HOTUBA YA MHESHIMIWA MIZENGO P. PINDA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA
MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA KUHITIMISHA SHUGHULI ZA MKUTANO WA 13 WA
BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
TAREHE 09 NOVEMBA, 2013
I: UTANGULIZI
a)
Masuala ya Jumla
Mheshimiwa
Spika,
1.
Leo
tunahitimisha shughuli za Mkutano wa Kumi na Tatu wa Bunge lako Tukufu. Ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu mwenye
wingi wa Rehema kwa kutufikisha salama siku ya leo.
Mheshimiwa
Spika,
2.
Mkutano huu ulijumuisha kazi kubwa zifuatazo:
Kwanza: Kujadili Mapendekezo
ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2014/2015;
Pili: Kujadili Muswada wa
Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali wa Mwaka 2013, [The Written Laws (Miscellaneous Amendments (No. 3) Bill 2013];
Tatu: Kujadili Muswada wa
Sheria ya Mfuko wa Akiba wa GEPF wa Mafao ya Wastaafu wa Mwaka 2013 [The GEPF Retirement Benefit Bill, 2013];
na
Nne: Kujadili Muswada wa
Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba (The Constitutional Review Act) sura ya 83.
3.
Nitumie
nafasi hii kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa kushiriki katika Kamati ya
Mipango hapa Bungeni kwa kujadili kwa kina mapendekezo yaliyowasilishwa na
Serikali kuhusu Mpango wa Maendeleo wa
Taifa wa mwaka 2014/2015. Napenda
kuwahakikishia kuwa, maoni na ushauri kama yalivyotolewa na Waheshimiwa Wabunge
yatazingatiwa na Serikali kila moja kwa uzito wake wakati wa maandalizi ya
Bajeti ya 2014/2015. Vilevile niwashukuru kwa kujadili na kupitisha Muswada wa
Sheria ya Mfuko wa Akiba wa GEPF wa Mafao ya Wastaafu.
b)
Maswali
Mheshimiwa
Spika,
4.
Pamoja na kukamilisha kazi hizo muhimu,
pia katika Mkutano huu, jumla ya maswali 120
ya msingi na 305 ya nyongeza ya
Waheshimiwa Wabunge yalijibiwa na Serikali.
Aidha, Maswali 6 ya msingi na
6 ya nyongeza yalijibiwa kwa
utaratibu wa Maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu.
c)
Kauli za Mawaziri/Maazimio
Mheshimiwa
Spika,
5.
Mkutano
huu pamoja na kazi za msingi zilizopangwa, Waheshimiwa Wabunge walipata
fursa ya kujadili Azimio
la Kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kuhusu msimamo wake katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
(d) Hotuba ya Mheshimiwa Rais,
Mheshimiwa Spika,
6.
Katika
Mkutano huu pia, Waheshimiwa Wabunge walipata fursa ya kumsikiliza Mheshimiwa
Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akizungumza
na Wananchi kupitia Bunge lako Tukufu.
Mtakubaliana nami kwamba hotuba ya Mheshimiwa Rais ilikuwa nzito na
yenye kuonesha umakini, umahiri na busara ambazo ni sifa mojawapo za Rais wetu
kati ya nyingi nzuri alizonazo. Tunachotakiwa ni kutumia maelekezo ya
Mheshimiwa Rais kwa kuyafikisha kwa Wananchi katika maeneo yetu ili nao waweze
kuelewa hali halisi ya yanayotokea katika Jumuiya yetu. Aidha, Hotuba ya Rais
imegusa maeneo mengine ambayo sisi Wabunge tunatakiwa kushirikiana na Wananchi katika
kujipanga vizuri namna ya kukabiliana na matatizo yaliyojitokeza.
II: UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI YA MWAKA
2013/2014
(a) Mwenendo wa Mapato na
Matumizi ya Serikali katika Robo ya
Kwanza ya Mwaka 2013/2014
Mheshimiwa
Spika,
7.
Hotuba
yangu kwa leo imejikita zaidi kuelezea utekelezaji wa Mpango wa Bajeti ya Mwaka
2013/2014 na maeneo machache katika Sekta ya Kilimo na Nishati. Lakini kabla ya
kuelezea mwenendo wa Mapato na Matumizi ya Serikali katika Robo ya Kwanza ya
mwaka 2013/2014, naomba kueleza kwa muhtasari kuhusu mwenendo wa baadhi ya
viashiria muhimu vya uchumi hususan Ukuaji wa Uchumi na Mfumuko wa Bei. Taarifa
za awali zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu zinaonesha kwamba Ukuaji wa
Pato la Halisi la Taifa katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2013, ulikuwa
Asilimia 7.0 ikilinganishwa na
ukuaji wa Asilimia 6.9 katika
kipindi kama hicho mwaka 2012. Sekta
zilizoonesha kuwa na Viwango vikubwa vya ukuaji ni pamoja na Sekta ya
Mawasiliano na Usafirishaji ambayo imekua kwa Asilimia 18.4, Sekta ya Fedha Asilimia 14.6
na Sekta ya Ujenzi Asilimia 8.7.
Mheshimiwa
Spika,
8.
Kwa
upande wa Mfumuko wa Bei, takwimu zinaonesha kuwa kasi ya upandaji bei
imepungua kutoka Wastani wa Asilimia 13.5
Mwezi Septemba, 2012 hadi Asilimia 6.1
Mwezi Septemba, 2013. Kushuka kwa Mfumuko wa Bei kumechangiwa zaidi na
upatikanaji wa chakula cha kutosha ndani ya Nchi. Mwenendo huu mzuri wa
viashiria vya uchumi jumla unatupa matumaini makubwa kwamba jitihada za
Serikali za kuimarisha usimamizi wa Uchumi na kuleta Maendeleo endelevu ya
Wananchi wetu zinaanza kuzaa matunda.
Mheshimiwa Spika,
9.
Katika
Robo ya Kwanza ya mwaka 2013/2014 kuanzia Mwezi Julai hadi Septemba 2013,
Mapato yote yaliyokusanywa na Hazina yalifikia Shilingi Trilioni 3.08; sawa na Asilimia 85.7 ya makadirio ya Shilingi Trilioni 3.59. Pamoja na mwenendo huo wa
ukusanyaji mapato, changamoto kubwa zinazokabili eneo la Mapato ya Serikali ni
kuchelewa kuanza kwa wakati kwa ukusanyaji wa Mapato katika baadhi ya vyanzo
vya mapato. Changamoto nyingine ni Miundombinu isiyokidhi mahitaji ya
usafirishaji endelevu hasa reli ya kati, bandari, usafiri wa Anga na barabara. Miundombinu Bora ni muhimu katika kuchochea
ukuaji wa Uchumi na Kukuza Ajira; na hivyo kuiwezesha Serikali kukusanya mapato
zaidi kutokana na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi. Serikali inafanyia kazi
changamoto hizo ili kuzipatia ufumbuzi mapema.
Mheshimiwa Spika,
10.
Kwa
upande wa matumizi, hadi kufikia
mwezi Septemba 2013; matumizi yalifikia Shilingi Bilioni 3,806.5, sawa na Asilimia 98.5
ya lengo la kutumia Shilingi Bilioni 3,854.2.
Kati ya matumizi hayo, Shilingi Bilioni 3,058 ni Matumizi ya Kawaida na Shilingi Bilioni 747.9 ni Matumizi ya Maendeleo. Katika kipindi hiki, sehemu kubwa ya matumizi
ya Serikali ya Kawaida na Maendeleo imeelekezwa katika maeneo yenye kuleta
ufanisi na tija kubwa kama vile kuboresha miundombinu ya barabara, ambayo mgao wake ulikuwa Shilingi Bilioni 182.5 za Matumizi ya Kawaida na Maendeleo,
Sekta ya Elimu Shilingi Bilioni 229.2; Sekta ya Nishati, Shilingi Bilioni 159.9;
Sekta ya Kilimo Shilingi Bilioni 119.6 na Sekta ya Maji Shilingi Bilioni 51.3.
Vilevile, Serikali imelipa Mishahara ya Watumishi wa Umma
kwa wakati. Changamoto kubwa iliyopo kwenye matumizi ya Serikali ni kuwepo kwa
mahitaji makubwa ya matumizi yasiyowiana na mapato; jambo ambalo linailazimu
Serikali kukopa kutoka Mabenki ya Ndani. Serikali itaendelea kuoanisha Matumizi
na ukusanyaji wa Mapato, hasa yale ya ndani pamoja na kuzingatia viwango vya Matumizi
vilivyoidhinishwa na Bunge. Aidha, Serikali itaendelea kuweka msisitizo wa
kuelekeza Matumizi kwenye vipaumbele vilivyoainishwa katika Bajeti ya Serikali
ambavyo ni vyanzo muhimu vya kuongeza Mapato, Kukuza Uchumi na Kupunguza
Umaskini.
III: UTEKELEZAJI
WA MFUMO MPYA WA TEKELEZA KWA MATOKEO MAKUBWA SASA (BIG RESULTS NOW - BRN)
(a)
Muundo wa Mfumo
Mheshimiwa
Spika,
11.
Waheshimiwa Wabunge watakumbuka kuwa Serikali ilianzisha Mfumo
mpya wa “Tekeleza kwa Matokeo Makubwa
Sasa au Big Results Now (BRN) ili kuongeza ufanisi katika usimamizi,
ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa Mipango yetu ya Maendeleo, hususan, Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano
(2011/2012 - 2015/2016). Hatua hii
ilichukuliwa baada ya kuona namna Mfumo kama huo ulivyoziwezesha Nchi kadhaa,
na hasa Nchi ya Malaysia, kupiga hatua kubwa za
kimaendeleo kiuchumi na kijamii katika kipindi kifupi. Kwa ukumbusho tu, Mfumo huo
unatekelezwa katika Maeneo Sita ya Matokeo muhimu Kitaifa (National Key Results Areas) katika awamu yake ya kwanza, ambayo ni Nishati ya Umeme; Uchukuzi; Kilimo; Elimu;
Maji na Ukusanyaji wa Mapato;
Mheshimiwa Spika,
12.
