Mheshimiwa
Anne Makinda, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa
Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
Mheshimiwa
Mizengo Pinda, Waziri Mkuu;
Waheshimiwa
Mawaziri na Naibu Mawaziri;
Mheshimiwa
Freeman Mbowe, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni;
Waheshimiwa
Wabunge;
Mabibi
na Mabwana;
Nakushukuru sana Mheshimiwa Spika kwa
kukubali ombi langu na kutenga muda wenu ili niweze kuzungumza na Wabunge wa Bunge
lako Tukufu kuhusu masuala muhimu kwa uhai, ustawi na maendeleo ya nchi yetu na
watu wake.
Mheshimiwa
Spika;
Nimeambiwa kuwa taarifa ilipotolewa
kuwa ninaomba kuja kuzungumza na Waheshimiwa Wabunge, kumekuwepo na dhana
mbalimbali. Wapo waliodhani kuwa nakuja kuzungumzia
mchakato wa kuunda Katiba mpya na hasa matukio ya wiki chache zilizopita. Wapo
waliodhani nakuja kuzungumzia “Operesheni Tokomeza”. Tena wapo waliokwenda mbali na kufikiria kuwa
nakuja kuwakaripia Waheshimiwa Wabunge waliotoa maoni yao kuelezea kasoro zilizojitokeza
katika utekelezaji wa Operesheni hii muhimu. Na wapo pia waliodhani ninakuja
kuzungumzia ushiriki wa majeshi yetu ya Tanzania katika Jeshi la Kulinda Amani
la Umoja wa Mataifa nchini Kongo.
Mheshimiwa
Spika;
Hayo si makusudio yangu. Kinachonileta mbele ya Bunge lako Tukufu ni
kuzungumzia Jumuiya ya Afrika Mashariki na mustakabali wa Tanzania katika
Jumuiya hiyo. Lakini, kwa sababu ya
umuhimu wa masuala hayo niliyoyataja na rai niliyopewa kuwa niyasemee japo
kidogo. Nimeona ni vyema nifanye hivyo.
Mheshimiwa
Spika;
Kuhusu mchakato wa Katiba mpya, napenda kusema kuwa tumefikia hatua
nzuri katika utekelezaji wake. Kama
mjuavyo Tume ya Mabadiliko ya Katiba imekamilisha, kwa mafanikio, hatua ya
mwanzo ya kusikiliza maoni ya wananchi kuhusu Katiba wanayoitaka. Pia walishatoa Rasimu ya Kwanza ya Katiba na
kukamilisha mchakato wa Mabaraza ya Katiba.
Kinachosubiriwa kwa hamu na sisi wote, ni Rasimu ya Pili ya Katiba
ambayo inatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 15 Desemba 2013 au kabla ya hapo.
Mheshimiwa
Spika;
Kwa upande wa Bunge lako Tukufu, tunategemea
kupata mambo mawili kutoka kwenu yatakayowezesha mchakato kutekelezwa vizuri
katika hatua zinazofuata. Jambo la
kwanza ni kutungwa kwa Sheria ya Kura ya Maoni na pili kufanyika kwa marekebisho
ya nyongeza ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kuhusu Bunge Maalum ili kuboresha
utekelezaji wake. Baada ya Bunge
kukamilisha kazi yake hiyo itafuatia uteuzi wa Wajumbe wa Bunge Maalum ili kazi
ya kujadili Rasimu ya Pili ya Katiba ifanyike na kutupatia Rasimu ya Mwisho.
Rasimu ambayo ikikubaliwa na wananchi katika Kura ya Maoni itakayofanyika
wakati wo wote mwakani, tutakuwa tumepata Katiba Mpya. Hivi sasa katika Serikali tunaendelea kufanya
tafakuri na tunachukua hatua za kuwezesha Bunge Maalum na Kura ya Maoni
kufanyika kwa mafanikio.
Operesheni
Tokomeza
Mheshimiwa
Spika;
Napenda kuwahakikishia Waheshimiwa
Wabunge wa Bunge lako Tukufu kuwa sikukasirishwa na maoni yao kuhusu madai ya kuwepo
kasoro katika utekelezaji wa Operesheni Tokomeza. Shabaha ya Operesheni hii ni
kuokoa maliasili za misitu na wanyamapori dhidi ya uvunaji haramu ambao umefikia
kiwango kinachotishia kutoweka kwa raslimali hizo. Kwa kweli hali inatisha. Miti inakwisha na ndovu na faru
wanaangamia.
