HOTUBA YA
MHESHIMIWA DK. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA
TANZANIA, KWENYE KILELE CHA SIKUKUU YA WAFANYAKAZI DUNIANI MEI MOSI 2016
ILIYOFANYIKA MJINI DODOMA
Mhe. Samia Hassan,
Makamu wa Rais;
Mhe. Kassim Majaliwa,
Waziri Mkuu;
Ndugu Gratian Mukoba,
Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA);
Mama Nortubunga Maskini,
Makamu wa Rais wa TUCTA;
Mheshimiwa Jenista
Mhagama, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira
na Wenye Ulemavu;
Mhe. Tulia Ackson,
Naibu Spika;
Balozi Injinia John
Kijazi, Katibu Mkuu Kiongozi;
Mheshimiwa Jordan
Rugimbana, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma;
Waheshimiwa Mawaziri wote,
na Waheshimiwa Wabunge mliopo;
Bi. Mary Kawar,
Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO), Ofisi ya Nchi za Afrika Mashariki;
Waheshimiwa Mabalozi mliopo;
Waheshimiwa Majaji,
Mheshimiwa Almas Maige,
Mwenyekiti wa Chama cha Waajiri Tanzania;
Dr. Aggrey Mlimuka,
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE);
Ndugu Nicholaus Mgaya,
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA);
Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi;
Viongozi na Maafisa wa Serikali mliopo;
Wawakilishi wa Vyama
vya Siasa mliopo; Mzee Mangula, Makamu Mwenyekiti wa CCM
Bwana Kimbisa (Mb),
Mwenyekiti wa CCM Mkoa;
Wanahabari;
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Dodoma;
Ndugu Wananchi;
Ndugu Wafanyakazi;
Mabibi na Mabwana.
Awali ya yote napenda
kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uhai na afya njema na kuweza kukutana hapa.
Leo ni siku muhimu sana. Tupo hapa kwa ajili ya kuenzi na kuthamini mchango wa
wafanyakazi wa Tanzania, wake kwa waume, walioko sekta binafsi na ya umma, na ambao kila siku tangu asubuhi hadi jioni
wamekuwa wakivuja jasho kwa ajili ya maendeleo ya taifa letu.
Hii si mara yangu ya
kwanza nashiriki Sherehe ya Siku ya Wafanyakazi, maarufu kama Mei Mosi. Nimeshiriki kwenye sherehe
hizi mara kadhaa. Lakini leo nashiriki kipekee kabisa. Nashiriki kwa mara ya
kwanza tangu nichaguliwe kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwezi
Oktoba 2015. Hivyo, napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru Viongozi wa
Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) na Vyama vyote vya Wafanyakazi
nchini kwa kunialika ili nijumuike nanyi kwenye Sherehe hizi za Siku ya Wafanyakazi
Duniani mwaka huu. Aidha, napenda kuwashukuru wafanyakazi wote wa Tanzania kwa
kunipa kura nyingi zilizoniwezesha
kuchaguliwa kuwa Rais wa nchi hii. Naahidi kwenu kuwa sitawaangusha.
Nitumie fursa hii pia
kuwapongeza sana wananchi wa Mkoa Dodoma
chini ya Uongozi wa Mkuu wa Mkoa, Mheshimiwa Jordan Rugimbana kwa kukubali kuwa
wenyeji wa Sherehe hizi pamoja na
maandalizi mazuri mliyofanya kufanikisha sherehe hizi. Sherehe zimefana,
hongereni sana! Nawashukuru pia wananchi wa Dodoma kwa kunipa kura nyingi
wakati wa uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.
Aidha, ninawashukuru
sana Wafanyakazi na Wananchi wote mliojitokeza hapa leo kwa wingi ili kujiunga
na wenzetu duniani kote kusherehekea siku hii muhimu ya Wafanyakazi Duniani.
Ndugu Wafanyakazi na Wananchi kwa ujumla;
Duniani kote
wafanyakazi ni nguzo muhimu ya maendeleo. Hakuna taifa lolote duniani ambalo limeweza
kuendelea bila kutegemea wafanyakazi wake. Hapa nchini, wafanyakazi wametoa
mchango mkubwa kwa maendeleo ya taifa letu tangu kipindi cha ukoloni hadi sasa.