Katika Hotuba yangu ya
kuahirisha Mkutano wa Kumi na Mbili wa Bunge, tarehe 6 Septemba 2013, nilitoa
taarifa ya awali kuhusu utekelezaji wa Mfumo huu Mpya kwa kipindi cha kuanzia
mwezi Julai hadi Septemba, 2013. Katika taarifa hiyo, nilieleza kuwa tumepiga hatua za kuridhisha katika
uundaji wa Mfumo wa kuleta matokeo ya
haraka, ikiwa ni pamoja na kuanzisha na kuteua Uongozi wa juu wa Taasisi Maalum
yaani "President’s Delivery Bureau
(PDB)” inayomsaidia Mheshimiwa Rais kusimamia ipasavyo utekelezaji wa
Miradi na Programu zilizoainishwa. Hivi
sasa zoezi la kuajiri Watumishi wa Taasisi ya "President’s Delivery Bureau” na Vitengo vya Wizara vya
Ufuatiliaji yaani Ministerial Delivery
Units (MDUs) watakaochukua nafasi za Watumishi walioazimwa kutoka kwenye
Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali, Sekta Binafsi, na Asasi Zisizo za
Kiserikali ambao walikuwepo katika hatua zake za maandalizi limeanza. Ninapenda
kutumia fursa hii kuwashukuru wote waliotumika katika chombo hiki tangu
kilipoundwa kwa uzalendo na weledi waliouonesha katika kipindi hiki cha mwanzo
na cha mpito;
Mheshimiwa
Spika,
13.
Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba hadi sasa
vitengo vya ufuatiliaji katika Wizara zote sita (6) zinazosimamia utekelezaji
chini ya Mfumo huu mpya vimeanzishwa na vinaandaa Taarifa za utekelezaji za
kila wiki na kila mwezi, na kuziwasilisha kwenye Chombo cha President’s Delivery Bureau. Aidha,
Kamati Maalum za kusimamia utekelezaji zinazoongozwa na Mawaziri husika
zinakutana kila mwezi kujadili mwenendo wa utekelezaji na kushughulikia
changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika utekelezaji. Baraza la Kusimamia
Mageuzi na Utekelezaji (Transformation
and Delivery Council – (TDC)) limeundwa na lilikutana tarehe 11 Oktoba,
2013. Katika Kikao hicho, Baraza lilipokea na kujadili muhtasari wa Taarifa ya
utekelezaji wa Mfumo mpya wa Kusimamia, Kufuatilia na Kutathmini Miradi ya
Kipaumbele katika Maeneo Sita ya Matokeo ya Kitaifa. Baraza liliridhika na hatua za awali za utekelezaji na lilitoa mwongozo
stahiki wa hatua za kuchukuliwa pale ilipohitajika. Baraza litaendelea kukutana mara kwa
mara ili kutathmini na kutoa mwelekeo wa utekelezaji wa Mikakati iliyowekwa ya
Mfumo huu mpya;
(b)
Utekelezaji wa Mikakati katika Maeneo Makuu
Sita ya Matokeo Kitaifa;
Mheshimiwa Spika,
14.
Utekelezaji wa mikakati katika maeneo makuu sita ya
matokeo kitaifa ulianza mara baada ya uchambuzi wa maabara kukamilika.
Mafanikio ya kuridhisha yamepatikana katika kila moja ya maeneo yale sita, hasa
ikizingatiwa kwamba Mfumo huu ni mageuzi makubwa sana katika utendaji
Serikalini. Katika kipindi cha miezi mitatu ya mwanzo ya mwaka huu wa fedha,
kuanzia mwezi Julai hadi Septemba, 2013; baadhi ya matokeo yaliyopatikana ni
pamoja na yafuatayo:
(a)
Katika Sekta ya
Kilimo, Serikali inatekeleza miradi 26
ya umwagiliaji kwa Wakulima wadogo na pia imekarabati maghala 26 ya mpunga kati ya 39 yanayotumiwa na wakulima katika
maeneo yaliyopewa kipaumbele hasa katika eneo la SAGCOT.
(b)
Katika Sekta ya
Nishati ya Umeme, jumla ya Wateja wapya 27,494
wameunganishwa na kupatiwa umeme, ikiwa ni Asilimia 18.3 ya lengo la kuunganisha wateja wapya 150,000 hadi mwisho wa mwaka 2013/2014. Aidha, vipande vya Bomba la
Gesi 20,491 vinavyotosheleza ujenzi wa
Kilomita 243.8 za Bomba la Gesi tayari
vimewasili Nchini, na uchomeleaji wa Bomba la Gesi Asilia kutoka Mtwara hadi
Dar es Salaam umekamilika kwa Kilomita 124.3.
Vilevile,
Kilomita 447 za njia ya Bomba la
Gesi zimesafishwa;
(c)
Katika Sekta ya
Elimu, Shule za msingi 5,916
zilipatiwa mitihani ya marejeo na mazoezi, sawa na Asilimia 100 ya lengo la
mwaka. Aidha, Mafunzo Kazini kuhusu ufundishaji yametolewa kwa Walimu katika
Shule 1,325 sawa na Asilimia 65 ya lengo la Shule 2,048 kwa mwaka huu wa fedha;
(d)
Kwa upande wa huduma za maji, wananchi wapatao 752,000 waishio Vijijini wamepatiwa huduma ya maji. Mafanikio haya yanafanya idadi ya Wananchi waishio Vijijini ambao wanapata
majisafi na salama kufikia takribani Milioni
15.9. Kasi hii ya upanuzi wa huduma za Maji Vijijini imewezekana baada ya Wizara
ya Maji kugatua madaraka ya usimamizi wa miradi
husika kwa Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri za Wilaya, jambo ambalo
limewafanya Watendaji kuwajibika na kuharakisha utendaji wao wa kazi. Aidha, hatua
zilizochukuliwa zimeiwezesha Wizara ya Maji kuongeza ufanisi katika masuala ya
ununuzi wa huduma, ikiwemo ujenzi na vifaa vyake, kutoka wastani wa siku 265 za hapo awali hadi siku 90 za sasa.
Mheshimiwa
Spika,
15.
Mafanikio haya na mengine mengi ambayo sikuyataja hapa
yameonyesha kuwa tukidhamiria, tunaweza kubadilisha kabisa matokeo ya juhudi
zetu na kuifikia dhamira yetu ya kuwa ni Taifa la Kipato cha Kati ifikapo mwaka
2025;
Mheshimiwa Spika,
16.
Kufuatia mafunzo yaliyotolewa mapema mwezi Juni, 2013 kwa
Watendaji wa Wizara husika, Wakuu wa Mikoa wote, Makatibu Tawala wa Mikoa na
Wakuu wa Wilaya zote Nchini, mnamo Mwezi Septemba 2013 nilikutana na Wakuu wa
Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa yote Tanzania Bara ili kujadili kwa kina
Taarifa za utekelezaji wa Miradi ya kipaumbele chini ya Mfumo huu. Aidha, katika
Vikao hivyo, nimezielekeza Wizara, Mikoa na Halmashauri zote Nchini kufanya
yafuatayo:-
(a)
Kuchambua miradi
iliyopangwa kutekelezwa katika mwaka huu wa fedha ambayo ipo nje ya Mfumo wa “Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa” kwa
kutambua manufaa yanayotarajiwa baada ya kukamilika na mahitaji halisi;
(b)
Kuipanga miradi hiyo kwa kipaumbele ili kuweka mkazo katika miradi itakayokamilika haraka
na kuwa na manufaa makubwa kwa Wananchi; na,
(c)
Kuweka utaratibu wa
Kimfumo na Kitaasisi wa kufuatilia utekelezaji wa miradi ya kipaumbele.
Mheshimiwa Spika,
17.
Ninafurahi kutoa taarifa kuwa Wizara na Tawala za Mikoa
na Mamlaka za Serikali za Mitaa zimeupokea mfumo wa Tekeleza kwa Matokeo
Makubwa Sasa kwa hamasa kubwa. Ili kuhakikisha azma yao ya kutekeleza majukumu
yao katika Mfumo huu kikamilifu, iliamuliwa kuwa Viundwe Vitengo vya kusimamia
utekelezaji katika Ngazi ya Mkoa (Regional
Delivery Units (RDUs), sambamba na vile Vitengo vya ufuatiliaji vya Wizara
ili utekelezaji katika Maeneo Makuu ya Matokeo Kitaifa ufanyike kwa ufanisi na
umakini stahiki. Hatua hii inazingatia umuhimu wa kuhakikisha kuwa maeneo kama
Elimu na Maji ambayo Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa zina mchango mkubwa
katika utekelezaji yanapata msukumo wa kutosha. Kazi hii imeshaanza, na taarifa
zilizowasilishwa ni za kutia moyo sana.
Mheshishimiwa Spika,
18.
Kwa
kuzingatia mafanikio ya awali yaliyopatikana, Serikali imetoa maelekezo kwa
Wizara, Idara na Taasisi ambazo bado hazijaingia katika Mfumo wa Tekeleza kwa Matokeo
Makubwa Sasa zisisubiri hadi zitakapoingia rasmi bali zianze kujipanga na
kutekeleza mipango, miradi na program zao kwa kutumia mbinu ambazo zinatumika
katika Mfumo huo pamoja na Rasilimali fedha na Wataalam waliopo. Msisitizo ni kwamba Wizara zote na Mikoa
ijipange upya na kuongeza ubunifu na kufanya vizuri zaidi katika kuimarisha
usimamizi wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha kwamba Taifa letu linafikia
malengo ya maendeleo tuliyojiwekea katika Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025.
