4x4

HOTUBA YA MGENI RASMI KATIBU TAWALA WA WILAYA YA ILALA, EDWARD MPOGOLO KATIKA UZINDUZI WA KAMPENI YA KIWILAYA YA SIKU 16 ZA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA, VIWANJA VYA SHULE YA MSINGI VINGUNGUTI, TAREHE 5 DESEMBA 2015

HOTUBA YA MGENI RASMI KATIBU TAWALA WA WILAYA YA ILALA, EDWARD MPOGOLO KATIKA UZINDUZI WA KAMPENI YA KIWILAYA YA SIKU 16 ZA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA, VIWANJA VYA SHULE YA MSINGI VINGUNGUTI, TAREHE 5 DESEMBA 2016

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala,
ACP. Salum Hamdani
Mbunge wa Jimbo la Segerea,
        Mhe. Bonnah Kalua
Naibu Meya wa Manispaa ya Ilala/Diwani wa Kata ya Vingunguti
        Mhe. Omar Kumbilamoto
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala,
        Ndugu Msongela Palela
Mkurugenzi wa WILDAF
        Mwakilishi wa Plan International
        Makamanda wa Polisi Mliopo hapa
Waheshimiwa Viongozi wote na mliopo hapa
Ndugu waandishi wa Habari, wageni waalikwa, mabibi na mabwana.    Itifaki imezingatiwa

Asalaam Alykuum! Bwana Yesu Asifiwe!

Utangulizi
Ndugu Wananchi. Awali ya yote, napenda kuchukua nafasi hii kutoa shukrani zangu za dhati kwa heshima kubwa ambayo mmempatia Mkuu wa
Wilaya ya Ilala kuwa mgeni rasmi kwenye Uzinduzi wa Kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia wenye kauli mbiu “Funguka, Pinga
Ukatili wa Kijinsia Elimu Salaama kwa Wote”.

Aidha, naomba kutumia fursa hii kuwakaribisha washiriki wote ambao mmejumuika nasi katika kufanikisha shughuli hii muhimu kwa ustawi wa
nchi yetu. Nimefahamishwa kuwa watu hawa, viongozi na makamanda wametoka maeneo mbalimbali katika Mkoa wa Dar es salaam, ambapo
wameacha shughuli zao za kila siku na kuja kujumuika nasi hapa Vingunguti. Asanteni kwa Kuja. Binafsi ninayo furaha kujumuika nanyi
kwenye uzinduzi huu kwani pamoja na mambo mengine imenipa nafasi ya kujifunza kutoka kwenye maelezo ya Kamanda wetu wa Mkoa wa Kipolisi
Kaka yangu Hamdun, maneno ya Kiongozi wa WiLDAF, maelezo ya Plan International na Ujumbe kutoka kwa wasanii wetu wa ngoma.

Ndugu Wananchi,
Naomba nitumie hadhara hii kulipongeza Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika (WiLDAF) Tawi la Tanzania kwa kudhamini na
kuratibu shughuli hii. Nafahamu kwamba maandalizi haya yalipewa msukumo na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala chini ya dawati la Jinsia,
sambamba na watu wa Plan International. Nawapongezeni nyote kwa kubeba dhamana kubwa ya kufanikisha maandalizi haya, kazi ambayo siyo tu ni
nzito bali umuhimu wake katika mchakato mzima wa kulinda na kutetea haki za binadamu hususan Wanawake (Mama Zetu) ni mkubwa.

Maadhimisho ya Siku 16 za Mapambano ya UWAKI
Ndugu Wananchi, Kama wengi wetu tunavyofahamu, chanzo cha maadhimisho haya ni mauaji ya kikatili ya wasichana wa Mirabelle huko nchini
Dominika mwaka 1960. Kutokana na hali hiyo, mwaka 1991,  Umoja wa Mataifa (UN) ulitenga Siku 16 kila mwaka kama siku ya kimataifa ya
kupinga unyanyasaji dhidi ya wanawake. Hivyo siku ya kuhitimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia ambayo ni tarehe 10 Desemba huwa ni
siku maalumu pia ya kuadhimisha Tamko la Haki za Binadamu.

Kuwepo kwetu hapa leo hii kunatokana na azma yetu sote kama taifa kuungana na Mataifa mengine duniani katika kuadhimisha siku hizi 16
kama sehemu ya majukumu yetu ya kimataifa na kwa sababu  taifa letu linaheshimu Haki na Utu wa mwanamke ambao ni nguzo yetu.

Juhudi za Serikali,
Ndugu Wananchi,
Masuala ya ukatili wa kijinsia yana wigo mpana na sura nyingi. Hivyo, yanataka jitihada za kila mwanajamii katika kuyashughulikia. Kwa
upande wa Serikali, tumejitahidi kuheshimu haki za binadamu na juhudi mbalimbali zimefanyika kwa uchache naomba nizitaje;-

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, Sura ya Kwanza, Sehemu ya Tatu inaelezea Haki ya Usawa. Kila mtu anastahili
heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa Utu wake; Sheria ya Makosa ya Kujamiina ya mwaka 1998 sheria hii inashughulikia vitendo vya
udhalilishaji;

Serikali inaendelea kufanyia mabadiliko makubwa katika sheria kandamizi kwa wanawake, mfano Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 na Sheria
ya Urithi na kutunga sheria za kuleta usawa wa kijinsia. Kuridhia kwa Mkataba wa Umoja wa Mataifa mwaka 1981 ambao unapinga aina zote za
ubaguzi dhidi ya wanawake (Convection on the Elimination of All Forms of Discrimination Against Women - CEDAW).