Mheshimiwa
Spika;
Wakati, tunapata Uhuru Tanzania
ilikuwa na ndovu waliokadiriwa kuwa takribani 350,000. Lakini, kwa sababu
ya ujangili uliokithiri katika miaka ya 1970
na 1980 ilipofika mwaka 1989 kulikuwa na ndovu wapatao 55,000
tu. Ilipofikia hali hiyo Serikali
ikaanzisha Operesheni Uhai iliyohusisha Jeshi la Ulinzi na kuongozwa na Meja
Jenerali John Walden (ambaye sasa ni
marehemu) kuendesha mapambano dhidi ya majangili. Kutokana na hatua hiyo na uamuzi
wa Shirika linalosimamia biashara ya wanyama walioko kwenye hatari ya kutoweka (CITES)
kupiga marufuku biashara ya pembe za ndovu duniani, idadi ya ndovu nchini
iliongezeka na kufikia 110,000 mwaka
2009.
Tumewaomba Fankfurt Zoological Society
ambao ni wabia wetu katika uhifadhi wa wanyama pori kwa miaka mingi wafanye
sensa maalum ya ndovu katika Hifadhi ya Selous na kote nchini ili tujue hali
halisi ikoje. Kazi hiyo inaendelea hivi
sasa.
Mheshimiwa
Spika;
Baada ya mwaka 2009 kumezuka
wimbi jipya, tena la nguvu kubwa, la kuua ndovu na faru nchini na kwingineko
katika Bara la Afrika ambako wanyama hao wapo.
Idadi kubwa ya meno ya ndovu yaliyokamatwa na yanaoendelea kukamatwa
nchini na kwingineko duniani inathibitisha ukweli huo. Kwa mfano, kati ya mwaka 2010 na Septemba, 2013,
hapa nchini, kwa jitihada zetu vipande 3,899
vya pembe za ndovu vyenye uzito wa kilo 11,212
na vipande 22 vya pembe za ndovu zilizochakatwa
zenye uzito wa kilo 3,978
vilikamatwa. Aidha, katika kipindi hicho
vipande 4,692 vya pembe za ndovu vilivyotokea
Tanzania vyenye uzito wa kilo 17,797
vilikamatwa nje ya nchi.
Mheshimiwa
Spika;
Kama nilivyokwisha sema hapo awali
matatizo ya kuuawa kwa wingi kwa ndovu na faru lipo pia katika nchi nyingine
Afrika zenye wanyama hao. Nchi za Gabon, Kenya, Afrika ya Kusini,
Jamhuri ya Afrika ya Kati, Uganda, Zimbabwe, Zambia na nyinginezo nazo zinakabiliwa
na matatizo kama yetu. Tatizo limekuwa
kubwa kiasi cha kuifanya Jumuiya ya Kimataifa kushtuka na kuamua kuingilia kati
kwa namna mbili. Kwanza kuunga mkono
juhudi za uhifadhi wa ndovu na faru katika nchi zenye wanyama hao. Na, pili, kuchukua hatua thabiti kudhibiti
biashara ya meno ya ndovu duniani. Ni
ukweli ulio wazi kuwa kama hakutakuwepo na wanunuzi wa meno ya ndovu na faru hakuna
ndovu au faru atakayeuawa.
Mheshimiwa
Spika;
Kutokana na ukweli ulivyo uamuzi wetu wa
kuendesha Operesheni Tokomeza ni sahihi kabisa.
Manufaa yaliyopatikana baada ya Operesheni Uhai ya mwaka 1989 yanatupa imani kuwa na safari hii pia
tutafanikiwa. Tusipochukua hatua kama
hii sasa ni sawa na kuwapa kibali majangili waendelee kumaliza ndovu na faru nchini. Hakika wanyama hao watakwisha. Itakuwa ni aibu kubwa kwetu na historia
itatuhukumu vibaya.
Mheshimiwa
Spika;
Tumeyasikia maelezo ya Wabunge kuhusu
kasoro mbalimbali zilizojitokeza katika utekelezaji wa Operesheni Tokomeza. Nawaahidi kuwa tutayafanyia kazi. Serikali imeahirisha kwa muda Operesheni hii
ili kujipa muda wa kurekebisha kasoro hizo na kujipanga upya. Watendaji wasiokuwa waadilifu na wale
wasiokuwa waaminifu wataondolewa. Halikadhalika,
kasoro za kimfumo nazo zitasahihishwa ili tutakapoanza upya Operesheni itekelezwe
kwa mafanikio yaliyokusudiwa.
Mheshimiwa
Spika;
Miongoni mwa mambo yaliyozungumzwa kwa
uchungu ni ukamataji wa mifugo iliyokutwa kwenye mapori ya hifadhi za wanyama
na vitendo vibaya walivyofanyiwa wenye mifugo na mifugo yenyewe. Narudia kusisitiza kuwa taarifa zote hizo zitafanyiwa
kazi na waliohusika watachukuliwa hatua zipasazo. Pamoja na hayo, napenda kuwakumbusha ninyi watunga
sheria wetu kuwa sheria ya hifadhi za wanyamapori hairuhusu mifugo kuchungwa
katika maeneo ya hifadhi.
Naomba tuwakumbushe wananchi
tunaowaongoza wajiepushe na kufanya hivyo.