Aidha, napenda kutumia fursa hii kutoa wito kwa Wizara, Mikoa na Mamlaka za
Serikali za Mitaa kuimarisha usimamizi wa Watendaji wao kwa kuzingatia taratibu
za uwajibikaji zilizowekwa chini ya mfumo huu mpya ili kuleta ufanisi na tija
ya utendaji Serikalini pamoja na kupata matokeo makubwa tarajiwa ya Kukuza
Uchumi na kuondoa umaskini;
IV: MAPENDEKEZO YA MPANGO WA MAENDELEO YA TAIFA
WA MWAKA 2014/2015
Mheshimiwa Spika,
19.
Mwanzoni mwa Mkutano huu
wa Bunge Serikali iliwasilisha Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo 2014/2015. Napenda kutumia
fursa hii tena kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge kwa maoni na michango yao mizuri
ambayo itatuwezesha kuboresha Mpango na Bajeti ya Mwaka ujao wa Fedha
2014/2015. Aidha, namshukuru Mheshimiwa Stephen Wasira (Mb.) pamoja na
Waheshimiwa Mawaziri wa Kisekta waliotoa maelezo fasaha ya ufafanuzi wa Hoja
zilizojitokeza wakati wa Mjadala wa Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo. Kwa
kuzingatia michango mizuri na yenye tija iliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge na
Waheshimiwa Mawaziri wakati wa kujadili Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya
Taifa wa mwaka 2014/2015, nami naomba uniruhusu kusisitiza mambo machache kama
ifuatavyo:
Mheshimiwa Spika,
20.
Kama
Waheshimiwa Wabunge watakavyokumbuka katika majadiliano
yaliyokuwa yanaendelea, moja ya jambo ambalo Waheshimiwa Wabunge
wamelizungumzia kwa kina, ni juu ya wingi wa vipaumbele vya Taifa. Aidha,
imeonekana pia kuwa miradi ya maendeleo
ni mingi sana kiasi kinachosababisha
miradi hiyo kutotekelezeka kutokana na ufinyu wa rasilimali fedha.
Napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa Vipaumbele vilivyopendekezwa na
Serikali vinategemeana na vinalenga kutanzua vikwazo vikuu vya kiuchumi Nchini
ili kufungua fursa za ukuaji wa uchumi wa Taifa na kuharakisha maendeleo na
ustawi wa Wananchi wa Tanzania. Pendekezo la Serikali ni kuwa njia bora si
kupunguza vipaumbele hivi sasa, bali ni kupanga vizuri mtiririko wa utekelezaji
wa miradi ndani ya kila kipengele ili kuongeza jitihada za kuongeza Mapato, na
kusimamia nidhamu ya matumizi.
Mheshimiwa Spika,
21.
Kwa kuwa Mpango huu wa
Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/2012 - 2015/2016) ni wa kwanza unaojenga msingi
wa mipango mingine ya maendeleo ya miaka
mitano itakayoandaliwa, ni dhahiri kuwa kasi ya utekelezaji wake itarahisisha
utengenezaji wa mipango mingine na kupunguza vipaumbele vya msingi katika
mipango ijayo. Hivyo, ninawaomba Waheshimiwa Wabunge washirikiane kwa karibu na
Serikali kuhakikisha kuwa miradi iliyopangwa katika ngazi zote inatekelezwa kwa ufanisi ili Mpango huu wa
mwanzo utekelezeke kama ilivyokusudiwa.
Mheshimiwa Spika,
22.
Mjadala na Hoja nyingine
zilijielekeza katika changamoto za upatikanaji wa Ajira kwa Vijana Nchini. Kulingana na Sensa ya Watu
na Makazi ya mwaka 2012, Asilimia 34.7
ya nguvu kazi ya Tanzania ni Vijana wa umri wa kati ya miaka 15 - 35. Kundi hili la Vijana ndilo
lenye kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira cha Asilimia 13.4 hapa Nchini. Pamoja na kuwa Vijana hawa wamekuwa wakipata kazi
hususan katika Sekta za Ujenzi, Kilimo na Hoteli, ajira zao nyingi zimekuwa za
muda.
23.
Katika kukabiliana na
changamoto hii, Serikali imeandaa Programu ya Ajira kwa Vijana itakayotekelezwa
kwa kipindi cha miaka mitatu. Malengo ni kupatikana fursa za ajira 840,000 kwa kuwezesha jumla ya Miradi 10,000 ya Wahitimu wa Elimu ya Juu
wapatao 30,000 kutoka Vyuo
mbalimbali ambao watatoa ajira za moja
kwa moja kwa wahitimu wengine 270,000
na ajira zisizo za moja kwa moja 540,000.
Programu hii itajengea Vijana uwezo katika stadi za kazi; ujasiriamali; na
kuwapatia Vijana mitaji, nyenzo na vifaa vya kufanyia kazi; na kuwapatia Vijana
maeneo ya uzalishaji na biashara. Serikali inatarajia kuelekeza fedha zaidi
katika kipindi husika ili kuwezesha utekelezaji wa Programu hiyo. Aidha,
naipongeza Sekta Binafsi kwa mchango wao mkubwa katika kukuza uchumi wa Nchi na
kuongeza ajira kwa vijana.
Mheshimiwa Spika,
24.
Kilimo ni moja ya maeneo
ya kipaumbele katika Mpango wa mwaka 2014/2015. Hili ndilo eneo kubwa kwa maana
ya kuongeza fursa za ajira na kipato kwa Wananchi wanaoishi Vijijini, kuongeza
kasi ya ukuaji wa uchumi kwa namna ambayo ni shirikishi ili kupunguza
umaskini. Hivyo, ili kujibu matatizo ya
msingi ya umasikini wa kipato Mpango wa Maendeleo 2014/2015 utatoa kipaumbele katika mambo
muhimu yafuatayo:
(i)
Utafiti wa kilimo cha
mazao, hususan katika uzalishaji wa mbegu bora, mifugo na uvuvi;
(ii)
Kuimarisha huduma za
ugani kwa kilimo, mifugo na uvuvi na
kuimarisha upatikanaji na matumizi ya mbolea kwa ajili ya kilimo;
(iii) Kuimarisha Ushirika wa Wakulima na Wafugaji;
(iv) Kuongeza fursa za mikopo kwa wakulima, wafugaji na wavuvi ikiwa ni pamoja
na kukamilisha uanzishwaji wa Benki ya Kilimo mwezi Januari 2014;
(v)
Kuwezesha upatikanaji wa
masoko ya mazao ya kilimo, na mifugo;
(vi)
Kujenga na kukarabati
skimu za umwagiliaji;
(vii)
Upatikanaji wa ardhi kwa
kilimo na mifugo kwa kuongeza kasi ya upimaji wa ardhi; na
(viii) Kuendeleza shughuli za kuongeza thamani ya mazao
ya kilimo, mifugo na uvuvi;
Mheshimiwa Spika,
25.
Mpango wa Maendeleo
huandaliwa katika ngazi zote Tano za Utawala kulingana na majukumu ya Serikali
ambazo ni:
Moja: Vijiji na Mitaa;
Pili: Kata;
Tatu: Mamlaka za
Serikali za Mitaa (Halmashauri);
Nne: Mikoa; na
Tano:
Wizara, Idara zinazojitegemea, Taasisi na Wakala wa Serikali.
Mamlaka husika katika ngazi zote zinatakiwa kuandaa Mipango yao kwa
kuzingatia maeneo ya vipaumbele kama yalivyoainishwa katika Mapendekezo ya
Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2014/2015. Mipango lazima ilenge katika maeneo
yenye kuleta matokeo makubwa na ya haraka hususan katika kuchochea maendeleo ya
maeneo mengine na Programu nyingine katika ukuaji wa uchumi na kupunguza
umaskini.
Katika kila ngazi, Wadau wengine kama vile Sekta Binafsi, Asasi Zisizo za
Kiserikali, Mashirika ya Dini na Washirika wa Maendeleo washirikishwe
kikamilifu. Wizara, Idara zinazojitegemea, Taasisi na Wakala wa Serikali
ziandae Mpango na kuuwasilisha Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango Wiki ya Nne ya
mwezi Januari, Mwaka 2014.
Katika ngazi za Mikoa na Wilaya, uandaaji uanze katika ngazi ya Kijiji na
Mtaa, Kata, Halmashauri na hatimaye kwenye Mkoa. Mpango uliopitishwa na Mkoa
uwasilishwe Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na
Wizara ya Fedha, Wiki ya Nne ya Mwezi Januari, 2014. Mpango wa Maendeleo wa Taifa utajadiliwa na
Bunge kuanzia Mwezi Aprili hadi Juni, 2014 na utekelezaji wake utaanza Mwezi
Julai 2014 hadi Juni 2015;
Mheshimiwa Spika,
26.
Mapendekezo ya Mpango wa
Maendeleo wa Mwaka 2014/2015 ndiyo yatatumika katika utayarishaji wa Mipango ya
Maendeleo ya Wizara, Idara za Serikali zinazojitegemea, Taasisi na Wakala wa
Serikali, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ya mwaka ujao wa fedha
2014/2015. Hivyo, nawaomba Waheshimiwa Wabunge kutumia taarifa zilizotolewa
hapa Bungeni kutoa ufafanuzi kwenye Vikao vya Baraza la Madiwani katika
Halmashauri zao wakati wa kujadili Mipango yao. Aidha, napenda kutumia fursa hii kuzihimiza Mamlaka za Serikali za Mitaa kuainisha vipaumbele vinavyolenga
katika maeneo yenye kuleta matokeo makubwa na ya haraka ya Kiuchumi na Kijamii;
na pia yenye kuchochea maendeleo ya maeneo mengine. Vilevile, vipaumbele vya
Halmashauri vilenge kufungulia fursa za ajira, kuongeza mapato ya ndani na
kuvutia uwekezaji wa Sekta Binafsi katika maeneo yao.
V: SEKTA YA KILIMO
a)
Hali ya chakula
Nchini
Mheshimiwa
Spika,
27.
