu na wasio na maadili.
Nafahamu, watumishi wazembe na wabadhirifu ni wachache. Lakini watumishi hao ndio wamekuwa wakiharibu sifa nzuri ya watumishi wa umma. Hawa ndio wamekuwa wakirudisha nyuma gurudumu la maendeleo la nchi yetu. Hawa ndio wamekuwa wakinufaika na kunyonya jasho la wafanyakazi walio wengi wa Tanzania.  Sasa mwisho wao umefika. Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kuwashugulikia popote walipo. Hatutawaonea aibu au huruma watumishi wa aina hii. Nimefurahi kusikia Vyama vya Wafanyakazi viko pamoja na Serikali na havitaunga mkono mtumishi mzembe, legelege na fisadi. Mmezidi kutupa nguvu zaidi ya kuendelea na jitihada tulizozianzisha za kurejesha nidhamu ya kazi kwenye utumishi wa umma. Niwaombe pia tushirikiane katika kushughulikia wafanyakazi hewa. Wafanyakazi hewa wameigharimu Serikali fedha nyingi ambazo zingeweza kuboresha maslahi ya wafanyakazi halali na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
 Hadi leo idadi ya wafanyakazi hewa waliopatikana ni 10,295. Kati ya wafanyakazi hao 8,373 ni kutoka Serikali za Mitaa na 1,922 ni wa Serikali Kuu. Kutokana na wafanyakazi hao hewa Serikali imekuwa ikilipa kiasa cha shilingi 11,603,273,799.41 kila mwezi sawa na shilingi 139,239,285,592.92 kwa mwaka sawa na shilingi 696,196,427,964.6 kwa miaka mitano. Fedha hizi zingeweza kujenga barabara za juu (flyovers) tano au kuboresha maslahi ya watumishi halali ama kuboresha huduma mbalimbali za jamii. Aidha, nafasi hizo hewa zingeweza kutoa ajira kwa wahitimu wa vyuo vikuu mbalimbali ambao wanatafuta kazi na hivyo kuleta manufaa kwa taifa.
Ndugu Wafanyakazi; 
Wakati nikitoa rai kwa watumishi legelege, wabadhirifu na wala rushwa kubadilika, napenda pia kutumia fursa hii kuwapa moyo wafanyakazi wote ambao ni wachapakazi na ambao wanatekeleza majukumu yao kwa ueledi na uadilifu. Endeleeni kufanya kazi kwa kujiamini, kujituma bila ya kuwa  wasiwasi wowote. Nafahamu wapo baadhi ya watu wamekuwa wakiwatisha na kuwaeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano haijali wafanyakazi. Wapuuzeni watu hao. Hao ndio wale waliokuwa wakinufaika au kushirikiana na watumishi mafisadi, wala rushwa na wabadhirifu. Sasa wanatapatapa baada ya kuona Serikali inachukua hatua mahsusi kwa watumishi wa namna hiyo. Serikali ya Awamu ya Tano haitambuguzi mfanyakazi yeyote ambaye anajituma na kufanya kazi kwa ueledi na uadilifu. Nipende kusema tu Serikali yangu itawalinda na kuwatetea wafanyakazi waadilifu na wachapakazi.
Ndugu Wafanyakazi;
Wakati wa Kampeni na hata nikifungua Bunge niliwaahidi wafanyakazi wote wa umma na sekta binafsi kuwa ningeboresha maslahi na mazingira yenu ya kufanya kazi, ikiwemo kuongeza mishahara, kuwapatia vitendea kazi, pamoja na kulinda na haki za msingi za hifadhi ya jamii kama huduma za afya na malipo ya pensheni baada ya kustaafu kazi.  Ahadi yangu hii bado ipo pale pale na nawaahidi tena sitawaangusha. Kwa bahati nzuri hata kaulimbiu ya Mei Mosi mwaka huu ambayo; Dhana ya Mabadiliko Ilenge Kuinua Hali ya Wafanyakazi inasisitiza umuhimu wa kuboresha maslahi na mazingira ya kazi ya wafanyakazi.