Bila shaka wengi wetu hapa tunafahamu namna wafanyakazi na vyama vya
wafanyakazi vilivyoshiriki kikamilifu katika harakati za ukombozi wa nchi yetu.
Baada ya nchi yetu kupata uhuru, wafanyakazi wameendelea kutoa mchango mkubwa
kwa maendeleo ya nchi yetu.
Nitumie fursa hii
kuwapongeza wafanyakazi kote nchini kwa kazi kubwa na nzuri mnayoifanya kwa
maendeleo ya taifa letu. Ninyi ndio mmejenga miundombinu mbalimbali
tunayoitumia hivi sasa, ninyi ndio mnahakakikisha Watanzania wanapata huduma bora
za elimu na afya lakini hata ulinzi na usalama wa taifa letu kwa kiwango kikubwa
unategemea ninyi wafanyakazi. Hongereni sana wafanyakazi!
Ndugu Wafanyakazi na Wananchi kwa ujumla;
Kama nilivyotangulia
kusema, hii ni sherehe yangu ya kwanza ya Mei Mosi tangu nimechaguliwa kuwa
Rais wa Awamu ya Tano wa nchi yetu. Hivyo, napenda kutumia fursa hii adimu
kuzungumza na wafanyakazi pamoja na wananchi kwa ujumla kuhusu masuala na
mipango mbalimbali ambayo Serikali ya Awamu ya Tano ninayoingoza imepanga
kutekeleza katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Serikali ya Awamu ya
Tano imejipanga kuona nchi yetu inapata maendeleo kwa manufaa ya Watanzania
wote. Tumejipanga kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025
pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala. Sote tunafahamu kuwa Dira ya Taifa
ya Maendeleo inalenga kuiwezesha nchi yetu kuwa ya uchumi wa kati unaongozwa na
viwanda. Ili kutekeleza Dira ya Maendeleo na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala,
tayari tumekamilisha Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano utakaotekelezwa
katika kipindi cha mwaka 2016/17 hadi mwaka 2020/21.
Mpango
huu unadhima ya kujenga uchumi wa viwanda ili kuchochea mageuzi ya kiuchumi na
maendeleo ya watu. Lengo kuu la Mpango huu ni kuhakikisha rasilimali na fursa
za nchi zinatumika vizuri ili kujenga uchumi wa viwanda na kupunguza umasikini.
Baadhi ya malengo mahsusi ni kuimarisha kasi ya ukuaji mpana wa uchumi kwa
manufaa walio wengi, kuongeza kasi ya kupunguza umaskini, kuongeza fursa ya
ajira kwa wote, kuongeza upatikanaji na ubora wa huduma za jamii na kuongeza
mauzo nje kwa bidhaa za viwandani.
Ndugu Wafanyakazi na
Wananchi;
Baadhi
ya masuala muhimu yaliyomo kwenye Mpango wa Maendeleo ambayo tutayatekeleza
katika kipindi cha miaka mitano ijayo ni pamoja na kufufua viwanda na kujenga
vipya, hususan vinavyotumia malighafi zinazopatikana kwa wingi hapa nchini,
teknolojia ya kati, nguvu kazi na ambavyo bidhaa zake zitatumika zaidi hapa
nchini, ikiwemo viwanda vya nguo na bidhaa za ngozi. Aidha, tunakusudia mazingira
ya uzalishaji na uendeshaji biashara kwa kuhakikisha tunajenga miundombinu ya nishati
ya umeme, reli, barabara, maji, madaraja, vivuko, bandari, viwanja vya ndege na
TEHAMA. Tunalenga pia kuhakikisha kuwa panakuwepo ardhi kwa ajili ya uwekezaji
na upatikanaji wa rasilimali-watu yenye ujuzi. Halikadhalika, tutaboresha sera,
sheria, taratibu, uratibu na ushirikiano wa kitaasisi.
Maendeleo
ya uchumi ni lazima yaende sambamba na maendeleo ya watu. Ili kuhakikisha hilo,
vipaumbele vitakuwa ni kuhakikisha watu wanaondokana na umaskini, njaa na
ukosefu wa ajira. Aidha, tutaboresha huduma za jamii, hususan afya na elimu, kwa
kuhakikisha zinapatikana kwa uhakika na ubora unaostahili. Tutahakikisha watu
wengi wanajiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii na pia panakuwepo na usawa wa
jinsia na watu wenye ulemavu, utawala bora, mipango miji na kuogeza juhudi za
kukabiliana na athari za tabianchi.