Kwa
ujumla hali ya upatikanaji wa Chakula Nchini hadi kufikia Mwezi Oktoba 2013 ni
ya kuridhisha kufuatia mavuno mazuri ya msimu wa kilimo wa 2012/2013 ambapo
mazao yake yanaendelea kuingia sokoni kutoka maeneo mbalimbali hapa Nchini. Tathmini
ya awali iliyofanyika mwezi Julai/Agosti, 2013 inaonesha kuwa uzalishaji wa
mazao ya chakula katika Msimu wa kilimo wa 2012/2013 utafikia Tani 14,383,845 za chakula zikiwemo Tani 7,613,221 za mazao ya nafaka na Tani 6,770,624 za mazao yasiyo ya
nafaka. Kiasi hicho cha chakula kilichozalishwa ni ongezeko la Tani 2,234,726 za chakula, ikilinganishwa
na mahitaji ya chakula kwa mwaka 2013/2014 ya Tani 12,149,120. Kiwango hicho
kinajumuisha Tani 354,015 za mahindi
na Tani 466,821 za mchele. Hivyo
napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge na Wananchi kwa ujumla kuwa tutakuwa
na chakula cha kutosha Nchini kwa Asilimia 118.
Mheshimiwa
Spika,
28.
Vilevile,
tathmini hiyo inaonesha kuwa, pamoja na kuwepo kwa chakula cha kutosha na cha
ziada, Halmashauri 61 katika Mikoa
ya Manyara, Shinyanga, Simiyu, Arusha,
Dodoma, Lindi, Tanga, Singida, Mara, Morogoro, Kilimanjaro, Mwanza, Pwani,
Mtwara, Kigoma na Tabora
zinatarajiwa kuwa na uhaba wa chakula.
29.
Natoa
wito kwa Halmashauri zinazohusika katika Mikoa hiyo kufuatilia kwa karibu
utaratibu wa kupata chakula kinachotolewa kutoka maeneo yenye ziada na kuhakikisha
kuwa kinafika mapema kwenye maeneo yao kabla Wananchi wa maeneo hayo hawajaanza
kulalamika.
(b)
Mwenendo wa Bei za
Vyakula Nchini
Mheshimiwa
Spika,
30.
Kutokana
na hali ya upatikanaji wa chakula kuwa nzuri, Bei za wastani za vyakula hasa
mahindi na mchele katika Soko Nchini zimeendelea kushuka. Kwa mfano, bei ya
mahindi ilishuka kutoka Shilingi 774.30
kwa kilo mwezi Februari, 2013 hadi Shilingi
535.40 kwa Kilo mwezi Septemba 2013. Kwa upande wa mchele, bei kwa kilo
moja imeshuka kutoka Shilingi 1,825.45 mwezi Februari, 2013 hadi
kufikia Shilingi 1,206.70 mwezi Septemba 2013, na bei ya
mchele imeshuka zaidi hadi kufikia Shilingi
1,146.70 katika mwezi Oktoba, 2013.
(c)
Hali ya Ununuzi na Akiba ya Chakula ya Taifa
Mheshimiwa
Spika,
31.
Serikali
kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula imepanga kununua Tani 250,000 za nafaka katika msimu wa
2013/2014. Hadi kufikia tarehe 23 Oktoba, 2013, Wakala alikuwa amekwishanunua
kiasi cha Tani 218,412 za nafaka sawa
na Asilimia 87.37 ya lengo
lililowekwa ambapo Tani 217,919 kati
ya hizo ni za Mahindi na Tani 493 ni
za mtama. Aidha, hadi kufikia tarehe 23 Oktoba 2013, maghala ya Wakala wa Taifa
wa Hifadhi ya Chakula yalikuwa na jumla ya Tani
232, 921 za nafaka, kati ya hizo Tani
232,419 ni za mahindi na Tani
493,103 ni za mtama. Kiasi hiki cha nafaka
kinajumuisha albaki ya Tani 25,452
za mahindi kutoka msimu uliopita wa 2012/2013.
Mheshimiwa
Spika,
32.
Serikali
inaendelea na tathmini ya kina ya hali ya chakula na lishe katika Halmashauri 61 zilizoainishwa kuwa na hali tete ya
chakula kwa lengo la kubainisha idadi ya watu wenye uhaba wa chakula ili
kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa tatizo hili. Nitumie fursa hii kwa mara nyingine
tena kuwaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuwahimiza Wakulima hasa walioko katika
maeneo yenye chakula cha ziada kuhifadhi Chakula cha kutosha kwa mahitaji ya
Kaya zao. Aidha, Wakala wa Taifa na Hifadhi ya Chakula wajipange vizuri
kuhamisha Chakula kutoka maeneo yenye ziada na kupeleka kwenye maeneo
yaliyoainishwa kuwa na hali tete mara taarifa ya upungufu itakapotolewa.
Mheshimiwa Spika,
33.
Pamoja na juhudi za Serikali za kuhakikisha kwamba kuna
chakula cha kutosha, natambua Changamoto zilizopo katika ununuzi wa Chakula
kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula. Natambua kuwepo kwa madeni
yanayotukabili kwenye ununuzi wa nafaka kwa ajili ya Wakala yaani NRFA. Hata hivyo, Mikoa inayohusika na madeni hayo
ni Arusha, Dodoma, Njombe, Shinyanga,
Ruvuma, Rukwa na Tanga. Serikali
itahakikisha deni hilo hilo linalipwa ndani ya mwaka huu wa fedha 2013/2014.
(d)
Mpango wa Pembejeo za
Ruzuku
Mheshimiwa Spika,
34.
Kama
nilivyoeleza katika Mkutano wa 12 wa Bunge, katika msimu wa 2013/2014 Serikali
imetenga jumla ya Shilingi Bilioni 112.564 kwa ajili ya ruzuku ya
mbolea, na pembejeo. Aidha, nilielezea kuhusu utaratibu mpya wa kutoa ruzuku
utakaohusisha uwiano wa Asilimia
80 kwa Vocha na Asilimia 20 mikopo. Ili kuhakikisha Mfumo huu mpya unatekelezwa
kikamilifu na kuleta matokeo yaliyotarajiwa, Serikali imetoa mafunzo ya utoaji
pembejeo kwa njia ya mikopo kwa Washauri wa Kilimo wa Mikoa, Maafisa Ushirika
wa Mikoa na Wilaya na Maafisa Kilimo wa Wilaya kwa awamu mbili. Awamu ya kwanza
ikihusisha Mikoa ya Shinyanga, Geita na Manyara; na Awamu ya Pili inahusu Mikoa
ya Ruvuma, Njombe, Mbeya na Iringa. Aidha,
uchambuzi wa takwimu za Vyama vya Ushirika na Vikundi vya Wakulima
watakaokopeshwa pembejeo za Kilimo mwaka 2013/2014 umefanyika katika Mikoa ya
Iringa, Ruvuma, Shinyanga, Njombe, Mbeya, Geita na Manyara. Takwimu zinaonesha kuna SACCOS 214, AMCOS 163 na Vikundi vingine 51
vyenye Wakulima 88,290 watakopeshwa
pembejeo za Kilimo. Natoa Wito kwa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika
kuendeleza mafunzo haya kwa Mikoa iliyobaki.
(e)
Hali ya Usambazaji wa
Vocha za Pembejeo
Mheshimiwa Spika,
35.
Kuhusu
hali ya Usambazaji wa Vocha za Pembejeo katika Msimu wa 2013/2014 napenda
kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, jumla ya Vocha 2,796,300 kwa ajili ya Kaya 932,100
zikiwemo Vocha 932,100 za mbolea ya
kupandia, 932,100 za mbolea ya
kukuzia, Vocha 441,100 za mbegu za
mahindi chotara; Vocha 432,000 za
mahindi ya OPV na Vocha 60,000 za
mbegu za mpunga zilisambazwa katika Mikoa yote hapa Nchini. Nitoe wito kwa
Viongozi wa Mikoa na Wilaya kwa kushirikiana na Waheshimiwa Madiwani na
Viongozi wengine kuhakikisha kuwa Wananchi wanapata na wanatumia Vocha hizi kupata
pembejeo kama ilivyokusudiwa. Aidha, tushirikiane kuhakikisha kuwa wale watakaokwenda
kinyume na utaratibu huu wa usambazaji wa Vocha hizo wanashughulikiwa kwa
mujibu wa Sheria.
(f)
Changamoto za Mbolea
ya Minjingu
Mheshimiwa
Spika,
36.
Juhudi za Serikali
katika kuhakikisha upatikanaji wa Pembejeo za ruzuku ziko dhahiri. Hata hivyo, imebainika kwamba katika mahitaji
ya mbolea, kilio kikubwa cha Wakulima ni kupatiwa mbolea kwa wakati. Aidha, wapo Wananchi wanaolalamikia mbolea ya
Minjingu Mazao ambayo ni kweli hapo awali ilikuwa na matatizo. Lakini sasa, mbolea hii imeboreshwa kwa
kiwango kikubwa kwa kuongezewa virutubisho.
Mheshimiwa
Spika,
37.
Mbolea
ya Minjingu ya awali ilikuwa na virutubisho vya udongo viwili tu vya Kalisiumu na Fosfeti. Mbolea ya Minjingu Mazao
imeboreshwa kwa kuongezwa virutubisho vinne zaidi na kufanya virutubisho hivyo
kuwa sita yaani Kalisiumu, Fosfeti,
Naitrojeni, Salfa, Boroni na Zinki.
38.
Kwa msingi huo, Mbolea ya Minjingu mazao
inaweza kutumika katika aina mbalimbali za udongo tofauti na ilivyokuwa awali.
Aidha, Mbolea ya Minjingu Mazao ni ya chengachenga (granulated) tofauti na ya awali ambayo ilikuwa katika mfumo wa unga
(dust) ambapo pengine matumizi yake
hayakuwa rafiki kwa mkulima. Baada ya kuboreshwa, kwa sasa Mbolea hii ya
Minjingu inatumika kwa mazao mengi hususan mahindi, mpunga na alizeti katika
sehemu mbalimbali na aina mbalimbali za udongo.
