4x4

SALAMU ZA MWAKA MPYA ZA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MHESHIMIWA DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE KWA WATANZANIA, TAREHE 31 DESEMBA, 2013

Utangulizi
Ndugu zangu;
Watanzania Wenzangu;
RAIS KIKWETE
Niruhusuni nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kutujalia uzima mpaka kufika  na kuiona siku hii ya leo ya kuuaga mwaka 2013 na kuukaribisha mwaka 2014.  Wapo ndugu, jamaa na marafiki zetu wengi ambao hawakupata bahati tuliyoipata sisi kwa vile wametangulia mbele ya haki.  Tuendelee kumwomba Mola wetu awape mapumziko mema na azilaze roho zao mahali pema peponi. Ameen.

Hali ya Usalama
Ndugu Wananchi;
Tunaumaliza mwaka 2013 nchi yetu ikiwa salama na tulivu. Mipaka iko salama na ile hali ya wasiwasi tuliyokuwa nayo kwa nyakati fulani mwaka huu sasa haipo tena. Uhusiano wetu na majirani ni mzuri na tutaendelea kufanya kila tuwezalo kuhakikisha kuwa hali inaendelea kuwa hivyo au hata kuwa bora zaidi mwaka 2014 na daima dumu.
Hali ya usalama wa ndani ya nchi nayo ni nzuri.  Hali ya wasiwasi tuliyokuwa nayo mwaka wa jana na mwanzoni mwa mwaka huu kuhusu uhusiano baina ya Wakristo na Waislamu haipo.  Ni matumaini yangu kuwa haitajirudia tena. Pepo mbaya amepita tuombe atokomee kabisa.

Ndugu zangu;
Watanzania wenzangu;
Napenda kurudia kuwasihi kuwa tuchague kuendelea kuishi pamoja kwa upendo, umoja, kuvumiliana na kushirikiana. Tuepuke kugeuza tofauti zetu za kisiasa, kidini, rangi, kabila au maeneo tutokayo kuwa chanzo cha uadui na mifarakano.  Kwa sasa tuna mwelekeo mzuri nawaomba tuudumishe. “Mjenga nchi ni mwananchi na mbomoa nchi ni mwananchi”. Tuchague kuijenga nchi yetu badala ya kuibomoa.  Tusiwasikilize watu hasidi wanaochochea uadui na mifarakano miongoni mwetu. Watatuvurugia nchi yetu nzuri.

Uhalifu
Ndugu Wananchi;
Katika mwaka 2013 vyombo vya dola vikishirikiana na wananchi viliendelea kupambana na vitendo vya uhalifu.  Mafanikio ya kutia moyo yameendelea kupatikana ingawaje bado kuna kazi kubwa ya kuendelea kufanya mwaka 2014 na miaka ijayo.

Dawa za Kulevya
Ndugu Wananchi;
Kati ya Januari na Desemba 2013, kilo 1,261 za heroin, kilo 3 za cocaine na kilo 89,293 za bangi zimekamatwa na watuhumiwa 1,631 wametiwa mbaroni.  Tatizo la biashara na matumizi ya dawa za kulevya ni kubwa na mapambano yanazidi kuwa makali. Mafanikio yanaendelea kupatikana ingawaje bado tuna kazi kubwa na ngumu ya kufanya mbele yetu. Ni makusudio yetu kuongeza maradufu nguvu ya kupambana dhidi ya uhalifu huu.
 Tupo hatua nzuri katika matayarisho ya kuanzisha Kikosi Maalum cha Kupambana na Dawa za Kulevya katika mwaka wa fedha 2014/15.  Pia tutaitazama upya sheria ya adhabu kwa makosa ya kufanya biashara ya dawa za kulevya ili kuifanya iwe na meno makali zaidi.  Vilevile, tutaongeza uwekezaji katika vituo vya tiba na kuwarekebisha watu wanaotumia dawa za kulevya. Mafanikio yanayopatikana Muhimbili na Mwananyamala yanatupa moyo wa kufanya zaidi.

Ujambazi
Ndugu wananchi;
Jeshi la Polisi limeendelea kupambana na ujambazi wa kutumia silaha na mafanikio yameendelea kupatikana. Matukio ya ujambazi yemepungua mwaka 2013 ukilinganisha na mwaka 2012.  Takwimu zifuatazo zinathibitisha ukweli huo.  Mwaka 2012 matukio ya ujambazi yaliyoripotiwa yalikuwa 6,872 na kwa mwaka 2013 yameripotiwa matukio 6,409.  Mwezi Julai mwaka huu, niliamua kulihusisha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania katika kupambana na ujambazi wa kutumia silaha na utekaji wa magari katika Mikoa ya Geita, Kagera na Kigoma. Katika Mikoa hiyo tatizo la ujambazi lilikuwa limefikia kiasi cha kulazimisha watu kusindikizwa na Polisi kutoka Ngara kwenda Karagwe, Biharamulo kwenda Muleba na kutoka Nyakanazi hadi Kakonko.  Hali hii haikubaliki na hatuwezi kuiacha iendelee.

Ndugu Wananchi;
Uamuzi wangu huo ndiyo ulioanzisha Operesheni Kimbunga ambayo imekuwa na mafanikio ya kutia moyo. Hali ya usalama katika Mikoa hiyo inaelekea kuimarika ingawaje ni mapema mno kusema tatizo limedhibitiwa.  Silaha nyepesi na nzito zipatazo 650 zikiwemo za kijeshi na za kiraia pamoja na mabomu ya kutupwa kwa mkono 11 zilikamatwa kwenye operesheni hiyo. Aidha, watu 31,203 waliokuwa wanaishi nchini kinyume cha sheria walirudi makwao.  Kati yao, watu 21,758 walirudi kwa hiari na 9,445 walirudishwa wakati wa Operesheni.

Ndugu Wananchi;
Nimepata minong’ono kuwa baadhi ya watu walioondoka wanarudi kinyemela. Napenda kuwatahadharisha kuwa wasifanye hivyo.  Wanajisumbua bure. Hawatadumu.  Ushauri wangu kwao ni kuwa kama wanapenda kuishi Tanzania wafuate njia halali za kufanya hivyo.

Ujangili wa Wanyamapori
Ndugu Wananchi;
Mwaka huu tuliongeza nguvu katika kupambana na ujangili wa wanyamapori na uvunaji haramu wa rasilimali za misitu. Hili ni tatizo la siku nyingi lakini katika miaka ya hivi karibuni limekuwa kubwa mno na kuwazidi nguvu Askari wa Wanyamapori na Maafisa Misitu.
Kwa nia ya kuwaongezea nguvu, mwaka 2010 niliagiza Jeshi la Polisi lisaidie Idara ya Wanyamapori  na Idara ya Misitu katika kupambana na uhalifu huo.  Operesheni kadhaa ziliendeshwa maeneo mbalimbali nchini na mafanikio ya kutia moyo yalipatikana.  Lakini, kwa kutambua ukubwa wa tatizo na hasa kwa upande wa aina ya silaha na mbinu zinazotumiwa na majangili niliamua kuhusisha vyombo vingine vya usalama likiwemo Jeshi la Ulinzi.  Nia ni kuongeza nguvu ya mapambano. Ndipo ilipoanzishwa “OPERESHENI TOKOMEZA”.