Ni uvunjifu wa Sheria za nchi. Naomba
pia, wananchi waelimishwe ili wajue kuwa wakifanya hivyo na kukutwa katika
maeneo hayo na mifugo yao kuna adhabu iliyotamkwa kwenye sheria. Hivyo tusiwalaumu wala kuwaona maafisa
wanyamapori kuwa ni watu wabaya. Wanatekeleza
Sheria iliyotungwa na Bunge hili. Pale
wanapotenda visivyo tuseme, watawajibishwa ipasavyo.
Jeshi
la Umoja wa Mataifa Kongo
Mheshimiwa
Spika;
Mapema mwaka huu (2013) Umoja wa Mataifa
uliomba nchi yetu ichangie kikosi kimoja cha wanajeshi katika Brigedi Maalum iliyoundwa
na Umoja huo kuongeza nguvu ya kudhibiti waasi Mashariki ya Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo. Lengo la msingi
ni kuiwezesha nchi hiyo kupata amani ya kudumu ambayo imekosekana kwa muda
mrefu kutokana na kuibuka kwa uasi mara kwa mara.
Mheshimiwa
Spika;
Tulikubali, kwani hata kabla ya kuombwa
na Umoja wa Mataifa tulishakubali maombi kama hayo yaliyotolewa kwenye Mkutano
wa Nchi za Maziwa Makuu. Ni miezi saba
(tangu Aprili) sasa tangu wanajeshi wetu waende Kongo na wamekuwa wanatekeleza
majukumu yao vizuri tena kwa weledi na nidhamu ya hali ya juu. Sifa hiyo kwa wanajeshi wetu imekuwa
inatolewa na viongozi wa juu wa Umoja wa Mataifa, viongozi wa juu wa Jeshi la
Umoja wa Mataifa Kongo (MONUSCO) na viongozi wa juu wa Serikali ya Kongo.
Mheshimiwa
Spika;
Majeshi ya Umoja wa Mataifa hupewa majukumu
na mamlaka ya namna mbili. Yapo yanayopewa
jukumu la kulinda amani tu. Wanajeshi
wake huwa hawapewi majukumu ya kimapigano na hata pale wanaposhambuliwa wanatakiwa
kujihami tu. Kwa kawaida majeshi yenye
jukumu hili hupelekwa mahali ambapo kumekuwepo na makubaliano ya kuacha
mapigano. Wanapelekwa kusaidia kuona
Mkataba unatekelezwa ipasavyo.
Aina ya pili ni ile ya majeshi
yanayopelekwa mahali ambapo hakuna amani hivyo wanapewa jukumu la kuchukua
hatua za kufanya amani ipatikane. Majeshi
haya hupewa mamlaka ya kutumia nguvu ya kijeshi dhidi ya wanaosababisha amani
ikosekane kama ni lazima kufanya hivyo.
Maana yake ni kwamba wanayo ruhusa kuingia katika mapigano dhidi ya watu
au vikundi vinavyovuruga amani. Tofauti
na wenzao wa kundi la kwanza, wanajeshi wa kundi la pili wako kwenye hatari zaidi
ya kupoteza maisha au kujeruhiwa kuliko wenzao ingawaje wapo wengi nao wameuawa
na kujeruhiwa.
Mheshimiwa
Spika;
Wanajeshi wetu wamekwenda Kongo chini ya
utaratibu huu wa pili ambao unahusu kuingia kwenye mapigano dhidi ya waasi kama
hapana budi kufanya hivyo. Wametekeleza
majukumu yao vyema na kwa ujasiri mkubwa na weledi wa hali ya juu. Bahati mbaya
tumepoteza vijana wetu watatu shupavu.
Daima tutawakumbuka na tutawaenzi ipasavyo mashujaa wetu hawa. Tuzidi kuwaombea kwa Mola awape mapumziko
mema. Ameen.
Wakati huo huo, Mheshimiwa Spika, napenda
kutumia nafasi hii kumpongeza Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo kwa mafanikio ya kihistoria waliyoyapata hivi majuzi dhidi ya waasi wa
M23. Tunamtakia yeye na wananchi wa
Kongo kila la heri katika kazi ngumu iliyo mbele yao ya kujenga upya eneo hilo
na kujenga mahusiano mapya miongoni mwa watu wa Kongo. Pia nawapongeza sana wanajeshi wa Brigedi
Maalum ya Umoja wa Mataifa kwa kazi nzuri waliyoifanya iliyowezesha mafanikio
kupatikana. Wanajeshi hao ni kutoka Afrika Kusini,
Tanzania na Malawi wanaoongozwa na Brigedia Jenerali James Aloisi Mwakibolwa wa
JWTZ.