Mheshimiwa Spika
39.
Mkulima
anahitaji kutumia mifuko miwili ya mbolea ya Minjingu Mazao ya kilo 50 kila mmoja kwa wakati mmoja
ikilinganishwa na mfuko mmoja wa kilo 50
wa mbolea ya DAP. Hata hivyo, ukilinganisha
na mbolea ya DAP, mkulima anayetumia Minjingu Mazao anawezesha shamba lake
kupata virutubisho zaidi. Kwa hiyo, Mbolea ya Minjingu Mazao ni nafuu ikilinganishwa
na Mbolea ya DAP.
40.
Bei ya mbolea ya Minjingu Mazao kwa mfuko mmoja ni Shilingi 32,500/= hivyo kwa mifuko miwili ni
Shilingi 65,000 katika Wilaya zote Nchini ikilinganishwa na bei ya wastani ya
Shilingi 75,000/= ya mfuko mmoja wa
DAP. Aidha, kwa aina zote mbili za mbolea zinapotumika kupandia, lazima mkulima
aweke mbolea nyingine ya kukuzia ambayo ina virutubisho vingi vya Naitrogeni kama CAN au UREA.
41.
Majaribio
ya kutumia Mbolea ya Minjingu yalianza mwaka 1977 kuendelea hadi mwaka 2006
ikiwa katika hali ya unga. Mwaka 2007 Mbolea hiyo iliboreshwa kwa kuiweka
katika hali ya chenga chenga (granulation)
ingawa virutubisho havikuboreshwa. Mbolea hiyo iliendelea kutumika katika hali
hiyo hadi mwaka 2009. Hivyo, mwaka 2010 Mbolea hiyo iliboreshwa kwa kuongezea
virutubisho ambavyo baada ya utafiti wa kuihakiki (validation) iliingizwa
Sokoni mwaka 2012.
42.
Kwa
sasa, Mbolea ya Minjingu Mazao inatumika katika Mikoa ya Iringa, Ruvuma, Rukwa,
Mbeya, Njombe, Katavi, Kigoma na Morogoro. Aidha, kuna mikoa mingine ambako
mbolea hii imepelekwa pamoja na mbolea nyingine kwa ajili ya Wakulima wenyewe
kufanya maamuzi ya kuchagua.
Mheshimiwa Spika
43.
Matumizi
ya Mbolea ya Minjingu Mazao katika mwaka 2012/2013 yamewezesha kuongezeka kwa
uzalishaji wa mahindi, mpunga na alizeti kwa ekari hususan katika mikoa ya
Nyanda za Juu Kusini. Changamoto kubwa ni elimu juu ya matumizi sahihi ya
Mbolea hiyo kwenye baadhi ya maeneo.
44.
Katika
kutatua changamoto hii, Wizara inashirikiana na Mmiliki wa Kiwanda cha Mbolea
cha Minjingu kuendesha mashamba darasa katika Wilaya mbalimbali Nchini. Vilevile, Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana
na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, inaendelea kufanya utafiti katika maeneno
mbalimbali ya Nchi ili kuboresha matumizi sahihi ya Mbolea hiyo katika aina
mbalimbali za udongo (site specific
validation trials).
45.
Changamoto
zinazohusiana na Mbolea ya Minjingu katika Wilaya ya Mbozi zitaangaliwa kwa
namna yake. Kitendo hicho ni cha udanganyifu kwani Mbolea ya aina nyingine ni
bei kubwa ikilinganishwa na ya Minjingu Mazao. Kutokana na kitendo hicho kuwa
kinyume na Sheria ya Mbolea ya 2009, Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea kwa
kushirikiana na Wakaguzi wa mbolea wa Wilaya ya Mbozi ilimkamata Wakala husika
na kumchukulia hatua za kisheria. Naagiza Viongozi wa Mikoa na Wilaya
kuchunguza mbolea inayopelekwa katika maeneo yao isije ikachakachuliwa.
Mheshimiwa Spika,
46.
Kwa kuzingatia Changamoto zilizojitokeza katika matumizi
ya mbolea ya Minjingu katika maeneo mbalimbali Nchini Serikali itaendelea
kuzitafutia ufumbuzi kwa kuchukua hatua zifuatazo:
(a)
Kutoa elimu kwa Wakulima kuhusu namna bora ya kutumia
Mbolea ya Minjingu Mazao kuongeza uzalishaji wa mazao kwa kuzingatia ushauri wa
kitaalam kuhusu aina ya udongo na mazao yanayofaa kwa mbolea hiyo. Vilevile,
kuwaelimisha Wananchi kuhusu ubora wa Mbolea ya Minjingu Mazao ikilinganishwa
na Mbolea za aina nyingine hasa kutokana na virutubisho vilivyoongezwa katika
mbolea.
(b)
Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea imeagizwa kufuatilia na
kufanya uchunguzi wa madai ya Wakulima kuhusu changamoto za matumizi ya mbolea
ya Minjingu Mazao hasa katika Wilaya ya Mbozi na sehemu nyingine zenye matatizo
ya matumizi ya mbolea hiyo Nchini.
(c)
Naomba kuiagiza Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika
kuendelea kushirikiana na Wadau kufanya utafiti katika maeneo mbalimbali
Nchini. Kutokana na utafiti huo itoe ushauri na mwongozo kwa Wakulima wote
Nchini kuhusu njia sahihi za kutumia Mbolea ya Minjingu Mazao katika aina
mbalimbali za udongo na mazao yanayofaa kulimwa. Lengo ni kuongeza tija katika
uzalishaji wa mazao ya kilimo kwa eneo.
Kwa Wilaya ya Mbozi Wizara itoe mwongozo kuhusu nini kifanyike kwa sasa
wakati hatua za utafiti na uchunguzi wa matumizi sahihi ya Mbolea hiyo
zinaendelea.
(g)
Uzalishaji na Ununuzi wa Mazao ya
Biashara
Mheshimiwa Spika,
47.
Katika
miaka ya hivi karibuni kumekuwa na Changamoto mbalimbali za uzalishaji na
ununuzi wa baadhi ya mazao ya biashara hapa Nchini ikiwemo Kilimo cha zao la
Pamba, Korosho, Tumbaku na Kahawa. Kwa kuzingatia ufinyu wa muda, leo naomba
mniruhusu nizungumzie kidogo kuhusu kilimo cha mazao mawili ya Pamba na
Korosho.
(h)
Uzalishaji na Ununuzi
wa Zao la Pamba
Mheshimiwa Spika,
48.
Serikali inaendelea
na jitihada za kuhakikisha kuwa Wakulima wa Pamba wanazalisha kwa tija kwa kutumia mbegu bora, utumiaji wa pembejeo (Viuadudu na Mbegu), kutoa huduma za ugani kupitia Maafisa wa Kilimo
katika Halmashauri za Wilaya na pia kuhamasisha Kilimo cha pamba kwa
kushirikiana kwa karibu na Wadau mbalimbali ikiwemo Sekta Binafsi.
49.
Katika kilimo hiki
cha Pamba, Zana za kilimo zinazotumika kwa sasa ni majembe ya kukokotwa na
wanyama kazi kwa ajili ya kulima nah ii ni dhahiri haiwezi kuongeza tija.
Ttahakikisha tunatumia Zana za Kisasa.
(i)
Mkakati wa Wizara kupata masoko ya uhakika ya pamba
50.
Serikali pia inaendelea
kuhakikisha kwamba pamba inaongezwa thamani hapa Nchini kwa kuhamasisha
uwekezaji katika ujenzi wa viwanda vya nyuzi na nguo. Uwekezaji mpya unafanyika
kwa kujenga kiwanda cha nyuzi na nguo cha Dahong Mkoani Shinyanga na pia Mradi
mkubwa wa kuzalisha pamba, kuchambua, kutengeneza nyuzi, kutengeneza vitambaa
na nguo unaotarajiwa kutekelezwa na
Kampuni ya Kijapani (NITORI) katika Wilaya ya Handeni. Kwa sasa mradi huo uko
katika hatua ya umilikishwaji wa Ardhi.
51.
Vilevile, Serikali
imeanzisha mafunzo ya Uhandisi na Ubunifu katika Viwanda vya Nyuzi na Nguo. Pia
tumeanzisha kozi ya ubunifu wa mitindo katika mitaala ya VETA na Mafunzo ya
Shahada ya uzamili katika “Textile”
katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Lengo ni kuhakikisha kuwa kuna watalaamu
wa kutosha katika mchakato wa kuongeza thamani ya pamba.
(j)
Tofauti za ubora wa mbegu za pamba manyoya na De – linted
Mheshimiwa Spika,
52.
Sina shaka Watanzania
wameshasikia kuwa kwa sasa tunazo aina mbili za mbegu za Pamba zinazotumika
hapa Nchini. Tunayo mbegu yetu ya asili
ya Pamba Manyoya na Mbegu mpya na ya kisasa ya Pamba isiyo na manyoya (De-linted). Aina hizi zinatofautiana sana kwa ubora na
bei. Mbegu ya manyoa ina uotaji wa chini ya Asilimia 50 wakati ile ya De
–linted ni zaidi ya Asilimia 90. Mbegu ya manyoya hutumika nyingi kwa eneo
(kilo 25 kwa Ekari), wakati De – linted ni kilo 6 tu kwa Ekari, sawa na Shilingi 7,200 kwa Ekari kwa bei ya Shilingi 1,200 kwa kilo. Mbegu ya manyoya ina tija ndogo (inazalisha kati ya
kilo 250 na 300 kwa Ekari) ikilinganishwa
ya mbegu ya De-linted inayozalisha Kilo 450 – 1200 kwa Ekari. Mbegu ya manyoya
ina uwiano mdogo wa pamba nyuzi (Asilimia 33) ikilinganishwa na mbegu De-linted
ambayo uwiano wake ni Asilimia 36.