Kama alivyosema Katibu Mkuu wa TUCTA kuwa tangu tumeingia madarakani, tumeweza kuongeza ukusanyaji wa mapato kutokana na kuziba mianya mingi ya ukwepaji kodi na kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima.  Hata hivyo, sio dhamira yetu na bila shaka sio dhamira ya Watanzania walio wengi kuona fedha zote tunazokusanya tunazitumia kwa ajili ya kulipia mishahara watumishi tu. Nasema hivi ili mfahamu kwamba mapato haya yanawahitaji wengi sana. Wananchi walio wengi wamepata matumaini kuwa kutokana na kuongeza kwa mapato sasa huduma mbalimbali zitapatikana kwa ubora na uhakika. Hivyo, niwajibu wetu sisi mliotukabidhi kuongoza Serikali kuhakikisha tunatumia vizuri rasilimali za nchi kwa manufaa ya Watanzania wote. Na ninapenda kutumia fursa hii kuwahakikishia kuwa tutaelekeza fedha tunazozipata katika maeneo muhimu ambayo yanamgusa kila Mtanzania, wakiwemo wafanyakazi.
Ndugu Mwenyekiti wa TUCTA;
Ndugu Katibu Mkuu wa TUCTA;
Ndugu Wafanyakazi;
Hivi punde nimetoka kusikia risala yenu nzuri iliyosomwa na Katibu Mkuu wa TUCTA, Bwana Nicholas Mgaya. Sitaweza kujibu hoja zote zilizotajwa kwenye risala yenu. Lakini napenda kuwahakikishia kuwa Serikali imezipokea hoja zenu zote na tutazifanyia kazi. Hata hivyo, naomba mniruhusu nieleze japo kwa uchache baadhi ya hoja mliyotaja kwenye risala yenu:
Kwanza, kuhusu suala la kupunguza kodi ya mapato ya mshahara (PAYE) kwa wafanyakazi.  Napenda kuwaarifu kuwa Serikali yangu kama nilivyoahidi wakati wa kampeni zangu nimeamua kuwapunguzia Wafanyakazi kodi ya Mapato ya Mishahara kutoka asilimia 11 ya sasa hadi asilimia 9 kuanzia mwaka wa fedha wa 2016/17 kutegemea Wabunge watakavyopitisha bajeti yetu. Tuna uhakika kwa kufanya hivyo, tutakuwa tumewapunguzia wafanyakzi mzigo mkubwa wa makato katika mishahara yao. Nimeamua kuanza na hili kwanza ili changamoto zilizopo sasa za kiuchumi tuweze kuzivuka na baadaye mambo yakiwa mazuri tutaangalia suala la kupandisha mishahara.
Pili, suala la tofauti ya mishahara. Tayari tumeanza kuchukua hatua kuhakikisha tunakuwa na mfumo wa mishahara ambao unazingatia vigezo vya uzito wa kazi na kupunguza tofauti kubwa ya malipo ya mshahara kwa kuoanisha mishahara ya watumishi wa Umma walioajiriwa Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, Taasisi na Mashirika ya Umma. Tunataka Watumishi wa Umma wafaidi matunda ya kazi kwa kuzingatia uzito wa kazi wanazozifanya kwa misingi ya haki na usawa. 
Aidha, kufuatia marekebisho ya Sheria ya Taasisi za Kazi Na.7 ya Mwaka 2004, tumeunda Bodi mbili za mishahara. Bodi ya mshahara katika Sekta Binafsi inayosimamiwa na Waziri mwenye dhamana ya masuala ya Kazi na Ajira, na Bodi ya Mshahara katika Utumishi wa Umma inayosimamiwa na Waziri mwenye dhamana ya Utumishi wa Umma. Majukumu ya Bodi hizi ni kufanya uchunguzi na kupendekeza kima cha chini cha mshahara katika sekta husika. Ni matarajio yetu kwamba bodi hizi zitatekeleza majukumu yake kwa weledi kwa kupendekeza viwango vinavyozingatia hali halisi ya uzalishaji, tija na uchumi wetu. Nilikwisha tamka sitarajii kuwa na mfanyakazi anayelipwa zaidi ya milioni 15 wakati wengine wanalipwa laki tatu kwa mwezi.
