TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Aliyekuwa
mgombea Urais wa UKAWA kupitia CHADEMA, Ndugu Edward Lowassa, Aprili 7, 2016
alifanya mazungumzo na Wanazuoni kutoka katika vyuo vikuu vya ndani na nje ya
nchi.
Katika
mazungumzo hayo, Ndugu Lowasa aligusia masuala mbalimbali ya Kitaifa yakiwemo hali
ya siasa nchini, kuachisha kazi watumishi wenye tuhuma mbalimbali, na kile
alichokiita tatizo la mfumo nchini.
Alichokifanya
Ndugu Lowassa ni kutaka kuwaaminisha Watanzania masuala yasiyo sahihi kwa
maslahi ya kisiasa, kwani ukweli ni kwamba; Mosi, Rais John Pombe Magufuli
hatafuti umaarufu, badala yake yeye na Serikali yake wanachapa kazi ili
kuwaletea maendeleo Watanzania kwa ujumla.
Pili,
kuhusu suala la mfumo, Tanzania haina tatizo la kimfumo, kwani iliyopo, iliyowekwa
tangu awali na waasisi wa Taifa letu, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere na Hayati Abeid Aman Karume ni imara na imekuwa ikiboreshwa kulingana
na mahitaji.
Ifahamike
hakuna mahali popote duniani ambako mfumo wa nchi unajiendesha wenyewe, siku
zote mfumo huongozwa na kuendeshwa na binadamu ambao kwa udhaifu wa ama kibinadamu
au wa kukusudia, hufanya makosa yanayohitaji kusahihishwa kwa taratibu
zilizowekwa.
Tatu,
Hakuna mtumishi aliyeachishwa au kusimamishwa kazi kwa sababu ya hali ngumu ya
uendeshaji wa Shirika lolote, isipokuwa hatua hiyo imechukuliwa ili kupisha uchunguzi kutokana na tuhuma
mbalimbali za ukiukaji na matumizi mabaya ya ofisi na madaraka, ubadhirifu,
uhujumu uchumi na ufisadi.
Chama
Cha Mapinduzi kina ushahidi wa utendaji wa Ndugu Lowasa akiwa Waziri Mkuu namna
alivyoendesha zoezi la kusimamisha na kufukuza kazi na kuwadhalilisha watumishi
bila kufuata taratibu, hali hiyo ni tafauti sana na hii ya sasa, kwani kila
anayesimamishwa kazi, anasimamishwa kwa kufuata taratibu zote, ili kuhakikisha
kila mtumishi anatendewa haki ya kusikilizwa.
Na
katika hili la kuwasimamisha kazi watumishi wa umma wanaotuhumiwa kwa ufisadi,
wizi na matumizi mabaya ya ofisi, Chama Cha Mapinduzi kitaendelea kuunga mkono,
kutokana na baadhi yao kuwa chanzo cha shughuli za maendeleo nchini.
Kiongozi
au mwanasiasa anayemkosoa Rais Magufuli katika hatua anazozichukua hivi sasa,
ikiwa ni pamoja na kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za umma, ni wa kutiliwa
shaka kwani kufanya hivyo ni sawa na kutetea wizi, ufisadi na uporaji wa rasilimali
za nchi.
Ndugu Christopher Ole Sendeka
MSEMAJI WA CCM
MJUMBE WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA,
MJUMBE WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA,
08/04/2016
Waziri mkuu aliyejiuzulu kwa tuhuma za ufisadi, Edward Lowassa hana jipya.
ReplyDelete