Ndugu Wananchi;
Kazi nzuri imefanyika chini ya Operesheni hiyo.  Mafanikio ya kuleta matumaini yameweza kupatikana.  Mitandao ya ujangili imeweza kutambulika na wahusika wake kadhaa wametiwa nguvuni.  Mitandao hiyo inahusisha watu wa aina mbalimbali.  Wamo raia wa kawaida, wapo watu maarufu, wapo watumishi wa idara mbalimbali za Serikali wakiwamo wa Idara za Wanyamapori na Misitu. Watu 1,030 walikamatwa pamoja na silaha za kijeshi 18,  za kiraia 1,579 na shehena kubwa za meno ya ndovu na nyara nyingine navyo vilikamatwa.Watu kadhaa tayari wameshafikishwa mahakamani.

Ndugu Wananchi;
Wahenga wamesema “kwenye wengi pana mengi”. Katika utekelezaji wa Operesheni hii kumekuwepo na taarifa za kufanyika makosa kinyume na malengo na madhumuni ya Operesheni.  Niliagiza baada ya kumalizika kwa awamu ya kwanza, zoezi lisitishwe kwa muda ili uchunguzi ufanyike, kasoro zitambuliwe na waliofanya makosa wachukuliwe hatua zipasazo. Wakati kazi hiyo inafanyika suala hilo lilijadiliwa Bungeni na Kamati Teule kuundwa.  Matokeo yake sote tunayajua.  Mawaziri wanne wamewajibika kisiasa.
   
Ndugu Wananchi;
Napenda kutumia nafasi hii kuwapa pole Mawaziri wetu hao kwa matatizo yaliyowakuta. Nawapongeza kwa uamuzi wa kukubali kuwajibika kwa makosa yaliyofanywa na maofisa wa chini yao. Wameonesha  ukomavu wa kisiasa na kiuongozi wa  hali ya juu na moyo wa uzalendo.
Kama mlivyosikia nitaunda Kamisheni ya Uchunguzi itakayoongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu. Uchunguzi wa kina utafanywa kuhusu kadhia yote hiyo.  Makosa yaliyofanyika yataainishwa na waliofanya kutambuliwa ili wachukuliwe hatua zipasazo kwa mujibu wa sheria na kwa mujibu wa kanuni za utumishi wa umma.

Ndugu Wananchi;
Ni muhimu kufanya hivi ili haki itendeke ipasavyo.  Mtindo wa mzigo wa makosa ya watumishi wa umma kubebwa na viongozi wa kisiasa pekee, tena wasiokuwa na hatia ya moja kwa moja, siyo sahihi.  Lazima kila mtu abebe mzigo wake inavyostahili.  Ni matumaini yangu pia kwamba katika siku za usoni kunapotokea matatizo ya namna hii uchunguzi uwe wa kina ili wale hasa waliohusika na kutenda makosa wawajibishwe.  Uwajibikaji wa wana-siasa peke yao hautoshi, kwani huwaacha waharibifu waendelee na kazi isivyostahili.  Mtindo huu utawafanya watumishi wasione umuhimu wa kutokurudia makosa.  Hata hivyo, pale kwenye ushahidi wa wazi kwamba kiongozi wa kisiasa angeweza kuchukua hatua za kuzuia madhara lakini hakufanya hivyo lazima kiongozi huyo awajibike.

Ndugu Wananchi;

Tunakamilisha matayarisho ya kuanza awamu ya pili ya Operesheni Tokomeza.  Ni muhimu kuendelea nayo kwani tusipofanya hivyo majangili wataendelea na vitendo vyao viovu.  Hali ni mbaya sana kwa upande wa uwindaji wa ndovu. Nilipolihutubia Bunge tarehe 7 Novemba, 2013, nilieleza kuwa tutafanya sensa ya ndovu katika Pori la Hifadhi la Selous.  Sensa hiyo imekamilika lakini taarifa yake inatisha.  Kuna ndovu 13,084 tu wakati mwaka 1976 walikuwa 109,419.  Tusipoendelea na Operesheni hii baada ya miaka michache ijayo hakutakuwa na ndovu hata mmoja.  Halikadhalika, zoezi la kuondoa mifugo katika mapori ya hifadhi ya taifa litaendelea.  Katika awamu ya pili ya Operesheni hii, washiriki watasisitizwa kutokutenda maovu yaliyofanyika katika awamu ya kwanza.

Mchakato wa Kuunda Katiba
Ndugu wananchi;
Tumefika mahala pazuri katika mchakato wetu wa kutayarisha Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  Jana Mwenyekiti wa Tume, Mheshimiwa Jaji Joseph Warioba, alitukabidhi Rasimu ya Pili ya Katiba, mimi na Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein.  Kama nilivyosema jana kinachofuata sasa ni kuitangaza Rasimu hiyo katika Gazeti la Serikali kwa kila mtu na hasa Wajumbe wa Bunge la Katiba, kuiona na kuisoma.  Baada ya hapo kitafuata kitendo cha kuifikisha Rasimu kwenye Bunge Maalum la Katiba kwa ajili ya kujadiliwa na hatimaye kupatikana Rasimu ya Mwisho itakayofikishwa kwa wananchi kupigiwa kura.

Ndugu Wananchi;
Mchakato wa kupata Wajumbe 201 watakaoungana na Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuunda Bunge Maalum la Katiba umeanza.  Ni matarajio yetu kuwa katika wiki ya tatu ya Januari, 2014, uteuzi utakamilika.  Siku 21 baada ya hapo Bunge la Katiba litaanza.  Hii ni kwa nia ya kuwapa nafasi Wajumbe hao kusoma Rasimu ya Katiba.  Baada ya Bunge la Katiba kumaliza kazi yake, utaanza mchakato wa Kura ya Maoni itakayopigwa na wananchi ndani ya siku 74 baada ya Rasimu ya Katiba kupitishwa na Bunge Maalum na kukabidhiwa kwa Rais.
 Iwapo Rasimu itakubaliwa na wananchi hapo tutakuwa tumepata Katiba Mpya. Lakini, iwapo Rasimu itakataliwa ina maana kuwa Katiba ya sasa itaendelea kutumika mpaka hapo mchakato mwingine utakapoanzishwa na Katiba mpya kupatikana.  Ni matumaini yangu na, ni maombi yangu na rai yangu kuwa Rasimu hiyo itakubalika ili nchi yetu isonge mbele.