Matumaini yetu ni
kwamba utekelezaji wa Mpango huu utaleta matokeo chanya kwa nchi yetu kwa kukuza
uchumi kutoka asilimia 7 mwaka 2015
hadi asilimia 10 mwaka 2020; kuongeza
mapato ya yatokanayo na kodi kutoka asilimia
12.1 ya pato la taifa mwaka 2014/15 hadi asilimia 17.1 mwaka 2020; kuongezeka kwa kasi ya kupunguza umaskini
ambapo pato la wastani kwa kila mwananchi litaongezeka kutoka wastani wa dola
za Marekani 1,006 mwaka 2015 hadi 1,500 mwaka 2020; umaskini wa mahitaji
ya msingi kupungua kutoka asilimia 28.2 mwaka 2011/12 hadi asilimia 16.7 mwaka 2020/21; huduma za msingi za afya na elimu
zitaimarika; kuongezeka kwa mauzo nje ya nchi ya bidhaa za viwandani; kuongeza
idadi ya watalii na kuongeza uwekezaji wa moja kwa moja kutoka dola la
kimarekani bilioni 2.14 mwaka
2014/15 hadi bilioni 5 mwaka 2021. Hayo
ndiyo malengo yetu.
Ndugu Wafanyakazi na Ndugu Wananchi
Utekelezaji wa Mpango
wa Maendeleo ya Taifa utagharimu takriban shilingi
trilioni 107, zikiwemo trilioni 59
kutoka Serikalini.Kwa kuanza, kwenye bajeti ijayo, Serikali imetenga kiasi cha jumla ya shilingi trilioni 11.82 kwa ajili ya bajeti ya
maendeleo sawa na asilimia 40 ya
bajeti yote kutoka asilimia 26 mwaka
uliopita. Kati ya fedha za bajeti ya
maendeleo, shilingi 8.702 trilioni
sawa na asilimia 74 ya bajeti ni
fedha za ndani na fedha za nje ni shilingi
3.117 trilioni sawa na asilimia 26.
Kama mnavyoona, sehemu
kubwa ya ugharamiaji wa mpango huu itafanyika kwa kutumia fedha za ndani. Hii
ishara tosha kuwa tumedhamiria kufanikisha azma yetu ya kutekeleza Dira ya
Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025 ili kuleta maendeleo nchini mwetu na
kuwaondolea wananchi kero mbalimbali.
Ndugu Wafanyakazi na Ndugu Wananchi;
Bila shaka baadhi yenu
mtashangaa kwa nini nimetumia Sherehe hii ya Wafanyakazi kuongelea malengo ya
Serikali ya Awamu ya Tano katika kipindi cha miaka mitano ijayo. Jibu ni moja
tu. Imenilazimu kueleza hayo yote ili sisi wafanyakazi wote hapa nchini
tufahamu kazi kubwa iliyopo mbele yetu. Sisi ndio tunategemewa kuwaongoza Watanzania
katika kutekeleza na kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025. Hivyo,
tunaposherehekea sikukuu hii ya wafanyakazi duniani hatuna budi kila mmoja wetu
kujiuliza ni kwa namna gani tutachangia katika kufanikisha utekelezaji wa
Mpango huu wa Maendeleo kwa nchi yetu. Kwa kifupi, naweza kusema kuwa mipango
yote mizuri niliyoieleza hapo juu haiwezi kufanikiwa kama wafanyakazi
hawatashiriki kikamilifu.
Hivyo basi, nitoe wito
kwa wafanyakazi kote nchi kila mmoja kwa nafasi yake kujipanga vizuri katika
kutekeleza Mpango huu. Ni lazima tufanye kazi kwa bidii na kujituma, ueledi
mkubwa na uadilifu. Nchi yetu haitaweza kufikia uchumi wa kati unaoendeshwa kwa
viwanda kama tutaendelea kulea uvivu, uzembe, ubadhirifu, rushwa, ukwepaji
kodi, kutotimiza wajibu wetu na wafanyakazi
hewa. Kwa kutambua hilo, Serikali yenu
imeanza kuchukua hatua za kuimarisha nidhamu na uwajibikaji kwa watumishi Serikalini.