(k)
Jitihada za Wizara kupunguza bei ya mbegu bora
Mheshimiwa Spika,
53.
Ili kuwawezesha
Wakulima kutumia mbegu bora (de-linted) Serikali imetoa ruzuku ya Shilingi
Billioni 4.8 ili kufanya mbegu hiyo
ipatikane kwa Shilingi 600 kwa kilo
kwa mkulima badala ya Shilingi 1,200
kwa kilo iliyotumika mwaka 2012/2013.
54.
Serikali pia
inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kutoa elimu kwa wakulima wa pamba
kuhusu mbegu bora. Kwa mfano, Viongozi wa maeneo yanayolima pamba (Wakuu wa
Mikoa, Wakuu wa Wilaya na baadhi ya Madiwani)
wamepelekwa katika kiwanda cha kuchakata mbegu bora za Pamba cha Kampuni ya Quton ili kupata maelezo na kujionea hali ya
utendaji wa mbegu bora katika kilimo.
55.
Kupitia programu ya
kuendeleza zao la pamba wakulima wawezeshaji (Lead Farmers) 3000 wa vikundi vya Kilimo cha Mkataba wanaendelea
kupewa mafunzo ya kilimo bora na matumizi ya mbegu bora ili watumike kupeleka
elimu hii kwa wakulima wenzao.
Mheshimiwa Spika,
56.
Katika msimu huu wa Kilimo
wa 2013/14, Serikali imejipanga kusimamia utekelezaji wa Kilimo cha Mkataba kwa
lengo la kuleta ufanisi katika Kilimo cha Pamba Nchini. Hatua hii inahusisha
pia kutoa elimu ya kutosha na kushirikisha kwa karibu Wadau katika
kuzipatia ufumbuzi changamoto zilizopo kwenye utaratibu mzima wa kilimo
hicho ambacho kina manufaa makubwa iwapo kitaeleweka na kutekelezwa vyema kwa
misingi ya haki miongoni wa wadau. Baadhi ya manufaa hayo ni:
(i)
Uhakika wa
upatikanaji wa pembejeo kwa mkulima kwa mkopo.
(ii)
Kuongeza tija kutokana
na kupata pembejeo na huduma za ugani.
(iii) Kuongeza ubora wa pamba kutokana na
matumizi makubwa ya pembejeo na huduma za
ugani pamoja na vikundi kutumika kama Mawakala wa kununua Pamba ya
wanachama wake hivyo kusimamia ubora
(iv) Uhakika wa soko la pamba ya mkulima
(v)
Kupunguza wizi kupitia
mizani ya mawakala
(vi) Wakulima kupata teknolojia kupitia uwekezaji
(vii) Kujenga na kuimarisha mfumo wa Ushirika kupitia vikundi vya wakulima.
(l)
Elimu ya kilimo cha mkataba kwa wakulima
Mheshimiwa Spika,
57.
Kupitia programu ya kuendeleza zao la pamba,
wakulima Wawezeshaji zaidi ya 3,000
wamekwisha pokea mafunzo ya kilimo cha Mkataba wanao tumika kupeleka elimu hii
kwa vikundi vya wakulima. Wagani wa Halmashauri wapatao 560 wameshapata mafunzo haya.
Chini ya Mpango huu kila mgani anaweza kuhudumia vikundi hadi 20.
58.
Napenda kuwaagiza
Viongozi na Wataalamu wa Kilimo waendelee kutoa elimu ya matumizi na faida ya
mbegu bora za De-linted au mbegu zisizokuwa na manyoya kwa Wakulima wa Pamba
Nchini. Aidha, mashamba darasa yatumike ipasavyo kuonesha
tija inayotokana na aina hiyo ya mbegu za Pamba inapolinganishwa na mbegu zenye
manyoya. Vilevile, Viongozi na Wataalamu
wa Kilimo waendelee kuwakumbusha Wakulima wa Pamba na Watanzania kuwa utaratibu
mpya wa Kilimo cha Mkataba una manufaa mengi na makubwa. Tuendelee kuwashawishi Wakulima kujiunga na
Kilimo cha Mkataba bila kuwashurutisha isipokuwa tuwape elimu hasa kupitia
mashamba darasa. Wale watakaoshawishika kuingia
katika utaratibu huu wasaidiwe kwa kila hali ili wanufaike na kilimo hicho huku
wakisaidia kutoa elimu kwa Wakulima wengine ili wajiunge na aina hii ya kilimo.
Ni matumaini yangu ndani ya muda mfupi Wakulima watafahamu faida ya kilimo cha
mkataba.
(m)
Zao la Korosho
Mheshimiwa
Spika,
59.
Kuhusu
Zao la Korosho, azma ya Serikali ni kuimarisha Viwanda vya Korosho na kufufua
vile vilivyopobinafsishwa ili viweze kusaidia kukuza Soko kwa wakulima wa
Korosho. Ili kutekeleza azma hiyo, Serikali imefanya tathmini na kubaini kuwa
Wawekezaji wengi katika Viwanda vya Korosho vilivyobinafsishwa wameshindwa
kutekeleza Mikataba ya Ubinafsishaji wa viwanda hivyo kutokana na sababu
mbalimbali zikiwemo ukosefu wa fedha za uendeshaji, ukosefu wa nishati ya
uhakika na Viwanda kutumia teknolojia zilizopitwa na wakati. Ili kukabiliana na
hali hiyo, Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kwa kushirikiana na Shirika
Hodhi la Mali za Mashirika ya Umma (CHC) pamoja na Wadau wengine inaandaa
mapendekezo ya hatua za kuchukua dhidi ya Wawekezaji walioshindwa kuendeleza
viwanda hivyo. Dhamira ya Serikali ni kwamba Mwekezaji ambaye ameshindwa
kuendeleza kiwanda alichonunua kwa kuzingatia Makubaliano ya ununuzi na
Serikali, mali hiyo irudishwe Serikalini na ifanyiwe tathmini na itangazwe upya
ili kupata Wawekezaji mahiri na wenye nia thabiti ya kuendeleza Viwanda husika.
Mheshimiwa Spika,
60.
Sambamba
na hatua hiyo, Bodi ya Korosho Tanzania imeandaa Mpango wa Ubanguaji wa miaka
mitatu kuanzia mwaka 2012/2013 ambao umelenga kuwasaidia wabanguaji wadogo na
wa kati kuendesha shughuli za ubanguaji kwa ufanisi kwa kuwapatia mafunzo,
vifaa vya kubangulia, na kuwatafutia masoko ya ndani, masoko ya kanda na masoko
ya nje;
61.
Hatua
iliyofikiwa kwa sasa ni kwamba, Mfuko wa Wakfu wa Kuendeleza Zao la Korosho kwa
kushirikiana na Bodi ya Korosho Tanzania umetenga fedha kwa ajili ya kujenga
viwanda vitatu katika Mikoa ya Ruvuma, Mtwara, na Pwani kwa ajili ya
kuwawezesha Wabanguaji wadogo na wa kati kumalizia baadhi ya hatua za ubanguaji
katika viwanda hivyo kwa ajili ya kukidhi matakwa ya masoko makubwa ya korosho
duniani.
Mheshimiwa Spika,
62.
Ili
kuboresha kilimo cha Korosho, katika mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea kutoa
ruzuku ya madawa kutoa huduma za ugani na kuhamasisha wakulima wahudumie
mikorosho na kupuliza madawa mapema.
Mheshimiwa Spika,
63.
Kuhusu
ununuzi wa Korosho, katika msimu huu wa 2013/2014 ununuzi wa Korosho utaendelea
kwa kutumia mfumo wa Stakabadhi za mazao Ghalani. Ukusanyaji wa Korosho kutoka
kwa wakulima umeanza katika maeneo mbalimbali Nchini. Kwa mfano, katika Mkoa wa
Mtwara, mnada wa kwanza wa Korosho ulianza tarehe 25 Oktoba, 2013 ambapo
ulihusisha Vyama vya Msingi vya Mkoa wa Mtwara. Korosho zote zilizokuwa
zimekusanywa na kutangazwa katika kila mnada zilinunuliwa. Bei ya Korosho
katika Mnada wa kwanza ilikuwa kati ya Shilingi 1,402/= na 1,520/= kwa kilo ikilinganishwa na bei dira ya
Shilingi 1,000/= kwa kilo. Mnada
uliofuatia bei ziliongezeka na kuwa kati ya Shilingi 1,481/= na 1,570/= kwa
kilo.
Mheshimiwa Spika,
64.
Kwa
upande wa Mkoa wa Lindi, Vyama vya Msingi vilivyobaki chini ya ILULU vilifanya
Mnada wa kwanza tarehe 2 Novemba, 2013 ambapo jumla ya Tani 783.593 ziliuzwa. Vyama vingine 51 vya kutoka Wilaya ya Ruangwa,
Nachingwea na Liwale ambavyo vilijiondoa kutoka usimamizi wa Chama Kikuu cha
ILULU vitafanya mnada baada ya taratibu za kupata Kamati itakayowasimamia
zitakapokamilika. Vyama hivyo vimeomba kufanyiwa Minada yake katika Wilaya ya
Nachingwea ambako ndiko walikoweka Ofisi yao.
Mheshimiwa Spika,
65.
Kwa
upande wa Wilaya ya Tunduru, bado haijapata mkopo mpaka sasa na juhudi za
kufuatilia zinaendelea. Taarifa kutoka Benki ya NMB inaonyesha kuwa kuna
uwezekano mkubwa wa Vyama vya Msingi vya TAMCU kupata mkopo msimu huu kwani
deni ambalo TAMCU walikuwa wanadaiwa na Benki hiyo ya NMB limelipwa na
Serikali.
Mheshimiwa Spika,
66.