Pongezi
Ndugu Wananchi;
Niruhusuni nitoe pongezi zangu za dhati kwa Mwenyekiti na Wajumbe wote wa Tume kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya.  Najua haikuwa kazi rahisi hata kidogo lakini wameweza.  Kwa namna ya pekee nawashukuru wananchi kwa ushiriki wao mzuri uliowezesha zoezi la mabadiliko ya Katiba kufikia hatua tuliyofikia sasa.

Ndugu Wananchi;
Ni matumaini yangu na ndiyo matumaini ya Watanzania wote kuwa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wataijadili Rasimu ya Katiba kwa makini na kufanya kila wawezalo kuiwezesha nchi yetu kupata Katiba nzuri itakayoimarisha na kudumisha Muungano wetu.  Katiba itakayoendeleza umoja, upendo, udugu, mshikamano na ushirikiano miongoni mwa wananchi wa Tanzania. Katiba itakayoihakikishia nchi yetu amani, utulivu na ustawi wa kiuchumi na kijamii.
 Ni imani yangu na ya Watanzania wote kuwa Wajumbe wa Bunge la Katiba wataweka mbele maslahi mapana ya taifa na watu wake. Wasiweke mbele maslahi yao binafsi au ya vikundi vyao vya kisiasa au kijamii. Wakifanya vinginevyo kuna hatari ya kupata Katiba isiyokidhi haja na itakuwa hasara kubwa kwa taifa letu na kwao pia.  

Uchumi
Ndugu wananchi;
Katika mwaka tunaoumaliza leo, Tanzania iliendelea kupata mafanikio katika nyanja mbalimbali za maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Jambo la kufurahisha ni kuwa mafanikio hayo yamepatikana licha ya kuwepo changamoto kadhaa hapa nchini na hali ya uchumi wa dunia kuwa bado haijatengemaa vya kutosha.
Pato la taifa limekua kwa asilimia 7.1 ukilinganisha na asilimia 6.9 mwaka jana.   Tunategemea kuwa mwaka 2014 pato la taifa litakua kwa asilimia 7.3.  Mfumuko wa bei umeshuka kutoka asilimia 12.1, Desemba, 2012 hadi asilimia 6.2, Novemba 2013. Lengo letu ni kufikia asilimia 5 mwezi Juni, 2014.

Ndugu Wananchi;
Hadi Novemba, 2013, Tanzania ilikuwa imeuza nje bidhaa na huduma zenye thamani ya dola za Marekani milioni 7,720.8 ukilinganisha na dola milioni 7,916.6 za mwaka ulioishia Novemba 30, 2012.  Kushuka kwa bei za kahawa, pamba, katani, chai, karafuu na dhahabu ndiko kulisababisha kupungua kwa mapato yetu ya fedha za kigeni.  Hali hii inatukumbusha umuhimu na uharaka wa kuendeleza viwanda vya kuongeza thamani mazao na bidhaa zetu tunazouza nje.  Jambo hili tutalipa msukumo maalum mwaka 2014 na kuendelea.
Pamoja na kushuka kidogo kwa mapato ya mauzo yetu ya nje akiba yetu ya fedha za kigeni iliendelea kuwa nzuri.  Hadi Novemba 30, 2013 akiba yetu ilikuwa dola za Marekani 4,538 milioni.  Hata hivyo, akiba hiyo inatuwezesha kuagiza bidhaa toka nje wa miezi 4.4 ni chini ya lengo letu la miezi 4.5.  Sina wasiwasi kuwa mwaka 2014 tutaliziba pengo hilo.

Ndugu Wananachi;
Sekta zilizochangia sana katika kasi ya ukuaji wa uchumi mwaka 2013 ni pamoja na mawasiliano asilimia 20.6, huduma ya fedha asilimia 13.2, uzalishaji viwandani asilimia 8.2, madini asilimia 7.8, ujenzi asilimia 7.8, biashara asilimia 7.7 na uchukuzi asilimia 7.1.  Bado kasi ya ukuaji wa sekta ya kilimo ilikuwa ndogo kwani ilikuwa asilimia 4.3.
Pamoja na hayo, kilimo kinaendelea kutoa mchango mkubwa kwa ustawi wa uchumi wa Tanzania na watu wake.  Kilimo kinachangia asilimia 24.7 ya pato la taifa na asilimia 10.7 ya mapato ya fedha za kigeni. Kilimo kimeiwezesha nchi yetu kujitosheleza kwa chakula na kuvipatia viwanda malighafi.    Kwa upande wa mazao ya chakula, kwa mfano, mwaka huu uzalishaji ulikuwa tani 14,383,845.  Ukilinganisha na mahitaji yetu ya chakula ya tani 12,149,120 hivyo tunajitosheleza na kuwa na ziada kidogo. Ziada hii ni kidogo mno hivyo inatulazimu mwaka ujao tuongeze maradufu juhudi na uwekezaji katika kutekeleza shabaha na malengo ya kilimo.

Ndugu Wananchi;
Kwa ajili ya uzalishaji wa chakula kuwa mzuri, mwaka huu Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula wameweza kununua tani 233,689.8 za nafaka hadi kufikia Desemba 27, 2013 kiasi ambacho hakijawahi kufikiwa miaka ya nyuma.  Mwaka 2012 wakati kama huu Wakala ilikuwa na kiasi cha tani 93,047.8 tu  na kutulazimisha kutafuta chakula nje ya nchi. Kwa ajili hiyo tulilazimika kuruhusu wafanyabiashara kuagiza mahindi, mchele na sukari kutoka nje kwa nafuu ya kodi.  Uamuzi huo umesaidia nchi kuwa na chakula cha kutosha na kuuzwa kwa bei nafuu kwa walaji.  

Ndugu Wananchi;
Ni matarajio yangu, na ndiyo hasa dhamira yetu, kwamba mwaka 2014 tutapata mafanikio makubwa zaidi kwa upande wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Naamini tutaweza kwa vile tumejipanga vizuri.  Tunayo miradi ya kimkakati iliyoainishwa vizuri katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano na chini ya Utaratibu wa Matokeo Makubwa Sasa.  Miradi hiyo kama itatekelezwa kama ilivyopangwa uchumi utakua kwa kasi kubwa zaidi, ajira nyingi zitapatikana na huduma za kiuchumi na kijamii zitaboreka sana.
Bahati nzuri tumeweka utaratibu mpya na mzuri wa kufuatilia utekelezaji wa mipango, miradi na shughuli za Serikali.  Katika Ofisi ya Rais kumeanzishwa Ofisi maalum ya ufuatiliaji ijulikanayo kama Presidential Delivery Bureau.  Na, kila Wizara ina kitengo cha namna hiyo kijulikanacho kama Ministerial Delivery Unit. Kwa ajili hiyo utekelezaji wa miradi ya kimkakati na shughuli za Serikali utakuwa mzuri zaidi.