Tayari tumeanza kuwashughulikia watumishi wachache ambao ni wazembe, wavivu, wala
rushwa, wabadhirifu na wasio na maadili.
Nafahamu, watumishi wazembe
na wabadhirifu ni wachache. Lakini watumishi hao ndio wamekuwa wakiharibu sifa
nzuri ya watumishi wa umma. Hawa ndio wamekuwa wakirudisha nyuma gurudumu la
maendeleo la nchi yetu. Hawa ndio wamekuwa wakinufaika na kunyonya jasho la
wafanyakazi walio wengi wa Tanzania. Sasa
mwisho wao umefika. Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kuwashugulikia popote
walipo. Hatutawaonea aibu au huruma watumishi wa aina hii. Nimefurahi kusikia Vyama
vya Wafanyakazi viko pamoja na Serikali na havitaunga mkono mtumishi mzembe,
legelege na fisadi. Mmezidi kutupa nguvu zaidi ya kuendelea na jitihada
tulizozianzisha za kurejesha nidhamu ya kazi kwenye utumishi wa umma. Niwaombe
pia tushirikiane katika kushughulikia wafanyakazi hewa. Wafanyakazi hewa wameigharimu
Serikali fedha nyingi ambazo zingeweza kuboresha maslahi ya wafanyakazi halali
na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Hadi leo idadi ya wafanyakazi hewa
waliopatikana ni 10,295. Kati ya
wafanyakazi hao 8,373 ni kutoka
Serikali za Mitaa na 1,922 ni wa
Serikali Kuu. Kutokana na wafanyakazi hao hewa Serikali imekuwa ikilipa kiasa
cha shilingi 11,603,273,799.41 kila
mwezi sawa na shilingi 139,239,285,592.92
kwa mwaka sawa na shilingi 696,196,427,964.6
kwa miaka mitano. Fedha hizi zingeweza kujenga barabara za juu (flyovers) tano
au kuboresha maslahi ya watumishi halali ama kuboresha huduma mbalimbali za
jamii. Aidha, nafasi hizo hewa zingeweza kutoa ajira kwa wahitimu wa vyuo vikuu
mbalimbali ambao wanatafuta kazi na hivyo kuleta manufaa kwa taifa.
Ndugu Wafanyakazi;
Wakati nikitoa rai kwa
watumishi legelege, wabadhirifu na wala rushwa kubadilika, napenda pia kutumia
fursa hii kuwapa moyo wafanyakazi wote ambao ni wachapakazi na ambao wanatekeleza
majukumu yao kwa ueledi na uadilifu. Endeleeni kufanya kazi kwa kujiamini,
kujituma bila ya kuwa wasiwasi wowote.
Nafahamu wapo baadhi ya watu wamekuwa wakiwatisha na kuwaeleza kuwa Serikali ya
Awamu ya Tano haijali wafanyakazi. Wapuuzeni watu hao. Hao ndio wale waliokuwa
wakinufaika au kushirikiana na watumishi mafisadi, wala rushwa na wabadhirifu.
Sasa wanatapatapa baada ya kuona Serikali inachukua hatua mahsusi kwa watumishi
wa namna hiyo. Serikali ya Awamu ya Tano haitambuguzi mfanyakazi yeyote ambaye
anajituma na kufanya kazi kwa ueledi na uadilifu. Nipende kusema tu Serikali
yangu itawalinda na kuwatetea wafanyakazi waadilifu na wachapakazi.
Ndugu Wafanyakazi;
Wakati wa Kampeni na hata
nikifungua Bunge niliwaahidi wafanyakazi wote wa umma na sekta binafsi kuwa ningeboresha
maslahi na mazingira
yenu ya kufanya kazi, ikiwemo kuongeza mishahara, kuwapatia vitendea kazi,
pamoja na kulinda na
haki za msingi za hifadhi ya jamii kama huduma za afya na malipo ya pensheni
baada ya kustaafu kazi. Ahadi yangu hii bado ipo pale
pale na nawaahidi tena sitawaangusha. Kwa bahati nzuri hata kaulimbiu ya Mei
Mosi mwaka huu ambayo; “Dhana ya Mabadiliko Ilenge Kuinua Hali ya
Wafanyakazi” inasisitiza umuhimu wa kuboresha maslahi na mazingira ya
kazi ya wafanyakazi.