Aidha, Jitihada nyingine ni pamoja na kufanyiwa marekebisho ya sheria ya ardhi mwaka 2004 iliyokuwa sheria ya Ardhi ya mwaka 1999 ambayo
kwasasa inawapa haki wanawake kupata, kushiriki, kutumia na kumiliki ardhi. Serikali pia imetoa muongozo wa kisera wa sekta ya afya wa
kuzuia na kupambana na ukatili wa kijinsia wa mwaka 2013 ili kukabili tatizo la Ukatili wa Kijinsia (UWAKI).

Mwisho lakini siyo kwa umuhimu, ningependa kumshukuru na kumpongeza Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa jitihada zake za
kuwainua wanawake, ameendelea kuwapa wanawake nafasi za maamuzi na uongozi katika nyanja mbalimbali za uongozi wa kisiasa na utendaji wa
Umma hapa nchini. Jitihada zote hizi za serikali ni katika utekelezaji
wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG) ifikapo 2030.

Ukubwa wa tatizo la UWAKI
Ndugu Wananchi,
Utafiti uliofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO) 2000 kuhusu afya ya wanawake na ukatili majumbani kwenye nchi 10 umebaisha kuwa,
ukatili dhidi ya wanawake upo sehemu nyingi ikiwamo Tanzania. Katika Mkoa wa Dar es salaam utafiti ulihusisha wanawake 1820 kati ya hao
asilimia 41 ya waliohojiwa  waliathirika na aina mbalimbali za UWAKI. Aidha, taarifa inaonyesha kati yao asilimia 15 hadi 71 waliathirika na
ukatili wa kimwili au wa kingono ulifanywa na wanaume au wenzi wao. Utafiti ulibaini pia zaidi ya asilimia 90 ya waathirika wa ubakaji
wanawafahamu wahalifu wao.

Katika Wilaya ya Ilala mwaka 2015 kesi zilizoripotiwa zilikuwa 633 na Wilaya ya Kipolisi iliyoongoza ni Wilaya ya Ukonga. Mwaka huu hadi
kufikia Septemba 2016  jumla ya kesi 1094 ziliripotiwa na Wilaya ya kipolisi inayoongoza hadi sasa ni Wilaya ya Buguruni. Taarifa
inaonyesha kesi zinazoongoza kati ya hizo ni ndoa za utotoni na ulawiti. Ongezeko hilo kubwa la kesi zinazoripotiwa linatokana na
elimu inayotolewa na uwepo wa Kituo cha pamoja (One Stop Center) kilichopo Amana kinachohusisha Jeshi la Polisi, Madaktari, Ustawi wa
Jamii na Wanasheria.

Changamoto za UWAKI
Ndugu Wananchi, licha ya jitihada zinazochukuliwa na serikali kwa kushirikiana na makundi mbalimbali ya kijamii, takwimu bado
zinaonyesha ongezeko la Ukatili Wa Kijinsia (UWAKI). Ongezeko hili linachangiwa na changamoto zifuatazo;-
(a)     Imani za Kishirikina,
(b)     Mila na desturi – Utamaduni wa kunyamaza/ Mamlaka juu ya mke na watoto
(c)     Umaskini
(d)     Ukosefu wa Nyumba salama (Safe House)
(e)     Elimu

Nini kifanyike
Ndugu Wananchi, baada ya kuona changamoto na kwa kuzingatia kaulimbiu ya mwaka huu ya “Funguka, Pinga Ukatili wa Kijinsia Elimu Salaama kwa
Wote” kila mmoja wetu ana wajibu wa kufanya yafuatayo;-
•       Kuendelea kutoa Elimu ya kuzuia ukatili wa kijinsia katika sekta mbalimbali kama vile mashuleni na kwenye maeneo yote ya huduma za
kijamii sambamba na kupambana na ukatili huo.
•       Kuhakikisha kuwa na Sheria moja  inayohusiana na Ukatili Wa Kijinsia (UWAKI)
•       Kuendelea kuwashirikisha wanaume kwenye vita hii ya UWAKI kwani tafiti zinaonyesha wanaume ndiyo watuhumiwa wa kwanza.
•       Kujenga hadhi ya familia. (Haki, Wajibu na Maadili katika familia)
•       Ushirikishwaji wa Makundi yote ya Jamii kupambana na UWAKI

Hitimisho
Mwisho, ningependa kurudia kuwashukuru Jeshi la Polisi kwa kupitia kwako Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala, WiLDAF tawi la
Tanzania, Plan International  na Mashirika na Taasisi zilizofanikisha maandalizi ya kampeni hii ya siku 16 ya kupinga ukatili wa kijinsia.
Napenda kuwashukuru wananchi, wanahabari na wote  mliojumuika nasi na kunisikiliza. Nitoe wito wa Kufunguka, Pinga Ukatili wa Kijinsia Elimu
Salaama kwa Wote.

Baada ya kusema hayo napenda kutamka kwamba Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia katika Mkoa wa Kipolisi wa Ilala zimezinduliwa Rasmi.

Asanteni kwa kunisikiliza.

0 comments:

Post a Comment