Jumuiya
ya Afrika Mashariki
Mheshimiwa
Spika;
Kama nilivyosema awali, haya mambo
matatu siyo hasa makusudio yangu nilipoomba kuja kuzungumza na Waheshimiwa
Wabunge wetu. Nimeyachomekea tu kwa sababu
ya umuhimu wake katika jamii kwa wakati tulio nao. Jambo lililonileta hapa leo ni kuzungumzia hali
ilivyo sasa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na nafasi ya Tanzania katika
Jumuiya hiyo. Nimeona nifanye hivyo
kutokana na maswali mengi ambayo Watanzania wanajiuliza kufuatia matukio ya
hivi karibuni ya viongozi wa nchi tatu wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
yaani Uganda, Rwanda na Kenya kukutana bila ya ushiriki wa viongozi wa Tanzania
na Burundi. Viongozi wenzangu hao
wamefanya mikutano mitatu yaani: tarehe 24-25 Juni, 2013 mjini Entebbe, Uganda;
tarehe 28 Agosti, 2013 mjini Mombasa, Kenya; na tarehe 28 Oktoba, 2013 mjini
Kigali, Rwanda.
Mheshimiwa
Spika;
Naomba kwanza niweke wazi jambo moja, kwamba
nchi mbili wanachama au zaidi hazikatazwi kuwa na makubaliano ya ushirikiano
katika kufanya mambo mbalimbali. Hata
sisi Tanzania tunao ushirikiano wa namna hiyo na nchi zote wanachama wa Jumuiya
ya Afrika Mashariki. Lakini, nchi
wanachama zinatakiwa kufanya hivyo kwa yale mambo ambayo hayako kwenye shughuli
za Jumuiya kwa maana kwamba hayamo katika Mkataba au Itifaki au hakuna uamuzi
wa msingi uliofanywa na vikao au taasisi za Jumuiya kuyashughulikia. Pia, tunaweza kufanya hivyo kwa mambo ambayo
yalishaamuliwa na Jumuiya yatekelezwe na ruhusa imetolewa kwa nchi yo yote
iliyokuwa tayari kutekeleza ama peke yake au kwa kushirikiana na nchi nyingine.
Mheshimiwa
Spika;
Kwa mujibu wa matamko ya pamoja (Communique)
yaliyotolewa baada ya mikutano hiyo, kuna mambo yapatayo manane ya msingi yaliyoamuliwa kufanywa na nchi hizo kwa lengo la
kuendeleza utengamano wa nchi hizo wanachama wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki. Mambo hayo ni haya yafuatayo:
(1)
Kujenga reli ya kisasa kutoka
Mombasa hadi Kampala, Kigali na Bujumbura.
(2)
Ujenzi wa Bomba la
Mafuta la kutoka Kenya hadi Uganda na Sudani ya Kusini.
(3)
Kujenga Kiwanda cha
kusafisha mafuta nchini Uganda.
(4)
Kuanzisha Himaya Moja ya Ushuru wa Forodha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na
kutekeleza vipengele vyote;
(5)
Kuharakisha Shirikisho la Afrika
Mashariki na kwamba itaundwa Kamati ya kuandaa rasimu ya Katiba ya Shirikisho.
(6)
Kuharakisha uanzishwaji wa Visa ya
pamoja ya Utalii ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (Single East African Community
Tourist Visa);
(7)
Kuandaa utaratibu wa kutumia
vitambulisho vya taifa kama hati ya kusafiria katika nchi zao; na
(8)
Kuongeza uzalishaji na usambazaji wa
umeme.
Mheshimiwa
Spika;
Ni dhahiri kwamba orodha hiyo
imechanganya mambo yale ambayo ni ya Jumuiya na yale yasiyo ya Jumuiya. Kwa mfano, mambo manne kati ya hayo manane
hayamo kwenye masharti ya kutokufanyika bila ya kuihusisha au kupata ridhaa ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki. Jambo la
kwanza ni uzalishaji na usambazaji wa umeme.
Ni kweli kwamba tunao mkakati wa kuwa na akiba ya pamoja ya nguvu ya
umeme (East African Power Pool). Hata
hivyo, bado jukumu la kuzalisha na kusambaza umeme huo limeachiwa nchi
wanachama zenyewe kuamua. Lakini, hivi
ndugu zetu hawa wanao muhali kuishirikisha Tanzania katika mpango ambao
kimsingi umebuniwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo sote ni
wanachama?
Jambo la pili, ni ujenzi wa kiwanda
cha kusafisha mafuta nchini Uganda. Hili
si suala la Jumuiya bali la nchi ya Uganda kuamua yenyewe peke yake au kwa
kushirikiana na wadau wengine. Rais
Yoweri Museveni alituarifu mpango huo na sote tuliupokea kwa furaha kwamba sasa
tutapata mafuta karibu na nyumbani. Alitualika
kushiriki katika ujenzi wake sijui sasa amebadili mawazo kwamba Tanzania siyo
muhimu.