Kama alivyosema Katibu
Mkuu wa TUCTA kuwa tangu tumeingia madarakani, tumeweza kuongeza ukusanyaji wa mapato
kutokana na kuziba mianya mingi ya ukwepaji kodi na kudhibiti matumizi yasiyo
ya lazima. Hata hivyo, sio dhamira yetu
na bila shaka sio dhamira ya Watanzania walio wengi kuona fedha zote tunazokusanya
tunazitumia kwa ajili ya kulipia mishahara watumishi tu. Nasema hivi ili mfahamu kwamba mapato haya
yanawahitaji wengi sana. Wananchi walio wengi wamepata matumaini kuwa kutokana
na kuongeza kwa mapato sasa huduma mbalimbali zitapatikana kwa ubora na
uhakika. Hivyo, niwajibu wetu sisi mliotukabidhi kuongoza Serikali kuhakikisha
tunatumia vizuri rasilimali za nchi kwa manufaa ya Watanzania wote. Na
ninapenda kutumia fursa hii kuwahakikishia kuwa tutaelekeza fedha tunazozipata
katika maeneo muhimu ambayo yanamgusa kila Mtanzania, wakiwemo wafanyakazi.
Ndugu Mwenyekiti wa TUCTA;
Ndugu Katibu Mkuu wa
TUCTA;
Ndugu Wafanyakazi;
Hivi
punde nimetoka kusikia risala yenu nzuri iliyosomwa na Katibu Mkuu wa TUCTA,
Bwana Nicholas Mgaya. Sitaweza kujibu hoja zote zilizotajwa kwenye risala yenu.
Lakini napenda kuwahakikishia kuwa Serikali imezipokea hoja zenu zote na
tutazifanyia kazi. Hata hivyo, naomba mniruhusu nieleze japo kwa uchache baadhi
ya hoja mliyotaja kwenye risala yenu:
Kwanza, kuhusu suala la kupunguza kodi ya mapato ya
mshahara (PAYE) kwa wafanyakazi. Napenda
kuwaarifu kuwa Serikali yangu kama nilivyoahidi wakati wa kampeni zangu
nimeamua kuwapunguzia Wafanyakazi kodi ya Mapato ya Mishahara kutoka asilimia 11 ya sasa hadi asilimia 9 kuanzia mwaka wa fedha wa
2016/17 kutegemea Wabunge watakavyopitisha bajeti yetu. Tuna uhakika kwa
kufanya hivyo, tutakuwa tumewapunguzia wafanyakzi mzigo mkubwa wa makato katika
mishahara yao. Nimeamua kuanza na hili kwanza ili changamoto zilizopo sasa za
kiuchumi tuweze kuzivuka na baadaye mambo yakiwa mazuri tutaangalia suala la
kupandisha mishahara.
Pili, suala la tofauti ya mishahara. Tayari tumeanza
kuchukua hatua kuhakikisha tunakuwa na mfumo wa mishahara ambao unazingatia
vigezo vya uzito wa kazi na kupunguza tofauti kubwa ya malipo ya mshahara kwa
kuoanisha mishahara ya watumishi wa Umma walioajiriwa Serikali Kuu, Serikali za
Mitaa, Taasisi na Mashirika ya Umma. Tunataka Watumishi wa Umma wafaidi matunda
ya kazi kwa kuzingatia uzito wa kazi wanazozifanya kwa misingi ya haki na
usawa.
Aidha, kufuatia
marekebisho ya Sheria ya Taasisi za Kazi Na.7 ya Mwaka 2004, tumeunda Bodi
mbili za mishahara. Bodi ya mshahara katika Sekta Binafsi inayosimamiwa na
Waziri mwenye dhamana ya masuala ya Kazi na Ajira, na Bodi ya Mshahara katika
Utumishi wa Umma inayosimamiwa na Waziri mwenye dhamana ya Utumishi wa Umma.