Mazingira ya Uwekezaji
Ndugu Wananchi;
Ni makusudio yetu kuwa kuanzia sasa tutaihusisha sekta binafsi kwa nguvu zaidi katika utekelezaji wa miradi na shughuli za maendeleo. Nimeagiza Presidential Delivery Bureau ishughulikie suala la uboreshaji wa mazingira ya uwekezaji nchini.  Sifa ya nchi yetu kuhusu mazingira ya uwekezaji siyo nzuri.  Kwa mujibu wa tathmini inayofanywa kila mwaka na Benki ya Dunia, mwaka 2007 nchi yetu ilikuwa kati ya nchi 10 bora duniani kwa kufanya mageuzi makubwa ya kupunguza gharama za kufanya biashara. Mwaka huo tulikuwa nchi ya 142 kati ya nchi 175.  Mwaka 2008 tukapanda na kuwa wa 130 kati ya nchi 176, mwaka 2012 tulikuwa wa 134 kati ya nchi 185 na sasa ni wa 145 kati ya nchi 185.  Hali hii si nzuri hata kidogo kwa uchumi unaokusudiwa kujengwa kwa kutegemea uwekezaji wa sekta binafsi.  Tunategemea PDB itatupa ushauri mzuri wa nini kifanyike kurekebisha mambo.

Ndugu Wananchi;
Utekelezaji wa miradi ya Big Result Now (BRN) katika kilimo, umeme, reli, barabara, bandari, maji, elimu na kuongeza mapato ya Serikali umeanza kwa kasi inayoleta matumaini. Kama upande wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali utakwenda inavyotarajiwa tutegemee mambo mengi mazuri kufanyika kuanzia mwaka 2014 mpaka 2016.
Mpaka sasa hali ya ukusanyaji wa mapato ya Serikali si mbaya.  Wastani kwa mwezi unakaribia shilingi bilioni 700 kuelekea shilingi bilioni 800.  Makusanyo ya mapato ya Serikali kwa miezi ya Julai hadi Novemba yaliongezeka kutoka shilingi bilioni 3,008.1 kipindi kama hicho mwaka 2012 hadi shilingi bilioni 3,555.5 mwaka 2013.  Hata hivyo makusanyo ya Julai hadi Novemba, 2013 ni asilimia 88.1 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 4,036.8. Lengo halijafikiwa kwa sababu ya kuchelewa kutekelezwa kwa baadhi ya marekebisho ya mfumo wa kodi, hususan tozo ya simcard, kodi za mishahara kutokana na kutokupandishwa kwa kima cha chini katika sekta binafsi na ya uhawilisho wa fedha (money transfer). Pia kuendelea kwa mvutano baina ya TRA na wafanyabiashara kuhusu bei za mashine za kodi.  Ni matumaini yangu matatizo hayo yatashughulikiwa na kumalizwa mapema iwezekanavyo ili tuweze kupata mafanikio makubwa zaidi katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali mwaka 2014.

Elimu
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa elimu tumeendelea kupata mafanikio katika kupunguza tatizo la upungufu wa walimu wa shule za msingi na sekondari. Mwaka huu tuliajiri walimu 28,666. Kwa ajili hiyo upungufu wa walimu ni 57,755 kati yao  20,625 wa shule za msingi na 37,130 wa shule za Sekondari.  Mapema mwaka ujao tutaajiri walimu wapya 36,100 kati yao 18,100 wa shule za msingi na 18,000 wa sekondari. Kufanya hivyo kutafanya pengo lililopo liwe dogo zaidi.
Kwa upande wa shule za sekondari, tatizo la walimu wa masomo ya sanaa tunakaribia kulimaliza. Changamoto yetu kubwa itakuwa kwa walimu wa masomo ya sayansi.  Upungufu ni walimu 26,998 na uwezo wa vyuo vyetu ni kutoa walimu wa sayansi 2,300 kwa mwaka.  Mapema mwaka 2014 tutakutana na wadau wa elimu nchini kujadiliana juu ya mkakati wa haraka wa kulikabili tatizo hili. Nilipanga tufanye hivyo mwaka huu lakini mambo yaliingiliana sana hatukuweza.

Ndugu Wananchi,
Tumeendelea kupunguza tatizo la uhaba wa vitabu na vifaa vya kujifunzia na kufundishia.  Tuliongeza fedha katika bajeti ya elimu kwa ajili ya vitabu.  Hivi sasa usambazaji wa vitabu vyenye thamani ya shilingi bilioni 76 za bajeti ya mwaka 2012/13 unaendelea.  Kwa sababu hiyo hivi sasa upungufu wa vitabu umeshuka na kufikia kitabu kimoja kwa wanafunzi 3. Naamini shilingi bilioni 49 zilizotengwa katika bajeti ya mwaka huu wa fedha kwa ajili ya vitabu itafanya mambo kuwa nafuu zaidi. Tukiendelea kuwekeza kama tufanyavyo sasa shabaha yetu ya kila mwanafunzi wa msingi na sekondari kuwa na kitabu chake kwa masomo yote ifikapo 2016 itatimia.

Ndugu Wananchi;
Mwaka huu tumeanza utekelezaji wa mpango mkubwa wa kujenga nyumba za walimu.  Kwa kuanzia tumetenga shilingi milioni 500 kwa kila Halmashauri. Tumeanza na Halmashauri 40, mwaka ujao na miaka inayofuata tutaongeza fedha zinazotengwa na kuzifikia Halmashauri zote.  Kwa upande wa ujenzi wa maabara katika sekondari za kata napenda kuwakumbusha Wakuu wa Mikoa na Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya na Miji, kuwa kila mmoja ahakikishe kuwa ifikapo Novemba, 2014 malengo yanatimia.  Wasisubiri kuulizwa.

Maji
Ndugu Wananchi;
  Kwa kutambua umuhimu wa maji kwa maisha ya wanadamu na uchumi katika bajeti ya mwaka huu wa fedha sekta ya maji imepewa upendeleo katika mgao wa fedha. Tutaendelea kuongeza fedha katika bajeti mbili zinazofuata ili watu wengi zaidi mijini na vijijini wapate maji safi na salama. Kama fedha zitapatikana kama ilivyopangwa na utekelezaji ukasimamiwa vizuri tunatarajia kuwa katika mwaka 2013/14 watu milioni 7.1 watapata maji.  Katika mwaka ujao wa fedha 2014/15 tumepanga kuwapatia maji watu wengine milioni 7 na mwaka utaofuata (2015/16) tutaongeza tena huduma hiyo kwa watu milioni 1.3 na kufanya tufikie asilimia 74 ya Watanzania wanaopata maji safi na salama ifikapo 2015/2016.
  
Afya
Ndugu wananchi;
Tumeendelea kupata mafanikio katika kuendeleza upatikanaji wa huduma ya afya kwa wananchi wa Tanzania.  Zahanati, vituo vya afya na hospitali zimeendelea kujengwa kote nchini. Aidha, hospitali za wilaya, mikoa, kanda na Hospitali ya Taifa Muhimbili zimeendelea kuboreshwa.  Kwa ajili hiyo idadi ya Watanzania wanaoweza kupata huduma ya afya iliyo bora inazidi kuongezeka.  Hali kadhalika, wataalamu wa afya wa fani mbalimbali wameongezeka na hali ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba imezidi kuboreshwa.  Pamoja na yote hayo bado kuna kazi kubwa ya kufanya mbele yetu.  Kufanya hayo ndiyo dhamira yetu kuu kwa mwaka 2014.