Tatu, suala la hifadhi ya jamii. Serikali ya Awamu ya tano inalenga katika kuhakikisha kwamba wananchi wengi zaidi watafaidika na mfumo wa hifadhi ya Jamii nchini kuliko ilivyo sasa.  Kwa mfano tunataka wananchi wengi zaidi wajiunge na Bima ya Afya ili wawe na uhakika wa matibabu. Tunaendelea na juhudi ya kupanua wigo wa Mfuko wa Bima ya Afya vijijini (Community Health Fund)  na pia kuwezesha wafanyakazi wengi wa sekta binafsi kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (National Health Insurance Fund). Aidha, Mifuko ya Hifadhi ya Jamii imeanza kusajili wananchama toka sekta isiyo rasmi.  Lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba wananchi wengi wanapata huduma za msingi za hifadhi ya jamii.
Kwa upande wa kuimarisha Mifuko ya hifadhi ya jamii pamoja nakuboresha malipo ya Pensheni, Serikali imekwishaelekeza Mifuko ya Hifadhi ya jamii kuachana na uwekezaji kwenye miradi isiyokuwa na tija. Wawekeze kwenye maeneo kama viwanda ili kuzalisha fursa za ajira na kujipatia wanachama zaidi. Aidha, ushauri wenu wafanyakazi kupitia shirikisho lenu la TUCTA kwa Serikali kuhusu kupunguza idadi ya Mifuko ya Pensheni nchini na matumizi yasiyo ya lazima umepokelewa na kukubalika. Lakini ni vyema mfahamu kwamba kutokana na historia tofauti ya kuanzishwa kwa mifuko ya hifadhi ya jamii iliyopo sasa, hatua zozote za marekebisho zinahitaji umakini mkubwa. Napenda niwahakikishie kwamba kazi ya kurekebisha mifuko ya Pensheni nchi tutaikamilisha ndani ya mwaka 2016/2017.
            Nne, suala la Vyama vya Wafanyakazi. Napenda kutoa rai kwa waajiri kote nchini  kutambua kwamba suala hili sio la hiari bali ni wajibu wao kuwaruhusu wafanyakazi kuanzisha na kujiunga kwenye vyama vya wafanyakazi sehemu za kazi bila ya kushurutishwa au kuchaguliwa chama cha kujiunga.  Hivyo, waajiri wote wanaovunja takwa hili la sheria watachukuliwa hatua kali. Lakini pia nitoe wito kwenu Viongozi na wafanyakazi vyama hivyo visitumike kuchocheo migogoro ya kikazi, uzembe na uvivu kazini na wala visiwe vyama vya kisiasa kazini. Vyama hivyo vinapaswa kutumika kuimarisha uhusiano kati ya waajiri na waajiriwa, kuhamasisha utendaji kazi na kuleta utulivu sehemu za kazi.
            Tano, suala la mikataba ya ajira. Waajiri wengi wamekuwa hawatekelezi matakwa sheria kama yalivyobainishwa katika Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na. 6 ya mwaka 2004 pamoja na marekebisho yake ambayo tumeyafanya mwaka 2015.  Bado yapo malalamiko mengi ya wafanyakazi kutokuwa na mikataba ya kazi, kufanya kazi bila vifaa kinga, michango ya pensheni kuchelewa kuwasilishwa au kutowasilishwa kabisa kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii. Serikali ya Awamu ya Tano ninayoongoza haitavumilia ukiukwaji huu wa sheria.