Majukumu ya Bodi hizi ni kufanya uchunguzi na kupendekeza kima cha chini cha
mshahara katika sekta husika. Ni matarajio yetu kwamba bodi hizi zitatekeleza
majukumu yake kwa weledi kwa kupendekeza viwango vinavyozingatia hali halisi ya
uzalishaji, tija na uchumi wetu. Nilikwisha tamka sitarajii kuwa na mfanyakazi
anayelipwa zaidi ya milioni 15 wakati
wengine wanalipwa laki tatu kwa
mwezi.
Tatu, suala la hifadhi ya jamii. Serikali ya Awamu ya
tano inalenga katika kuhakikisha kwamba wananchi wengi zaidi watafaidika na
mfumo wa hifadhi ya Jamii nchini kuliko ilivyo sasa. Kwa mfano tunataka wananchi wengi zaidi
wajiunge na Bima ya Afya ili wawe na uhakika wa matibabu. Tunaendelea na juhudi
ya kupanua wigo wa Mfuko wa Bima ya Afya vijijini (Community Health Fund) na pia kuwezesha wafanyakazi wengi wa sekta
binafsi kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (National Health Insurance
Fund). Aidha, Mifuko ya Hifadhi ya Jamii imeanza kusajili wananchama toka sekta
isiyo rasmi. Lengo la Serikali ni
kuhakikisha kwamba wananchi wengi wanapata huduma za msingi za hifadhi ya
jamii.
Kwa upande wa
kuimarisha Mifuko ya hifadhi ya jamii pamoja nakuboresha malipo ya Pensheni,
Serikali imekwishaelekeza Mifuko ya Hifadhi ya jamii kuachana na uwekezaji
kwenye miradi isiyokuwa na tija. Wawekeze kwenye maeneo kama viwanda ili
kuzalisha fursa za ajira na kujipatia wanachama zaidi. Aidha, ushauri wenu
wafanyakazi kupitia shirikisho lenu la TUCTA kwa Serikali kuhusu kupunguza
idadi ya Mifuko ya Pensheni nchini na matumizi yasiyo ya lazima umepokelewa na
kukubalika. Lakini ni vyema mfahamu kwamba kutokana na historia tofauti ya
kuanzishwa kwa mifuko ya hifadhi ya jamii iliyopo sasa, hatua zozote za
marekebisho zinahitaji umakini mkubwa. Napenda niwahakikishie kwamba kazi ya
kurekebisha mifuko ya Pensheni nchi tutaikamilisha ndani ya mwaka 2016/2017.
Nne,
suala la Vyama vya Wafanyakazi. Napenda kutoa rai kwa waajiri kote nchini kutambua kwamba suala hili sio la hiari bali
ni wajibu wao kuwaruhusu wafanyakazi kuanzisha na kujiunga kwenye vyama vya
wafanyakazi sehemu za kazi bila ya kushurutishwa au kuchaguliwa chama cha
kujiunga. Hivyo, waajiri wote wanaovunja
takwa hili la sheria watachukuliwa hatua kali. Lakini pia nitoe wito kwenu Viongozi
na wafanyakazi vyama hivyo visitumike kuchocheo migogoro ya kikazi, uzembe na
uvivu kazini na wala visiwe vyama vya kisiasa kazini. Vyama hivyo vinapaswa
kutumika kuimarisha uhusiano kati ya waajiri na waajiriwa, kuhamasisha utendaji
kazi na kuleta utulivu sehemu za kazi.
Tano,
suala la mikataba ya ajira. Waajiri wengi wamekuwa hawatekelezi matakwa sheria
kama yalivyobainishwa katika Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na. 6 ya mwaka
2004 pamoja na marekebisho yake ambayo tumeyafanya mwaka 2015. Bado yapo malalamiko mengi ya wafanyakazi
kutokuwa na mikataba ya kazi, kufanya kazi bila vifaa kinga, michango ya
pensheni kuchelewa kuwasilishwa au kutowasilishwa kabisa kwenye mifuko ya
hifadhi ya jamii. Serikali ya Awamu ya Tano ninayoongoza haitavumilia ukiukwaji
huu wa sheria.