Ndugu wananchi;
Tumeendelea kupata ushindi katika mapambano dhidi ya magonjwa yanayoua watu wengi nchini.  Kwa upande wa malaria, kwa mfano, maambukizi ya ugonjwa huo kwa watoto na mama wajawazito yamepungua kutoka asilimia 18 hadi 9.5. Tutaendelea kugawa vyandarua kwa wajawazito na watoto kwa kutumia hati punguzo pamoja  na kusisitiza matumizi ya dawa mseto na kupulizia dawa ya kuua mbu majumbani.   Aidha, tunatarajia kupata mafanikio zaidi miaka ijayo kiwanda cha kuzalisha viuadudu vya kuua viluilui vya mbu wanaoeneza malaria kitapoanza kazi.

Ndugu Wananchi;
Mambukizi ya UKIMWI yameshuka hadi asilimia 5.1. Inaleta faraja kuona watu wengi wamejitokeza kupima afya zao kwa hiari.  Mpaka sasa watu milioni 18 wamepima. Tunao watu 1,298,402 walioorodheshwa kwa ajili ya kupata huduma ya tiba na kati yao 485,715 wanapata dawa.  Waliosalia watapata wakati wao ukifika.    
  Mpaka sasa vituo 4,603 vinavyotoa huduma ya kuzuia maambukizi ya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto vimeanzishwa nchini kote tangu mpango huo uzinduliwe tarehe 1 Desemba, 2012.  Idadi yake inaendelea kuongezeka. Ni dhamira yetu kuendeleza jitihada za kupunguza maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwa Watanzania.  Mafanikio ya kampeni hii pamoja na ile dhidi ya malaria ndiyo chachu ya mafanikio tuliyopata katika kupunguza vifo vya watoto nchini na kufikia lengo la Milenia mwaka huu.

Magonjwa ya Moyo
Ndugu Wananchi;
Katika mwaka 2013 tunaoumaliza leo, tumeshuhudia mambo kadhaa mazuri yakifanyika yanayoelezea mafanikio tunayoendelea kuyapata katika jitihada zetu za kujenga uwezo wa tiba kwa maradhi tunayopeleka wagonjwa nje ya nchi.  Niruhusuni niyataje baadhi yake.  La kwanza, ni kuanza kazi kwa Kituo cha Tiba na Mafunzo ya Magonjwa ya Moyo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Hiki ni kituo kikubwa na cha aina yake cha matibabu ya maradhi ya moyo hapa nchini.  Huduma za kisasa za uchunguzi na matibabu ya maradhi ya moyo ambazo zamani zilikuwa zinapatikana nje ya nchi sasa zinaweza kupatikana hapa hapa nchini.  Kwa kuwa na vitanda 100 vya kulaza wagonjwa, Watanzania wengi wataweza kuhudumiwa na maisha yao kuokolewa.
  
Ndugu Wananchi;
Katika kituo hiki watu wanaweza kufanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo (open heart surgery), uwekaji wa mashine ya kuongezea nguvu  kwenye moyo (pacemaker), uwekaji wa vyuma vidogo katika mishipa ya damu ya moyo ambayo imebanana (stent).   Tangu kituo kianze kazi rasmi tarehe 30 Aprili, 2013 mpaka sasa watu 347 wamefanyiwa upasuaji wa moyo na watu watatu wamewekewa pacemaker tangu huduma hiyo ianze Novemba, 2013.  Mapema mwakani kituo kinatarajiwa kuanza huduma ya kuweka stent.
Kituo hiki ni kipya hivyo katika mwaka 2014 tutaendelea kukijengea uwezo wa vifaa tiba, wataalamu na mahitaji mengine muhimu ili kulipunguzia taifa mzigo wa kupeleka wagonjwa nchi za nje. Serikali, pia itaendeleza ushirikiano wake na uongozi wa Hospitali ya Kanda ya Bugando kuboresha huduma ya upasuaji mkubwa wa moyo katika hospitali hiyo.  Huduma hiyo ilizinduliwa tarehe 26 Oktoba, 2013 na Makamu wa Rais Mheshimiwa Daktari Mohamed Ghalib Bilal.

Saratani
Ndugu Wananchi;
  Kwa upande wa maradhi ya saratani, Februari, 2013 jengo jipya la kulaza wagonjwa 170 lilifunguliwa katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road. Kufunguliwa kwa jengo hilo kumeongeza uwezo wa taasisi yetu hiyo kulaza wagonjwa 290 badala ya 120 tu kabla ya hapo. Ujenzi wa jengo hili jipya umesaidia sana watu wengi zaidi kuhudumiwa na kupunguza msongamano mkubwa wa wagonjwa uliokuwepo.

Figo
Ndugu Wananchi;
Kuhusu maradhi ya figo mwaka huu pia tumeshuhudia huduma ya usafishaji wa figo zenye matatizo ikipanuliwa.  Huduma hiyo imeanzishwa tena katika Hospitali ya Kanda ya Mbeya na imeanzishwa kwa mara ya kwanza katika Chuo cha Tiba katika Chuo Kikuu cha Dodoma.  Pale Mbeya tayari wagonjwa 93 wamehudumiwa mwaka huu na kuwapa matumaini mapya ya maisha yao.  Kwa pale Chuo Kikuu cha Dodoma, ujenzi wa kituo kikubwa kitakachobobea kwa magonjwa ya figo unaendelea na unategemewa kukamilika mapema mwaka 2014.

Mafunzo
Ndugu Wananchi;
Katika mwaka 2013 tumefungua ukurasa mpya katika jitihada zetu za kuongeza wataalamu wa afya nchini.  Chuo cha Sayansi ya Tiba katika Chuo Kikuu cha Dodoma kimefanya mahafali yake ya kwanza ambapo wanafunzi 50 wa Shahada ya Uuguzi walihitimu.  Tunatarajia kuanza kupata madaktari kuanzia mwaka 2014.
Kwa upande wa mchakato wa kujenga makazi mapya ya Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili kule Mloganzila mchakato umeanza. Ujenzi wa miundombinu ya barabara, maji na umeme unaendelea hivi sasa.  Mwaka 2014 ujenzi wa Hospitali ya kisasa ya kufundishia yenye vitanda 650 utaanza. Ujenzi wa Mlonganzila ukikamilika Chuo Kikuu cha Muhimbili kitaweza kuchukua wanafunzi 15,000 wa fani zote  ukilinganisha na 3,060 wa sasa.  Hatua hiyo itaongeza sana uwezo na kasi yetu ya kupunguza uhaba wa Madaktari, Wauguzi na wataalam wengine wa afya.