Mheshimiwa
Spika;
Jambo la tatu ni ujenzi wa bomba la
mafuta kutoka Kenya hadi Sudani ya Kusini na Uganda. Hili si jambo linalobanwa na masharti ya
Jumuiya. Ni juu ya nchi hizi tatu kuamua kufanya ili kuwezesha mafuta yao
kufika kwenye masoko. Hata hivyo,
nimeambiwa kuwa Jumuiya imeshazungumzia bomba la mafuta kutoka Eldoret hadi
Uganda, Rwanda na Burundi kuwa nalo lifike Tanzania kupitia upande wa Kaskazini
Magharibi mwa Tanzania. Inaelekea mpango
huo sasa haupo maana hatujausikia kutajwa katika ujenzi wa bomba hilo.
Mheshimiwa
Spika;
Jambo la nne ni ujenzi wa reli ya
kisasa kutoka Mombasa – Kampala – Kigali – Bujumbura. Hili nalo hatuna tatizo nalo. Si mradi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ni jambo
lililo chini ya mamlaka ya nchi wanachama husika. Hata hivyo, ni vyema kutambua ujenzi wa
miundombinu ya reli, barabara na usafiri wa anga na majini kuunganisha nchi za
Afrika Mashariki ni miongoni mwa mambo ya kipaumbele cha juu yanayoshughulikiwa
na Jumuiya yetu. Jumuiya hutengeneza
mikakati ya pamoja na ndiyo maana tuna East African Railway Masterplan, tuna
East African Road Network, na tuna Lake Victoria Development Programme kwa ziwa
Victoria.
Kwa ajili hiyo, nilitegemea kuwa reli
ya kutoka Mombasa hadi Kigali na Juba ingekuwa na tawi linalounganisha reli
hiyo na reli ya Tanzania kama ilivyo reli ya Moshi – Voi – Taveta aliyotuachia
mkoloni. Tulitegemea hivyo kwa minajili ya kuunganisha soko la Afrika Mashariki
ambapo naamini Tanzania ni mdau muhimu.
Lakini inaelekea kwa maoni ya wenzetu hivyo sivyo.
Mheshimiwa
Spika;
Lazima nikiri kuwa inashangaza na
tunayo kila sababu ya kuuliza kwa nini wenzetu wameamua kufanya hivi. Kumetokea nini toka tukutane pale Arusha
Aprili 28, 2013 na Juni 24, 2013 walipokutana kuamua kufanya mambo ya kujenga
na kuimarisha utengamano wa Afrika Mashariki kwa kubaguana, Haijawahi kuwa hivi kabla.
Mheshimiwa Spika;
Katika mambo manne yaliyosalia ambayo yaliamuliwa
na kuwekewa utaratibu wake wa utekelezaji na Jumuiya ya Afrika Mashariki mawili
hatuna maneno nayo. Mambo hayo ni
matumizi ya vitambulisho vya taifa kama hati ya kusafiria na Visa ya Pamoja ya
Utalii kwani tuliamua kwa pamoja kuwa nchi wanachama zilizokuwa tayari
waanze. Lakini, kwa upande wa kuanzishwa
kwa Himaya Moja ya Ushuru wa Forodha (Single Customs Territory) na Shirikisho
la Afrika Mashariki tunadhani wenzetu wamekiuka uamuzi wetu wa pamoja.
Mheshimiwa Spika;
Katika
Mkutano Maalum wa 11 wa Wakuu wa Nchi wanachama uliofanyika tarehe 28 Aprili,
2012 Jijini Arusha, tulipokea na kuridhia mapendekezo ya kuanzisha Himaya Moja
ya Ushuru wa Forodha (Single Customs Territory). Kwa mujibu wa mapendekezo hayo kila nchi
mwanachama itasimamia shughuli zake za kiforodha na kukusanya mapato yake kama
ilivyo sasa. Hata hivyo, kwa bidhaa
zinazopitia nchi moja kwenda nchi nyingine mwanachama, ukaguzi na ukusanyaji wa
mapato utafanyika katika kituo cha kwanza bidhaa hizo zinapoingilia. Mapato hayo yatawasilishwa kwa nchi husika
baada ya kuthibitisha kuwa bidhaa zilivuka mpaka.
Mheshimiwa Spika;
Kutokana
na uamuzi huo, Wakuu wa Nchi waliagiza Baraza la Mawaziri kuunda Kikosi Kazi
cha kujadiliana na kuandaa utaratibu wa utekelezaji wa mfumo huo. Taarifa ya kikosi kazi inatakiwa kutolewa
katika Mkutano wa 15 wa Wakuu wa Nchi utakaofanyika Kampala, Uganda tarehe 30 Novemba,
2013. Iweje leo nchi tatu wanachama ziamue
peke yao kuanza kutekeleza? Wanatekeleza
nini na kwa nini wafanye hivyo?
Mheshimiwa Spika;
Kuhusu Shirikisho la Kisiasa la Afrika
Mashariki hadithi yake inafanana na hii ya Himaya ya Forodha. Katika Mkutano wa 14 wa Wakuu wa Nchi wanachama uliofanyika tarehe
30 Novemba, 2012, Nairobi, tulipokea taarifa ya hatua iliyofikiwa kuhusu
mchakato wa kutaka kuanzishwa kwa Shirikisho.