Kwa
upande wa Mkoa wa Pwani, uwezekano wa Vyama vilivyo chini ya Chama Kikuu cha
Coast Region Cooperative Union (CORECU) kupata Mkopo ni mdogo kutokana na
kudaiwa fedha nyingi zaidi ya Shilingi Bilioni
7 za msimu wa mwaka 2010/2011. Serikali imefanya Ukaguzi Maalum katika
Vyama hivyo na kubaini kwamba madeni hayo kwa kiwango kikubwa yamesababishwa na
ubadhirifu wa Viongozi na Watendaji wa Vyama hivyo. Hivyo, kupitia Ofisi ya
Mrajis wa Vyama vya Ushirika hatua za kisheria zimechukuliwa ikiwa ni pamoja na
kuwataka wahusika wa ubadhirifu huo kufidia hasara hiyo. Kwa upande mwingine,
Wahusika wamekata rufaa, lakini Mamlaka yenye dhamana imezitupilia mbali rufaa
hizo zote 434, na kuwataka Wahusika
walipe kiasi cha fedha kinachodaiwa na Vyama vyao. Kutokana na hali hiyo,
Wakulima wa Mkoa wa Pwani wanashauriwa kupeleka mavuno ya Korosho katika
maghala yaliyoteuliwa. Minada ya Korosho itafanyika katika maghala hayo na
wakulima watalipwa mara moja baada ya minada kufanyika.
Mheshimiwa
Spika,
67.
Kutokana
na jitihada za Serikali zinazoendelea natoa wito kwa Bodi ya Korosho na Wakuu
wa Mikoa husika kuendelea kusimamia kikamilifu taratibu wa ununuzi wa Korosho
ili kuhakikisha kwamba Wakulima wanauza Korosho zao walizovuna na kulipwa
malipo yao halali kwa wakati.
(n)
Hali ya mwenendo wa
Mvua za vuli mwaka 2013 na athari kwa mazao ya vuli
Mheshimiwa
Spika,
68.
Taarifa
ya utabiri wa mwelekeo wa hali ya hewa hususan mvua katika kipindi cha Oktoba
hadi Disemba 2013 iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini inaonesha kuwa
mvua za vuli zinatarajiwa kuwa chini ya wastani katika Mikoa ya Dar es Salaam,
Pwani, Tanga, Kaskazini mwa Morogoro, Kilimanjaro, Arusha, Manyara na baadhi ya
maeneo katika mikoa ya Mwanza, Simiyu, Shinyanga Kagera, Geita na Mara. Pamoja
na kwamba mvua za msimu wa vuli zimechelewa kuanza katika maeneo mengi ambayo
yalitarajiwa kupata mvua za vuli, mvua hizi hazitarajiwi kuwa na mtawanyiko wa
kuridhisha.
(o)
Athari za mvua za
vuli zinazonyesha chini ya Wastani
Mheshimiwa Spika,
69.
Kutokana
na utabiri huo wa Hali ya Hewa, tathmini ya awali iliyofanyika katika maeneo yaliyotarajiwa
kupata mvua za vuli inaonesha kuwa:
i.
Hali ya mazao hasa
katika Nyanda za juu Kaskazini na ukanda wa Pwani Kaskazini si ya kuridhisha,
ii. Mategemeo ya mavuno ya vuli ni kidogo isipokuwa katika baadhi ya maeneo ya
ukanda wa Ziwa Viktoria hususan katika Mikoa ya Kagera na Geita ambayo yamepata
mvua za wastani hadi chini ya wastani,
iii. Mchango wa mavuno ya vuli ambao ni kati ya Asilimia 28-30 ya Chakula
kinachozalishwa katika maeneo yanayopata mvua hizo au Asilimia 18 Kitaifa hauwezi kufikiwa katika hali
hii ya mvua.
iv. Hali hii inaashiria kuwa kutakuwepo na upungufu wa Chakula katika maeneo
hayo niliyotaja hapo juu.
Mheshimiwa Spika,
70.
Kutokana
na hali hii, natoa wito kwa Wakulima katika maeneo haya kuzingatia ushauri wa
kupanda mazao yanayostahimili ukame na yanayokomaa kwa muda mfupi. Wakuu wa
Mikoa na Wilaya katika Halmashauri husika wasimamie suala hili kwa ukamilifu;
ili kuepusha upungufu wa Chakula unaotarajiwa.
VI: NISHATI
(a) Kuongezeka kwa upatikanaji
wa Nishati Vijijni (Miradi ya REA) na hali iliyofikiwa
Mheshimiwa
Spika,
71.
Wakati
wa Kuhitimisha Mkutano wa 12 wa Bunge nilieleza Mikakati ya Serikali katika
kueneza umeme Vijijini na matarajio ya baadaye. Napenda kulieleza Bunge lako
Tukufu kwamba tumeweza kupiga hatua katika baadhi ya maeneo katika kuelekea
kwenye malengo tuliyojiwekea. Tayari Wakala
wa Nishati Vijijini (REA) ulitangaza zabuni mwezi Desemba 2012 kwa ajili ya
kuwapata Wakandarasi wa kupeleka umeme Vijijini na kujenga vituo vya kupoozea
umeme. Baada ya tathmini kufanyika, zabuni 15 za kupeleka umeme Vijijini
zilipata Wakandarasi. Mikoa ambayo
ilipata Wakandarasi katika
awamu hiyo ni
pamoja na Arusha, Dodoma, Iringa, Katavi, Kilimanjaro, Mara, Mtwara, Mwanza, Njombe,
Ruvuma, Shinyanga, Simiyu, Singida na
Tabora. Aidha Wakandarasi kwa
ajili ya ujenzi
wa vituo vya
kupozea umeme vya msongo wa Kilovoti 11 na 33 vya Ngara, Kibondo,
Kasulu, Kigoma, Tunduru na
Mbinga walipatikana. Kwa sasa Wakala unaendelea na kulipa malipo
ya awali (advance payments) na Wakandarasi
wanaendelea na ukamilishaji wa taratibu za kuanza kazi. Miradi hii yenye thamani
ya Shilingi Bilioni 430.82 inatarajiwa
kukamilika mwezi Juni, 2015.
Mheshimiwa
Spika,
72.
Mwezi
Mei, 2013 zabuni nyingine 10 ya Miradi yenye thamani ya Shilingi Bilioni 450 zilitangazwa kwa
ajili yakuwapata Wakandarasi wa kupeleka umeme Vijijini
katika Mikoa ya Geita, Kagera,
Kigoma, Lindi, Manyara, Mbeya,
Morogoro, Pwani, Rukwa na Tanga. Kwa sasa tathmini ya zabuni
hizo inaendelea. Inatarajiwa kwamba Wakandarasi kutokana na Tathmini hiyo
watajulikana ifikapo tarehe 15 Novemba, 2013.
(b) Suala
la Fidia, Sera; na Miongozo ya usambazaji Umeme Vijijini:
Mheshimiwa Spika
73.
Ili
kuharakisha maendeleo ya upatikanaji wa Nishati Vijijini, suala la Wananchi kuchangia nguvu kazi na kutoa njia
na maeneo ya kupitisha nyaya za umeme
bila fidia pale
inapowezekana limekuwa likisititizwa na Serikali kutokana na ufinyu wa
bajeti. Upo ukweli kwamba, Miradi mingi imechelewa kutekelezwa kutokana na
Wananchi kudai fidia ya miti na mazao ya msimu yanayokutwa kwenye njia ya
umeme. Kwa mfano miradi ya Awamu ya
Kwanza katika Mkoa wa Pwani imechelewa kuanza na kukamilishwa kutokana na
Wananchi kudai fidia ilipwe kwanza ndio ujenzi uendelee. Pia, kwa sasa ujenzi
umesimama katika maeneo ya Bungu-Nyamisati na Kisiwa cha Mafia kutokana na
Wananchi kudai fidia kwanza.
Mheshimiwa Spika,
74.
Ni
kweli kwamba kulingana na Sheria zilizopo kama katika njia ya kupitisha umeme
yapo mazao yanayostahili kulipwa fidia. Hata hivyo kutokana na bajeti finyu
Wakala wa Nishati Vijijni unashindwa kutoa fidia inayohitajika na kuona ni bora
wale wanaojitolea maeneo yao wapelekewe umeme haraka kuliko kusubiri bajeti kwa
ajili ya fidia. Serikali inatoa rai kwa Viongozi na Wananchi kuona umuhimu wa kujitolea
maeneo yao ili waweze kupata huduma hii muhimu mapema. Nawaomba Waheshimiwa
Wabunge tushirikiane katika kuwahamasisha Wananchi katika maeneo yetu kuhusu
umuhimu wa kupata umeme mapema kwa maendeleo ya maeneo yetu.
(c)
Utekelezaji wa Ujenzi wa Bomba la Gesi
Asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam
Mheshimiwa Spika,
75.
Shughuli
za ujenzi wa Bomba la Gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam zinaendelea vizuri.
Mpaka sasa usafishaji wa njia ya kulaza bomba unaendelea
na tayari Kilometa 484.17 kati ya Kilometa
517 zimekamilika. Aidha jumla ya
mabomba 20,491 yanayotosheleza kulazwa
umbali wa Kilometa 243.8
yamekwishawasili Nchini. Kazi ya kuchimba mtaro, kuyapanga mabomba katika
mstari mmoja kwenye mkuza na kuyaunganisha pamoja kwa kuchomelea inaendelea na
hadi sasa Kilometa 124.3
zimeshaunganishwa. Kazi zinazoendelea ni ujenzi wa kambi, nyumba za wafanyakazi
katika maeneo ya Songo Songo na Madimba, pamoja na maandalizi ya ujenzi wa
mitambo ya kusafirishia Gesi Asilia. Tutaendelea kutoa taarifa ya hatua iliyofikiwa
ya utekelezaji wa Mradi huu muhimu kwa Taifa letu.
76.