Nyumba
Ndugu Wananchi;
Katika mwaka 2013 ujenzi wa nyumba 35 za kuishi watumishi wa afya katika mikoa ya Mtwara (5), Rukwa (20) na Singida (10) umekamilika.  Ujenzi wa nyumba 100 unaendelea.  Nyumba hizo ni sehemu ya mpango wa ujenzi wa nyumba 580 zinazojengwa kwa ushirikiano kati ya Serikali na Global Fund kwa awamu mbili.  Awamu ya kwanza zinajengwa nyumba 310 ambapo taasisi ya Benjamin William Mkapa Foundation ndiyo mtekelezaji wa ujenzi huo.  Napenda kutumia nafasi hii kutoa shukrani za dhati kwa Rais Mstaafu Mheshimiwa Benjamin Mkapa kwa mchango wake mkubwa alioutoa na anaoendelea kutoa kwa maendeleo ya nchi yetu na watu wake.

Ujenzi wa Miundombinu
Ndugu wananchi;
Katika mwaka 2013, tumeendelea kupata mafanikio makubwa katika kuboresha miundombinu ya usafiri wa ardhini, majini na angani. Kasi ya ujenzi wa barabara imeendelea kufanyika kote nchini. Kazi ya ujenzi ingekuwa nzuri zaidi kama mtiririko wa malipo kwa Wakandarasi ungekuwa mzuri.  Tatizo hili tutalitafutia ufumbuzi mwaka 2014 ili kasi ya ujenzi wa barabara za lami nchini iwe nzuri zaidi.
Pamoja na hayo mwaka huu kilomita 877 za barabara zimekamilika. Ujenzi wa daraja la Malagarasi nao umekamilika kinachosubiriwa ni sherehe za uzinduzi. Ujenzi wa daraja la Kilombero umeanza na ule wa daraja la Kigamboni unaendelea vizuri. Tunatarajia kuwa mwakani tutaongeza zaidi kasi ya ujenzi wa barabara zilizosalia ikiwa ni pamoja na kujenga baadhi ya barabara kwa ubia na sekta binafsi.  Kwa kasi na mwenendo tunaoendelea nao sasa naamini ifikapo mwaka 2015 tutakuwa tumefikia hatua ya juu sana katika shabaha yetu ya kuunganisha mikoa yote nchini kwa barabara za lami.
  
Ndugu Wananchi;
Jitihada za kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam zimeendelea kutekelezwa.  Barabara kadhaa zilipanuliwa na kazi inaendelea.  Ujenzi wa njia ya kupita mabasi yaendayo haraka umeendelea kwa kasi ya kuridhisha.  Mchakato wa ujenzi wa barabara za juu ya nyingine katika njia panda za TAZARA na Ubungo umeshaanza.  Mwaka ujao huduma ya usafiri wa treni kusafirisha abiria Dar es Salaam itaongezwa ili watu wengi zaidi wanufaike.

Ndugu wananchi;
Mwaka huu, kwa upande wa reli ya kati, kazi ya kuboresha njia ya reli imeendelea kufanyika na itaendelea mwaka 2014.  Mwakani (2014) Shirika la Reli litapokea injini mpya 13, mabehewa ya mizigo 274 na breki 34 hivyo kuboresha sana huduma katika reli ya kati.  Kuhusu ujenzi wa reli mpya ya upana wa kimataifa ni matarajio yetu kuwa kama kila kitu kitaenda sawa mchakato wa ujenzi utaanza katika nusu ya pili ya mwaka 2014.

Ndugu Wananchi;
Tumetoa kipaumbele cha juu katika kuboresha huduma ya usafiri wa anga nchini.  Mwaka huu, tumeendelea na ukarabati, upanuzi na ujenzi wa viwanja vya ndege vya Mikoa ya Kilimanjaro, Kigoma, Tabora, Mwanza, Arusha, Mtwara na Kagera.  Ni jambo la kufurahisha kuona Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe ukianza kutumika. Hatimaye ndoto imetimia.  Mwaka wa 2014 ujenzi wa majengo mengine ya kuhudumia abiria, mizigo na ndege utaendelea katika uwanja huo.
Pia ni furaha iliyoje kwamba upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Mafia na ujenzi wa gati la Kilindoni vimekamilika.  Kero ya miaka mingi imepatiwa ufumbuzi.  Kazi ya ujenzi wa jengo jipya la abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere itaanza rasmi mwaka 2014.

Nishati
Ndugu wananchi;
Dhamira yetu ya kutaka Tanzania iwe na umeme wa uhakika na unaonufaisha watu wengi imepata sura na mwelekeo mzuri mwaka huu 2013.  Ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara na Songosongo kuja Dar es Salaam umeanza na utekelezaji unakwenda vizuri.  Kama ujenzi wa bomba utakamilika kama inavyotarajiwa na ujenzi wa mitambo ya kuzalisha umeme Kinyerezi utaenda kama ilivyopangwa, ifikapo mwaka 2015 Tanzania itafikia lengo la kuzalisha megawati 3,000 za umeme.

Ndugu Wananchi;
Bahati nzuri mwaka huu, kufuatia kuongezewa fedha za bajeti, kasi ya usambazaji umeme imekuwa nzuri.  Tunaumaliza mwaka huku idadi ya Watanzania waliounganishiwa umeme ikiwa imefikia asilimia 24 ukilinganisha na asilimia 21 mwaka 2012 na asilimia 10 mwaka 2005. Haya si mafanikio madogo. Kwa mwelekeo huu, kufikia lengo la asilimia 30 ya Watanzania kupata umeme mwaka 2015 ni jambo la uhakika kabisa sasa. Tena kuna uwezekano mkubwa wa kulivuka lengo hilo.

Ushirikiano wa Kanda
Watanzania Wenzangu;
Katika mwaka 2013, nchi yetu imeendelea kushiriki vizuri katika shughuli za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambazo sisi ni wanachama.   Mwezi wa Agosti, 2013 tulikabidhi Uenyekiti wa chombo cha SADC kinachoshughulikia Siasa, Ulinzi na Usalama kwa Namibia. Tulikuwa tumemaliza kipindi chetu cha mwaka mmoja.
Katika kipindi chetu cha uongozi tulishiriki kwa ukamilifu kutafuta suluhu kwa mizozo na migogoro ya kisiasa na kiusalama nchini Zimbabwe, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Madagascar.  Tunafurahi kuona kwamba mambo katika nchi zote hizo sasa yanakwenda vizuri. Nchini Zimbabwe utulivu umerejea baada ya kufanyika kwa uchaguzi mwezi Julai, 2013. Nchi ya Madagascar nayo imemaliza duru ya pili ya uchaguzi wa Rais kwa usalama. Matokeo yanatarajiwa kutangazwa tarehe 7 Januari, 2014.  Ni matumaini yetu kuwa watu wa nchi hiyo watayapokea matokeo hayo na wataelekeza nguvu zao katika kujenga umoja na maridhiano ili wajenge upya uchumi wa nchi yao.
Kwa upande wa Mashariki ya Kongo, tishio kubwa la  usalama kutokana na vitendo vya kundi la waasi la M23 limezimwa na Jeshi la Kongo kwa kushirikiana na Jeshi la Umoja wa Mataifa.  Kama mjuavyo Tanzania ni moja ya nchi zinazochangia maafisa na askari wa Jeshi hilo.