Mkutano huo uliagiza nchi
wanachama kujadiliana zaidi kuhusu mpango kazi wa kufikia Shirikisho la Kisiasa
na mpango wa kutekeleza mapendekezo mengine yaliyotolewa na Timu ya Wataalamu. Inategemewa kuwa Baraza la Mawaziri
litawasilisha mapendekezo ya majadiliano hayo katika Mkutano wa 15 wa Wakuu wa
Nchi mwezi Novemba, 2013. Iweje leo
wenzetu hawa waamue kuanzisha mchakato wao wa kuharakisha Shirikisho la Afrika
Mashariki.
Mheshimiwa Spika;
Kwa
kweli huwa najiuliza maswali mengi na kukosa majibu kuhusu nini kinachoendelea kufanywa
na viongozi wenzangu watatu na kwa nini! Nakosa majibu ya uhakika. Je wenzetu wamekosa imani na Jumuiya ya
Afrika Mashariki na je wanataka kuunda yao?
Je wanaichukia nchi yetu na hivyo wameamua kutufanyia vitimbi
tutoke! Au sijui wanachuki na mimi! Napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge
kuwa hatuna mpango wa kutoka (kama vijana
wasemavyo hatoki mtu hapa). Tupo na
tutaendelea kuwepo!
Mheshimiwa Spika;
Tanzania haijafanya jambo lo lote baya
dhidi ya Jumuiya au nchi yo yote mwanachama.
Na ukweli ni kwamba ni mwanachama mvumilivu, mtiifu na mwaminifu kwa
Jumuiya. Tunatimiza ipasavyo wajibu wetu
kwa Jumuiya na kushiriki kwa ukamilifu katika ujenzi wake na utengamano ndani
ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Sabahu
ya wenzetu watatu kuamua kufanya mambo yahusuyo Jumuiya yetu peke yao kwa kweli
haieleweki.
Mheshimiwa Spika;
Tunasikia
eti kuwa baadhi yao walipoulizwa kwa nini wengine hatupo wakasema kuwa wao
wametangulia na sisi tutakapokuwa tayari tutajiunga. Yaani wana Umoja wa Waliokuwa Tayari
(Coalition of the Willing). Hivi ni nani
hayuko tayari (who is not willing?)
Haiwezekani watu waitane wenyewe bila ya kutualika halafu wadai kuwa wao
ndiyo wako tayari na kujenga dhana kuwa sisi wasiotualika ndiyo ambao hatuko
tayari. Madai hayo hayana ukweli. Ni vyema waseme ukweli. Kama walitualika tukakataa ndiyo wanaweza
kusema hayo.
Mheshimiwa Spika;
Kumekuwepo
na madai kutoka kwa baadhi ya wenzetu, eti kwamba Tanzania haina moyo wala
dhamira ya dhati ya kuendeleza utengamano
wa Afrika Mashariki. Kwa sababu hiyo inasemekana
eti nchi yetu imekuwa kikwazo kwa maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na kwamba
Tanzania tunawachelewesha wengine kupiga hatua za haraka. Wanadai kama siyo hivyo Jumuiya ya Afrika
Mashariki ingekuwa mbali kwa maendeleo. Maneno hayo yamekuwa yanarudiwa au
kujirudia mara nyingi kiasi cha kuwafanya baadhi ya watu wa Afrika Mashariki na
hata kwingineko duniani waamini hivyo.
Mheshimiwa Spika;
Napenda
kusema kwa dhati ya moyo wangu kwamba madai hayo hayana ukweli wo wote. Isitoshe hata sababu zinazotolewa kuthibitisha
ukweli wake hazina mashiko. Hazifanani
na ukweli kuhusu Tanzania na Watanzania walivyo. Tanzania ni muumini wa dhati wa umoja na utengamano
wa nchi za Afrika Mashariki na Afrika.
Tumethibitisha hivyo kwa vitendo kwa kuunganisha nchi zetu mbili huru yaani
Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika na kuwa taifa moja liitwalo
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Muungano
wa nchi zetu mbili ndio pekee uliodumu kwa muda mrefu kuliko yote Afrika.
Mheshimiwa Spika;
Tanzania ni mwanachama mwaminifu wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki kwa maana ya kutekeleza Mkataba ulioanzisha Jumuiya hiyo, kwa Itifaki
zake na maamuzi halali ya vikao na taasisi za Jumuiya. Kama lipo jambo ambalo hatujalifanya ilivyotakiwa
itakuwa ni kwa sababu za msingi na siyo kwa sababu ya kupuuza Jumuiya. Tunaithamini
sana Jumuiya na tumeipa kipaumbele cha juu.