            Ili kuhakikisha waajiri wanatekeleza kwa hiari bila shurti sheria za kazi, tuanza kurekebisha tena Sheri ya Ajira na mahusiano kazini kwa kuanzisha adhabu za papo kwa papo ambapo waajiri watalazimika kulipa faini kwa kila kosa la kutotekeleza sheria za kazi. Pia, katika mwaka huu wa fedha, Serikali imetenga fedha kuajiri maofisa kazi zaidi wapatao 21 ili kuimarisha huduma za ukaguzi sehemu za kazi. Nitoe wito kwa Vyama vya wafanyakazi, kushirikiana kwa karibu na Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu). Aidha, ninaziagiza Mamlaka zinazohusika kusimamia utekelezaji wa Sheria za kazi kusimamia sheria husika bila woga kwa lengo la kuwalinda wafanyakazi wasiendelee kutumikishwa na kunyonywa.
            Aidha, naziagiza mamlaka husika kushughulikia suala la ajira za wageni ambazo zinaweza kufanywa na wazawa. Hakuna nchi yoyote duniani ambayo jukumu lake kubwa ni kuwatafutia ajira wageni kazi ambazo ingeweza kufanywa na wazawa. Naagiza Wizara zote zisimamie hili suala kwa nguvu zote ili wazawa wapate ajira kwanza. Sambamba na hilo, wahusika wote mshirikiane pia kuwafichua wale wote watakaofanya kazi bila vibali. Nakumbuka zoezi hili lilianza sitaki kuamini kuwa ilikuwa ni nguvu za soda. Mheshimiwa Waziri tafadhali simamia hili.
            Suala jingine ambalo nalo limekuwa ni tatizo sugu ni baadhi ya waajiri kushindwa kuwasilisha michango ya wafanyakazi wao kwenye mifuko ya hifadhi kwa wakati.  Ingawa wafanyakzi wamekuwa wakikatwa kila mwezi lakini fedha hizo hazifiki kunakohusika. Tatizo hili pia linaihusu Serikali kutokana na Hazina kutopeleka michango. Hivyo, natoa wito kwa waajiri wote nchini kuwasilisha michango ya wafanyakazi wao kila mwezi bila kukosa. Hivyo, natoa wito kwa waajiri wote nchini kuwasilisha michango ya wafanyakazi wao kila mwezi bila kukosa.
            Kwa upande wa Serikali tayari tumeanza kulishughulikia suala hili la michango kwa kutambua wafanyakazi wote halali ili michango yao iwasilishwe. Mathalan, kwenye Mfuko wa PSPF Serikali ilikuwa ikidaiwa shilingi takriban bilioni 710 bilioni lakini hadi sasa tumelipa takriban shilingi 500. Ni imani yangu kuwa michango ya inayotakiwa kulipwa na Serikali kwenye Mifuko ya Hifadhi itapungua kutokana na zoezi la kuwaondoa wafanyakazi hewa. Tunaomba Vyama vya Wafanyakazi vishirikiane na Serikali kufichua watumishi hewa.
Ndugu Mwenyekiti wa TUCTA;
Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu
Waheshimiwa Mawaziri na Waheshimiwa Wabunge mliopo;
Ndugu Katibu Mkuu wa TUCTA;
Wageni Waalikwa;
Ndugu Wafanyakazi;
Mabibi na Mabwana:
            Napenda kuhitimisha hotuba yangu kwa kuwashukuru tena Viongozi wa TUCTA na Vyama vya Wafanyakazi nchini kwa heshima mliyonipa ya kushiriki kwenye Sherehe hizi. Aidha, napenda  kurudia tena wito wangu kwa Wafanyakazi na wananchi wote kwa ujumla, tuendelee kufanya kazi kwa bidii, kwa  nguvu zetu zote, kwa maarifa yetu yote na kwa kuzingatia misingi ya uwajibikaji na uadilifu ili tuweze kusukuma gurudumu la maendeleo ya nchi yenu. Tuachane na mazoea ya watu kuingia kazini asubuhi na kuondoka saa nne.
            Tukumbuke ya kuwa kazi ni utu, kazi sio fursa ya kupata mshahara kwa manufaa ya familia zetu tu bali ni fursa nzuri ya kutoa mchago kwa taifa lako kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Mungu Wabariki Wafanyakazi Watanzania!
Mungu Ibariki Tanzania!


“Ahsanteni kwa Kunisikiliza”.