Ndugu Wananchi;
Napenda kutumia nafasi hii, kwa mara nyingine tena kutoa pongezi zangu za dhati kwa wanajeshi wetu kwa kazi yao nzuri na iliyotukuka waliyoifanya huko Mashariki ya Kongo. Pia nawapongeza wanajeshi wetu walioko Darfur na Lebanon kwa kazi yao njema waifanyayo. Wote nawaomba waendelee kudumisha nidhamu na weledi, mambo yaliyowafanya wapewe sifa nyingi na kuheshimiwa. Wameiletea nchi yetu heshima kubwa.
Bahati mbaya, katika kutimiza wajibu wao huo wa kimataifa tumepoteza vijana wetu 10, saba Darfur na watatu Kongo.    Narudia kutoa pole kwa Jeshi letu na familia za marehemu kwa msiba mkubwa uliowakuta.  Napenda kuwahakikishia kuwa daima tutauthamini na kuuenzi mchango wao.  Wanajeshi wote tunawatakia heri na fanaka tele katika mwaka 2014.

Jumuiya ya Afrika Mashariki
Ndugu Wananchi;
Mwaka huu, ushiriki wetu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki umepita katika mtihani kidogo kufuatia ndugu zetu wa Uganda, Rwanda na Kenya kufanya mambo ambayo yalijenga hisia ya kuwepo mifarakano.  Pia yalileta hofu kuwa hata uhai wa Jumuiya yenyewe ulikuwa mashakani.  Katika mkutano uliopita wa Wakuu wa Nchi wanachama wa Jumuiya uliofanyika tarehe 30 Novemba, 2013 mambo hayo tuliyazungumza kwa uwazi na kidugu.  Tumeelewana kuwa yaliyopita si ndwele tugange yajayo.

Ndugu Wananchi;
Katika mkutano wa Kampala tuliamua mambo matatu makubwa na muhimu katika kuendeleza agenda ya utangamano wa Afrika Mashariki. La kwanza,  tulikubaliana kuhusu Itifaki ya kuanzisha Umoja wa Fedha wa Afrika Mashariki na kutia saini.  Hii ndiyo hatua ya juu ya utangamano wa kiuchumi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.  Tumekuwa tunashirikiana katika kuwianisha sera za uchumi, fedha na bajeti, kwa uamuzi huu sasa tunaelekea kwenye kuwa na sera moja ya fedha na bajeti kwa mambo hayo na hatimaye sarafu moja.  Baada ya hatua hii, inayofuata ni ile ya utangamano wa kisiasa, yaani Shirikisho la Kisiasa.  Katika mkutano wetu wa Kampala tulikubaliana kuwa nchi wanachama ambazo hazijakamilisha kutoa maoni yao, zifanye hivyo kisha baada ya hapo tuzungumzie jambo hilo na kulipa mwelekeo.

Ndugu Wananchi;
Vilevile katika kikao chetu cha Kampala, tuliridhia mpango wa utekelezaji wa uamuzi wetu wa awali wa kuanzisha Himaya Moja ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.  Lengo la mfumo au utaratibu huu ni kufanikisha utekelezaji wa malengo na madhumuni ya Umoja wa Forodha wa Afrika Mashariki.  Utaratibu huu utarahisisha na kuharakisha uingizaji na utoaji wa bidhaa katika bandari na mipaka ya nchi za Afrika Mashariki. Pia, utaondoa vikwazo visivyokuwa vya kodi katika uingizaji na usafirishaji wa bidhaa kutoka nchi wanachama kwenda nchi nyingine. Kwa jumla, Himaya Moja ya Forodha itasaidia biashara kukua na hivyo uchumi wa nchi wanachama kukua na kuboresha ustawi wa wananchi wa Afrika Mashariki.
 Narudia kuwakumbusha wenzetu wa Wizara ya Afrika Mashariki na Wizara ya Fedha kutengeneza utaratibu mzuri wa kuelimisha jamii kuhusu Umoja wa Fedha na Himaya Moja ya Forodha.  Nawataka Wizara ya Fedha, Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Afrika Mashariki, Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Uchukuzi, Mamlaka ya Bandari, Mamlaka ya Mapato na Jeshi la Polisi, kuhakikisha kuwa taratibu zote husika kuhusu Himaya Moja ya Forodha zinakamilishwa mapema.  Nia yangu na yetu sote ni kuona utekelezaji unaanza mara moja.  Hili ni jambo lenye maslahi makubwa kwa nchi yetu.

Medani za Kimataifa
Ndugu Wananchi;
Katika medani za kimataifa, mwaka 2013 ulikuwa mzuri kwa Tanzania. Nyota ya nchi yetu iliendelea kuangaza vizuri. Tumeendelea kuwa na uhusiano mwema na mataifa yote duniani  na hakuna nchi ambayo tuna uadui nayo. Pia tuna uhusiano mzuri na mashirika  ya kimataifa na kikanda yanayoshughulikia masula ya siasa, fedha na maendeleo.  Vile vile, tuna uhusiano mzuri na watu mashuhuri na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yanayoshughulikia masuala ya maendeleo na ya kibinadamu.
Kwa sababu hiyo tumepata misaada mingi ya maendeleo na ya kibinadamu iliyochangia katika mafanikio tuliyoyapata katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii mwaka 2013.  Napenda kwa niaba yenu nitumie nafasi hii kutoa shukrani zangu za dhati kwa nchi, mashirika na watu waliochangia katika maendeleo ya nchi yetu mwaka huu. Wakati tukiwashukuru, napenda kuwakumbusha kuwa misaada yao bado tunaihitaji mwaka ujao (2014) na miaka inayofuatia.

Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa wageni, mwaka huu ulikuwa wa baraka sana kwa Tanzania.  Tumepata heshima ya aina yake ya kutembelewa na Rais wa China, Mheshimiwa Xi Jiping tarehe 24 – 25 Machi, 2013 na Rais wa Marekani Mheshimiwa Barack Obama tarehe 01 - 02 Julai, 2013.  Pia tulitembelewa na Rais wa Sri Lanka Mheshimiwa Mahinda Rajapaksa tarehe 26 – 27 Juni, 2013.  Waziri Mkuu wa Thailand, Mheshimiwa Yingluck Shinawatra tarehe 30 Julai mpaka Agosti 1, 2013 Pamoja na hao, tulipokea Wakuu wa Nchi na Serikali 19 waliokuja kushiriki mkutano wa Smart Partnership Dialogue uliofanyika Dar es Salaam tarehe 28 Juni, 2013.