Hatuwezi kuhangaika kwa gharama kubwa ya muda wetu, fedha zetu na kutoa
mchango wa hali na mali kuianzisha, kujenga na kuifikisha Jumuiya hapa ilipo
halafu tuwe ni watu tunaoongoza kutokuipenda na kudhoofisha maendeleo na ustawi
wake. Ni maneno ya kushangaza na wala hayaingii akilini. Ama kweli akutukanae hakuchagulii tusi.
Mheshimiwa Spika;
Nionavyo mimi msimamo wetu kuhusu
kuharakisha Shirikisho na masuala ya ardhi, ajira, uhamiaji, pengine ndiyo yanayotuletea
hisia zisizokuwa sahihi juu yetu. Mimi
siamini kama kuna mengine. Hata hivyo,
napata taabu kuamini kwamba kutofautiana kwa mawazo katika mambo hayo
kutapelekea baadhi ya wenzetu wasipende hata kushirikiana nasi kwa mambo ambayo
hayana matatizo na tumekuwa tunashirikiana vizuri.
Mheshimiwa Spika;
Tanzania
imekuwa inawasihi wanachama wenzetu kuwa tujenge Jumuiya yetu hatua moja baada
ya nyingine kama ilivyo kwenye Mkataba ulioanzisha Jumuiya ya Afrika
Mashariki. Hatuna tatizo la kuongeza
kasi ya ujenzi wa Jumuiya lakini tusivuke hatua yo yote. Tusiende kasi ya kupindukia. Mkataba
unaelekeza tunaanza na Umoja wa Forodha, inafuatia Soko la Pamoja kisha Umoja
wa Kifedha na hatimaye Shirikisho la Kisiasa.
Mheshimiwa Spika;
Ni
kweli kabisa hatukuunga mkono kuharakisha Shirikisho la Kisasa kabla ya
kukamilisha baadhi ya hatua. Na,
tulifanya hivyo kwa nia njema ya kutaka Shirikisho lijengwe juu ya msingi
imara. Na, msingi huo si mwingine bali
utengamano wa kiuchumi kwa maana ya Umoja wa Forodha, Soko la Pamoja na Umoja
wa Kifedha zilizojengeka vizuri na kufanya kazi ipasavyo na kunufaisha
wanachama wote sawia.
Mheshimiwa Spika;
Lazima tutambue ukweli kuwa kunufaika kiuchumi
ndicho kichocheo kikubwa cha nchi kujiunga na kuendelea kuwa mwanachama wa
Jumuiya yetu. Kama mambo ya kiuchumi yakipangika
vizuri na kila nchi ikanufaika sawia, unajenga msingi imara kwa Shirikisho la
Kisiasa kustawi na kudumu. Kama ngazi
hizi tatu za awali hazitashughulikiwa vizuri na nchi wanachama zikahisi
hazinufaiki ipasavyo, Shirikisho litayumba au kuyumbishwa hivyo kudumu kwake
kutakuwa kwa mashaka.
Mheshimiwa Spika;
Tanzania ni kati ya zile nchi zinazotaka
ngazi zote za mchakato wa utengamano zitekelezwe moja baada ya nyingine bila
kuruka hata moja. Kwa msimamo na mtazamo
wetu, Shirikisho iwe ndiyo hatua ya
mwisho. Na huo siyo msimamo wangu au wa
Serikali peke yake, ndiyo msimamo wa Watanzania walio wengi.
Bila ya shaka sote tutakumbuka kuwa
mwaka 2006 Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya waliunda Kamati Maalum katika
kila nchi kukusanya maoni ya wananchi kuhusu kuharakisha Shirikisho la Afrika
Mashariki. Kwa hapa nchini Kamati hiyo
iliongozwa na Profesa Samwel Wangwe na katika taarifa yake, Kamati ilieleza kuwa asilimia 74.4 ya Watanzania wanaunga mkono kuwepo kwa Shirikisho
lakini ni asilimia 25.4 tu ndiyo waliunga mkono
kuharakishwa kwake.
Mheshimiwa Spika;
Takwimu hizi zinaelezea ukweli kuhusu
hisia za Watanzania, kuhusu kuwepo kwa Shirikisho na kasi ya utekelezaji
wake. Watanzania wengi sana wanaunga
mkono kuwepo kwa Shirikisho la Afrika Mashariki lakini wanataka jambo hilo lisifanywe
haraka haraka. Wanataka lifanywe kwa
umakini mkubwa na tuende hatua kwa hatua kama ilivyoainishwa katika Mkataba
uliounda Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Spika;
Sera na msimamo wa Serikali ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania inakwenda sambamba na ile ya wananchi wa Tanzania. Ndiyo maana tumeafiki mapendekezo ya Kamati ile
ya mwaka 2004 iliyoongozwa na
Mheshimiwa Amos Wako wakati ule akiwa Mwanasheria Mkuu wa Kenya. Kamati hiyo iliundwa kupendekeza namna ya
kuharakisha utekelezaji wa mchakato wa utengamano wa Afrika Mashariki.
Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
umetamka muda wa kutekeleza ngazi ya Umoja wa Forodha lakini uko kimya kuhusu
ngazi zilizofuata. Ili kuondoa kasoro
hiyo na kwa nia ya kuharakisha Shirikisho Kamati ilipewa jukumu la kutoa maoni
na mapendekezo juu ya namna ya kufanya hivyo.
Kamati ilifanya kazi nzuri ya kupata maoni na hisia za watu wa makundi
mbalimbali katika nchi wanachama kuhusu ujenzi wa Jumuiya na utengamano.
Mheshimiwa Spika;
Kwa upande wa Tanzania kwa mfano,
Kamati ya Mheshimiwa Amos Wako ilitambua hisia za Watanzania kuhusu ardhi na
ajira na kupendekezwa kuwa masuala hayo yabaki kwenye mamlaka ya nchi wanachama
kuamua. Kuhusu mchakato wa utengamano Kamati
ilipendekeza kwanza kwamba mchakato wa ujenzi wa Umoja wa Forodha uachwe mpaka
ufike ukomo wake wa miaka mitano. Baada
ya hapo muda wa kutekelezwa ngazi zinazofuata unaweza kupunguzwa. Kwa mfano walipendekeza kuwa matayarisho ya
kuunda Soko la Pamoja yaanze hata kabla ya mchakato wa Umoja wa Forodha kufika
mwisho ili mara wakati huo ukifikiwa Soko la Pamoja linaanze. Hivyo hivyo mara baada ya ngazi hiyo kuanza
matayarisho ya kuanza ngazi ya Umoja wa Kifedha yanaanza. Ngazi hiyo nayo ikianza matayarisho ya kuunda
Shirikisho yanaanza. Kamati pia imetoa
mapendekezo ya namna ya kufikia uamuzi kuhusu Shirikisho kwamba wananchi wa
nchi wanachama wataamua kwa kura.
Tukifuata mapendekezo ya Kamati ya Mheshimiwa Amos Wako na wenzake kama
tufanyavyo sasa Tanzania haina matatizo nayo.
Mheshimiwa Spika;
Baada ya kazi kubwa na nzuri
iliyofanywa na wana-Afrika Mashariki kuhusu ujenzi wa Jumuiya yao inasikitisha
kuona vinafanyika vitendo vinavyoanzisha mivutano kuhusu mambo yaliyokwisha fanyiwa
kazi na kuamuliwa. Tunapata taabu zaidi
pale watu wanapobagua wenzao na wanapofanya mambo yanayopingana na Mkataba wa
Jumuiya na Itifaki zake. Kwa kweli kama
mwenendo huu hautabadilika sijui mambo yatakuwaje mbele ya safari.
Mheshimiwa Spika;
Nchi
yetu inapenda kuona kuwa tunakuwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyo imara na
iliyo endelevu. Jumuiya ambayo
inaendeshwa vizuri, mambo yake ni mazuri na nchi zote wanachama na watu wake
wananufaika nayo, na hivyo wanaifurahia.
Tanzania haina tatizo na kuharakisha mchakato wa utengamano, lakini
tunapata taabu kuruka baadhi ya hatua kabla hazijakamilika. Tunawaomba wenzetu kuwa makini katika kila
hatua tunayochukua. Bila ya kufanya
hivyo, Jumuiya yetu itakuwa imejengeka
katika msingi dhaifu hivyo ustawi na uhai wake utakuwa na changamoto
nyingi. Hatupendi ya mwaka 1977 yatokee
tena.
Mheshimiwa Spika;
Napenda
kuwahakikishia kuwa Tanzania itaendelea kushiriki katika shughuli za Jumuiya ya
Afrika Mashariki na kuimarisha utengamano wa Afrika Mashariki kwa kuzingatia
matakwa ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Itifaki zake. Tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha kuwa Jumuiya
haidhoofiki wala kufa. Na iwapo
itadhoofika au kufa kamwe hatutaki Tanzania inyooshewe kidole kuwa chanzo wala kichocheo
chake. Ndiyo maana, hatutachoka
kuzungumza na wenzetu kuhakikisha kuwa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki
inaendelea kustawi.
Tutaendelea
kukumbushana umuhimu wa kufanya mambo yanayojenga na kuepuka yale yanayoweza
kubomoa. Tutakumbushana umuhimu wa
kuheshimu matakwa na masharti ya Mkataba ulioanzisha Jumuiya, Itifaki zake na
maamuzi halali ya vikao rasmi na asasi za Jumuiya. Tukifanya hivyo Jumuiya ya Afrika ya
Mashariki itadumu, itazidi kustawi na kunufaisha nchi wanachama na watu wake
kama yalivyo malengo na madhumuni ya kuundwa kwake.
Mungu Ibariki Afrika
Mungu Ibariki Tanzania
Idumu Jumuiya ya Afrika Mashariki
Mheshimiwa Spika na
Waheshimiwa Wabunge;
Asanteni sana kwa
kunisikiliza
0 comments:
Post a Comment