Ili
kuhakikisha waajiri wanatekeleza kwa hiari bila shurti sheria za kazi, tuanza
kurekebisha tena Sheri ya Ajira na mahusiano kazini kwa kuanzisha adhabu za
papo kwa papo ambapo waajiri watalazimika kulipa faini kwa kila kosa la
kutotekeleza sheria za kazi. Pia, katika mwaka huu wa fedha, Serikali imetenga
fedha kuajiri maofisa kazi zaidi wapatao 21 ili kuimarisha huduma za ukaguzi
sehemu za kazi. Nitoe wito kwa Vyama vya wafanyakazi, kushirikiana kwa karibu
na Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu). Aidha,
ninaziagiza Mamlaka zinazohusika kusimamia utekelezaji wa Sheria za kazi
kusimamia sheria husika bila woga kwa lengo la kuwalinda wafanyakazi
wasiendelee kutumikishwa na kunyonywa.
Aidha,
naziagiza mamlaka husika kushughulikia suala la ajira za wageni ambazo zinaweza
kufanywa na wazawa. Hakuna nchi yoyote duniani ambayo jukumu lake kubwa ni
kuwatafutia ajira wageni kazi ambazo ingeweza kufanywa na wazawa. Naagiza
Wizara zote zisimamie hili suala kwa nguvu zote ili wazawa wapate ajira kwanza.
Sambamba na hilo, wahusika wote mshirikiane pia kuwafichua wale wote
watakaofanya kazi bila vibali. Nakumbuka zoezi hili lilianza sitaki kuamini
kuwa ilikuwa ni nguvu za soda. Mheshimiwa Waziri tafadhali simamia hili.
Suala jingine ambalo nalo limekuwa ni
tatizo sugu ni baadhi ya waajiri kushindwa kuwasilisha michango ya wafanyakazi
wao kwenye mifuko ya hifadhi kwa wakati.
Ingawa wafanyakzi wamekuwa wakikatwa kila mwezi lakini fedha hizo
hazifiki kunakohusika. Tatizo hili pia linaihusu Serikali kutokana na Hazina
kutopeleka michango. Hivyo, natoa wito kwa waajiri wote nchini kuwasilisha
michango ya wafanyakazi wao kila mwezi bila kukosa. Hivyo, natoa wito kwa
waajiri wote nchini kuwasilisha michango ya wafanyakazi wao kila mwezi bila
kukosa.
Kwa
upande wa Serikali tayari tumeanza kulishughulikia suala hili la michango kwa
kutambua wafanyakazi wote halali ili michango yao iwasilishwe. Mathalan, kwenye
Mfuko wa PSPF Serikali ilikuwa ikidaiwa shilingi takriban bilioni 710 bilioni lakini hadi sasa tumelipa
takriban shilingi 500. Ni imani yangu kuwa michango ya inayotakiwa kulipwa na Serikali
kwenye Mifuko ya Hifadhi itapungua kutokana na zoezi la kuwaondoa wafanyakazi
hewa. Tunaomba Vyama vya Wafanyakazi vishirikiane na Serikali kufichua
watumishi hewa.
Ndugu Mwenyekiti wa TUCTA;
Mheshimiwa Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu
Waheshimiwa Mawaziri na
Waheshimiwa Wabunge mliopo;
Ndugu Katibu Mkuu wa TUCTA;
Wageni Waalikwa;
Ndugu Wafanyakazi;
Mabibi na Mabwana:
Napenda
kuhitimisha hotuba yangu kwa kuwashukuru tena Viongozi wa TUCTA na Vyama vya
Wafanyakazi nchini kwa heshima mliyonipa ya kushiriki kwenye Sherehe hizi. Aidha,
napenda kurudia tena wito wangu kwa Wafanyakazi
na wananchi wote kwa ujumla, tuendelee kufanya kazi kwa bidii, kwa nguvu zetu zote, kwa maarifa yetu yote na kwa
kuzingatia misingi ya uwajibikaji na uadilifu ili tuweze kusukuma gurudumu la
maendeleo ya nchi yenu. Tuachane na mazoea ya watu kuingia kazini asubuhi na
kuondoka saa nne.
Tukumbuke
ya kuwa kazi ni utu, kazi sio fursa ya kupata mshahara kwa manufaa ya familia zetu
tu bali ni fursa nzuri ya kutoa mchago kwa taifa lako kwa manufaa ya kizazi cha
sasa na kijacho.
Mungu Wabariki Wafanyakazi Watanzania!
Mungu Ibariki Tanzania!
“Ahsanteni kwa Kunisikiliza”.
No comments:
Post a Comment