Aidha, katika
kuhakikisha kwamba miradi hii inatekelezwa na kuleta manufaa katika Nchi yetu, ninayo
furaha kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa, Serikali ilipitisha Sera ya Gesi
Asilia tangu tarehe 10 Oktoba 2013, Utaratibu wa kuichapisha sera hiyo katika lugha
ya Kiswahili na Kiingereza unaendelea. Vilevile Serikali kupitia Wizara ya
Nishati na Madini imeandaa Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa Utekelezaji wa
Sera ya Gesi na imeanza kutayarisha Rasimu ya Sheria ya Gesi. Ni matumaini
yangu kwamba vitu vyote hivi vikikamilika Sekta ya Gesi Asilia itaimarika.
VII: MIFUGO
(a)
Operesheni Ondoa Mifugo Katika Maeneo Mbalimbali Nchini
Mheshimiwa
Spika,
77.
Kwa
muda mrefu sasa maeneo mbalimbali hapa Nchini yamekuwa yakikumbwa na migogoro
inayotokana na matumizi ya Ardhi hususan kwa Wafugaji wanaohama kutoka maeneo
yaliyokatazwa kisheria kwenda eneo lingine pasipo na maandalizi ya kutosha ya kuwapokea.
Utafiti unaonesha kuwa, migogoro ya ardhi hapa Nchini ina
sura nne:
Moja: Migogoro kati ya Wakulima na Wafugaji,
Pili: Migogoro kati ya Wananchi na Wawekezaji,
Tatu: Migogoro kati ya Wananchi na Serikali, na
Nne: Migogoro kati ya Mamlaka moja na Mamlaka nyingine ndani ya
Serikali inayotokana na migongano ya kimaslahi.
Mheshimiwa Spika,
78.
Kuna
ukweli kwamba, kuongezeka kwa idadi ya Watu na kuongezeka kwa matumizi ya ardhi
kutaendelea kuongeza kasi na vipaumbele katika kugawa maeneo yaliyoko wazi. Hali hii imeanza kuonekana katika maeneo ya Wafugaji ambayo yameendelea
kupungua siku hadi siku. Aidha, shughuli za kilimo, maendeleo ya makazi, na
matumizi mengine ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa Vijiji kunakotokana na
ongezeko la idadi ya watu kumeendelea kupunguza eneo la malisho.
Mheshimiwa Spika,
79.
Kuna
ukweli pia kwamba, mabadiliko ya tabianchi na kuongezeka kwa mifugo katika
maeneo ya Nchi kwa ajili ya kutafuta malisho na maji kumeendelea kuchangia
migogoro mingi kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi. Kati ya mwaka
2005 na sasa, tumeshuhudia uhamiaji wa mifugo kutoka mikoa ya Kaskazini na
Kanda ya Ziwa kwenda katika Mikoa ya Kusini na Mashariki mwa Nchi. Uhamiaji huo
licha ya kusababisha migogoro kati ya watumiaji wengine pia imesababisha
uharibifu mkubwa wa mazingira kwenye maeneo ya vyanzo vya maji na hifadhi za
Taifa. Baadhi ya maeneo hayo ni pamoja na hifadhi za Wanyama pori za Burigi,
Maswa na Meatu, Bonde la Usangu na Bonde la Kilombero.
Mheshimiwa Spika,
80.
Ni
matumaini yangu kwamba, maadam suala hili limepewa umuhimu na Bunge lako Tukufu
na hivyo kuunda Kamati ya kufuatilia migogoro hii, ni dhahiri tutapata ufumbuzi
wa kudumu katika tatizo hili. Niwaombe Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote kwa
ujumla wanaotoka katika maeneo yenye migogoro inayotokana na Wafugaji na
Wakulima kutoa ushirikiano katika kutoa taarifa muhimu kwa Kamati iliyoundwa
ili kulisaidia Taifa katika kutatua migogoro hii.
VIII: HALI YA ULINZI NA
USALAMA NCHINI.
Mheshimiwa
Spika,
81.
Kwa
ujumla hali ya Ulinzi na Usalama Nchini imeendelea kuwa shwari, isipokuwa
katika maeneo machache ambako kulijitokeza vitendo vinavyoashiria kuwepo kwa
vikundi vya uhalifu na ujambazi. Serikali kupitia Jeshi la Polisi imeendelea kujipanga kukabiliana na
matishio mbalimbali ya kiusalama ikiwemo ugaidi. Tukio lililotokea Nchini Kenya
hivi karibuni na matukio ya kukamatwa kwa Vijana 12 kule Mtwara na lile lililotokea Wilaya ya Kilindi Mkoani Tanga
ambapo zaidi ya watuhumiwa 46
wamefikishwa mahakamani kwa makosa mbalimbali yanaashiria kwamba ugaidi hauna
mipaka unaweza kutokea katika Nchi yoyote.
Mheshimiwa Spika
82.
Katika kuhakikisha kuwa
amani na utulivu vinaendelea kudumu Nchini, Serikali imejipanga katika maeneo
hayo kama ifuatavyo:
(i)
Kuhakikisha Vikao vya
Kamati za Ulinzi na Usalama vya Mitaa, Vijiji na Vitongoji vinafanyika mara kwa
mara kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Serikali za Mitaa katika kila
Kata/Shehia kwa kuwashirikisha madiwani ili kujadili na kubaini kero mbalimbali
na kuzitafutia ufumbuzi.
(ii) Kufufua mpango wa Daftari la Wakazi na Wageni katika kila Mtaa/Kitongoji
kwa Tanzania Bara na Zanzibar ili kila Kiongozi wa Mtaa, Kijiji na Kitongoji
ajue Watu wanaoishi katika himaya yake. Zoezi hili litasaidia kuepuka tatizo la
wageni wasiojulikana au wahamiaji haramu. Aidha kamati za Ulinzi na Usalama za
Serikali za Mitaa na Vijiji zinahimizwa kutekeleza mkakati wa Halmashauri wa
kuzuia uhalifu kwa kuimarisha vikundi vya ulinzi shirikishi/ulinzi jirani, kwa
kuzingatia Sheria ya Serikali za Mitaa na Sheria Ndogo zilizotungwa ili
kuimarisha usalama katika Halmashauri
husika.
(iii) Kuhimiza wafanyabiashara wasaidiane na vikundi vya ulinzi shirikishi/ulinzi
jirani vilivyo kwenye maeneo jirani na biashara zao kama sehemu ya kuimarisha
usalama wa maeneo yao ya biashara. Pia, kwa wafanyabishara wenye biashara kubwa
zenye mikusanyiko ya Watu wengi wanaagizwa kufunga “CCTV Camera” na
kuziunganisha kimtandao na “Control Room”
ya Polisi ili kutoa msaada wa kuzuia na kutanzua mapema uhalifu wowote
utakaojitokeza.
(iv)
Kuendelea kuunda Zonal Task Force za Jeshi la Polisi
katika kila Tarafa/Jimbo ili kukusanya taarifa za uhalifu na kufanya operesheni
za kuzuia uhalifu katika kila Kata au Shehia zilizo ndani ya Tarafa husika. Kwa kufanya hiovyo
tutaokoa maisha ya watu wengi.
(v)
Kuendelea
kutoa elimu kwa jamii kuhusu mbinu mbalimbali za kuzuia na kupambana na uhalifu
kwa kutumia vyombo mbalimbali vya habari, mihadhara, mikutano, maonesho na
usambazaji wa machapisho na vipeperushi.
Mheshimiwa
Spika,
83.
Jukumu la kuhakikisha
Ulinzi na Usalama katika Nchi yetu ni letu sote. Kila Mwananchi popote alipo anawajibika
kushiriki kwa vitendo kwa kubaini vitendo vyovyote vya uhalifu katika sehemu za
kazi, biashara na maeneo tunamoishi.
Wito wangu kwa Waheshimiwa Wabunge wote, ni kuwaomba tuwahimize Wananchi
kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha Nchi yetu inadumu katika hali ya Amani
na Utulivu.
IX: HITIMISHO
Mheshimiwa
Spika,
84.
Kwa
kuhitimisha, naomba nitumie nafasi hii ya mwisho kuwashukuru wote waliosaidia
kufanikisha Mkutano huu. Kipekee nikushukuru wewe Mheshimiwa Spika, pamoja na
Naibu Spika kwa kutuongoza vizuri.
Niwashukuru Wenyeviti wa Bunge kwa kazi nzuri ya kuongoza vikao vya Bunge
lako Tukufu. Aidha, niwashukuru tena
Waheshimiwa Wabunge kwa kazi nzuri na kwa michango mbalimbali wakati wa Mkutano
huu. Namshukuru Katibu wa Bunge na Wasaidizi wake wote pamoja na Wataalam wote
wa Serikali na Taasisi zake ikijumuisha Taasisi za Sekta Binafsi, kwa misaada
ya Kitaalam na huduma mbalimbali za kufanikisha Mkutano huu. Niwashukuru pia
Waandishi wa Habari kwa kazi nzuri walizofanya kuhakikisha kuwa taarifa za
majadiliano na maamuzi mbalimbali ya hapa Bungeni zinawafikia Wananchi. Niwashukuru Madereva kwa kazi nzuri
waliofanya ya kuwasafirisha kwa usalama Waheshimiwa Wabunge,Viongozi
mbalimbali, Wataalam na Wasaidizi wote walioshiriki katika Mkutano huu.
Mheshimiwa
Spika,
85.
Nimalizie
kwa kuwatakia wote safari njema mnaporejea kwenye maeneo yenu ya kazi na katika
majimbo yenu. Baada ya kusema hayo,
naomba sasa kutoa hoja kwamba, Bunge lako Tukufu liahirishwe hadi tarehe 3 Desemba, 2013 saa 3:00 Asubuhi
litakapokutana katika Mkutano wa 14 kwenye Ukumbi huu hapa Dodoma.
Mheshimiwa
Spika,
86.
Naomba
kutoa hoja.
0 comments:
Post a Comment