Ndugu Wananchi;
Vilevile, tulitembelewa na Marais Wastaafu wa Marekani, Mheshimiwa Bill Clinton na Mheshimiwa George W. Bush.  Nchi yetu inanufaika na misaada inayotolewa na mashirika yao katika nyanja za afya na kilimo.  Napenda kutumia nafasi hii kuwashukuru wageni wetu wote hao kwa uamuzi wao wa kuja kututembelea.  Wameipa nchi yetu heshima kubwa.  Ni matumaini yetu kuwa mwaka 2014 utaendelea kuwa wa baraka kama huu tunaoumaliza leo. Pia nawashukuru sana Watanzania wenzangu kwa kuwapokea vizuri wageni wetu.  Wameondoka nchini wakiwa na furaha kubwa na kumbukumbu nzuri kuhusu nchi yetu.
Licha ya kutembelewa, mimi na viongozi wenzangu Wakuu wa Nchi yetu tulialikwa na kufanya ziara katika nchi mbalimbali duniani.  Pia tumeshirikishwa katika mikutano mbalimbali ya kimataifa.   Ziara hizo zimekuwa na manufaa makubwa kwa nchi yetu.

Ndugu Wananchi;
Katika kikao cha Wakuu wa Nchi wa Umoja wa Afrika kilichofanyia mwezi Januari, 2013 nilichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Wakuu wa Nchi za Afrika ya kushughulikia masuala ya mabadiliko ya tabia nchi.  Mwenyekiti wa Kamati hiyo ndiye huwa mwakilishi na msemaji wa Bara la Afrika katika majukwaa ya kimataifa ambapo masuala hayo yanazungumzwa au kushughulikiwa.
Kwa ajili hiyo nilikwenda Warsaw, Poland kuhudhuria Mkutano Mkuu wa 19 wa Mabadiliko ya Tabia Nchi uliofanyika tarehe 11 – 22 Novemba, 2013.  Katika mkutano huo hatukufanikiwa vya kutosha. Hivi sasa matumaini yetu yapo katika mkutano wa mwakani (2014) nchini Peru.  Iwapo tutafanikiwa tutakuwa tumejenga msingi mzuri utakaowezesha Mkutano wa Paris mwaka 2015 kufanikiwa kupatikana Mkataba wa Kimataifa unaozifanya nchi ziwajibike kisheria kwa masuala yahusuyo kupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi.  Ikishindikana Peru na kama mataifa yataendelea kukaidi katika mkutano wa Paris, hatma ya dunia yetu itakuwa mashakani kwani hali si nzuri hata kidogo.

Ndugu Wananchi;
Mwaka huu tunaoumaliza nchi za SADC tumepoteza mmoja wa viongozi wetu mashuhuri, shujaa Nelson Mandela.  Nilipata nafasi ya kuwawakilisha katika sala ya kitaifa, kutoa heshima za mwisho na mazishi yake. Kule Qunu, nilipewa nafasi ya kuzungumza ambayo niliitumia kuelezea uhusiano wetu na shujaa Mandela, ANC na mchango wa Tanzania kwa ukombozi wa kusini mwa Afrika.  Hotuba yetu ilipokelewa vizuri sana na wenyeji kwani niliwaelezea baadhi ya mambo ambayo walikuwa hawayajui.  Watu wengi wa Afrika Kusini na duniani kwa jumla sasa wanaufahamu vizuri mchango mkubwa wa nchi yetu kwa ukombozi wa Afrika Kusini.  Tuendelee kumuomba Mwenyezi Mungu ailaze mahala pema, peponi roho ya shujaa Nelson Mandela.

Miaka 50 ya Mapinduzi na Muungano
Ndugu Wananchi;
Mwaka ujao (2014) ni wa aina yake katika historia ya nchi yetu.  Ni mwaka ambao tunatimiza miaka 50 tangu Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Januari 12,1964 na miaka 50  ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika ziungane na kuzaliwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Aprili 26, 1964. Ni mwaka wa kutambua na kusheherekea mafanikio tuliyoyapata.  Lakini, ni mwaka wa kuweka nadhiri ya kupata mafanikio makubwa zaidi miaka 50 ijayo na kuendelea. Tutakiane heri katika kusheherekea siku hizo adhimu.

Shukurani
Ndugu Wananchi;
Napenda kuchukua nafasi hii adhimu kuwashukuru kwa dhati Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Pinda, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Balozi Seif Ali Idd.  Viongozi Wakuu wenzangu hao nawashukuru kwa msaada mkubwa walionipa na wanaoendelea kunipa katika kuiongoza nchi yetu mwaka 2013. Naomba tuendelee hivyo mwaka 2014 kwa maslahi ya nchi yetu na watu wake.
Nawashukuru pia Mawaziri na viongozi wengine wa Serikali zetu mbili kwa kazi nzuri waliyofanya ya kuongoza na kusimamia utekelezaji wa miradi na shughuli mbalimbali za Serikali.  Kazi yao nzuri ndiyo iliyotupatia mafanikio tunaojivunia leo. Naomba sote tutambue kuwa bado zipo mbele yetu kazi nyingi na changamoto kubwa na nzito za kushughulikia katika jitihada zetu za kuwaletea wananchi na nchi yetu maendeleo.  Tunao wajibu wa kudumisha umoja, mshikamano, amani na utulivu wa nchi yetu.  Hatuna budi kuendelea kushirikiana na kusaidiana pamoja na kufanya kazi kwa bidii zaidi mwaka ujao 2014 kwa niaba na kwa maslahi ya watu waliotuchagua.

Ndugu Wananchi;
Kwa namna ya pekee nawashukuru sana Watanzania wote po pote pale walipo kwa kuunga mkono juhudi za Serikali na kufanya kazi kwa bidii na maarifa kujiletea maendeleo.  Hali kadhalika nawapongeza kwa uelewa wenu ulioiwezesha nchi yetu kuendelea kuwa kisiwa cha amani. Nawaomba tuendelee na moyo huo wa kuipenda nchi yetu na kujitolea kwa ajili ya utulivu wake na maendeleo yake na yetu sote.
Naomba pia nimalize kwa kuwashukuru viongozi wetu wa dini wa madhehebu mbalimbali pamoja na waumini wao kwa sala na maombi katika kipindi chote cha mwaka unaoisha leo. Sala zao na maombi yao yametupa nguvu na faraja katika vipindi vigumu ambavyo tumevipitia. Naomba muendelee kuliombea taifa letu ili lipate baraka na neema ya Mwenyezi Mungu.

Mwisho
 Ndugu Wananchi;
Naomba tuzidi kuombeana heri ili mwaka ujao uwe wa baraka na  mafanikio makubwa zaidi. Twendeni tukasherehekee mwaka mpya kwa amani na utulivu. Nawatakia heri na fanaka tele katika  mwaka mpya wa 2014.
Mungu Ibariki Tanzania,
Mungu Ibariki Afrika.
Asanteni sana kwa kunisikiliza.

0 comments:

Post a Comment